14: Historia

Enzi za China

Enzi ya Xia

Enzi ya Xia ni enzi ya kwanza katika historia ya China, ambayo ilikuweko kwa miaka karibu 500 kati ya karne ya 21 kabla ya Kristu na karne ya 16 kabla ya Kristu.

Enzi ya Xia ilianzishwa na shujaa Da Yu ambaye alitengeneza miradi ya maji ya kunufaisha watu. Inasemekana kuwa alifungwa mkono na watu wa eneo lake kutokana na kufanikiwa kurekebisha mtu Manjano uliofurika na kuleta maafa mara kwa mara, na hatimaye alianzisha enzi ya Xia, tokea hapo China iliingia jamii yenye utaratibu wa kitumwa.

Mwishoni mwa enzi ya Xia, ufisadi wa kisiasa ulikithiri katika utawala wa mfalme, hususan mfalme wa mwisho Xia Jie alijua kuponda raha tu wala hakujali hali ya shida ya watu. Mwishoni jeshi lake lillishindwa na waasi, na enzi ya Xia ikaanguka.

Wataalamu wa historia wana maoni tofauti kuhusu kuweko enzi ya Xia kutokana na data kidogo zisizokamilika. Tokea mwaka 1959 wataalamu wa mabaki ya kale walianza kufanya uchunguzi kuhusu "magofu ya enzi ya Xia". Hivi sasa wataalamu wengi wanaona kuwa magofu ya Erlitou mkoani Henan ni vitu muhimu kwa utafiti kuhusu utamaduni wa enzi ya Xia.

Vyombo muhimu vya kazi za uzalishaji vilivyofukuliwa katika magofu ya Erlitou ni vyombo vya mawe ingawa vyombo vya aina nyingine vya pembe na mifupa ya mwanyama pamoja na kauri za baharini pia zilitumika. Ingawa watu hadi hivi leo bado hawajaona vyombo vikubwa vya shaba nyeusi vilivyofukuliwa kutoka kwenye magofu ya enzi ya Xia, lakini kulikuwa na vyombo na silaha za shaba nyeusi zikiwemo visu, patasi, tindo, vichwa vya mishale na vyombo vya kunywea pombe.

Katika kumbukumbu zilizoandikwa vitabuni, kitu muhimu ni matumizi ya kalenda katika enzi ya Xia. Hii inaonesha kuwa wakati ule watu waliweza kujua miezi kutokana na mahali zilipofika na kuzunguka nyota za Charles's Wain .

Enzi ya Shang

Wataalamu husika wanaona kuwa Xia ni enzi ya kifalme ya zamani zaidi nchini China, lakini takwimu husika za kihistoria kuhusu enzi ya Xia, lakini hadi hivi sasa bado hazijathibitishwa na mabaki ya kale isipokuwa kuelezwa na maandishi ya vizazi vilivyofuatia. Enzi ya kwanza katika zamani za kale nchini China, ambayo imethibitishwa na mabaki ya kale ni enzi ya kifalme ya Shang. Enzi ya Sahgn iliyodumu kwa kiasi cha miaka 600, iliasisiwa katika karne ya 16 kabla ya Kristu na iliangamia katika karne 11 kabla ya Kristu. Enzi ya Shang ilihamisha mji mkuu mara kadhaa, na mara ya mwisho mji mkuu ulihamishwa hadi mji wa Yin, ambao ni karibu na mji wa Anyang, mkoa wa Henan wa hivi sasa. Mabaki ya kale yaliyofukuliwa kutoka ardhini yamethibitisha kuwa katika kipindi cha mwanzo cha enzi ya Shang, ustaarabu wa China ulikuwa umeendelezwa kwenye kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na utamaduni wa maandishi yaliyochongwa kwenye magamba ya kobe na vyombo vya shaba nyeusi. Magofu ya mji wa Yin, ambayo yaligunduliwa mwaka 1928, ni ugunduzi mkubwa kuhusu mabaki ya kale nchini China katika karne 20. Baada ya hapo mabaki mengi yenye thamani yalifukuliwa kwa wingi.

Enzi ya Zhou ya Magharibi

Zhou ni enzi ya tatu baada ya enzi ya Xia na Shang nchini China katika zamani za kale. Enzi ya Zhou, ambayo ilidumu kwa miaka zaidi ya 770, ilianzishwa mwaka 1027 kabla ya Kristu na kuangushwa na nchi ya Qing mwaka 256 kabla ya Kristu. Kabla ya mji mkuu kuhamia kwa upande wa mashariki, nchi hiyo iliitwa kuwa Zhou ya magharibi, na kuitwa Zhou ya mashariki baada ya mji mkuu wa nchi kuhamia kwa upande wa mashariki. Enzi ya Zhou ya mashariki iligawanyika katika vipindi viwili vya Chunqiou na Zhanguo.

Baada ya mji mkuu kuhamia mji wa Gao ulioko sehemu ya mashariki, mfalme wa kwanza wa enzi ya Zhou aliyejulikana kwa Wu aliongoza majeshi kushambulia enzi ya Shang na kuasisi enzi ya kifalme ya Zhou.

Mwaka 770 wa kabla ya Kristu hadi mwaka 476 wa kabla ya Kristu ilikuwa enzi ya Chunqiu. Pamoja na ongezeko la idadi ya watu na maendeleo ya uchumi, yalizushwa mapigano makali ya kugombea umiliki kati ya nchi kubwa. Hali ya jamii ilitokewa na mabadiliko makubwa. Katika uzalishaji wa kilimo, wakulima walianza kutumia vyombo vya kilimo vilivyotengenezwa kwa chuma, kutumia ng'ombe kulima mashamba na kujenga miradi ya maji, hatua hiyo iliongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo. Chunqiu ni kipindi cha mpito ambapo utaratibu wa jadi wa kisiasa na kijamii wa Zhou ya magharibi ulisambaratika hatua kwa hatua.

Confucius, ambaye alikuwa mwana nadharia mkubwa na mwanaelimu mkubwa nchini China, alizaliwa katika kipindi cha mwisho cha Chunqiu. Kwenye msingi wa kujumlisha utamaduni na mawazo ya zamani, Confucius akifikiria hali halisi ya jamii yenye mgogoro, alitoa mfumo wa maoni ya nadharia kuhusu utu, uadilifu na masuala ya kijamii na kisiasa, na kuanzisha kundi la wasomi wenye mawazo ya confucius katika zamani za kale.

Kipindi cha Zhanguo (toka mwaka 403 kabla ya Kristu hadi mwaka 221 kabla ya Kristu) ni kipindi ambacho watawala wa sehemu mbalimbali nchini waligombea madaraka baada ya Zhou ya mashariki. Katika kipindi hiki, mabadiliko makubwa yalitokea nchini China: nchi nyingi ndogo ndogo zilimezwa na nchi kubwa na hatimaye zikabaki nchi 7 kubwa. Katika kipindi hicho, nchi mbalimbali zilifanya mageuzi, hususan nchi ya Qin.

Ingawa katika kipindi cha Zhanguo zilitokea vita mwaka hadi mwaka, lakini hali hiyo haikuathiri maendeleo ya utamaduni wa kale nchini China, shughuli za kundi la watu wenye elimu kubwa walistawisha utamaduni wa fani maalumu. Katika kipindi hicho utamaduni wa mawazo ulifikia kileleni katika historia ya kale ya China yakiwemo makundi ya Confucius na Menfucius; kundi la kidao lililowakilishwa na Laozi, Zhuangzi na Liezi; kundi la wanasheria lililowakilishwa na Hanfei; na kundi la Mozi, makundi hayo yaliungwa mkono na kuheshimiwa na vizazi vya baadaye. Hali ya kuweko kwa makundi yenye mawazo tofauti yalihimiza maendeleo ya siasa na uchumi kwa wakati ule, tena inaendelea hadi hivi sasa.

Mwaka 230, mfalme Yingzheng wa enzi ya Qin akitumia muda wa miaka 9 aliangusha nchi nyingine 6 na kuunganisha sehemu zote za China katika mwaka 230 kabla ya Kristu. Hadi hapo hali ya mfarakano uliodumu kwa karibu miaka 600 ilimalizika.

Qin-Enzi ya Kwanza ya Kimwinyi

Baada ya kupita miaka zaidi ya 2,000 ya jamii yenye utaratibu wa umilikaji wa watumwa, enzi ya kwanza ya kimwinyi nchini China iliasisiwa mwaka 221 kabla ya Kristu. Kuasisiwa enzi ya Qin kuna maana muhimu katika historia ya China. Mwaka 255 hadi mwaka 222 kabla ya Kristu China iliingia katika kipindi cha mwisho cha jamii yenye utaratibu wa umilikaji wa watumwa. Wakati ule kulikuwa na nchi nyingi ndogo ndogo, ambazo zilipigana vita, hatimaye zikabaki nchi 7 kubwa. Enzi ya Qin kati ya nchi hizo 7, iko katika sehemu ya kaskazini magharibi, ilifanya mapema mageuzi ya kijeshi na kilimo, ambapo nguvu ya Qin iliimarika. Mwaka 247 kabla ya Kristu, Ying Zheng mwenye umri wa miaka 13 alirithi ufalme, alipoanza kutawala alipotimiza umri wa miaka 22, alianza kutekeleza mpango wake wa kuteka nchi nyingine 6. katika muda wa miaka 10 kutoka mwaka 230 kabla ya Kristu hadi mwaka 221 kabla ya kristu mfalme Yingzheng aliangusha nchi nyingine 6 na kuunganisha sehemu zote za China. Kuunganishwa kwa sehemu zote nchini na kuimarisha umoja wa China kulikuwa na maana muhimu katika historia ya China. Kwanza mfalme Yingzheng alianzisha serikali za mitaa ambazo ni pamoja na mikoa 36 na wilaya zake ambazo baadhi ya majina yake yanatumika hadi hivi sasa. Pili, mchango mkubwa uliotolewa na enzi ya Qin ni kutumia maneno ya aina moja, hatua ambayo ilichangia urithi wa utamaduni wa China. Tatu, ulianzishwa utaratibu wa upimaji wa namna moja kote nchini ikiwa ni pamoja na upimaji wa urefu, ujazo, ukubwa na uzito, hatua hiyo ilianzisha mazingira bora kwa maendeleo ya uchumi wa nchi, hali kadhalika kwa uimarishaji wa hadhi ya utawala wa serikali kuu. Mfalme Yingzheng aliunganisha sehemu zote za China na kumaliza hali ya mfarakano na kujenga nchi kubwa ya kimwinyi yenye makabila mengi, ambayo kabila la wahan ni uti wa mgongo na kufungua ukurasa mpya wa historia.

Kabila la Wahan

Mwaka 206 kabla ya Kristu hadi mwaka wa 8 ni kipindi cha enzi ya Han ya magharibi katika historia ya China. Liu Bang ambaye aliyekuwa mfalme Gao aliasisi enzi ya Han na kuchagua Changan kuwa mji mkuu.

Katika miaka ambayo mfalme Hangaozu alikuwa madarakani, aliimarisha utawala wa serikali kuu na kubuni sera za kuboresha maisha ya wananchi. Mwaka 159 kabla ya Kristu, mfalme Hangaozu alifariki, Hui alirithi ufalme wake, lakini wakati ule madaraka ya serikali, yalikuwa mkononi mwa malkia Lu, ambaye ni mke wa mfalme Hangao. Malkia Lu alitawala kwa miaka 16, na ni mmoja wa watawala wachache wa wanawake katika historia ya China. Mwaka 183 kabla ya Kristu, Wen alirithi ufalme, yeye na mtoto wake ambaye alirithi ufalme (toka mwaka 156 kabla ya Kristu hadi mwaka 159 kabla ya Kristu) waliendelea kutekeleza sera za kuboresha maisha ya wananchi, kupunguza kodi na kukuza uchumi wa nchi.

Kutokana na sera bora za wafalme wa hao, nguvu ya enzi ya Han iliimarika. Mwaka 141 kabla ya Kristu Wu alirithi ufalme na kutuma Wei Qing na Huo Qubing kwenda kupigana vita na kabila la waxiongnu, hatimaye walishinda vita na kupanua ardhi ya enzi ya Han ya magharibi, na kufanya uchumi na utamaduni kupata maendeleo katika sehemu ya kaskazini.

Kutokana na kutekelezwa kwa sera za kukuza uzalishaji mali na kuboresha maisha ya wananchi, nguvu ya enzi ya Han iliimarika, lakini katika wakati huo huo, nguvu ya mikoa pia iliimarika ha kuhatarisha utawala wa kifalme. Mwaka wa 8 baada ya Kristu, Wang Mang alijinyakulia ufalme na kuasisi enzi ya Xin.

Enzi ya Han ya magharibi ni moja ya enzi yenye nguvu kubwa katika historia ya China, hivyo enzi ya Han ilikuwa katika hali ya utulivu kwa miaka yote ya utawala wake. Mfalme Wu alisikiliza pendekezo la waziri Dong Zhognshu la "kuacha nadharia nyingine na kuheshimu nadharia ya Confucius peke yake." Tokea hapo, nadharia na elimu ya Confucius vikawa sera za kutawala kwa enzi zote zilizofuata.

Tokea mwaka 25 hadi mwaka 220 ni kipindi cha enzi ya Han ya mashariki, ambayo iliasisiwa na Liu Xiu ambaye alijiita mfalme Guangwu.

Katika miaka ya mwanzo ya enzi ya Han ya mashariki, utawala wa serikali kuu uliimarisha maelewano na utawala wa kikanda, utawala wa nchi ulielekea hali ya utulivi, kiwango cha uchumi, utamaduni, sayansi na teknolojia kilizidi kile cha enzi ya Han ya magharibi. Mwaka 105 Cai Lun alivumbua teknolojia ya utengenezaji wa karatasi. Katika upande wa sayansi ya kimaumbile, Zhang Heng alivumbua zana za kuchunguza hali ya sayari na tetemeko la ardhi. Katika kipindi cha mwisho cha enzi ya Han ya mashariki, dakatari Hua Tuo alifanya upasuaji kwa wagonjwa kwa kutumia dawa ya nusukaputi.

Nchi za Wei, Jin na Enzi za Kusini na Kaskazini

Kipindi cha Wei na Jin (mwaka 220 hadi mwaka 589) mwishoni mwa karne ya 2, utawala wa Han ya mashariki ulizorota, historia ya China iliingia kipindi cha muda mrefu cha mfarakano. Mwanzoni ni nchi tatu zilizokabiliana za Wei, Shu na Wu (mwaka 189 hadi mwaka 265), hali hiyo ya kukabiliana ilimalizwa na Jin ya magharibi, lakini umoja wa Jin ya magharibi ulidumu kwa muda mfupi (mwaka 265 hadi mwaka 316), hali ya mfarakano ikatokea tena. Jamaa za mfalme wa Jin ya magharibi walianzisha nchi ya Jin ya mashariki (mwaka 317 hadi mwaka 420), mgogoro wa mapigano ulitokea katika sehemu ya kaskazini, ambapo zilianzishwa nchi 16.

Katika kipindi hicho, uchumi wa sehemu ya kusini ulikuwa na maendeleo makubwa. Makabila yaliyokuwa katika sehemu za magharibi na kaskazini yalihamia sehemu ya kati kwa mfululizo, ambapo uhamiaji na kuishi kwa kuchanganyika pamoja vilihimiza kuungana na kuingiliana. Katika upande wa utamaduni, elimu kuhusu uhai ilienea kwa haraka, ambapo dini za kibudha na kidao zilikuzwa katika mgongano, lakini kwa kawaida watawala walilinda dini ya kibudha. Katika upande wa fasihi na sanaa kulikuwa na maandishi na mashairi mengi, michoro ya sanaa iliyoko katika mapango ya mawe ya Denghuang ni sanaa murua ya kudumu.

Katika upande wa sayansi na teknolojia, Zu Chongzhi alikuwa mtu wa kwanza aliyefanya hesabu kuhusu ulinganifu kati ya mzingo wa duara na urefu wa kipenyo hadi tarakimu 7 nyuma ya nukta (3.1415926).

Katika kipindi cha enzi za kusini na kaskazini, uchumi ulikuzwa zaidi katika sehemu ya kusini, kwa kuwa watu walioishi sehemu ya kati walihamia sehemu ya kusini kwa kujiepusha na vita, hali ambayo si kama tu iliongeza nguvukazi ya sehemu ya kusini, bali pia ilihimiza sana maendeleo ya uchumi ya sehemu ya kusini kutokana na kuingia huko kwa teknolojia ya kisasa.

Katika kipindi hicho, maingiliano na nchi za nje yaliendelezwa kwa nguvu na kufikia hadi Japan, Korea kwa upande wa mashariki, Asia ya kati na Rome kwa upange wa magharibi na kufikia sehemu ya Asia ya kusini mashariki.

Ingawa maendeleo ya uchumi yalikwama katika enzi za sehemu ya kusini na enzi za sehemu ya kaskazini, lakini kutokana na utawala wa makabila yaliyotoka nje, makabila yaliyoko katika sehemu ya kati yaliungana pamoja,. Katika hali ya namna hiyo, makabila mengine yaliyotoka sehemu ya kaskazini yaliunganishwa na kabila la wahan na kuwa kabila moja. Hivyo, mfarakano wa enza za kusini na kaskazini ulifanya kazi muhimu ya kuunganisha makabila ya China, na ni moja ya sehemu muhimu ya maendeleo ya China.

Enzi za Sui na Tang

Tangu Yang Jian ambaye alikuwa ni mfalme kuasisi enzi ya Sui mwaka 581, hadi Yang Guang ambaye alikuwa mfalme Yang aliponyongwa mwaka 618, enzi ya Sui ilidumu kwa miaka 37 tu. Mchango aliotoa mfalme Wen ulikuwa mkubwa zaidi ambao ni pamoja na kubatilisha utaratibu wa zamani wa enzi ya Zhou ya kaskazini, kubuni sheria mpya ambayo siyo yenye adhabu kali kama ya enzi ya Nanbei.

Tangu kuanzishwa enzi ya Tang mwaka 618 hadi enzi hiyo kuangushwa na Zhu Wen mwaka 907, enzi ya Tang ilidumu kwa miaka 289. Enzi ya Tang inagawanyika katika vipindi viwili kutokana na uasi wa Anshi. Katika kipindi cha kwanza enzi ya Tang ilistawi, na katika kipindi cha pili Tang ilizorota. Tanggaozu aliasisi enzi ya Tang, lakini Li Shimin ambaye alikuwa mfalme Tangtaizong aliongoza jeshi kuunganisha nchi nzima kwa kutumia miaka kumi. Baada ya kutokea uasi wa Xuanwumen, Li Shimin alikuwa mfalme, baada ya juhudi kubwa, enzi ya Tang ilistawi kuliko enzi zote za China, na iliongoza duniani katika siasa, uchumi na utamaduni. Lakini ilipofika kipindi cha mfalme Tangxuanzong licha ya kutokea hali ya ustawi vilevile ilianza kuzorota baada ya kutokea uasi wa Anshi.

Katika kipindi cha mwisho, siasa ya enzi ya Tang ilijaa ufisadi, uasi ulitokea huku na huku, hatimaye ulitokea uasi mkubwa wa Huang Chao, mmoja wa kiongozi aliyeongoza uasi huo Zhu Wen alijisalimisha kwa enzi ya Tang, na hapo baadaye alinyakua madaraka ya utawala wa enzi ya Tang na kuwa mfalme, aliasisi enzi ya Liang ya kipindi cha pili.

Enzi ya Song

Mwaka 960, Zhao Kuangyin aliongoza uasi wa kijeshi na kuasisi utawala wa Song, ambao uliodumu kwa miaka 319 na uliangushwa na enzi ya Yuan mwaka 1279. Enzi ya Song ilipitia vipindi viwili vya Song ya kaskazini na Song ya kusini. Katika wakati huo huo, watu wa kabila la Qidan waliasisi nchi ya Liao ambayo ilidumu kuanzia mwaka 947 hadi mwaka 1125; Watu wa kabila la Dangxiang waliasisi nchi ya Xia ya magharibi (1038-1227) kwenye sehemu ya kaskazini magharibi ya enzi ya Song; Mwaka 1115 watu wa kabila la Nuzhen walianzisha nchi ya Jin (1115-1234) katika sehemu ya kaskazini. Mwaka 1125 nchi ya Jin ilimeza nchi ya Liao, na katika mwaka 1127 iliteka Kaifeng, mji mkuu wa enzi ya Song na kuwateka nyara wafalme wa Hui na Qin. Zhaogou wa enzi ya Song alichukua wadhifa wa ufalme katika Henan, hapo baada ye alitorokea Linan, ambayo hivi sasa inajulikana kwa Hangzhou iliyoko sehemu ya kusini, na kuasisi enzi ya Song ya kusini.

Enzi ya Song ya kaskazini baada ya kuunganisha sehemu za kaskazini, yalikuwa na maendeleo makubwa katika jamii, uchumi, utamaduni pamoja na biashara na nje baada ya nchi ya Jin kuangusha utawala wa Song ya kaskazini, Song ya kusini ilikalia sehemu ya kusini ambayo haikuwa na wazo la kushambulia sehemu ya kaskazini na kuunganisha upya sehemu ya kaskazini.

Katika kipindi hiki yalipatikana maendeleo makubwa katika sayansi na teknolojia hususan kuvumbua dira, teknolojia ya uchapishaji na baruti. Teknolojia iliyovumbuliwa na Bishen ya uchapishaji kwa kutumia chapa za neno moja moja ilitangulia kwa miaka 400 kuliko ile teknolojia ya Ulaya. Mbali na hayo, katika upande wa utamaduni walijitokeza wananadharia pamoja na kuenezwa kwa dini za kidao, kibudhaa pamoja na dini zilizotoka nchi za nje. Katika fasihi, walijitokeza waandishi wakubwa wa vitabu pamoja na maandishi na michoro mashuhuri.

Enzi ya Yuan

Tiemuzhen wa Mongolia aliasisi nchi yake mwaka 1206, ambayo ilipewa jina la Yuan na mfalme Hubilie mwaka 1271. Enzi ya Yuan iliiangusha enzi ya Song mwaka 1279 na kuuchagua mji wa Daou, ambao ni Beijing kwa hivi sasa, kuwa mji mkuu wake.

Mwanzoni kabisa kabila la wamongolia lilikuwa katika sehemu ya kaskazini ya jangwa kubwa, Tiemuzhen alishinda makabila yote madogo madogo ya huko na kuazisha nchi ya Mongolia, naye akajiita kuwa mfalme Chengjisihan. Kabla ya hapo jeshi la Mongolia liliishambulia sehemu ya magharibi hadi Asia ya kati, Ulaya ya mashariki na Uajemi. Nchi hiyo kubwa, ambayo kitovu chake ni Jamhuri ya Watu wa Mongolia ya hivi sasa ilifarakana na kugawanyika kuwa nchi kadhaa za kifalme, ambazo kwa jina zilikuwa chini ya mfalme wa Chengjisihan.

Katika enzi ya Yuan, nchi zilizokuwa sehemu ya kaskazini zilipigana vita kwa miaka mingi na kuleta uharibifu mkubwa. Mfalme wa kwanza wa enzi ya Yuan aliweka kipaumbele katika kilimo na kurekebisha mto Manjano.

Katika enzi za Tang, Song na Yuan China ilikuwa nchi iliyoendelea kabisa duniani, ambayo uchumi na utamaduni vilivutia sana nchi jirani. Katika kipindi kile mabalozi, wafanyabiashara na wasomi wengi wa nchi za mashariki na magharibi walitembeleana, na uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na nchi za nje ulikuzwa kwa haraka. Nchi ya Yuan ilikuwa na uhusiano mkubwa na Japan pamoja na nchi za Asia ya kusini mashariki, na kwenye bahari merikebu (mashua kubwa) nyingi za China zilikuwa zikisafiri kati ya China na India. Uvumbuzi mkubwa tatu za uchapaji, baruti na dira zilienezwa hadi Ulaya kwa kupitia Uarabu katika enzi ya Yuan. Elimu ya sayari, tiba na hisabati ziliingia China na dini ya kiislamu ilienezwa katika China. Mawasiliano kati ya China na peninsula ya uarabuni licha ya kupitia baharini kulikuwa na njia ya kupitia mkoa wa Yunan kwenye nchi kavu, ambapo vyombo vya kauri vya China vilisafirishwa hadi Afrika ya mashariki hata nchini Morocco. Mwaka 1275, mtoto wa mfanyabiashara mashuhuri wa Venice alifuatana na babake walifika China na kuishi kwa miaka 17, kitabu walichoandika kijulikanacho kwa "kumbukumbu ya matembezi" kilikuwa kitabu muhimu kuhusu kuifahamu China na Asia kwa watu wa nchi za magharibi katika karne kadhaa.

Katika upande wa utamaduni, walijitokeza watungaji wa michezo ya opera wakiwa ni pamoja na Guan Hanqing, Wang Shipu, Bai Pu na Ma Zhiyuan.

Utawala wa Mongolia uliwakandamiza sana watu wa kabila la wahan, ambao ulisababisha upinzani mkubwa. Mwaka 1333, wakulima waliounganishwa kwa shughuli za kidini na jumuiya mbalimbali walifanya uasi sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 1351 wakulima waliopelekwa kurekebisha mto Manjano walifanya uasi mkubwa wakijitambulisha kwa kufunga skafu nyekundu vichwani. Mwaka 1341 jeshi la "skafu nyekundu" liliangusha utawala wa Yuan na kuanzisha enzi ya Ming.

Enzi ya Ming

Mwaka 1368 Zhu Yuanzhang alikuwa mfalme katika mji wa Nanjing na kuanzisha enzi ya Ming. Kwa muda wa miaka 31 tangu awe mfalme, mfalme Ming Taizu aliimarisha madaraka ya udikteta wa kimwinyi, kuua mawaziri wenye mafanikio na wapinzani ili kuimarisha utawala wake. Baada ya mfalme Ming Taizu kufariki, mjukuu wake Jianwen alirithi ufalme, lakini alishindwa kwa jeshi la baba yake mdogo. Tokea hapo Zhuli akawa mfalme na kujiita kuwa Ming Chengzu. Mwaka 1421 alihamishia mji mkuu mjini Beijing.

Ingawa enzi ya Ming iliimarisha madaraka ya kifalme, lakini wafalme wengi ama walikuwa mbumbumbu au walikuwa bado watoto na kutoshughulikia mambo ya nchi, hivyo madaraka yalitwaliwa na watumishi wa jumba la mfalme, ambao walitamani mali, kuwaua mawaziri adilifu na kusababisha mgongano wa kijamii. Ingawa wakulima walifanya uasi mara kadhaa katikati ya kipindi cha enzi ya Ming, lakini wote walikandamizwa.

Katika enzi ya Ming alikuwepo mwanasiasa mashuhuri Zhang Juzheng, aliyefanya mageuzi ili kupunguza mgongano wa kijamii na kuimarisha nguvu ya utawala wa enzi ya Ming.

Kilimo kilikuwa na maendeleo makubwa zaidi katika enzi ya Ming kuliko enzi za zamani, ambapo sekta nyingine za nguo, vyombo vya kauri, uchimbaji wa madini ya chuma, utengenezaji wa vyombo vya shaba, karatasi na uundaji wa marikebu pia vilipata maendeleo. Katika enzi ya Ming uhusiano wa kiuchumi na kiutamaduni ulikuzwa. Msafiri mkubwa Zheng He alisafiri mara 7 baharini hadi nchi na sehemu zaidi ya 30 za Asia na Afrika. Lakini baada ya hapo, Enzi ya Ming ilivamiwa na Japan, Hispania, Ureno na Uholanzi.

Katika kipindi cha mwisho cha enzi ya Ming, jamaa za wafalme na majemedari walikuwa na mashamba mengi, kodi za serikali pia zilikuwa nyingi, hali hiyo ilisababisha mgongano mkubwa wa kijamii. Baadhi ya maofisa walitarajia kupunguza mgongano wa kijamii, wakidai kudhibiti haki maalumu za watumishi wa jumba la mfalme na mabwenyenye, lakini walikandamizwa na wenye madaraka, hali ambayo ilizidisha hali ya wasiwasi.

Mwaka 1627 yalitokea maafa ya makubwa ya kimaumbile, lakini maofisa waliwalazimisha wakulima kulipa kodi, jambo ambalo lilisababisha wakulima kufanya uasi. Mwaka 1644 jeshi la wakulima liliuteka mji wa Beijing, na mfalme Chongzhen alijiua.

Enzi ya Qing

Enzi ya Qing ilikuwepo kuanzia mwaka 1644 hadi mwaka 1911, muda ambao kulikuwa na wafalme 12 na kutawala China kwa miaka 268.

Enzi ya Qing ilipokuwa na nguvu kubwa kabisa ilikuwa na ardhi yenye eneo la kilomita za mraba milioni zaidi ya 12. Mwaka 1616 Nuerhachi alianzisha enzi ya Jin ya pili, mwaka 1636 mfalme Huangtaiji alibadilisha jina la nchi kuwa Qing. Mwaka 1644 jeshi la wakulima lililoongozwa na Li Zicheng liliangusha enzi ya Ming, mfalme Chongzhen wa enzi ya Ming alijiua. Jeshi la Qing liliingia sehemu ya kati ya China na kutumia nafasi hiyo kulishinda jeshi la wakulima na kuuchukua Beijing kuwa mji mkuu wa Qing. Enzi ya Qing ilivunjilia mbali majeshi ya wakulima yaliyokuwa kwenye sehemu mbalimbali za China na kuunganisha sehemu zote za China hatua kwa hatua.

Ili kupunguza mgongano wa kijamii, mwanzoni enzi ya Qing ilihamasisha wakulima kufyeka mashamba na kutekeleza sera za kupunguza kodi, hatua hiyo iliyochukuliwa ilileta maendeleo ya jamii na uchumi kwenye sehemu za ndani na mipakani. Ilipofika katikati ya karne ya 18, uchumi wa enzi ya Qing ulikuzwa zaidi na kufika kileleni, nguvu ya nchi ilikuwa kubwa, utaratibu wa jamii ulikuwa shwari, na idadi ya watu ilifikia kiasi cha milioni 300.

Mwaka 1661 Zheng Chenggong aliongoza kundi la manowari kuvuka mlango bahari wa Taiwan na kuwashambulia wakoloni wa uholanzi waliokalia Taiwan kwa miaka 38. Mwanzoni mwa mwaka uliofuata, wakoloni wa Uholanzi walisalimu amri, na Taiwan ilirejea China.

Katika miaka ya mwisho ya karne ya 16 Urusi ya Tsar ilijipanua kwa sehemu ya mashariki. Wakati jeshi la Qing lilipoingia sehemu ya kati ya China, mfalme Tsar wa Urusi alitumia nafasi hiyo kukalia sehemu kadhaa zikiwemo Yaksa na Nibuchu. Serikali ya Qing ilitaka wavamizi wa Urusi waondoke kutoka ardhi ya China. Mwaka 1685 na mwaka 1686 mfalme Kangxi aliamuru jeshi la Qing kushambulia jeshi la mfalme Tsar wa Urusi lililoko Yaksa, ambapo lililazimika kukubali kutatua suala la mpaka wa sehemu ya mashariki kati ya China na Urusi kwa njia ya mazungumzo. Mwaka 1689, wawakilishi wa China na Urusi walikuwa na mazungumzo huko Nibuchu na kusaini rasmi "mkataba wa mpaka wa Nibuchu".

Katika kipindi cha kati cha enzi ya mfalme Qianlong, serikali ilituliza kundi la wafarakanishaji la Geerdan wa sehemu ya Zhungeer na uasi uliofanywa na kabila la wahui, kuunganisha sehemu zote za Xinjiang na kutekeleza sera kadhaa za kuhimiza uchumi, utamaduni na mawasiliano ya sehemu ya mpakani.

Kabla ya kipindi cha mfalme Daoguang, enzi ya Qing ilipata maendeleo makubwa katika mambo ya utamaduni, ambapo walijitokeza waandishi wakubwa wa vitabu na vitabu vikubwa mashuhuri. Vilevile maendeleo mengi katika eneo la sayansi na teknolojia hususan katika sekta ya ujenzi wa majengo.

Mwaka 1840 vilizuka vita vya kasumba, baada ya hapo nchi za kibeberu ziliishambulia China, ambapo utawala wa enzi ya Qing ulisaini mikataba mingi isiyo ya haki, kuzipa ardhi, kutoa fidia na kufungua milango ya miji ya pwani kwa shughuli za biashara, Jamii ya China ilibadilika hatua kwa hatua kuwa nchi ya nusu kimwinyi na nusu ya kikoloni. Katika kipindi cha miaka ya mwisho siasa ya enzi ya Qing ilijaa ufisadi, kushikilia wazo lile la kizamani, kuwa waoga na unyonge na kuzorota mwaka hadi mwaka. Watu wa China waliishi kwa taabu kubwa walianzisha harakati za kupinga ubeberu na umwinyi. Ili kujiokoa watawala walifanya baadhi ya mageuzi wakijaribu kufanya China kushika njia ya ustawi, lakini hatimaye walishindwa kabisa. Mashujaa wengi walipigana vita kufa na kupona wakijitahidi kuiokoa China. Mwaka 1911 yalitokea mapinduzi ya Xinhai ambayo yaliuangusha utawala wa enzi ya Qing na kumaliza utaratibu wa kimwinyi uliodumu kwa miaka zaidi ya 2,000, tokea hapo China iliingia katika kipindi kipya.


1 2 3 4 5 6