17: Watu Mashuhuri Katika China ya Kale

Wafalme wa China ya Kale

Mwanzilishi wa Utawala wa Kiini Kimoja, Qin Shihuang

Qin Shihuang ni mwanzilishi wa utawala wa kiini kimoja nchini China. Mwishoni wa kipindi cha madola ya kivita (225—222 K.K.) madola yaliyobaki yalikuwa saba yenye nguvu, nayo ni Qin, Chu, Qi, Yan, Han, Zhao na Wei. Kati ya madola hayo dola la Qin lilikuwa na nguvu zaidi. Tokea mwaka 236 K.K. hadi 221 K.K. dola hilo kwa nyakati tofauti liliyateka madola mengine sita na kusisisi nchi ya kwanza yenye muungano na utawala wa kidikteta wenye kiini kimoja katika historia ya China, Enzi ya Qin.

Mwaka 221 K.K. Qin Shihuang alifanikisha lengo lake la kuiunganisha China. Tokea hapo historia ya China yenye madola mengi ya kujitawala ilikuwa imemalizika na badala yake imekuwa nchi yenye kiini kimoja cha utawala.

Muungano wa China ulioletwa na Qin Shihuang una maana kubwa na ni mchango mkubwa katika historia ya China. Kwanza, kwa upande wa siasa mfalme Qin Shihuang alibatilisha mfumo wa kila sehemu kujitawala na badala yake aliigawa China katika mikoa 36, na chini ya mikoa aliweka wilaya, maofisa wa ngazi zote aliwachagua au kuwaachisha kazi yeye mwenyewe, na maofisa hawakuruhusiwa kurithisha nyadhifa zao. Mfumo huo wa utawala ulioanzishwa katika enzi ya Qin uliendelea kutumika katika historia yote ya kimwinyi, kwa miaka zaidi ya elfu mbili nchini China, na baadhi ya majina ya wilaya yalitumika katika enzi ya Qin yanatumika hadi leo. Kadhalika, Qin Shihuang pia alisawazisha upimaji, kwani upimaji wa urefu, uzito na ujazo ulikuwa tofauti katika kipindi cha madola ya kivita na tofauti hizo zilikwamisha uchumi. Mfalme Qin Shihuang pia alisawazisha sarafu na kuzifanya sheria ziwe za namna moja, hivyo alikuwa ameleta hali nzuri ya kuendeleza uchumi na pia kutilia mkazo utawala wake wenye kiini kimoja nchini China.

Ili kuwapumbaza kimawazo watu wake alitumia hata sera ya kuchoma moto vitabu ambavyo havikuliangana na mawazo yake ya utawala na kuwatesa wasomi wa Confucius; pia watu ambao walitofautiana naye kimawazo aliwazika wakiwa hai ili kudumisha utawala wake. Pamoja na hayo mfalme huyo aliamrisha kujenga na kukarabati kuta zilizojengwa na madola ya Qin, Zhao, Yan na madola mengine na kuziunganisha kuwa ukuta mmoja mrefu. Zaidi ya hayo alitumia fedha nyingi na watu laki 7 kujijengea kaburi lake. Mwezi Julai mwaka 210 K.K. Qin Shihuang alifariki.

Liu Bang

Liu Bang ni mwanzilishi wa Enzi ya Han Magharibi (206 K.K.—220).

Liu Ban alizaliwa katika ukoo wa wakulima, mwanzoni aliwahi kuwa ofisa mdogo katika Enzi ya Qin, kwa sababu aliwaachia wafungwa huru alitorokea mbali na kujificha ili kukwepa adhabu ya mfalme wa Qin. Mwaka 209 aliwakusanya wakulima wa maskani yake kujiunga na jeshi la uasi lililoongozwa na Chen Sheng na Wu Guang. Baadaye jeshi aliloongoza lilitangulia kufika kwenye mji mkuu wa Enzi ya Qin, Xianyang, na kumaliza utawala wa Enzi ya Qin. Katika mji mkuu wa Qin alifuta sheria na kodi na kuweka kanuni "aliyeua mtu auliwe, aliyejeruhi mtu au kuiba aadhibiwe". Kutokana na hayo alikaribishwa na raia.

Tokea hapo, Liu Bang alipambana na jeshi la Xiang Yu kwa miaka minne. Mwaka 202 jeshi la Liu Bang lenye askari laki tatu lilizunguka jeshi la Xiang Yu, Xiang Yu alijiua, Liu Bang alipata ushindi kamili na katika mwaka 202 alikuwa mwalme wa Enzi yake Han Magharibi.

Liu Bang alikuwa hodari wa kuchagua wasaidizi wake ambao mara nyingi walimsaidia kusalimika katika hatari. Hali iliyokuwa hatari kubwa ni kushiriki kwenye karamu ya Hong Men iliyoandaliwa na Xiang Yu. Wakati huo jeshi la Xiang Yu lilikuwa na nguvu kubwa kuliko jeshi la Liu Bang na Xiang Yu alitamani kumwangamiza Liu Bang na kuwa mfalme. Baada ya kufahamu hali hiyo Liu Bang alikwenda kwenye karamu akiwa pamoja na mshauri wake Zhang Liang. Kwenye karamu, jemadari wa Xiang Yu alijitokea kwa kucheza kitara kwa kisingizio cha kuchangia furaha ya karamu akitaka kumwua Liu Bang. Mshauri Zhang Liang aliona hali ilikuwa hatari, alimwamuru askari kumlinda. Dakika chache baadaye Liu Bang alitumia kisingizio cha kwenda chooni alitoroka na kurudi kwa siri. Kisha mshauri wake aliingia kwenye ukumbi wa karamu na kutoa zawadi kwa Xiang Yu, na kumwambia Xiang Yu kuwa Liu Bang keshaondoka. Baadaye Liu Bang alikusanya nguvu zake zote kulishinda kabisa jeshi la Xiang Yu na kuansisha Enzi ya Han Magharibi.

Baada ya kuwa mfalme, Liu Bang alitunga sera nyingi za kuendeleza uzalishaji. Kutokana na vita vya miaka mingi, idadi ya watu ilipungua, aliwaachia wafungwa na watumwa huru, aliwaachia askari wake warudi nyumbani kushughulika na kilimo.

Liu Bang alibeza wasomi, aliona kuwa utawala wake ulipatikana kwa vita, mashairi na vitabu kwake vilikuwa havina maana. Waziri wake Lu Jia alisema, "Kitu kilichopatikana kutoka mgongo wa farasi kinaweza kutumika katika utawala?" Kusikia hayo alimwagiza Lu Jia aandike kitabu cha kueleza sababu za enzi iliyotangulia kushindwa ili kuboresha utawala wake. Liu Bang alikaa madarakani kwa miaka 12, katika mapambano dhidi ya waasi alipigwa mshale, baada ya kuugua muda alikufa.

Da Yu

Miaka 4000 iliyopita mafuriko makubwa yalitokea katika sehemu za bonde la Mto Huanghe. Kutokana na mchango wa kuondoa mafuriko, Da Yu aliheshimiwa sana miongoni mwa raia, mtemi wa kabila la Wachina Shun alimwachia nafasi yake. Hadithi kuhusu Da Yu ilielezwa kizadi hadi kizazi.

Inasemekana kwamba katika miaka Yao alipokuwa madarakani mafuriko yaliyokea, maji yaligharisha mimea na nyumba, watemi wa makabila yote walimchagua baba wa Da Yu kwenda kupambana na mafuriko. Baada ya miaka tisa kupita mafuriko yaliendelea, baba yake aliuawa kwa adhabu na mtoto wake Da Yu aliagizwa kupambana na mafuriko.

Da Yu hakufuata baba yake alivyopambana na mafuriko, bali alichimba mifereji na kuyaongoza maji baharini. Da Yu alifanya kazi sawa na raia, kwa juhudi za miaka 13 mwishowe alifanikiwa kuyapeleka mafuriko kwenye bahari.

Da Yu alianza kupambana na mafuriko baada ya siku chache kuoa. Siku moja alipopita mbele ya nyumbani alisikia kilio cha mtoto wake mchanga, lakini hakuingia nyumbani kutokana na shughuli.

Kutokana na mchango wake mkubwa wa kuondoa mafuriko, watu walimchagua kuwa kiongozi wa muungano wa makabila.

Baadaye kabila la Da Yu lilimpendekeza mtoto wa Da Yu, aliyeitwa Qi, kurithi kiti cha Da Yu, tokea hapo utaratibu wa uchaguzi wa muungano wa makabila ulifutwa na badala yake utaratibu wa kurithisha kiti cha ufalme ulitokea.

Enzi ya kwanza ya kifalme, Xia, ilitokea katika mfumo wa jamii ya utumwa nchini China.

Yao na Shun

Kiasi cha miaka 4000 iliyopita, walitokea watu kadhaa mashuhuri, Yao, Shun, Da Yu na wengine. Yao na Shun walikuwa ni wafalme wawili wa mwanzo kabisa nchini China katika masimulizi ya mapokeo, watu hao wawili ndio walioanzisha historia ya China. Katika vitabu vingi vya hekaya na masimulizi ya mapokeo, kuna mengi yaliyoeleza kuhusu Yao na Shun.

Yao alikuwa ni mtemi mwishoni mwa jamii ya kiasili, ni mwakilishi wa utamaduni wa mwanzo kabisa nchini China. Kutokana na masimjulizi ya mapokeo, Yao alikuwa ni kizazi cha babu wa taifa la China Huangdi, alikuwa mtu mwenye akili, roho nzuri na aliheshimiwa sana. Alipokuwa na umri wa miaka 16 aliendekezwa kuwa mtemi. Watu wa kabila la Yao waliishi katika sehemu ya kaskazini ya China, mji wa Baoding mkoani Hebei wa sasa. Kwa kushirikisha makabila mengine yaliyoko katika sehemu yake alipigana na wavamizi na kuwapokea kuwa watu wa kabila lake. Kutokana na nguvu za kabila lake kuongezeka haraka, Yao alikuwa mkuu wa muungano wa makabila kadhaa, watu wa baadaye walimwita mfalme Yao.

Yao alikuwa mfalme mwema, aliishi kama raia wa kawaida na kutenda mambo kwa uadilifu. Alithamini sana maofisa walio wema, alikagua maofisa wake kazi walizofanya na kuwasifu wale walio bora na kuwaadibu walio wabaya. Kutokana na hayo, kazi za utawala wake zilikuwa na utaratibu mwema. Aliweka ofisa wa unajimu ili watu waweze kushughulika na kilimo kwa misimu, watu wa kale wa China walisema, kipindi cha utawala wa Yao kilikuwa kipindi cha maendeleo ya haraka katika kilimo. Yao alikuwa anatilia maanani sana uhusiano mwema kati ya makabila na kuwashawishi watu wake waishi kwa majirani wema, hali ya jamii ilikuwa tulivu na ilijaa upendo.

Yao alikuwa madarakani kwa miaka 70, alikuwa mfalme wa kwanza kabisa kumwachia mrithi wake kiti cha ufalme kwa mujibu wa uhodari wa mtu.

Inasemekana kwamba aliwataka watu na maafisa wa sehemu mbalimbali wawapendekeze watu walio hodari, hata mtu huyo akiwa hana hadhi katika jamii. Mwishowe watu walimpendekeza mtu mmoja maskini aliyeitwa Shun. Inasemekana kwamba wazazi walikuwa wakali kwa Shun na ndugu zake pia walikukwa wajeuri kwa Shun, lakini Shun aliishi nao vema. Watu waliona kuwa Shun ni mtoto mwema kwa wazizi na ni mwenye maadili mema, alistahili kuwa mtawala na anaweza kuongoza vivuri taifa. Yao alimchunguza kwa pande zote, aliona kuwa Shun kweli ni mtu mwenye maadili mema na pia ni hodari. Baada ya miaka mitatu alimwachia Shun kiti chake cha ufalme badala ya kumwachia mtoto wake Dan Zhu. Kitendo hicho kisichokuwa na tamaa binafsi kwa ajili ya maslahi ya wananchi, kinasifiwa kuwa ni demokrasia ya mwanzoni kabisa nchini China.

Baada ya kuwa mfalme, Shun alistawisha zaidi siasa ya demokrasia. Alitunga sheria ya adabu na adhabu, aliwateua maofisa wa kazi mbalimbali kusimamia mambo ya utawala, uchumi, elimu, shughuli za bidhaa za kazi ya mikono, muziki, na pia alitunga sheria ya kuwachunguza maofisa, hivyo utaratibu wa utawala wa taifa ulizidi kukamilika kwa kiasi kikubwa.

Shu alitilia mkazo katika uzalishaji, uchimbaji wa mifereji na visima, na kuweka urafiki na watu wengi. Katika kipindi cha utawala wa Shun kilimo na ufundi vyote vilipata maendeleo ya kasi. Shun alikuwa mfano wa maadili mema kwa vitendo, alishirikiana na wananchi katika dhiki na faraja. Katika kipindi cha utawala wake watu walikuwa na maadili mema, watiifu, na waliishi bila usumbufu, kipindi chake kilikuwa kipindi chenye siasa bora, uzalishaji mkubwa na ustawi wa muziki. Kuhusu urithi wa kiti cha ufalme, Shun pia alitumia njia kama ya mfalme Yao, alimwachia kiti chake Yu (Da Yu), mtu aliyetoka mchango mkubwa katika shughuli za kupambana na mafuriko.

Shen Nong (Yandi)

Miaka 5000 iliyopita, Shen Nong alikuwa mtemi wa kabila moja. Katika zama za kale, mtemi alikuwa sawa na watu wa kawaida kufanya kazi mashambani, na alipokuwa analima alivumbua plau ambayo ilisaidia sana kwenye maendeleo ya kilimo. Kutokana na mchango wake huo watu walimwita Shen Nong (mkulima hodari).

Zama alipoishi Shen Nong zilikuwa ni kipindi cha mwanzo wa komuna ya ubaba, kulikuwa hakuna unyonyaji wala ukandamizaji, watu wote walikuwa sawa. Kutoka na maandishi ya kale, katika zama hizo wanaume walifanya kazi shambani na wanawake walifuma vitambaa, kulikuwa hakuna gereza wala adhabu, wala kulikuwa hakuna jeshi wala polisi.

Shen Nong pia alikuwa mtaalamu wa dawa wa mwanzo kabisa nchini China. Inasemekana kwamba aliona usumbufu sana alipoona watu wanavyougua. Alifikiri kwamba mazao yanaweza kusaidia afya basi majani na mizizi pengine inaweza kusaidia kuondoa ugonjwa. Katika masimulizi ya mapokeo, Shen Nong alichuma aina mbalimbali za mimea na kuonja, na alikuwa mara kwa mara alipatwa na sumu. Aliwahi kuandika kitabu cha "Dawa za Mitishamba za Shen Nong", kikieleza maelezo ya tiba ya magonjwa.

Kadhalika, Shen Nong pia alikuwa mnajimu kwa ajili ya kukumbuka mambo na kupiga ramli. Zaidi ya hayo, alipoona watu wanaolima mazao mengi kuliko mahitaji, na baadhi ya mazao wanayohitaji walikuwa hawajui kulima, aliweka mahali maalumu kwa ajili ya kubadilishana mazao, hivyo kulitokea soko.

Shen Nong alikuwa madarakani miaka 140, baadaye Huandi alichukua nafasi yake. Alizikwa katika mji wa Changsha wa leo, mpaka sasa kuna kaburi lake, watu wanaliita kaburi lake kuwa kaburi la Yandi.

Fu Xi

Kutoka na maandishi ya kale, Fu Xi alikuwa mmoja wa wafalme wa mwanzo kabisa nchini China, aliishi katika miaka 5000 iliyopita.

Fu Xi alikuwa mnajimu, alivumbua namna ya kukumbuka mambo badala ya kwa kupiga fundo la kamba.

Kamba zilikuwa ziada, basi aliwafundisha watu kufuma wavu kwa ajili ya kuvua samaki na kutega wanyama. Shen Nong aliwafundisha namna ya kupata moto kwa kupekecha, na kula chakula kwa kuchoma, hivyo watu walikuwa wameagana kabisa na maisha ya kiasili ya kula nyama mbichi.


1 2 3 4 5