15: Fasihi ya Kale

Tenzi

"Utenzi wa Mfalme Gesar"

Utenzi wa Mfalme Gesar ni utenzi wa kale na mrefu kabisa duniani, na mpaka sasa unaimbwa kumsifu mfalme shujaa Gesar katika Tibet.

Utenzi wa Mfalme Gesar ulipatikana tokea miaka mia mbili K.K. hadi karne ya sita kutoka masimulizi ya mapokeo, na ifikapo karne ya 12 utenzi huo ulikuwa umekamilika, na kuenea mpaka sasa mkoani Tibet.

Utenzi wa Mfalme Gesar unasimulia hadithi kama ifuatayo: Katika zama za kale, maafa makubwa yalitokea katika Tibet, licha ya maafa ya kimaumbile pia mashetani walifanya uovu na kuwanyanyasa watu kiholela. Mungu mdogo wa kike mwenye huruma Pu Sa alimwomba Buddha awapeleke askari wake kushuka duniani kuwaangamiza mashetani. Buddha alimteua Gesar awe mfalme na kupambana na mashetani na awaletee maisha bora watu wa Tibet. Watungaji wa utenzi huo walitunga shujaa mwenye nusu binadamu na nusu mungu. Gesar alikuwa hatarini mara kadhaa lakini kutokana na ulinzi wa mungu kila mara alisalimika, na aliwaua mashetani wengi. Tokea alipozaliwa Gesar alianza kuwaokoa watu kutoka kwenye misiba mingi. Alipokuwa na umri wa miaka 12 alishinda katika mashindano ya mbio za farasi na alichaguliwa kuwa mfalme. Tokea hapo alianza kuonesha ushupavu wake wa kupambana na mashetani huku na huko na kuwaua mashetani wengi. Mchango wake ulikuwa ni mkubwa na baada ya kumaliza jukumu lake duniani alirudi mbinguni.

Utenzi wa Gesar ni mrefu, una beti zaidi ya milioni moja wenye maneno milioni 20 katika juzuu 120, ni utenzi mrefu kabisa duniani.

"Jiangger"

"Jiangger" ni utenzi wa kabila la Wamongolia na ulitokea katika karne ya 15 hadi 17.

Mhusika mkuu katika utenzi huo Jiangger, alipokuwa na miaka miwili wavamizi wakatili wa Mangusi waliishambulia sehemu ya maskani yao, wazazi wake waliuawa, Jiangger akawa yatima. Ili kulipiza kisasi kwa ajili ya wazazi wake, alipokuwa na umri wa miaka mitatu alianza kupigana vita huku na huko na alipokuwa na umri wa miaka saba alipata ushindi mkubwa, alichaguliwa kuwa kiongozi wa kabila lao. Lakini wavamizi wa Mangusi walikuwa hawakubali kushindwa, walikuwa mara kwa mara wakifanya uvamizi dhidi ya kabila la Jiangger. Jiangger aliwaongoza majemadari 35 na askari hodari elfu 8 na kuwashinda wavamizi. Jiangger kwa hekima yake alijenga nchi iliyotamanika. Kwamba watu wanaoishi katika nchi hiyo hawazeeki, mimea inastawi mwaka mzima. Wananchi wanaishi kwa furaha tele na kicheko cha furaha kinasikika kila mahali.

Utenzi huo ulimwelezea shujaa aliyependwa sana na watu wa kabila lake kwa akili zake na ushupavu wake. Huu ni utenzi wenye taathira kubwa kwa fasihi ya kabila la Wamongolia, hivi sasa ni utamaduni unaohifadhiwa na serikali ya China.

"Manasi"

Utenzi "Manasi" ulitokea kati ya karne ya 9 hadi 10 mkoani Xinjiang. Manasi ni shujaa katika masimulizi ya mapokeo mkoani Xinjiang, ni hadithi inayoeleza Manasi alivyoongoza watu kupambana na watawala wa kabila jingine waliowanyanyasa na kupigania uhuru wa kabila lake. Utenzi huo una beti laki 2.1 na maneno milioni 20. Katika utenzi huo watu zaidi ya 100 walieleziwa ambao wako wazee waliomwunga mkono na marafiki, pia wako watu wabaya, mfalme, wahaini na mashetani.

Utenzi "Manasi" umetafsiriwa kwa Kichina kutoka lugha ya kikabila na baadhi ya sehemu za utanzi huo zilitafsiriwa kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kijapan. Kutokana na umaarufu wa utenzi huo UNESCO iliwahi kuamua mwaka 1995 kuwa ni "Mwaka wa Manasi Duniani".


1 2 3 4 5