8: Elimu, Sayansi na Teknolojia

Mfumo wa Elimu

Elimu ya Chekechea

Elimu ya chekechea ya China ni elimu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 6. Elimu ya chekechea hutolewa katika shule za chekechea na madarasa ya watoto wasiotimiza umri wa kwenda shule. Wizara ya elimu ya China imetunga mwongozo wa elimu kwa watoto wadogo kutokana na uwezo na umaalum wao. Vyombo vinavyotoa elimu ya watoto wadogo vinawafundisha watoto jinsi ya kuhisi mambo, lugha na tabia ya maisha.

Nchini China, shule za chekechea za kawaida huwapokea watoto wenye umri kuanzia miaka 3 hadi 6, baadhi ya shule hizo pia zinawapokea watoto wadogo zaidi. Hivi sasa China kuna shule takriban laki 1 na elfu 50 za chekechea, ni asilimia 30 tu ya watoto wadogo wanapata elimu shuleni, wengine hutunzwa na walezi wao kutokana na umri na hali ya kiuchumi.

Shule za chekechea za China zinagawanyika shule za serikali na za watu binafsi. Zile zinazoendeshwa na serikali zina uzoefu zaidi wa kutoa elimu kwa watoto wadogo, tena zinatoza ada kidogo zaidi, na zile zinazoendeshwa na watu binafsi hutoza ada kubwa, lakini zina sifa zake, na zinaweza kufanya marekebisho kwa urahisi kutokana na mahitaji ya soko. Kutokana na maendeleo ya uchumi wa soko huria, shule za chekechea zinazoendeshwa na watu binafsi zinaongezeka kwa haraka, sasa zimechukua asilimia 30 ya shule zote za chekechea nchini China.

Elimu ya Msingi

Elimu ya msingi nchini China inaanza kutoka umri wa miaka 6. Kutokana na sheria ya elimu ya lazima ya China, serikali inawapatia watoto elimu ya lazima bila ada, wanatakiwa tu kulipa gharama za vitabu kiasi cha yuan mia kadhaa hivi kwa mwaka.

Elimu ya msingi ya China ni ya miaka 6, inafundisha masomo ya Kichina, hisabati, sayansi, lugha ya kigeni, maadili, muziki, mchezo wa riadha na kadhalika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, hivi sasa China ina shule zaidi ya laki nne za msingi zenye wanafunzi milioni 120, ambao wanachukua asilimia 98 ya idadi ya watoto wanaotimiza umri wa kwenda shule.

Kwa kuwa elimu ya msingi ni elimu ya lazima, hivyo shule nyingi za msingi nchini China zinaendeshwa na serikali, wanafunzi huwa wanasoma karibu na shule za nyumbani. Hivi sasa idara za elimu za China zinajitahidi kuboresha hali ya shule zenye vifaa duni ili kuwawezesha wanafunzi wote wapate elimu sawa. Katika sehemu Fulani za vijijini ambapo wakazi wanaishi huku na huko, serikali huwapeleka watoto kusoma katika shule za bweni zenye hali bora zaidi.

Elimu ya Sekondari ya Chini

Elimu ya sekondari ya chini nchini China pia ni elimu ya lazima, inatumia miaka mitatu. Masomo yanayofundishwa ni Kichina, hisabati, lugha za kigeni, fizikia, kemikali, maadili, upashanaji habari na kadhalika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, China ina shule zaidi ya elfu 60 za sekondari ya chini zenye wanafunzi milioni 60, ambao wanachukua asilimia 90 na zaidi ya idadi ya watoto wanaotimiza umri wa kwenda shule ya sekondari. Shule nyingi kabisa za sekondari ya chini zinaendeshwa na serikali.

Kwa kuwa elimu ya sekondari ya chini ni elimu ya lazima, hivyo wanafunzi hawana haja ya kufanya mtihani wa kujiunga na sekondari ya chini, wanaweza kuchagua shule kutokana na mahali wanakoishi na matakwa yao yenyewe. Katika sehemu za vijijini, wanafunzi wanapelekwa katika shule zenye hali nzuri zaidi, wanalala shuleni. Hivi sasa China inajitahidi kukuza elimu kwa kupitia mtandao wa kompyuta ili kutimiza lengo la kutumia pamoja vyanzo vya elimu vya sehemu mbalimbali.

Elimu ya Sekondari ya Juu

Elimu ya sekondari ya juu ya China ni elimu inayotolewa baada ya kumaliza elimu ya sekondari ya chini. Kuna sekondari ya kawaida, sekondari ya ufundi na shule ya kozi maalum. Elimu ya sekondari ya juu ya China si ya lazima, wanafunzi wanatakiwa kulipa ada. Ada hutofautiana kutokana na hali ya kiuchumi ya sehemu mbalimbali, lakini kwa wastani ni yuan elfu mbili hivi kwa mwaka.

Elimu ya sekondari ya juu nchini China huchukua miaka mitatu, ina masomo ya Kichina, hisabati, lugha za kigeni, fizikia, kemia, biolojia, upashanaji habari na kadhalika. Sekondari nyingi za juu huendeshwa na serikali, lakini katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na sekondari za watu binafsi.

Nchini China, wanafunzi wanatakiwa kufanya mtihani wa kujiunga na sekondari ya juu, na kwa mujibu wa matokeo ya mtihani na mapendekezo yao wanapokelewa na shule. Mtihani wa kujiunga na sekondari ya juu hutolewa na idara za elimu za sehemu mbalimbali. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, China ina sekondari za juu zaidi ya elfu 30 zenye wanafunzi milioni 30, ambao wanachukua asilimia 40 ya watoto wa rika moja. Katika miaka ya hivi karibuni, idara za elimu za China zinajitahidi kukuza elimu ya sekondari ya juu ili kutosheleza mahitaji ya wanafunzi kujipatia elimu zaidi.

Elimu ya Juu

Elimu ya juu ya China imegawanyika kuwa elimu ya vyuo vya diploma, elimu ya vyuo vikuu, na mafunzo ya shahada ya pili na ya udaktari. Kuna vyuo vikuu, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu vinavyotoa mafunzo kwa njia ya televisheni na radio, na vyuo vikuu vya watu wazima.

Elimu ya juu nchini China ina historia zaidi ya miaka mia moja. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, China ina vyuo vikuu 3000 vya aina mbalimbali, ambapo theluthi mbili vinaendeshwa na serikali, na theluthi moja vinaendeshwa na watu binafsi. Kuna wanafunzi milioni 20 wa vyuo vikuu, ambao wanachukua asilimia 17 ya idadi ya Wachina wa rika moja.

Nchini China wanafunzi wanatakiwa kufanya mtihani wa kujiunga na chuo kikuu, vyuo vikuu vinawaandikisha wanafunzi kutokana na matakwa yao na matokeo yao ya mtihani.

Katika miaka miwili iliyopita, idara za elimu za China zinafanya juhudi kukuza elimu ya juu, ambapo vyuo vikuu vya serikali vimeongeza kuwaandikisha wanafunzi, na elimu ya shahada ya pili na ya udaktari pia imepata maendeleo mazuri.

Elimu Nje ya Shule

Licha ya elimu ya shuleni, China pia ina vyombo vingi vinavyotoa elimu kwa njia mbalimbali, Wachina wengi wanajiandikisha katika vyombo hivyo ili kujitosheleza matakwa yao ya kupata elimu zaidi.

Vyombo muhimu vya utoaji elimu nje ya shule ni pamoja na vituo vya watoto, vituo vya shughuli za aina mbalimbali, madarasa ya kuwasaidia wanafunzi nje ya shule na mafunzo yanayotolewa kwa njia ya mtandao. Watoto wa China hujifunza muziki, dansi, uchoraji kutokana na ushabiki na mahitaji yao, kufanya mazoezi ya waliyojifunza shuleni, kushiriki katika shughuli za sayansi na teknolojia ili kuongeza uwezo wao na maisha yao.


1 2 3 4 5 6 7