• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China imeipa kipaumbele ustawi wa raia wake na hali njema duniani

    (GMT+08:00) 2020-05-23 09:37:07

    China imeipa kipaumbele ustawi wa raia wake na hali njema duniani

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Macho yote kwa sasa yameelekezewa China wakati huu ambapo viongozi na wabunge nchini humo wanakutana tena kwa mkutano wa bunge wa mwaka, jijini Beijing. Hii hasa inatokana na kuzuka kwa maradhi ya covid-19 ambayo imeyumbisha uchumi wa dunia kwa kiwango ambacho kamwe haijawahi kushuhudiwa.

    Ukweli kote ulimwenguni ni kwamba janga hili litasambaratisha uchumi wa karibu mataifa yote ya dunia. Hii ni kwa sababu sekta muhimu ambazo ni msingi wa uchumi zimekwama.

    Kando na ilivyo desturi nchini China, serikali ya nchi hiyo imedinda kutangaza matarajio ya ukuaji maalum wa uchumi wa kila mwaka kwa mwaka 2020. Badala yake, nchi hiyo inayoongozwa na chama cha kikomunisti inasema kuwa itazingatia kudumisha hali ya kiuchumi iliyopo, huku ikiweka kipaumbele kwa ustawi wa raia wake.

    "Kutoweka lengo maalum kwa ajili ya ukuaji wa uchumi itatuwezesha kuzingatia kuhakikisha misingi ya uchumi wetu ni imara. " Waziri Mkuuu Li Keqiang alisema.

    Akizungumza wakati wa kutoa ripoti ya kazi ya serikali katika jumba la Great Hall of the People jijini Beijing, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bwana Li Keqiang alibainisha kwamba "kutokana na athari za janga hilo, ni vigumu sana kutabiri kiwango cha ukuaji wa uchumi wa nchi."

    "Nchi yetu itakuwa na mambo kadhaa ambayo ni vigumu kutabiri katika maendeleo yake kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu lini janga hilo litamalizika ulimwenguni na mazingira ya kiuchumi na kibiashara ya dunia," alisema Waziri Mkuu.

    Katika ripoti ya kazi ya 2020, masuala kama vile usalama wa kazi, mahitaji ya kimsingi ya maisha, shughuli za soko, utoshelevu wa chakula na nishati, viwanda imara na uendeshaji wa kawaida wa shughuli za serikali za ngazi za msingi yatapewa kipaumbele.

    Kwa kweli, janga hilo limegharimu pakubwa uchumi wa China na hata ingawa uchumi huo unatarajiwa kufufuka kutokana na sera nzuri za serikali, China inaonekana imesadiki hali halisi ya ugumu, pamoja na hatari zinazotokana na hali ya kutokuwa na uhakika, na imeshawishika kuchukua hatua za dharura.

    Na ili kukinga raia wake kutokana na athari za janga hilo, serikali imeahidi kupunguza kodi na ada zaidi kwa makampuni yenye lengo la kupunguza mzigo, huku wakiimarisha msaada wa kifedha kwa shughuli za biashara kubwa.

    "Kwa sasa na katika siku zijazo, China itakabiliwa na hatari na changamoto chungu nzima," Bwana Li alikiri.

    Hata hivyo, alibainisha kwamba China ina uwezo wa kipekee wa kisiasa na kitaasisi, pamoja na msingi imara wa kiuchumi, uwezo mkubwa wa soko, na mamia ya mamilioni ya raia wenye akili na bidii itakayoiwezesha kushinda changamoto hizi zote.

    Ripoti hiyo inazungumzia umuhimu wa kupanua nafasi za ajira huku serikali hiyo ikilenga kutoa ajira zaidi ya 9,000,000 zitakazoundwa mwaka huu pekee.

    Waziri Mkuu hata hiyo alisisitiza kwamba kutoweka lengo maalumu ya uchumi wa mwaka haimaanishi kuwa China imelemaza azma yake ya kuafikia ukuaji thabiti.

    Serikali ya China inaelezea imani yake kwamba uchumi wake bado una matarajio angavu ya kutimiza matakwa ya maendeleo kote nchini huku ikitimiza wajibu wake kwa washirika wake wa kimataifa. Haswa Waziri Mkuu Li alisisitiza kuwa nchi yake itazidi kununua bidhaa kutoka nchi za nje.

    Mwaka wa 2020 ni muhimu kwa China, kwa vile nchi hiyo iko katika hatua yake ya mwisho ya kuondoa umasikini na kujenga jamii yenye mafanikio katika mambo yote. Katika mpango huu, serikali ina nia ya kutoa makazi ya kutosha, vifaa vya matibabu pamoja na huduma nyingine za umma kwa raia wote.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako