Wasikilizaji wapendwa, mliyosikia ni hali motomoto kwenye tamasha la Aken Aites la kabila la wakhazak mkoani Xinjiang. Majira ya joto ni majira mazuri zaidi kwenye sehemu za mbuga za malisho, ambapo wafugaji wa kabila la wakhazak wanafurahia sana tamasha kubwa linalokuja baada ya kuhamahama kwa siku nyingi katika majira ya mchipuko. Tamasha kubwa linalofanyika kwenye mbuga ya Xinjiang ni kama sikukuu kwa wafugaji hao wakhazak.
Watu wa kabila la wakhazak wanaoishi katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uyghur, kaskazini magharibi mwa China ni wa watu kabila lenye historia ndefu sana. Tamasha la Aken Aites ni tamasha la mashindano ya kuimba. Aken, katika lugha ya Kikhazak ni jina la heshima la mshairi wa kabila la wakhazak, na Aites maana yake ni majibizano. Kwenye Tamasha la Aken Aites, wa-aken wawili, yaani washairi wawili, mmoja wa kiume na mwingine wa kike wanakaa chini, kila mmoja anachagua mashairi ya kuimba, na wanaimba kama wanabijizana huku sauti zao zikisikika kwenye mbuga. Baada ya kusikia sauti zao, wakhazak wanaoishi kwenye mbuga wanaweza kupanda farasi kwa haraka kwenda walipo kujumuika pamoja ili kujiburudisha kwa furaha kwenye tamasha hilo.
Mfugaji mmoja wa kabila la wakhazak Bw Murat, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa wakhazak wote wanapenda tamasha la Aken Aites. Wakhazak wanaoishi katika sehemu mbalimbali wanaweza kwenda kushiriki kwenye tamasha hilo bila kujali kama kuna jua kali au kuna mvua kubwa. Alisema:
"Tamasha la Aites ni kama nguzo ya kiroho kwa wakhazak, tamasha hilo linawawezesha wakhazak wanaoishi kwenye mbuga wajiburudishe na kupata furaha kubwa, na wote wanapenda Aites kama nyuki wanavyopenda chavua."
Kwenye tamasha la Aites, wa-aken wanaimba mashairi mbalimbali yanayomithilisha vitu vyote duniani; wakikumbusha historia, kueleza ufahamu kuhusu jua, mwezi, nyota, milima na mito, wanyama wa aina mbalimbali pamoja na historia ya familia za wakhazak, na mambo ya utawala wa serikali. Kuna baadhi ya wakati, waimbaji wanajibizana vikali, na hata wanaweza kuimba kwa kujibizana kwa usiku mmoja mpaka mshindi apatikane. Ndiyo maana, waimbaji yaani wa-aken, wanapaswa kujiandaa kabla ya kushiriki kwenye tamasha hilo. Mwimbaji wa kike Aysham Gul alisema:
"Kwenye Tamasha la Aken Aites, waimbaji mashairi wanatakiwa kuwa na ujuzi kuhusu mambo mengi mbalimbali. Katika zama za hivi sasa, mbali na ujuzi kuhusu mila na desturi, historia na utamaduni wa jadi, wa-aken wanapaswa kusoma vitabu vingi na kupata ujuzi kuhusu mambo ya kisasa, kwa kufanya hivyo wataweza kuimba na kujibizana bila taabu yoyote."
Wasikilizaji wapendwa, mliosikiliza ni uimbaji wa sauti kubwa ukifuatwa na upigaji kinanda wa muziki, kinanda hicho kinaitwa Dongbula, ambacho ni kinanda maarufu cha kabila la wakhazak. Kinanda hicho hubebwa na mwimbaji kila anakokwenda, kwenye mbuga kila ukiwaona wakhazak wakiwa kwenye farasi, utawaona wakiwa wamebeba kinanda cha Dongbula. Bw Berik Tolepbergen ni mwalimu wa upigaji wa kinanda Dongbula katika chuo cha ualimu cha Ili, alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:
"Sisi watu wa kabila la wakhazak tunaishi kwenye mbuga, tunapenda kujifananisha na tai wanaoruka angani, na kinanda Dongbula ni kama mabawa yetu, ni kama rafiki yetu mkubwa, tunapenda kupanda farasi kutembea popote kwenye mbuga tukiwa na kinanda Dongbula, tunaona kinanda hicho kinaweza kutuongezea ari na uchangamfu. Mwimbaji kwenye tamasha akiwa hodari wa kupiga vizuri kinanda Dongbula, uimbaji wake utakuwa na mvuto zaidi."
Wasikilizaji wapendwa, sasa tunawatumbuiza kwa muziki uitwao "Bata maji weupe" uliopigwa kwa kinanda cha Dobula na Berik Tolepbergen.
Wakhazak siku zote wanaishi mbugani, wanafuga na kuhamahama kwa kufuata malisho kwa ajili ya mifugo yao. Mbuga ni kubwa, wafugaji hutapakaa katika sehemu mbalimbali za malisho. Hali hii inawazuia kujumuika kila mara ili kupata habari mpya na kuwasiliana vizuri. Lakini wakhazak wanapolisha mifugo yao wanapenda kuandika mambo yote wanayoona na huku wakiimba wanayofikiri, njia hiyo ya kipekee ya maisha ya wakhazak imevumbua utamaduni wa Aken Aites, huu ni utamaduni wa mtindo wa kipekee, na ni usanii wa kabila la wakhazak.
Utamaduni wa kabila la wakhazak umerithiwa na kuenziwa vizazi hadi vizazi kupitia maisha ya wakhazak ya kufuga na kuhamahama kwenye mbuga kufuata malisho, huku wakiimba mambo yote wanayojionea njiani. Ofisa wa ofisi inayoshughulikia urithi wa utamaduni usioonekana katika Idara ya utamaduni ya Mkoa wa Xinjiang Bw. Ma Yingsheng anasema:
"Waimbaji wa kabila la wakhazak wanapoimba na kujibizana wanawapasha habari nyingi wenzao, kwani mashairi wanaoimba yanahusu historia ya kabila lao, matukio makubwa, mila na desturi, pamoja na sheria na kanuni za jadi, hivyo uimbaji wao una thamani kubwa katika kukumbusha historia, kurithi na kuenzi utamaduni, mila na desturi, na kufanya uvumbuzi wa kiutamaduni pamoja na burudani za wakazi."
Mwezi Mei mwaka 2006, utamaduni wa Aken Aites uliwekwa kwenye orodha ya urithi wa taifa wa utamaduni usioonekana. Tangu hapo Aken Aites inayosifiwa kuwa ni "chimbuko la kabila la wakhazak", imehifadhiwa, kurithiwa na kuenziwa kwa utaratibu kamili na kwa pande zote. Bw. Ma Yingsheng anasema, ili kuwezesha wasanii wa kabila la wakhazak kuongeza hamasa ya kushiriki kwenye mashindano, na kuongeza mvuto wa tamasha la Aken Aites, serikali ya mkoa wa Xinjiang imeweka utaratibu wa kufanyika kwa tamasha la Aken Aites kila baada ya muda fulani, sasa ufanisi wa kuhifadhi Aken Aites umepatikana baada ya utaratibu huo kutekelezwa katika miaka 6 iliyopita. Bw. Ma anasema:
"Utaratibu huo umesaidia wilaya, miji na tarafa mkoani Xinjiang kupata jukwaa la kuonesha ustadi wa usanii wa Aken Aites, kufanya mawasiliano, kufundishana, na kuinua kiwango cha usanii huo, serikali inawasaidia kukuza utamaduni wao, wakazi wanafurahia sana."
Mbali na kutilia mkazo kurithi na kuenzi utamaduni wa Aken Aites miongoni mwa wakazi, kazi hiyo pia imewekwa kwenye mfumo wa elimu wa sehemu hiyo. Mkurugenzi wa Taasisi ya uhifadhi na utafiti wa urithi wa utamaduni usioonekana katika Tarafa inayojiendesha ya kabila la wakhazak ya Ili mkoani Xinjiang Bw. Ohap Nurahmet anasema:
"ili kurithi usanii wa Aites, ni lazima kuwe na wa-aken, yaani waimbaji wa mashairi. Hivi sasa kuna darasa la kozi ya Aken Aites katika chuo kikuu cha ualimu cha Ili, kozi hiyo ina lengo la kusaidia kupata waimbaji mashairi wanaosaidia kurithi na kuenzi utamaduni wa Aken Aites."
Wasikilizaji wapendwa, mliyosikia ni sauti ya tamasha la tatu la Aken Aites lililofanyika katika mji wa Kuiton wa tarafa ya Ili. Wanafunzi 32 waliokuwa wamevaa mavazi ya sikukuu ya wakhazak, ambao wanachukua kozi ya utamaduni wa Aken Aites wa kabila la wakhazak katika Chuo kikuu cha ualimu cha Ili mkoani Xinjiang, wanaimba mashairi kwa sauti kubwa, kupiga vinanda vya Dongbula kwa ustadi murua, huku wakibijizana na kuonesha ujuzi mwingi waliopata, na kutimua vumbi kwenye jukwaa la maonesho.
Mkurugenzi wa Taasisi ya uhifadhi na utafiti wa urithi wa utamaduni usioonekana ya Xinjiang Bibi Li Xiolian anasema, kuwaandaa waaken katika chuo kikuu kutasukuma mbele kazi ya kurithi na kuenzi usanii wa Aites. Alisema:
"Wanafunzi wanaoandikishwa kwenye kozi ya Aken Aites katika chuo kikuu cha ualimu huwa wana sauti nyororo, pia wanajua kupiga vinanda, ambao elimu yao iko kwenye kiwango kinachotakiwa. Wakisoma katika chuo kikuu wanapata ujuzi mwingi zaidi, baada ya kuhitimu masomo watapata ajira, kwa upande mwingine wanafunzi hao watakuwa nguvu ya kurithi na kuenzi utamaduni wa Aken Aites ya kabila la wakhazak.|"
"Ukipenda mtu ni lazima umpende kwa moyo wote na katika maisha yako yote. Tunapenda Aken Aites kama tunavyothamini mapenzi ya watu."
"Baba yangu ni Aken maarufu wa sehemu tuliko, ninapaswa kujifunza vizuri usanii wa Aites, ili baba yangu ajivunie, muhimu zaidi ni kuenzi fahari tuliyonayo sisi wakhazak kuhusu utamaduni wetu wa Aken Aites."
"Mimi ni lazima nimfundishe mtoto wangu usanii wa Aken Aites, ili kurithi na kuenzi vizazi hadi vizazi utamaduni unaong'ara wa Aken Aites."
Kama walivyoimba kuwa, "sisi ni waaken, ni lazima wajitokeze waaken hodari wa vizazi vijavyo. Tunapenda maisha, tuna ari na hamasa katika uzalishaji, tunapenda taifa letu na familia zetu, hatuwezi kusahau kabila letu na mila na desturi zetu", wakhazak wameeleza nia yao imara ya kurithi na kuenzi utamaduni wao wa jadi, na pia wameonesha fahari na kujivunia kabila lao lenye uhodari na utamaduni wa jadi wenye mvuto.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |