• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ahadi ya China kwa washirika wa kiuchumi ni habari njema hasa kwa Afrika

    (GMT+08:00) 2020-05-26 17:12:05

    Ahadi ya China kwa washirika wa kiuchumi ni habari njema hasa kwa Afrika

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Dunia kwa sasa inapambana vurugu inayotokana na janga la chamuko la homa ya Corona. Waangalizi wengi wanashikilia mtazamo kwamba janga hili litavuruga uchumi wa dunia kwa kiwango ambacho kamwe haijawahi kutokea. Hata ingawa ukubwa kamili wa athari zake haujadhihirika kwa sasa, siku za baadaye kwa nchi nyingi hasa katika mataifa yanayoendelea yamejaa mashaka.

    Ili kustahimili dhoruba ya janga hili, mataifa lazima yapigane na ugonjwa huu kwa pamoja. Katika vita hivi, mimi, kama wengine wengi walivyohoji, kwa maoni yangu, hakuna yeyote anayefaa kuachwa nyuma. Huu si wakati wa mwenye nguvu mpishe bali hii ni safari ambapo mwenye nguvu lazima amsaidia aliye dhaifu.

    Mara nyingi inasemekana kuwa urafiki halisi uonekana wakati wa shida. Na hivyo basi, akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Huu kwa hakika ni wakati mwafaka wa kutafuta ishara hizi.

    China ilikuwa taifa la kwanza kugundua na kuripoti kisa cha kwanza cha ugonjwa wa covid-19. Jinsi taifa hilo lilivyoshughulikia mkurupuko huo umepokea uungwaji mkono kutoka kwa wengi hasa kutoka kwa Shirika la afya duniani, WHO.

    Baada ya hatua madhubuti za kuingilia kati, dalili zote zinaonyesha kwamba China imekabili hali sambamba na yaelekea kushinda ugonjwa huu. Lakini hata katika ushindi huo, serikali, kupitia ripoti ya kazi ya mwaka huu, imesadiki kwamba inapambana na pigo la kiuchumi kutokana na ugonjwa huo.

    Baada ya kupita kwa wakati mgumu ndani ya mipaka yake, China ilianza kutupa macho yake kwa hali ilivyo katika mataifa ya nje. Wakati ambapo virusi hivyo vimekuwa vikienea kwa kasi katika maeneo mengine ya dunia, China ilituma msaada wa vifaa vya matibabu kwa nchi nyingi, hasa katika Afrika, huku ikishiriki ujuzi wake katika kupambana na maradhi hayo. Ishara hii imeonyesha kwamba China ni taifa linalowajibika.

    Msaada kwa Afrika

    Lakini hii si mara ya kwanza kwa China kujitokeza na kuisaidia Afrika wakati wa mgogoro wa afya ya umma. Wakati wa mchipuko wa ugojwa wa Ebola, China ilitoa msaada wa madaktari wabingwa, vifaa, fedha na teknolojia ili kupiga jeki juhudi za kupigana na ugonjwa huo hatari.

    Athari za kiuchumi za janga hili tayari zimekumba nchi nyingi za Kiafrika. Baadhi ya sekta kuu zilizoathirika ni pamoja na ile ya angani, ukarimu, na utalii. Wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi, wafanyakazi wa kawaida, na wenye malipo ya kila siku katika sekta rasmi wamejipata taabani kwani viwanda vimekwamisha kabisa au kusitisha shughuli kwa muda.

    Katika baadhi ya mataifa, sekta ya kilimo tayari ilikuwa katika shida. Kabla ya chamuko la covid-19, sehemu kadhaa za bara la Afrika zilikuwa zikipambana na uvamizi wa nzige. Bilas haka, wakati ushindi dhidi ya corona utakapotangazwa, sekta ya kilimo itahitaji mpango mahsusi wa ufufuzi ili iweze kuinuka tena.

    Kwa hiyo, ilikuwa jambo la kutia moyo kupokea uhakikisho wa utawala wa Rais Xi Jinping wiki hii kwamba China kamwe haitakosa kutimiza ahadi zake kwa washirika wake wa kimataifa.

    Ukweli ni kwamba wakati China haikua imetoa taarifa yake rasmi kuhusu mipango yake kwa miaka yanayofuatia, baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa bunge wa mwaka, kwa karibu miezi mitatu, kulikuwa na hali ya wasiwasi.

    Wengine walizungumzia wasiwasi wao kuwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Asia labda ingepunguza mipango yake ya kiuchumi nje ya nchi baada ya janga la covid-19 kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wake.

    Lakini mkutano huo mkuu hatimaye uliitishwa na unaendelea na uamuzi umetolewa. China imeapa kuwa haitageuka washirika wake ambao wameenea duniani kote, hasa bara la Afrika, ambalo ni mshirika mkubwa zaidi wa China kibiashara wakati huu.

    Akihutubia waandishi wa habari pembeni mwa kikao cha kitaifa cha wabunge cha kila mwaka linaoendelea, Waziri wa mambo ya nje wa China, bwana Wang Yi, kwa uwazi alizungumzia hatua zitakazochukuliwa na nchi yake kusaidia Afrika kupambana na janga hili.

    Ahadi yake kwamba China itaendelea kusaidia nchi za Afrika yaliyo chini ya matatizo makubwa kupitia njia ya ushirikiano wa pande zote mbili ili kustahimili kipindi kigumu, itapokelewa vyema.

    Pili, ufichuzi wa Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu kwamba China itafanya mazungumzo pamoja na wanachama wa G20 ili kutekeleza mpango wa kusitishwa kwa muda kwa madeni ili kupunguza mzigo wa madeni kwa nchi za Afrika, umekuja kwa wakati ufaao.

    Akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Wang alibainisha kuwa China pia itajitahidi kudumisha "udhabiti wa viwanda vikuu kote ulimwenguni, na kuimarisha biashara na uwezeshaji ili kukabiliana na shinikizo kwa uchumi wa dunia."

    Kwa njia ya msaada huo, Wang alikuwa mwepesi kutaja kwamba China kamwe haina lengo lingine fiche la kiuchumi, na wala haina haja ya kuambatanisha msaada wake na masharti yoyote ya kisiasa.

    Hivi karibuni, China ilipunguza vizuizi ili kuwezesha uwekezaji wa kigeni na kuingia kwa bidhaa za kigeni katika masoko yake. Mauzo ya Afrika kuelekea China kwa sasa ni pamoja na chakula na bidhaa za kilimo. Lakini kiwango cha sasa cha uzalishaji hairidhishi. Ikilinganishwa na mataifa mengine yanayoendelea, uzalishaji wa kilimo wa Afrika umeachwa nyuma. Baada ya China kufungua milango yake, ni vyema kutumia fursa hii kufaidi raia wa Afrika.

    Aidha, nchi za Afrika lazima zianze kukumbatia majukwaa kama vile China International Import Expo ambayo yanatoa njia mbadala kwa wafanyabishara na nchi kufanya biashara katika ngazi ya kimataifa.

    Itakumbukwa kwamba kupitia mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja, China imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na teknolojia katika bara la Afrika. Miradi yaliyoanzishwa chini ya mpango huu yametatizwa na mkurupuko wa virusi vya Corona. Ili kuafikia maendeleo endelevu, ni muhimu kwamba miradi hii yatarejelewa baada ya janga hili, kwani mengi yanategemea kuendelezwa kwao.

    Hii ndio sababu ahadi ya bwana Wang kwamba China itaendelea kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine kupitia mpango huo, huku nchi yake ikiiunga mkono muungano wa mataifa kwa lengo la pamoja, pia ni habari njema kwa bara hili.

    Chamuko la Corona limeonyesha kuwa hakuna taifa linaloweza kusimama pekee. Uamuzi wa China kupinga juhudi za kutengwa kwa nchi yoyote lazima uungwe mkono na wote wenye nia njema. Ili kusonga mbele na kuafikia maendeleo mahsusi, mataifa yanapaswa kushirikiana kujenga jamii yenye mustakabali wa pamoja.

    Serikali ya China imetoa ishara na kuonyesha nia njema ya kisiasa na kiuchumi kwa kutoa usaidizi unaohitajika ili mataifa yaweze kushinda janga hili. Ishara sawia au kubwa kuliko hii ndio kile Afrika inatarajia kutoka kwa mataifa mengine yaliyoendelea.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako