7: Majengo

Majengo ya Kale ya China

Muhtasari

Majengo husifiwa kama ni "muziki uliotulia", ni aina moja ya utamaduni wa binadamu. Majengo ya kale nchini China mengi ni ya mbao ya kabila la Wahan na pia kuna majengo mengine mazuri ya makabila madogo madogo. Mtindo wa majengo ya Kichina ulipevuka nchini China kutoka karne ya pili mpaka karne ya 19, usanii wake umejaa utamaduni mkubwa. Sanaa za ujenzi wa Kichina ni moja ya sanaa zenye historia ndefu, ambayo ipo katika sehemu nyingi nchini China. Na sanaa hiyo iliathari ujenzi wa majengo hata nchini Japan, Korea na Viet-Nam, na baada ya karne ya 17 iliwahi kuathiri hata ujenzi wa majengo ya Ulaya.

China ni nchi kubwa yenye makabila mengi, wahenga wa China walijenga majengo yenye miundo na mitindo tofauti kutokana na mazingira na jiografia tofauti. Kwenye mabonde ya mto Huanghe, kaskaizni mwa China, wahenga walijenga nyumba kwa mbao na udongo ili kukinga upepo wa baridi na theluji; lakini katika sehemu ya kusini ya China, kutokana na joto wahenga walijenga nyumba kwa mianzi na matete, na ili kukwepa unyevunyevu, nyumba husimamishwa kwa nguzo na kuacha chini wazi; kwenye sehemu za milima, wahenga walikuwa wakijenga nyumba kwa mawe.

Ujenzi wa kale nchini China uliwahi kupamba moto katika vipindi vitatu, navyo ni enzi za Qin na Han, enzi za Sui na Tang na enzi za Ming na Qing. Katika vipindi hivi vitatu, majengo mengi mazuri yalitokea yakiwa ni pamoja na kumbi za kifalme, makaburi, majengo ya kukinga maadui na majengo ya uhandisi wa kuhifadhi maji. Kati ya majengo hayo ukuta mkuu uliojengwa na Qinshihuang (mfalme wa kwanza wa Enzi ya Qin), daraja la Zhaozhou lililojengwa katika Enzi ya Sui (581-618), na kasri la kifalme lililojengwa katika enzi za Ming na Qing mjini Beijing, mpaka sasa majengo hayo yanavutia sana kutokana na hekima za watu wa kale wa China.

Lakini kwa sababu ya miaka mingi, uharibifu wa mvua na upepo, vita, baadhi ya majengo ya kale yametoweka, na yaliyobaki sasa yaliyo mengi ni ya baada ya Enzi ya Tang (baada ya karne ya 7). Yafuatayo ni maelezo kuhusu majengo hayo.

Majengo katika Enzi ya Tang

Enzi ya Tang (618-907) ni kipindi ambacho uchumi na utamaduni katika jamii ya kimwinyi nchini China ulifikia kwenye kilele, ufundi na sanaa za ujenzi wa majengo pia zilikuwa zimeendelea sana. Majengo katika Enzi ya Tang yalikuwa makubwa na ya adhama.

Majengo katika Enzi ya Tang yalikuwa ni makubwa, na mpangilio wa fungu la majengo ni wa busara. Katika mji mkuu wa Enzi ya Tang, Chang An (mji wa Xi'an kwa leo), na mji wa Luoyang kuna makasri makubwa na majumba ya maofisa. Mji wa Chang An ulikuwa mji mkubwa duniani katika enzi hiyo, na mpangilio wa majengo yake ulikuwa wa busara kabisa katika miji yote ya China ya kale, ndani ya mji huo kasri la Daming lilikuwa na eneo zaidi ya mara tatu kuliko Kasri la Kifalme la Beijing.

Majengo katika Enzi ya Tang yanaonesha sayansi ya muundo wa mbao, mshikamano baina ya nguzo na maboriti umeonesha ushirikiano mzuri wa nguvu. Ukumbi wa Buddha katika Hekalu la Foguang mlimani Wutaishan umeonesha wazi mtindo wa majengo ya Enzi ya Tang.

Kadhalika, majengo ya matofali na mawe pia yalikuwa yameendelea sana katika Enzi ya Tang, mifano ya majango hayo ni pagoda ya Dayanta, pagoda ya Xiaoyanta na pagoda ya Qianxunta katika mji wa Xi'an.

Majengo katika Enzi ya Song

Enzi ya Song (960-1279) ilikuwa ni enzi iliyodidimia katika siasa na mambo ya kijeshi, lakini uchumi, viwanda vya kazi za mikono na biashara vilikuwa na maendeleo kwa kiasi fulani, na hasa katika sayansi na teknolojia, hali hiyo iliufanya ufundi wa majengo ufikie kiwango kipya. Majengo katika enzi hiyo yalibadilika kuwa madogo na yenye makini ya mapambo badala ya yale ya majengo makubwa na ya adhama ya Enzi ya Tang.

Katika miji ya Enzi ya Song yalitokea maduka kwenye barabara, na maduka yalipangwa kwa aina ya bidhaa, na majengo ya shughuli za zimamoto, mawasiliano, uchukuzi, maduka na madaraja, yote yaliendelea kwa hatua kubwa. Sura ya mji mkuu wa Enzi ya Song, Bianliang, (mji wa Kaifeng kwa leo) ilionesha wazi hali ya biashara katika miji ya Enzi ya Song. Katika enzi hiyo, nchini China majengo makubwa makubwa hayakujengwa sana, lakini mapambo na rangi za majengo yalizingatiwa zaidi. Ukumbi katika hekalu la Jinxi mkoani Shanxi ni mfano wa majengo hayo.

Majengo ya matofali yaliendelea zaidi katika Enzi ya Song, majengo hayo yalikuwa ni pagoda ya dini ya Buddha na madaraja. Pagoda katika hekalu la Huilingsi mkoani Zhejiang, pagoda la Fanta katika mji wa Kaifeng mkoani Henan na daraja la Yongtong wilayani Zhaoxian mkoani Hebei yote yanastahili kuwa kama ni mifano ya majengo ya matofali katika Enzi ya Song.

Uchumi wa Enzi ya Song uliendelea kwa kiasi fulani, katika enzi hiyo, ujenzi wa bustani ulianza kustawi. Ujenzi wa bustani ulitilia mkazo muunganisho wa uzuri wa bandia na wa kimaumbile, bustani katika enzi hiyo ilikuwa inapambwa kwa milima bandia, maji, maua na miti ili kuleta mazingira kama ya kimaumbile.

Katika Enzi ya Song kulikuwa na kitabu cha "Ufundi wa Ujenzi wa Nyumba". Kitabu hiki kinaeleza kanuni za usanifu na ufundi wa ujenzi wa nyumba, ambacho kinaonesha kuwa ujenzi wa nyumba katika Enzi ya Song ulikuwa umefikia kiwango kipya.

Majengo ya Enzi ya Yuan

Enzi ya Yuan (1206-1368) nchini China ilikuwa ni dola la kifalme lililoundwa na watawala wa kabila la Wamongolia, lakini katika enzi hiyo, majengo hayakuwa na maendeleo, na majengo mengi yalikuwa ya kawaida kutokana na kuzorota kwa uchumi na utamaduni.

Mji mkuu wa Enzi ya Yuan, Dadu (sehemu ya kaskazini ya Beijing kwa leo) ni mwanzo wa mji mkuu wa enzi mbili za Ming na Qing, Beijing. Shughuli za ujenzi katika mji mkuu huo zilikuwa hasa katika ujenzi wa majengo ya ukumbi na bustani, Bustani ya Beihai ya leo mjini Beijing ni kumbukumbu halisi ya enzi hiyo.

Katika Enzi ya Yuan dini ilikithiri sana, hasa dini ya Buddha ya madhehebu ya Kitibet, kwa hiyo mahekalu ya dini yalikuwa mengi.

Majengo ya mbao katika Enzi ya Yuan yaliurithi ufundi wa enzi iliyotangulia ya Song, lakini kutokana na uchumi uliokuwa mbaya na uhaba wa magogo, majengo katika enzi hiyo yalikuwa ya kawaida yakilinganishwa na majengo ya Enzi ya Song iwe kwa ukubwa au kwa umakini.

Majengo ya Enzi ya Ming

Kuanzia Enzi ya Ming (1368-1644) China iliingia katika kipindi cha mwisho cha jamii ya kimwinyi. Mitindo ya majengo katika enzi hiyo mingi zaidi ilirithi mitindo ya majengo ya enzi iliyotangulia ya Song bila kuwa na mabadiliko makubwa, lakini ukubwa wa majengo uliongezeka kwa ajili ya kuonesha adhama.

Katika enzi hiyo, mpangilio wa ujenzi wa mji na majengo ya makasri yote yalirithishwa na watu wa baadaye. Majengo yaliyobaki sasa katika mji wa Beijing na Nanjing yote yalianzia enzi hiyo ya Ming, na enzi iliyofuata ya Qing ilipanua na kuimarika tu katika msingi wa enzi ya Ming. Mji wa Beijing wa enzi ya Qing ulijengwa kwa msingi wa mji wa enzi ya Ming, mji huo unagawanyika mji wa ndani, wa nje na mji wa kifalme.

ukuta mkuu

Katika enzi ya Ming, jengo kabambe la kujikinga dhidi ya maaduni yaani Ukuta Mkuu liliendelea kujengwa, na ufundi wa jengo hilo ulikuwa ni wa hali ya juu kuliko zamani. Ukuta huo katika enzi ya Ming ulianzia ukingo wa Mto Yalujiang kutoka mashariki na kufikia Jiayuguan upande wa magharibi, jumla una urefu wa kilomita 5660, na kipande cha ukuta huo cha Badaling kiungani mwa Beijing kina thamani kubwa katika sanaa.

Majengo ya Enzi ya Qing

Enzi ya Qing (1616-1911) ni enzi ya mwisho ya kifalme nchini China. Majengo katika enzi hiyo mengi zaidi yalirithi mtindo wa enzi iliyotangulia ya Ming ingawa yalitokea mabadiliko kidogo ya kufanya majengo yawe ya kifahari zaidi.

Mji wa Beijing katika enzi hiyo ulikuwa sawa na enzi ya Ming. Kwenye kuta za mji kuna malango 20 na ndani ya mji kuna makasri makubwa. Katika enzi hiyo bustani nyingi za kifalme zilijengwa, kati ya bustani hizo zilizo kubwa na maarufu ni bustani ya Yuan Ming Yuan na kasri la majira ya joto (Summer Palace).


1 2 3 4 5 6