17: Watu Mashuhuri Katika China ya Kale

Wanasiasa na Wanafikra wa China ya Kale

Hanfeizi

Hanfeizi aliishi katika Enzi ya Vita vya Kivita (475 K.K.--221K.K.), alikuwa ni mwanafalsafa, na mwanasheria. Alikuwa wa kwanza kutoa nadharia ya kisheria kwa ajili ya utawala taifa wenye kiini kimoja.

Hanfeizi aliishi katika karne ya tatu ambapo ilikuwa ni kipindi cha mwisho cha Enzi ya Kivita. Alikuwa na kigugumizi, hakuwa hodari wa kusema, lakinialikuwa ni hodari wa kuandika vitabu.

Kitabu alichoandika "Hanfeizi" kilikusanya maandishi yote ya wanasheria wa Enzi ya Qin. Kitabu hicho kinachopatikana sasa kina makala 55 zenye maneno zaidi ya laki moja, na makala nyingi ni zake mwenyewe. Alitetea siasa ya kutoa zawadi kubwa kwa watu waliokuwa na mchango na kutoa adhabu kali kwa watu waliokuwa wahalifu, na kutilia maanani kilimo na nguvu za kupigana vita. Kadhalika alitetea kuwa madaraka ya mfalme yanawakilisha nia ya mungu. Tokea Enzi ya Qin yenye utawala wa kidikteta katika jamii ya kiumwinyi nadharia ya Hanfeizi ilikuwa na athari kubwa.

Zhuangzi

Zhuangzi aliishi katika karne ya nne katika dola la Song, aliwahi kuwa ofisa mdogo, alikuwa mwenye akili na aliwahi kutembelea kila mahali. Kutokana na werevu wake aliwahi kualikwa na mfalme wa Dola la Chu, lakini alikataa na tokea hapo hakuwahi kuwa ofisa, alijitenga na jamii na kuishi kwa kusuka viatu kwa majani. Inasemekana kwamba aliandika vitabu vyenye maneno zaidi ya laki moja.

Zhuangzi aliona kuwa maisha ya binadamu lazima yawe ya uhuru kabisa wala sio kuwa na mali nyingi au sifa za bure.

Pamoja na fikra za Zhouyi, Laozi, fikra za Zhuangzi pia zilikuwa athari kubwa katika Enzi ya Tang (618—907).

Fikra za Zhuangzi hazielezwi kwa nadharia tupu bali kwa hekaya. Kitabu chake kilikuwa kama ni mkusanyiko wa hekaya.

Mencius

Mencius alikuwa ni mwanafikra mkubwa, aliishi Enzi ya Madola ya Kivita (karne ya 5 K.K. hadi karne ya 3 K.K.) ni mmoja wa wawakilishi wa fikra za Confucius nchini China.

Mencius alirithi na kuendeleza fikra za Confucius, alikuwa ametofautisha wazi tabaka la watawala na tabaka la watawaliwa, alisema kuwa "wanaofanya kazi kwa akili wanatawala, na waliofanya kazi kwa nguvu za mwili wanatawaliwa" na aliweka matabaka toka mfalme hadi makabwera. Na wakati huo alitetea kuwa uhusiano kati ya watawala na watawaliwa kama ni wazazi na watoto, na kusema kwamba watawala wawatendee vema raia kama wazazi wao na raia wawatii watawala kama wanavyowatii wazazi wao.

Mencius aliunganisha nadharia yake pamoja na siasa. Alisisitiza kuwa maadili mema ni msingi wa siasa. Alisema, "utawala ni msingi wa taifa, na msingi wa taifa ni familia, na msingi wa familia ni maadili ya kila mmoja." Alisema kuwa kama kila mmoja aliwatendea wengine kwa maadili mema, utawala wa kimnwinyi unahakikishwa.

Ili kufahamisha nadharia yake alisema, asili ya binadamu ni utu, aliona kuwa ingawa kuna tofauti ya kazi na watu wanaishi katika matabaka tofauti, lakini utu ni mmoja.

Ingawa fikra za Mencius zilikuwa na athari kubwa katika historia ya China katika siasa, fikra, utamaduni na maadili, lakini haikuthaminiwa na mtawala wa enzi yake.

Confucius

Mtu yeyote anapozungumzia utamaduni wa China hawezi kuacha kumtaja Confucius. Kwenye miaka ya 70 ya karne iliyopita, msomi mmoja wa Marekani alipoorodhesha watu 100 wenye taathira kubwa kabisa katika historia ya dunia, Confucius alipangwa wa tano, nyuma tu ya Yesu, mwanzilishi wa dini ya Buddha, Sakyamuni, na wengine wawili. Lakini miongoni mwa watu wa China, Confucius ni wa kwanza kabisa, kwani kila mmoja hakika ameathiriwa na fikra zake kwa kiasi fulani.

Katika miaka zaidi ya 200 iliyopita nchini China, fikra za Confucius sio tu zilikuwa zikiathiri sana siasa na utamaduni, bali pia ziliathiri fikra za kila Mchina, kiasi kwamba hata baadhi ya wasomi wa nchi nyingine walidhani kuwa fikra za Confuciusi ni imani ya dini fulani nchini China. Lakini kwa kweli fikra za Confucius zilikuwa ni moja tu ya falsafa kadhaa zilizokuwepo katika China ya kale, ni aina ya falsafa, na wala haikuwa imani ya dini. Hata hivyo katika jamii ya kimwinyi ya miaka zaidi ya 2000 nchini China fikra zake zilikuwa zimetukuzwa kama ni fikra sahihi kabisa na zilikuwa na heshima ya kipekee. Fikra za Confucius sio tu zimeathiri kwa kina utamaduni wa China bali pia nchi nyingi za Asia. Hadi leo, kwa sababu Wachina wametapakaa kila pembe ya dunia, fikra za Confucius pia zimevuka China na Asia, na kuenea duniani kote.

Confucius alizaliwa mwaka 551 K.K. na kufariki mwaka 479 K.K., aliishi kabla ya msomi maarufu wa Ugiriki ya kale, Aristotle, kwa zaidi ya miaka 100. Alipokuwa na umri wa miaka mitatu Confucius alifiwa na baba yake, kisha yeye pamoja na mama yake wakaweka makazi yao katika mkoa wa sasa Shandong uliopo mashariki mwa China. Jina lake la ukoo kwa Kichina ni Kong na jina lake ni Qiu, Wachina humwita "Kong Zi" kwa heshima. Katika jamii ya China ya kale mbele ya jina la ukoo likiongezewa neno "Zi" ina maana ya heshima kwa mtu huyo.

Zama alizoishi Confucius zilikuwa ni kipindi cha "Spring na Autumn" katika historia ya China. Katika kipindi hicho China iliyoungana ilisambaratika na kuwa madola mengi madogo madogo, na dola alilokuwa akiishi liliitwa Dola la Lu, dola ambalo lilistawi zaidi kiutamaduni kuliko madola mengine.

Maishani mwake, Confucius hakuwahi kuwa afisa mkubwa, lakini alikuwa na elimu kubwa. Katika China ya kale waliokuwa na fursa maalumu ya kupata elimu walikuwa ni watu kutoka familia za kitajiri tu. Lakini Confucius alivunja utaratibu huo, na alipokea wanafunzi bila kujali wanatoka katika familia gani, ikiwa tu watalipa vitu, ikiwa kama ni karo. Confucius aliwaelimisha wanafunzi msimamo wake wa kisiasa na nadharia yake. Inasemekana kuwa jumla walikuwepo wanafunzi elfu 3, na kati ya hao waliibuka wanafikra kadhaa wakubwa kama Confucius, ambao walirithi na kuendeleza fikra zake na kuzieneza sana.

Lakini je, ni kwa nini fikra za Confucius zilienziwa mpaka zikashika nafasi ya utawala katika zama za kimwinyi nchini China? Hili ni suala ambalo haliwezi kuelezwa kwa maneno machache. Lakini kwa kifupi, fikra zake zilizowagawa watu katika matabaka tofauti na mageuzi yake ya kisiasa yalilingana na manufaa ya tabaka la utawala, na katika zama hizo fikra zahizo zilileta matokeo ya kutuliza na kuendeleza jamii. Confucius alitilia sana mkazo katika utaratibu wa maadili, akiona kwamba ni kosa kubwa kwa watu wa chini kutowaheshimu wakubwa, au watoto kutowaheshimu baba zao. Kutokana na nadharia yake, jukumu la wafalme ni kutawala vyema taifa na jukumu la raia ni kutii wafalme. Pengine mmoja anaweza kuwa na nafasi kadhaa kwa pamoja, maana pengine yeye ni mwana na huku ni baba wa mtu, na labda pia ni afisa, lakini kutokana na mazingira tofauti anapaswa ajiweke katika nafasi yake. Hivyo taifa litakuwa shwari, maisha ya raia yatakuwa ya utulivu.

Nadharia ya Confucius ilipoibuka haikuwa wazo tawala mara moja hadi kabla ya karne ya pili, China ilipokuwa nchi ya muungano yenye kiini kimoja cha madaraka na ilistawi kwa nguvu. Wakati huo watawala waliona kuwa nadharia ya Confucius inasaidia sana kuleta utulivu wa jamii, ndipo nadharia yake ikatukuzwa na kuwa nadharia ya kutawala taifa.

Fikra za Confucius zimekusanywa katika kitabu kimoja, nacho ni "Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius". Katika China ya kale kitabu hicho kilikuwa kama msahafu sawa na biblia ilivyokuwa katika nchi za Magharibi. Raia wa kawaida walikuwa wanajichunga kwa mawazo ya kitabu hicho; Endapo watu walitaka kupata nyadhifa iliwabidi kusoma kitabu hicho kwa undani. Katika historia ya China kuna usemi unaojulikana sana, nao ni "Nusu kitabu cha 'Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius' yanaweza kutawala dunia nzima" maana yake ni kuwa mradi tu ukifuata nusu na nadharia ya Confucius utaweza kabisa kutawala taifa.

Kwa kweli Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius sio kitabu cha mahubiri ya maadili tu bali vile vile ni kitabu chenye mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusoma vitabu, kuhusu muziki, utalii na kujenga urafiki n.k. Katika kitabu hicho, imeandikwa kuwa mwanafunzi wake mmoja aliyeitwa Zi Gong alimwuliza Confucius kwamba, ikiwa lazima afute moja kati ya jeshi, chakula na raia katika utawala wake, basi ni bora afute lipi? Bila wasiwasi, Confucius akamjibu: Jeshi.

Nadharia ya Confucius inagusia mambo mengi, na baadhi ya mambo hayo yanafuatwa hata katika zama zetu, na maneno aliyosema yalikuwa mengi katika kitabu hicho, hadi sasa baadhi yamekuwa usemi unaojulikana kwa wote, mathalan, "Kati ya watu watatu, hakika mmoja anafaa kuwa mwalimu wangu", maana yake ni kuwa kila mmoja huwa na sifa zake, wanadamu wanapaswa kujifunza kutoka kwa wengine.

Laozi

Laozi, jina lake la ukoo ni Li na jina lake ni Er, jina Laozi ni jina lake alilopewa na watu kwa heshima. Alikuwa mtu wa Dola la Chu katika Enzi ya Spring na Autumn (770 K.K.—476 K.K.). inasemekana kwamba yeye alikuwa ni mtu mrefu mwenye masikio makubwa, kipaji kipana na midomo minene. Aliwahi kuwa mtunza vitabu, na kutokana na kazi hiyo alikuwa na elimu kubwa. Confucius aliwahi kwenda kukutana naye kutaka kujifunza. Laozi aliandika kitabu cha "Maadili", kitabu hicho kilikuwa na maneno elfu tano. Katika kitabu hicho aliandika kwamba mambo yote duniani yanahusiana na kusaidiana. Na pia katika kitabu hicho alieleza kuwa mambo yanaweza kubadilika, kwamba mambo mazuri yanaweza kubadilika kuwa mambo mabaya na mambo mabaya yanaweza kubadilika kuwa mazuri, na ndani ya mambo mazuri kuna sehemu ya kuyafanya mambo mazuri kuwa mabaya na ndani ya mambo mabaya kuna sehemu fulani ya kuyafanya mambo mabaya kuwa mambo mazuri. Alisema mbegu ndogo inaweza kuchipuka na kua kuwa mti mkubwa, chembe za udongo zinaweza kujenga jukwaa kubwa. Alisema watu haifai kutishika na taabu, ili mradi tu akiwa na nia ya kufanya juhudi kutoka kazi ndogo ndogo bila kuacha atapata mafanikio makubwa.

Laozi alipinga sana vita. Alisema, mahali palipokuwa na vita patakuwa vichaka, na baada ya vita hakika kutakuwa na maafa ya kilimo, na pia alipinga watawala kuishi maisha ya anasa na kutoza kodi kupita kiasi.

Fikra za Laozi ni muhimu katika historia ya falsafa ya China, na fikra zake zilikuwa na taathira kubwa kwa wanafikra wa kimaendeleo na wanamageuzi ya jamii.


1 2 3 4 5