15: Fasihi ya Kale

Riwaya za Kale za China

Pu Songling na Riwaya Yake "Hadithi za Mashetani"

Mwanzoni mwa karne ya 18, kitabu maarufu cha hadithi fupi fupi yaani "Hadithi za Mashetani" kiliibuka nchini China, Pu Songling kwa ustadi wake aliandika hadithi nyingi za mashetani na bweha.

Pu Songling alizaliwa mwaka 1640 na kufa mwaka 1715, alikuwa mwanafasihi katika Enzi ya kifalme ya Qing. Alizaliwa katika ukoo wa wafanyabiashara, lakini alifanya kazi ya ualimu. Katika maisha yake aliandika makala mengi na kitabu chake cha mkusanyiko wa hadithi fupi yaani "Hadithi za Mashetani" ndicho kilichompatia umaarufu.

Kitabu cha "Hadithi za Mashetani" kimekuksanya hadithi 430, ambapo miongoni mwa hadithi hizo iliyo fupi kabisa ina maneno mia mbili au tatu hivi, na ile ndefu sana ina maelfu kadhaa ya maneno. Kitabu kizima kinaeleza hadithi za mashetani na bweha kikilaani pingu za maadili ya kimwinyi, ubovu wa mitihani ya kifalme ya kuchagua maofisa na kudai uhuru wa maisha ya binadamu. Katika kitabu hiki hadithi za kupendeza sana ni zile za mapenzi kati ya mashetani na bweha ambazo zilionesha matumaini ya binadamu kuvunja pingu za maadili ya kimwinyi kati ya wanaume na wanawake.

Katika kitabu cha "Hadithi za Mashetani" bweha hujitokeza kama kisura. Miongoni mwa hadithi hizo, maarufu zaidi ni "Hadithi ya Xiao Cui". Hadithi hiyo iliandikwa kwa vituko vingi vya kuwavutia wasomaji, ambapo mwandishi alimsawiri kwa ustadi msichana mmoja mwenye akili, roho nzuri na wa kupendeza. Mwishoni mwa hadithi hiyo mwandishi alibainisha kwamba Xiao Cui alikuwa bweha mdogo, kwa sababu mama yake aliwahi kukimbia janga nyumbani kwa wale wazee, akajigeuza kuwa binadamu ili kuwalipa wema wao.

Katika kitabu cha "Hadithi za Mashetani", pia wako bweha wenye sura mbaya lakini roho nzuri. Hadithi ya "Bweha Mwenye Sura Mbaya" ilieleza jinsi bweha mmoja mwenye sura ya kuchukiza alivyomkuta msomi mmoja, ambaye alikuwa maskini hahehohe hata chakula kilikuwa ni shida kwake achilia mbali nguo. Bweha huyo alimsaidia maisha yake. Lakini baada ya msomi huyo kupata nguo safi, nyumba za fahari na kila kitu kwa maisha ya starehe alimwomba mchawi amfukuze bweha. Bweha alihamaki sana kutokana na msomi huyo kukosa shukrani, ndipo licha ya kurudisha yote aliyompa msomi, alimtuma shetani kumwadhibu vibaya. Kwa masimulizi ya hadithi hii mwandishi anawaonya watu wenye roho mbaya.

Katika kitabu cha "Hadithi za Mashetani" mwandishi Pu Songling pia alitunga hadithi ya bweha kisura lakini mwenye roho katili. Hadithi ya "Kuchora Ngozi ya Mrembo" ilieleza kuwa bweha mmoja alijifunika kwa ngozi yenye sura nzuri akiishi kwa kufyonza damu za binadamu, bweha huyo mwishowe aliuawa na binadamu.

Kwa kifupi, Pu Songling aliwaelezea wasichana wengi kwa sura ya bweha, na wasichana hao walikuwa na maadili mengi mazuri ambayo binadamu hawakuwa nayo.

"Hadithi za Mashetani" ni maandishi makubwa katika historia ya fasihi ya Kichina. Katika miaka mia mbili iliyopita hadithi hiyo imetafsiriwa kwa lugha zaidi ya 20, na hadithi nyingi zilitengenezwa kuwa filamu na michezo ya televisheni.

"Safari ya Kwenda Magharibi"

"Safari ya Kwenda Magharibi" ni riwaya nzuri katika historia ya fasihi ya kale ya China. Riwaya hii ilitungwa kwa mujibu wa vituko vilivyomkuta sufii wa dini ya Kibuddha, Tang Zeng (Tang Xuanzang), alipokuwa katika safari yake ya kwenda India kuchukua msahafu katika karne ya 7 K.K. Katika riwaya hiyo Wu Chengen alibuni wafuasi watatu kufuatana na sufii huyo. Mmoja wa wafuasi wake alikuwa mfalme kima Sun Wukong. Sun Wukong alikuwa na nguvu za kudura ya mungu, anaweza kujigeuza sura 72 na fimbo yake ya kupambana na mashetani yaweza kurefushwa kuwa ndefu hadi mbinguni na kufupishwa kuwa ndogo hadi kama sindano ya kutia sikioni. Mfalme kima Sun Wukong ndiye aliyeonesha matumaini ya mwandishi kwamba mambo yote maovu yatatokomezwa kabisa katika jamii.

Wu Chengen ni mwenyeji wa wilaya ya Huai An mkoani Jiangsu. Tangu alipokuwa mtoto alikuwa mwerevu na mshabiki wa mambo mengi. Alikuwa hodari wa kuchora picha, usanii wa maandiko ya Kichina kwa brashi ya wino, pia alipenda kukusanya na kuhifadhi picha na maandiko ya watu mashuhuri. Alipokuwa kijana jina lake lilikuwa maarufu sana katika sehemu ya makazi yake kwa sababu ya kipaji chake cha fasihi. Lakini mara nyingi alishindwa katika mitihani ya kifalme ya kuchagua maafisa, na maisha yake yakawa ya shida. Kutokana na hayo akagundua ubovu ulioenea miongoni mwa maafisa na jinsi jamii ilivyotatanika, akawa na kinyongo moyoni mwake. Katika shairi lake moja alisema kwamba ubovu wa jamii unatokana na mfalme kuwatumia maafisa wabovu. Alitaka kubadilisha hali hiyo lakini hakuweza kufanya lolote ila kuipigia kite. Hivyo aliweka matumaini na kinyongo chake kwenye riwaya yake ya "Safari ya Kwenda Magharibi".

"Safari ya Kwenda Magharibi" iliandikwa na Wu Chengen katika miaka yake ya uzeeni, lakini matayarisho ya riwaya hiyo yalimtumia maisha yake yote. Alipokuwa mtoto mara kwa mara alifuatana na baba yake kwenda kwenye misitu minene na mahekalu, na baba yake humweleza hadithi za ajabu zilizotokea huko. Hamu yake ya kusikiliza hadithi utotoni mwake haikupungua hata baada ya yeye kuwa mzima. Baada ya kutimiza miaka 30 alikuwa amekusanya hadithi nyingi za ajabu akanuia kuandika riwaya. Alipofikia umri wa miaka 50 hivi alikuwa amemaliza sura 10 za mwanzo za riwaya yake ya "Safari ya Kwenda Magharibi", lakini baadaye kwa sababu fulani aliacha kwa miaka mingi hadi baada ya kujiuzulu kazi na kuwa nyumbani.

"Safari ya Kwenda Magharibi" iliandikwa hadithi moja moja lakini kila hadithi pia ni sehemu ya riwaya nzima. Ndani ya riwaya hiyo walitokea mashetani na miungu mingi ambao wanawakilisha haki na uovu. Kasri ya mbinguni ilionekana adhama sana lakini kwa kweli mungu aliyekuweko ndani ya kasri hiyo alikuwa mbabaishaji wa watu wema na wabaya, akilenga mfalme duniani; na kasri ya dunia ya pili ingawa ilionekana ukakamavu, lakini maofisa wanasaidiana katika hatia, walikuwa hawajali sheria na wadhulumiwa hawakuweza kupata haki. Hayo alilenga katika hali ya utawala wa kifalme. Mashetani walikula na kuwaua watu huku wakiwa wachoyo wa mali na kupenda warembo na kufanya uovu watakavyo. Katika hayo mwandishi alifananisha madhalimu na maofisa wa kifalme. Kwa upande mwingine Wu Chengen alifanikiwa kusawiri shujaa kima Sun Wukong, ambaye alikuwa mtetezi wa haki, alikuwa na nguvu za kudura ya mungu na mwenye msimamo bayana kati ya watu wema na wabaya, fimbo yake ina nguvu za ajabu. Hii inaonesha tarajio la Wu Chengen la kukomesha maovu yote katika jamii aliyoishi.

Riwaya ya "Safari ya Kwenda Magharibi" inajulikana sana kwa wote wa China kutoka kizazi hadi kizazi na katika miaka mia kadhaa iliyopita riwaya hii ni kama chimbuko la kutunga hadithi kwa watoto na michezo ya filamu na televisheni.

"Madola Matatu ya Kifalme"

Hii ni riwaya iliyoandikwa na Luo Guanzhong, riwaya hiyo inayojulikana kwa wote wa China. Luo Guanzhong aliishi kati ya mwaka 1330 hadi 1400, kwani maisha ya mwandishi huyo hayajulikani sana.

Riwaya ya "Madola Matatu ya Kifalme" iliandikwa kwa msingi wa historia ilivyokuwa kati ya mwaka 184 hadi 280 nchini China. Wakati huo madola matatu ya kifalme yaani Wei, Shu na Wu yalikuwa katika hali ya kulingana kwa nguvu. Lakini kila moja lilikuwa likitaka kuliangamiza lingine ili kuitawala China nzima, kwa hiyo vita vilikuwa haviishi. Kutokana na msingi wa masimulizi miongoni mwa raia kuhusu vita baina ya madola hayo matatu mwandishi Luo Guanzhong alihariri na kuandika riwaya hiyo kwa msaada wa maandishi ya historia, akieleza mivutano iliyotatanisha kati ya madola matatu katika mambo ya kijeshi, siasa na kidiplomasia. Riwaya hiyo ambayo hasa inaeleza mapambano ya kijeshi, inavutia kwa hila za kivita. Kwa ufanisi riwaya hiyo imesawiri sura za watu zaidi ya 400.

Riwaya "Madola Matatu ya Kifalme" sio tu ina thamani kubwa katika fasihi, na pia ni maandishi yaliyoeleza jamii kutoka pande mbalimbali. Kwa hiyo wasomi wengi zaidi na zaidi wanachunguza riwaya hiyo kwa ajili ya kutafiti historia, fasihi, saikolojia, hila za kivita, kwa ajili ya matumizi ya leo. Riwaya hiyo imetafsiriwa kwa lugha nyingi na inapendwa sana na wasomaji.

"Ndoto katika Jumba Jekundu"

Katikati ya karne ya 18, kilikuwa ni kipindi cha ustawi mkubwa katika Enzi ya Qing, lakini katika kipindi hicho ilitokea riwaya ndefu iliyoashiria mporomoko utakaotokea katika jamii ya kimwinyi, riwaya hiyo ni "Ndoto katika Jumba Jekundu".

"Ndoto katika Jumba Jekundu" ni riwaya iliyoandikwa na Cao Xueqin ambaye aliishi kati ya mwaka 1715 hadi 1763. Hapo mwanzo riwaya hiyo ilienea katika jamii kwa kunukuu kutoka wasomaji hadi wengine, kwa sababu riwaya hiyo ilishukiwa kuwa ililenga utawala wa wakati huo, kitabu chake cha kuchapwa rasmi lilikuwa ni jambo la baadaye. Mwandishi wa riwaya hiyo alizaliwa katika ukoo wa maofisa uliokuwa ukiporomoka kizazi hadi kizazi. Babu na baba wa mwandishi huyo wote walikuwa ni maofisa wakubwa katika utawala wa kifalme na walikuwa na uhusiano wa karibu na ukoo wa kifalme, lakini hadi miaka wakati ukoo wa mwandishi huyo ulipoporomoka kwa madaraka na hadhi, hata maisha yalikuwa magumu. Wengi wanaona kuwa Cao Xueqin aliandika riwaya hiyo kwa mujibu wa hali ya ukoo wake ilivyokuwa, na kutokana na umaskini mwandishi Cao Xueqin alifariki kabla kumaliza riwayake. Kitabu hicho kilipoenea kutokana na kunukuu alikuwapo mwandishi aliyeitwa Gao E, huyo ndiye aliyemmalizia riwaya yake na kuifanya riwaya hiyo kuwa na sura 120 za sasa.

Riwaya hiyo imeeleza jinsi jamii ya wakati ule ilivyokuwa kupitia maelezo kuhusu koo nne kubwa za "Jia, Shi, Wang na Xue", hasa maelezo kuhusu jinsi ukoo wa Jia ulivyostawi na kuporomoka. Uhodari mkubwa katika riwaya hiyo ni kueleza maisha halisi yalivyokuwa na sura halisi za wahusika walivyo. Ndani ya riwaya hiyo wahusika wafikia zaidi ya 400 na kila mmoja ana tabia na hulka yake mwenyewe, hakuna aliyefanana na mwingine, ikionesha ustadi mkubwa wa fasihi wa mwandishi. Maelezo kuhusu maisha ya kila siku yanachukuliwa kama ni maelezo halisi ya maisha ya wakazi wa Beijing yalivyokuwa katika karne ya 18. Riwaya ya "Ndoto katika Jumba Jekundu" inakubalika kwa wote kuwa ni kilele cha utunzi katika fasihi ya kikale ya China.


1 2 3 4 5