23: Ala za Muziki

Ala za Muziki kwa Kupulizwa

Xibili

Xibili ni ala ya kabila la Wakorea wanaokaa mkoani Jilin. Sauti yake ina ladha nzito ya muziki wa kabila la Wakorea.

Xibili ina sehemu mbili, moja ya filimbi kwa bua la tete na paipu ya mwanzi. Urefu wake ni sentimita 20-25, ina vitundu 7.

Mpigaji wa ala hiyo anaziba vitundu vitatu kwa vidole vya mkono wa kushoto na kuziba vitundu vinne kwa vidole vya mkono wa kulia. Ala hiyo inaweza kutoa sauti 20, na inaweza kutoa sauti mbili tofauti kwa pamoja, lakini ufundi wa kupiga ala hiyo ni mgumu.

Houguan

Houguan ni moja ya ala za muziki wa Ki-guangdong. Hapo awali ilipigwa kwa ajili ya biashara barabarani. Katika miaka ya 20 ya karne ya 20 ala hiyo imeanza kutumika katika muziki wa Kiguangdong.

Houguan ina sehemu tatu, yaani filimbi, paipu na tarumbeta. Paipu inatengenezwa kwa mwanzi au plastiki, lakini paipu ya mwanzi inatoa sauti nzuri zaidi. Kwenye paipu kuna vitundu saba, na tarumbeta hutengenezwa kwa shaba kwa umbo kama V ili kupaaza sauti, na pia ni pambo.

Sauti ya Houguan ni nene na kidogo inafanana na sauti inayotoka puani.

Katika miaka ya 60 ya karne ya 20 wanamuziki walifanya mageuzi na kuifanya ala hiyo iwe na eneo kubwa la sauti.

Xiao

Xiao ni ala nyingine inayotoa sauti kwa kupuliza. Ala hiyo ilipatikana zamani sana nchini China, na tokea mwanzo ala hiyo ilikuwa na jina hilo hilo. Kwenye paipu kuna vitundu na kwa kuziba vitundu hivyo kubadilisha sauti.

Mwanzoni Xiao ilitokea katika mikoa ya Sichuan na Gansu, na katika karne ya kwanza ala hiyo ilianza kuenea katika sehemu ya kaskazini.

Xiao inafanana sana na filimbi, lakini ni ndefu kuliko filimbi. Ala hiyo inatengenezwa kwa mwanzi, na kuna vitundu tano, vitundu vinne viko mbele na kimoja kiko nyuma, na kwenye sehemu ya mwisho kuna vitundu vitatu au vinne ambavyo vinasaidia kufanya sauti itoke zaidi.

Xiao inafaa kueleza hisia za upendo au za huzuni kutokana na sauti yake laini na nene, kwa hiyo mara nyingi hupigwa peke yake, lakini vile vile inatumika katika muziki wa Ki-guangdong na muziki wa opera kwa kushirikiana na ala nyingine.

Kuna aina nyingi za Xiao kutokana na urefu na unene tofauti.

Muziki maarufu "Bata buniki Wanaoelea Angani" unaeleza vizuri jinsi ndege walivyozunguka pole pole angani.

Guanzi

Guanzi ni aina nyingine ya paipu. Ala hiyo ilianza katika Enzi ya Han Magharibi miaka elfu mbili iliyopita mkoani Xinjiang nchini China, na baadaye ilienea katika sehemu ya kaskazini ya China.

Sauti ya Guanzi ni kubwa, ni ala ya muziki isiyoweza kukosekana katika muziki wa kienyeji wa sehemu ya kaskazini ya China. Ala hiyo inaweza kutoa sauti za aina mbalimbali hata kuiga milio ya wanyama.

Guanzi inagawanyika katika aina tofauti kutokana na ukubwa tofauti.

Muziki maarufu wa Guanzi peke yake "Mlango Mdogo" unapendwa sana na wasikilizaji kutokana na muziki wenyewe unavyoonesha jinsi watu wanavyofurahi.

Xun

Xun ni ala ya muziki kwa kupulizwa, imekuwa na historia ya milenia nchini China.

Hapo awali, Xun ilikuwa donge la udongo au la mawe lililofungwa kamba kwa ajili ya kuua ndege na wanyama. Baadhi ya madonge yalikuwa na matundu, na yaliporushwa yalikuwa yanalia, baadaye watu walitumia kama ni ala ya muziki.

Hatimaye ala hiyo ilitengenezwa kwa vigae, kwa maumbo ya duara, samaki na tunda la pea. Mwanzoni ala hiyo ilikuwa na tundu moja tu, hadi mwishoni mwa karne ya tatu ala hiyo ilikuwa na matundu sita.

Mwishoni mwa miaka ya 30 ya karne ya 20 wanamuziki walivumbua Xun yenye vitundu tisa. Ala hiyo inafaa kuonesha hisia ya huzuni.

Tokea Xun kuwa na vitundu tisa, ala hiyo imekuwa muhimu katika ala za muziki za Kichina.

Katika miaka ya karibuni wanamuziki waliendeleza ala hiyo kuwa na vitundu kumi. Hivyo eneo lake la sauti limekuwa kubwa zaidi.

Katika historia, Xun ilitumika zaidi katika muziki uliopigwa ndani ya kasri la kifalme. Kuna aina mbili za Xun ambazo zinatofautiana kwa ukubwa. Xun ndogo ina ukubwa kiasi cha yai, sauti yake ni ya juu, na aina nyingine ni kubwa na sauti yake ni nene.

Sheng

Sheng ni ala ya muziki yenye miaka mingi nchini China.

Sheng iligunduliwa mwaka 1978 katika kaburi la zama za kale mkoani Hubei, Sheng hiyo imekuwa na miaka zaidi ya 2400, ambayo ni ya miaka mingi sana katika ugunduzi wa Sheng nchini China.

Sheng inaweza kufuatiliwa mpaka miaka 3000 iliyopita. Hapo mwanzo Sheng ilikuwa ni paipu kadhaa zinapangwa kwa pamoja na kutoa sauti kwa kupuliza vitundu, baadaye watu walitia kilimi, yaani kipande kidogo chembamba kinachotoa sauti kwa kupulizwa.

Sheng ina paipu zaidi ya kumi na kufungwa kwa umbo la kwato la farasi.

Baada ya Jamhuri ya Watu wa China kuasisiwa, wanamuziki walifanya mageuzi na kuifanya ala hiyo kuwa na eneo kubwa la sauti.

Sheng ni ala muhimu katika bendi ya muziki wa Kichina. Kuna aina tatu za Sheng kutokana na ukubwa na tofatu za sauti.

Huluxiao

Huluxiao ni ala ya muziki ya makabila madogo nchini China, na hasa inatumika sana miongoni mwa watu wa kabila la Wadai, Waachang na Wawa.

Huluxiao ilianza kutokea katika Enzi ya Qin (kabla ya mwaka 221).

Huluxiao ni ala yenye umbo la ajabu, kwamba ni tunguri lilinalochomeka paipu tatu tofauti kwa unene, na linachomeka kipande cha mwanzi kwa ajili ya mdomo kupuliza. Kila paipu ina kilimi chake kinachotoa sauti kwa kupulizwa, paipu ya katikati ni nene na ina vitundu saba kwa ajili ya kubadilisha sauti, na paipu mbili pembeni ni kama boksi la kukuza sauti.

Sauti ya Hulusheng ni ndogo lakini ni laini, na inampa msikilizaji hali ya mang'amung'mu.

Ala hiyo imeenea sana miongoni mwa watu wa makabila madogo madogo mkoani Yunnan wakati wanapoimba nyimbo za mapenzi.

Hatimaye, wanamuziki wakafanya mageuzi na kuifanya ala hiyo iwe na sauti kubwa, na sasa ala hiyo hata inapigwa katika muziki wa Kichina unaooneshwa katika nchi za nje.

Filimbi

Filimbi inatengenezwa kwa mwanzi.

Filimbi ina vitundu sita vya kubadilisha sauti na kitundu kimoja cha kutoa sauti kwa kupulizwa na kitundu kingine kwa kuwamba utando.

Ingawa filimbi ni ndogo lakini ina historia ya miaka elfu saba, hadi karne ya 10 filimbi imekuwa ala muhimu katika muziki wa Kichina.

Filimbi inaweza kuonesha hisia mbalimbali na inaweza kuiga sauti mbalimbali za ndege.

Kuna aina nyingi za filimbi, ambazo licha ya ukubwa tofauti, pia kuna filimbi yenye vitundu saba, na kumi na moja.

Filimbi kubwa na ndefu hutumika katika sehemu ya kusini ya China. Kutokana na sauti yake nene filimbi ya aina hiyo hutumika kueleza hisia za mapenzi.

Filimbi fupi hutumika katika sehemu ya kaskazini ya China, kwa muziki wa kuonesha furaha.


1 2 3 4 5 6 7