• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nchi zalenga kupanua uhusiano wa kibiashara na China kupitia maonyesho ya Shanghai

    (GMT+08:00) 2020-11-03 08:50:59

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Katika kile kinachoonyesha hali tofauti kabisa na hali ya mambo katika maeneo mengine ya dunia, China inajipanga kuandaa maonyesho ya kila mwaka ya China International Import Expo, kuashiria kurejea kwa hali ya kawaida katika taifa hilo lenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani.

    Hatua ya kuandaa maonyesho hayo ya kibiashara pia inaonekana kuwa thibitisho kwamba juhudi za China za kuzuia na kudhibiti janga la covid-19, ambalo limesababisha mgogoro mkubwa wa kijamii na kiuchumi, zimefanikiwa.

    Lakini mbali na chamuko la corona, kwa miaka ya hivi karibuni, maonyesho haya yamekuwa jukwaa la kubadilishana mawazo, kuingiliana, kuonyeshana bidhaa, na kufanya bidhaa kujulikana kwa umma nchini China, ambayo ndiyo soko kubwa kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.

    Maonyesho hayo maarufu kama CIIE, pia yamewezesha mwingiliano wa viungo na washirika wapya wa biashara, iwe ni katika eneo la magari, huduma za afya na vifaa vya matibabu, biashara, chakula na bidhaa za kilimo, bila kusahau sekta ya teknololojia na habari.

    Hali kadhalika, inatarajiwa kwamba bidhaa, teknolojia, na huduma mpya zitazinduliwa kwa mara ya kwanza katika maonyesho ya mwaka huu. Maonyesho hayo ambayo ni ya tatu tangu kuanzishwa kwake, yatafanyika katika kitovu cha fedha cha China, Shanghai, tarehe 5 hadi 7 Novemba.

    Katika ujumbe wake wa makaribisho, afisi ya maonyesho haya ilibainisha kuwa iko wazi kushirikiana na nchi zote, maeneo na mashirika ya kimataifa "kuifanya CIIE kuwa maonyesho yenye kiwango cha kimataifa, yenye kutoa nafasi murua kwa nchi na maeneo kufanya biashara, kuimarisha ushirikiano na kukuza ustawi wa pamoja wa uchumi wa dunia na biashara."

    Hata ingawa dunia imekumbwa na janga hili la kihistoria, maonyesho haya yamewavutia wengi kwani zaidi ya watu 500,000 kutoka duniani kote wamejiandikisha kwa ajili ya kushiriki. Kwa mujibu wa usimamizi wa mji wa Shanghai, maonyesho haya pia yamewavutia zaidi ya wajumbe 100 wa serikali za kigeni.

    Idadi kubwa ya maombi ya kushiriki maonyesho hayo yaonekana kuchochewa na haja ya kuelewa wateja walioko China na kutimiza matarajio yao.

    Asilimia kubwa ya makampuni ambayo yameomba kushiriki maonyesho hayo yanachukulia jukwaa hilo kama fursa ya kipekee ya kuchunguza soko la China na kukuza mauzo ya nje kwa kuandikisha mikataba ya ushirikiano.

    Kupitia maonyesho haya, idadi kubwa ya makampuni, baadhi yao kutoka Afrika, yamesaini makubaliano ya ushirikiano, ambayo tayari yamezaa matunda.

    Mwaka jana, kwa mfano, takwimu kutoka afisi inayoshughulikia tukio hilo zinaonyesha kuwa mikataba yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 71 za Marekani zilikubaliwa.

    Kama ilivyo desturi, makampuni kadhaa ya Kichina pia yatakuwa tayari kubadilishana maoni na kuanzisha mahusiano na jamii ya kibiashara kutoka ulimwenguni kote.

    Uwepo wa makampuni haya katika maonyesho pamoja na washindani mbalimbali wa kimataifa, unatoa fursa nzuri ya kuchambua na kuelewa mwenendo mpya wa soko ambao ni muhumi katika kusaidia kuboresha ubora wa bidhaa.

    Afrika iko kwenye nafasi nzuri ya kufaidika kupitia maonyesho haya hasa, kwani kati ya maeneo ya maonyesho sita, eneo la bidhaa za matumizi imetunukiwa nafasi kubwa zaidi, kwani imechukuwa kumbi nne za jengo hilo la maonyesho.

    Taarifa zilizopo kwenye tuvuti ya usimamizi wa hafla hiyo zinaonyesha kuwa maonyesho ya bidhaa za chakula na kilimo yamewavutia wafanyabiashara wengi - zaidi ya 1,000 kutoka nchi na maeneo 100.

    Aidha, haja ya maendeleo ya kiteknolojia katika bara la Afrika imeangaziwa sana katika siku za hivi karibuni. Hivyo, kushiriki kwa wawekezaji kutoka sekta ya umma na sekta binafsi barani afrika ni muhimu kwani uvumbuzi mpya wa teknolojia ya habari utatolewa na makampuni yanayoongoza ya uhandisi.

    Itakumbukwa kwamba maonyesho haya ya kimataifa ya uagizaji wa China yanawakilisha maono ya Rais Xi Jinping ya kubadilisha ulimwengu kuwa jamii yenye mustakabali wa pamoja kwa binadamu.

    Xi ameitaja CIIE kama mradi ambao una jukumu muhimu katika kupanua mageuzi ya China na kufungua milango kwa dunia, na kwamba hii inadhihirisha utayari wa China kufanya kazi na mataifa yote. Hii, kulingana na wataalam wanafuatilia masuala haya kwa karibu, inaonyesha maono ya maendeleo ya pamoja.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako