Vijana 25 wa kabila la Wauighur wanajumuika, wakipiga vinanda vya Sataer, Eijieke, Kalun, Tanbuer, filimbi za mwanzi na ala nyingine nyingi za muziki na kuimba sehemu moja ya wimbo wa Muqam iitwayo "Airef na Synime" ambayo inawafurahisha sana watu. Wanaimba wimbo huo kwa sauti kubwa bila kusoma maandishi yoyote, na bila kuwa na mwongozo wowote. Vijana hao wenye umri wa miaka 20 hivi ni wanafunzi wa chuo cha usanii cha Xinjiang, ambao wanajifunza uchezaji wa ngoma ya Muqam. Wao wana nywele zenye mawimbi, nyusi nzito, pua inayochongoka na macho maangavu. Yote hayo yanayofanana na sura za wageni kutoka nchi za nje, ni sawa na usanii wa Muqam, yanavutia watu wengi.
Mkoa wa Xinjiang uko kaskazini magharibi mwa China, ni sehemu yenye mambo mbalimbali ya kuvutia. Watu wa kabila la Wauyghur wanaoishi katika mkoa huo wanathamini sana sehemu zao wanazoishi zenye miti na chemchemi katika jangwa. Sehemu hizo ni maskani yao ya kuzaliana na kukua kwa watu kizazi baada ya kizazi.
Katika miaka elfu 2 iliyopita, sehemu hizo zenye miti na chemchemi katika njia ya hariri, zilikuwa daraja la mawasiliano na maingiliano kati ya sehemu mbalimbali zenye tamaduni tofauti. Utamaduni wa Ugiriki, utamaduni wa China na utamaduni wa kiarabu unaungana katika sehemu hiyo, na kuunda sanaa ya Muqam ambayo inaunganisha nyimbo, ngoma na muziki.
"Muqam 12" ni sehemu muhimu ya sanaa ya Muqam, ambayo ina Muqam 12, kila Muqam inaundwa na sehemu 3, yaani Naghma, Dastan na Mashrap, na muda wa kuonesha mchezo wa sanaa hiyo ya Muqam zote 12 utakuwa zaidi ya saa 20 .
Uliyosikia ni sehemu moja ya Dastan wa mchezo wa sanaa ya Muqam 12, ambayo ni sehemu moja kwenye shairi moja refu la mapenzi liitwalo "Airef na Synime". Shairi hilo linasimulia hadithi kuhusu mvulana aitwaye Airef na msichana aitwaye Synime, waliokabiliana na changamoto nyingi na hatimaye kuishi pamoja kwa furaha. Hadithi hiyo inajulikana kwa watu wengi katika sehemu wanayoishi wauyghur kwa wingi, na kupokezana kizazi baada ya kizazi.
Mrithi wa usanii wa Muqam Bw. Osman alituambia kuwa shairi hilo refu la Airef na Synime lilitungwa na mshairi wa kabila la wauyghur Bw. Yusuf Aji katika karne 10 kwa mujibu wa utenzi ulioimbwa na wenyeji. Na Muqm 12 ilichukulia aya moja moja za shairi hiyo kuwa maneno ya wimbo. Aina hiyo ya kuongea na kuimba inapendwa na kukaribishwa sana na wauyghur.
Hadithi hiyo inaeleza kuwa, "Katika Karne ya Kati, mfalme Abbas na waziri mkuu wake walikwenda kuwinda. Walimkuta mbuzi mmoja mwenye mimba. Walimwonea huruma mbuzi huyo, hivyo hawakumwua, wakamwacha tu aende. Kutokana na jambo hilo, walianza kuwaoza watoto wao wakiwa matumboni mwa wake zao. Kwa bahati mbaya, waziri mkuu huyo alifariki dunia. Na mtoto wake Airef na mtoto wa kike wa mfalme Synime walikua kwa pamoja wakiwa wanapendana. Waziri mkuu mpya alitaka kuchukua madaraka, hivyo alimchochea mtoto wake ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa mfalme Abdulashat kumnyang'anya Airef mpenzi wake, na hata kumsengenya. Mfalme Abbas aliamini maneno yake, akawatuma watu wote wa familia ya Airef kwenda sehemu nyingine mbali. Synime aliona uchungu moyoni na kuumwa sana. Airef alikabiliana na taabu na matatizo magumu mbalimbali, lakini kutokana na msaada wa wanavijiji, Airef alirudi katika kasri la mfalme na kumuua Abdulashat. Alimwambia mfalme ujanja wa Abdulashat. Mfalme alijuta sana, na baadaye akakubali Airef na Synime wafunge ndoa.
Mzee Samsack Amat wa kabila la Wauighur ana umri wa miaka 85, anaishi katika kijiji cha Bostan wilaya ya Kalatale mjini Aksu. Mwaka 1940, alikuwa ni mtoto anayechunga mbuzi, alianza kujifunza usanii wa Muqam 12 wakati akichunga mbuzi mlimani ili kuondoa upweke. Hajui kusoma, hivyo alilazimika kukumbuka muziki na utenzi wa Muqam.
Ingawa zaidi ya miaka 70 imepita sasa, mzee huyo bado anaweza kueleza vilivyo hadithi hiyo ya mapenzi. Alisema kwenye Muqam 12, tunaweza kuhisi mapenzi kati ya Airef na Synime walipokuwa watoto, uchungu waliopata wakati walipotenganishwa katika sehemu tofauti, na vilevile kuhisi furaha waliyopata baada ya hali ngumu. Mzee Samsack alipokuwa akisema hayo, alianza kupiga ngoma ya mkono Dapu, na kuimba pamoja na wanafunzi wake.
Ili kuonesha mapenzi kati ya Airef na Synime, mrithi wa kitaifa wa usanii wa Muqam Bw. Osman Amat alituimbia sehemu moja ya Muqam, ambayo Airef alionyesha upendo wake kwa Synime:
Mwishowe, Airef na Synime walikutana tena na kuanza kuishi kwa furaha. Hadi hapo uchungu moyoni mwao ulikuwa umeondolewa, na muziki ukabadilika kuwa na midundo ya furaha ambayo inaonesha hisia za furaha miyoni mwao na matarajio yao kwa siku za mbele.
Mkurugenzi wa ofisi ya utafiti wa elimu ya Muqam katika chuo cha sanaa cha Xinjiang Bw. Mijisiyunus alituambia kuwa, muziki huo wenye midundo ya furaha unaonesha hadithi hiyo ya mapenzi imeeleza mpaka mwisho. Alisema,
"Sehemu hiyo ya Muqam inaonesha hali ya shamrashamra ya harusi ya Airef na Synime, mfalme amekubali ndoa yao, hivyo midundo ya muziki ni ya haraka ili kuonesha furaha za watu."
Hadithi hiyo inatukumbusha usemi mmoja wa kabila la wauyghur usemao, "ni baada ya kupita jangwa la Gobi, ndipo utafika sehemu yenye miti na chemchem". Vilevile, watu wanaopendana wakipitia taabu na mateso, ndipo watakapoweza kupata penzi la dhati.
Hadithi hiyo pia ilitungiwa filamu katika mwaka 1980, na kupata mafanikio makubwa nchini na nchi za nje. Mwimbaji maalum Daolang pia alitunga wimbo mmoja uitwao Airef na Synime:
Mwaka 2005, Usanii wa Muqam wa kabila la wauyghur wa Xinjiang uliorodheshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuwa "Urithi wa utamaduni usioonekana ambao unarithishwa kwa njia ya masimulizi". Mwaka 2010, mkoa wa Xinjiang ulitoa kanuni ya kuhifadhi usanii wa Muqam wa kabila la Wauyghur. Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa sanaa ya Xinjiang, ambaye pia ni mkurugenzi wa kituo cha uhifadhi na utafiti wa urithi wa utamaduni usioonekana cha Xinjiang Bibi Li Jilian anasema, usanii wa Muqam ni Ensaiklopidia iliyohifadhiwa kwa njia ya masimulizi, inayoonyesha mila na desturi za watu, na hivyo uhifadhi wa usanii wa Muqam kwa kiasi kikubwa unaonekana kuwa uungaji mkono kwa warithi wa usanii hiyo. Alisema,
"Kila mrithi wa kitaifa wa usanii wa Muqam anapata ruzuku ya kiserikali yuan elfu 10 kwa mwaka, yuan 3600 kutoka serikali ya mkoa, baadhi ya wasanii wa wilayani pia watapata ruzuku yuan 200 hadi 500 kila mwezi kutoka serikali ya wilaya. Ruzuku hizo ni kwa ajili ya kuwafanya warithi hao kuurithi usanii hiyo kizazi kwa kizazi."
Kuna usemi wa Xinjiang usemao, m-uyghur akijua kusema anaweza kuimba, na akijua kutembea anaweza kucheza ngoma. Hivi sasa, kila wilaya ina kundi la usanii wa Muqam lisilo la kiserikali, na kila m-uyghur anaweza kuimba, au kucheza sehemu moja ya Muqam. Muqam imeingia katika maisha yao, na pia ni furaha yao ya maisha.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |