Tumetembelea Mlima unaowaka katika eneo la Turpan mkoani Xinjiang. Tumepata fursa ya kujionea mapango ya ma-Buddha. Kitu cha kipekee kilichonifurahisha ambacho kwa watu wengine kilikuwa kero ni joto kubwa zaidi ya sentigredi 45. Kwangu nimependa kwa kuwa ni jambo jipya maishani mwangu na nitalikumbuka kwa muda mrefu sana maishani mwangu.
Aidha, tumetembelea mpango wa kumwagilia zabibu kwa njia ya jadi katika eneo hili. Ni handaki ndefu ambayo imechimbwa na wananchi kufanikisha utiririkaji wa maji toka milimani hadi mashambani. Tumefika katika eneo la wakulima na kupewa maelezo juu ya aina za zabibu zinazolimwa eneo hili la Turpan, namna ya upandaji na utunzani na tukaelezwa pia historia ya kilimo cha zabibu kwa eneo hili.
Wanasema 'Kuona ni kuamini'. Serikali imeweka miundombinu muhimu kuhakikisha wananchi wanafanya kilimo bila kuumia sana. Maji, barabara safi, nyumba za makazi n.k. Kwa bara letu la Afrika (si Tanzania pekee) bado tuna safari ndefu. Serikali zetu zikithamini wakulima kama ifanyavyo serikali ya mkoa wa Xinjiang basi Afrika itakombolewa. Maeneo kama haya viongozi wetu wanatakiwa kupelekwa ili waweze kujifunza namna ya kuwahudumia wananchi wao.
Mpango wa uzalishaji wa umeme (nje kidogo ya Urumqi kuelekea Turpan) kwa njia ya upepo umenivutia sana, upepo unaotumika wala haufikii ule wa Makambako (Iringa) wala wa Singida. Uwezo tunao, viongozi wetu wanatakiwa kuamua ili kulisaidia taifa na wananchi wake. Viongozi wetu waendelee kuimarisha ushirikiano na China na waombe kupewa namna rahisi ya kuzalisha umeme kwa njia hii na waombe kujua teknolojia rahisi ya kufanikisha uzalishaji.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |