24: Wanamuziki

Waimbaji

Tang Can

Mwimbaji mashuhuri Bw. Tang Can alizaliwa katika mji wa Zhuzhou, mkoani Hunan, alishinda mtihani wa kuingia kikundi cha nyimbo na ngoma cha taifa na kuwa mwimbaji wa kikundi hicho. Katika mashindano ya 7 ya televisheni ya waimbaji vijana ya China alipata tuzo ya "mwimbaji hodari", na alipata tuzo katika mashindano ya 5 ya muziki wa televisheni ya "Kombe la Konka".

Majira ya mwaka 1998 mafuriko makubwa yalitokea katika baadhi ya sehemu nchini China, licha ya kushiriki kwenye maonesho ya kuchangisha fedha alijigharimia upigaji filamu ya muziki wa televisheni "Mashujaa" kwa kuonesha heshima yake kwa mashujaa waliopamnana na mafuriko.

Mbali na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kikundi alichokuwepo, pia anashiriki kwenye shughuli za kuchangisha fedha kusaidia sehemu maskini na kutoa msaada kwa watoto walioacha masomo kutokana na matatizo ya kiuchumi kwenye familia zao.

Katika tamasha la michezo ya sanaa ya siku kuu ya mwaka mpya lililoandaliwa na televisheni ya taifa, wimbo walioimba Bw. Tang Can na mwenzake bibi Huo Feng ujulikanao kwa "Hali motomoto ya Mwanzoni" ulipendwa sana na wasikilizaji na kutengenezwa kuwa video. Katika tamasha la kukaribisha milenia mpya lililofanyika mwaka 2000, waliimba tena wimbo huo na kupata pongezi kubwa.

Ili kuadhimiisha miaka 50 ya China mpya, wimbo alioimba Bw. Tang Can "Ninalitakia kila la heri taifa langu", ambao ulitungwa na mwanamuziki Bw. Meng Qingyun, ulitengenezwa kuwa MTV, wimbo huo ulipendwa na watu wengi, wimbo huo uliimbwa pia katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya China mpya zilizoandaliwa na vituo vya televisheni vikiwemo vya mikoa ya Hunan, Hubei, Zhejiang na mji ya Shanghai.

Wimbo wa "Ninalitakia kila la heri taifa langu" ulipata tuzo ya wimbo bora na kupata tuzo ya dhahabu ya muziki wa televisheni.

Mwaka 2000 Bw. Tang Can aliimba wimbo uliotungwa na mwanamuziki Fu Ke "Furaha Milele" katika kipindi cha "Wimbo wa Wiki" cha Televisheni ya taifa, ambao wimbo huo wa kienyeji uliimbwa kwa mtindo wa kisasa na kupendwa na watu wengi. Hapo baadaye Bw. Tang Can aliimba wimbo mwingine "Kwetu Maridadi", ambapo umepongezwa sana na watu.

Mwaka 2001, Bw. Tang Can alipata tuzo ya dhahabu ya waimbaji wanaopendwa na wasikilizaji katika mashindano ya kwanza yaliyoandaliwa na idara kuu ya utangazaji ya China.

Yan Weiwen

Bw. Yan Weiwen ni mwimbaji wa sauti ya juu ya kiume ya kikundi cha nyimbo na ngoma cha idara kuu ya siasa ya jeshi, mwanachama wa jumuiya ya waimbaji ya China, mwimbaji wa ngazi ya kwanza anayepata kiunua mgongo maalumu cha serikali.

Bw. Yan Weiwen alijifunza uimbaji kutoka kwa profesa Jin Tielin, tena anajifunza ubora wa waimbaji mbalimbali. Sauti yake ni nzito na kupendeza, sasa amekuwa mwimbaji hodari na kupendwa na watu

Bw. Yan Weiwen ametengeneza mkusanyiko wa nyimbo alizoimba na aliimba nyimbo kwa ajili ya makumi ya filamu zikiwemo za "Mfalme wa mwisho" na "Kikosi cha msalaba mwekundu". Aliiwakilisha China kutembelea nchi na sehemu zaidi ya 20 zikiwemo Marekani, Japan, Canada, Ufaransa, Ujerumani na Italia, ambapo maonesho yake yalipendwa sana na watu wa huko.

Bw. Yan Weiwen alipata tuzo mara nyingi katika mashindano ya uimbaji ya taifa na ya jeshi, zikiwani pamoja na tuzo ya nafasi ya kwanza ya uimbaji wa jadi wa mashindano ya tatu ya waimbaji vijana ya China yaliyofanyika mwaka 1988, tuzo ya ngazi ya kwanza katika maonesho ya sanaa ya jeshi yaliyofanyika mwaka 1989.

Yang Hongji

Bw. Yang Hongji ni mwimbaji mashuhuri wa China, mwanachama wa jumuiya ya wanamuziki ya China na mwanachama wa jumuiya ya wanamichezo ya opera ya China.

Bw. Yang Hongji alizaliwa katika mji wa Dalian mkoani Liaoning. Alipenda kuimba nyimbo tangu utotoni mwake, mwaka 1959 alijiunga na kikundi cha nyimbo na ngoma cha Dalian na alifaulu mtihani wa kujiunga na kikundi cha michezo ya opera cha idara kuu ya siasa ya jeshi mwaka 1962.

Bw. Yang Hongji alijifunza mwenyewe nadharia ya muziki anayopaswa kusoma mwanafunzi wa chuo cha muziki zikiwa ni pamoja na upigaji wa piano, elimu ya harmonic , mazoezi ya kuimba na kusikiliza pamoja na lugha ya Kitaliana. Vitu hivyo vimemsaida sana kupata mafanikio makubwa.

Mwaka 1979 mwongozaji mashuhuri wa bendi Bw. Seiji Ozawa wa Japan alifika China na kuonesha muziki wa Beethoven Symphony No. 9 kwa kushirikiana na bendi ya taifa ya China. Miongoni mwa makumi ya waimbaji nchini China, Bw. Yang Hongji aliteuliwa, uimbaji wake katika maonesho ulisifiwa na Bw. Seiji Ozawa. Mwaka 1984 kutokana na kupendekezwa na profesa Shen Xiang mwenye uraia wa Marekani alishirikiana na bendi ya Hong Kong na mwongozaji bendi Bw. Mo Yongxi aliimba nyimbo za zamani zinazojulikana kwa majira (seasons) kwa lugha ya Kingereza. Hususan ni kuwa katika mwaka 1998 alikuwa mhusika Qu Yuan katika mchezo wa opera aliotunga mwanamuziki Shi Guangnan unaojulikana kwa "Quyuan" na kupata mafanikio.

Bw.Yang Hongji alipata tuzo ya "Maua ya Plum" ya michezo ya opera ya taifa na tuzo kubwa "Wenhua" ya baraza la serikali. Na aliimba nyimbo za filamu za sinema makumi kadhaa zikiwemo "Hadithi ya Nchi Tatu" na "Kwa Heri Moscow".  

Lu Jihong

Baada ya kumaliza masomo yake katika chuo cha muziki cha Xian mwaka 1982, Bw. Lu Jihong alikuwa mwalimu wa muziki katika shule ya ualimu ya Lanzhou, alihamishwa katika kikundi cha nyimbo na ngoma cha Gansu mwaka 1985, na alijiunga na kikundi cha nyimbo na ngoma cha jeshi la baharini mwaka 1989.

Bw. Lu Jihong alipata nafasi ya kwanza mara tatu katika mashindano ya uimbaji ya mkoa wa Gansu, na alitapa nafasi ya pili katika mashindano ya uimbaji wa jadi ya waimbaji vijana ya China. Mwaka 1995 alipata tuzo ya dhahabu ya serikali katika mashidano ya nyimbo mpya ya utangazaji.

Katika miaka ya karibuni, licha ya kupata tuzo nyingi Bw. Lu Jihong aliimba nyimbo kwa ajili ya filamu zikiwemo "Majemedari wa Ukoo wa Yang" na "Kurejea Sichuan". Uimbaji wake umejaa hisia na uhamasa unaonesha ilivyo mtindo wa uimbaji wa makabila mbalimbali. Alikuwa mhusika katika opera ya "Marijani nyekundu", na kushiriki tamasha la uimbaji la Televisheni ya taifa na mikoa.

Mwaka 2001 katika mashindano ya muziki wa MTV ya Televisheni, "Wimbo wa China kusonga mbele" alioimba pamoja na wenzake wengine wawili kwa pamoja ulipata tuzo ya dhahabu.

Bw. Lu Jihong akiwakilisha China na jeshi alitembelea Ujerumani, Urusi, Philippines, Thailand na Marekani na kupendwa na watu wa huko.

Liao Changyong

Bw. Liao Changyong ni mmoja wa waimbaji wachache wanaofanya maonesho katika jukwaa la kimataifa. Yeye alijifunza uimbaji kutoka kwa mwalimu Zhou Xiaoyan na mwimbaji wa kiume wa sauti ya juu Bw. Luo Wei, mwaka 1995 alihitimu masomo yake na kupata shahada ya pili katika chuo cha muziki cha Shanghai.

Katika miaka ya karibuni Bw. Liao Changyong alipata tuzo nyingi kubwa za mashindano ya uimbaji duniani yakiwemo mashindano International Toulouse Singing, Placido Domingo Opera World na Queen Songja International Music.

Katika miaka ya karibuni Liao Changyong alialikwa Bw. Placido Domingo kushirikiana naye kufanya maonesho katika tamasha ya muziki ya mwaka mpya huko Tokyo. Muda si mrefu uliopita Bw. Liao Changyong aliimba upya opera ya Maria Stuarda kwenye ukumbi wa Carnegie, uimbaji wake ulipendwa na wasikilizaji wanaopenda kutoa ukosoaji kuhusu waimbaji.

Akiwa mwanafunzi anayependwa sana na mwalimu wake Bw. Domingo, alialikwa na mwalimu huyo kufanya maonesho katika sehemu nyingi duniani. Mwaka 2001 alifanya ushirikiano tena na Bw. Domingo kuimba opera ya Offenbach. Mwaka 2002 Bw. Domingo alimwalika tena kufanya maonesho katika sherehe ya kuadhimisha miaka 10 ya mashindano ya opera ya kimataifa ya Domingo.

Hivi sasa, Bw. Liao Changyong ni profesa wa chuo cha muziki cha Shanghai na kuwa mkurugenzi wa kitivo cha uimbaji.

Guo Lanying

Bibi Guo Lanying ni mwimbaji maarufu sana nchini China. Alizaliwa mwezi Desemba mwaka 1930 katika ukoo wenye matatizo ya kiuchumi mkoani Shaxi. Alipokuwa na umri wa miaka 6 alikwenda kujifunza uimbaji wa opera ya Zhonglubangzi, na alianza kufanya maonesho alipokuwa na umri wa miaka 7. Opera za jadi alizoimba ni zaidi ya 100, na alianza kujulikana nchini.

Katika majira ya Autumn mwaka 1946 aliondoka katika kikundi cha Opera ya Zhangjiakou na kushiriki kwenye kikundi cha wasanii cha Lianda kilichoko sehemu ya kaskazini ya China na kuanza kuimba opera za kisasa.

Mwaka 1947 bibi Guo Lanying alikuwa akisoma katika idara ya opera ya chuo kikuu cha Lianda huku akishiriki kwenye maonesho. Mwezi Agosti mwaka 1948 alijiunga na kikundi cha kwanza cha sanaa cha chuo kikuu hicho, ambapo maonesho yake yalipendwa na watu. Mwezi Aprili mwaka 1949 alishiriki kwenye ujumbe wa vijana wa China na kufanya maonesho katika tamasha la 2 la kimataifa la amani na urafiki la wanafunzi vijana huko Hungary na kupata tuzo.

Mwaka 1949 baada ya kuasisiwa kwa China mpya, bibi Guo Lanying alikuwa mhusika katika vikundi vya michezo ya opera, na kuwa mjumbe wa shirikisho la nne la utamaduni la taifa, aliimba opera nyingi maarufu na kuwa mwimbaji aliyependwa na watu wengi. Bibi Guo Lanying alishiriki kwenye ujumbe wa China na kutembelea nchi kiasi cha 20 zikiwemo Urusi, Romania, Poland, iliyokuwa inaitwa Czechoslovakia, Yugoslavia, Italia na Japan.

Bibi Gu Lanying aliacha kuimba kwenye jukwaa la muziki mwaka 1982 na kuwa mwalimu wa chuo cha muziki cha China. Mwaka 1986 alianzisha shule ya sanaa ya Guo Lanying huko Guangdong na kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo. Mwaka 1989 alipata tuzo ya sahani ya dhahabu kwenye mashindano ya kwanza ya taifa. Sauti ya Guo Lanying ni nyororo na pana. Alipokuwa msichana alipewa mafunzo makali ya opera, hivyo ana msingi madhubuti wa sanaa. Nyimbo zake zinazopendeza zaidi ni pamoja na "wimbo wa uhuru wa wanawake", "Shangazi Wang anataka amani" na "Mito na milima" ya opera ya Liu Hulan.

Zhang Ye

Bibi Zhang Ye alizaliwa mkoa wa Hunan, hivi sasa yeye ni mwimbaji hodari wa nyimbo za jadi za China. Alimaliza masomo yake mwaka 1991 katika chuo cha muziki cha China, mwaka 1995 alipata shahada ya pili, sasa yeye ni mwalimu kijana wa uimbaji katika chuo cha muziki cha China.

Mwaka 1988 Zhang Ye alichukua nafasi ya tatu katika mashindano ya taifa ya televisheni ya waimbaji vijana na alipata tuzo ya dhahabu ya mashindano ya waimbaji hodari ya taifa. Tokea mwaka 1980 hadi mwaka 1995 alipata tuzo nyingi ikiwa ni pamoja na medali ya fedha katika mashindano ya 4 ya taifa ya muziki wa MTV ya China na tuzo ya medali ya dhahabu ya mashindano ya muziki wa MTV ya kombe la Konka.

Katika masomo na maonesho yake Zhang Ye alikuwa mhusika mkuu katika opera nyingi, vilevile aliimba nyimbo nyingi kwa ajili ya filamu za sinema. Aidha, alifanya maonesho katika Uingereza, Ufaransa, Uswisi, Ujerumani, Sweden, Ubelgiji, Luxembourg, Japan na nchi za Asia ya kusini mashariki.

Bibi Zhang Ye anafaa kuimba nyimbo za jadi za mitindo mbalimbali, sauti yake ni nyororo, tulivu na wazi. Kuna waelezaji wa muziki ambao walisema kuwa sauti ya nyimbo ya bibi Zhang Ye ni kama maji ya theluji ya mlimani, safi na tamu.

Wu Bixia

Bibi Wu Bixia ni mwimbaji mwenye sauti ya juu ya mtindo wa nchi za magharibi. Alizaliwa mkoani Hunan na alipokuwa na umri wa miaka 12 alianza kufanya maonesho ya uimbaji. Kutokana na kipaji chake na kufanya mazoezi kwa bidii anaweza kuimba nyimbo za jadi za China pamoja na nyimbo za nchi za magharibi.

Bibi Wu Bixia alipata tuzo nyingi zikiwa ni pamoja na tuzo ya fedha katika mashindano ya uimbaji yaliyoandaliwa na jumuiya ya wanamuziki ya China na wizara ya utamaduni ya China kwa pamoja mwaka 1993, tuzo ya nafasi ya kwanza ya uimbaji wa jadi katika mashindano ya uimbaji ya taifa mwaka 1996, tuzo ya nafasi ya kwanza katika mashindano ya uimbaji ya kimataifa yaliyofanyika nchini China. Tuzo ya nafasi ya kwanza ya mashindano ya uimbaji ya kimataifa yaliyofanyika huko Bicbao nchini Hispania na tuzo ya nafasi ya pili katika mashindano ya uimbaji ya kimataifa ya Tchaikovsky, ambayo yanachukuliwa kuwa ni mashindano ya "Olimpiki" ya waimbaji duniani.

Toka mwaka 2000 bibi Wu Bixia alifanya maonesho yake ya uimbaji katika Beijing, Hunan, na Singapore, licha ya hayo alifanya ushirikiano na bendi za nchini na duniani katika maonesho ya muziki. Mwezi Desemba mwaka 2001 kutokana na mwaliko wa kamati ya maandalizi ya uimbaji wa kimataifa na jumba la opera ya Arriaga la Hispania alikuwa mhusika mkuu wa kike katika opera ya Rigoletto.

Mafanikio ya uimbaji ya bibi Wu Bixia yamefuatiliwa na vyombo vya habari vya China na duniani, CCTV ilitengenezesha video ya uimbaji wake, magazeti ya Hispania yalimsifu kuwa na "Sauti iliyotoka mbinguni", vyombo vya habari vya Russia vilimsifu kuwa ni "malaika mwimbaji aliyetoka mashariki".

Cheng Zhi

Bw. Cheng Zhi ni mwimbaji wa sauti ya juu, yeye ni mwanachama wa jumuiya ya wanamuziki ya China na mwimbaji wa ngazi ya kwanza wa kikundi cha nyimbo na ngoma cha idara ya kuu ya siasa ya jeshi. Alizaliwa mwaka 1946, aliingia katika kikundi hicho cha nyimbo na ngoma mwaka 1965, alihitimu masomo yake katika chuo cha muziki cha taifa.

Maneno katika nyimbo alizoimba yanasikika vizuri, sauti yake ni madhubuti na wazi. Anafahamu sana uimbaji wa jadi wa Italia, vilevile anaweza kuimba vizuri nyimbo za jadi za China. Alikuwa mhusika mkuu katika opera ya "Shangshi" iliyotungwa na mtunzi hayati Shi Guangnan na alisifiwa na wataalamu wa nchini na wa nchi za nje.

Mmoja wa waimbaji mashuhuri wa kike duniani ambaye ni kiongozi wa kundi la opera ya New York, Marekani bibi Bevery Bechi alimsifu kuwa ni "mmoja wa waimbaji wachache sana wa sauti ya juu na ni mwimbaji wa mtindo wa kweli wa Italia". Katika miaka ya karibuni Bw. Cheng Zhi alifanya maonesho mara nyingi katika sehemu mbalimbali duniani akiwa msanii wa China, vilevile alifanya maonesho ya uimbaji katika miji mingi ambayo ni pamoja na Beijing, Shanghai, Guangzhou, Shenzhen na Hong Kong.

Song Zuying

Bibi Song Zuying (1966--- ) ni mmoja wa waimbaji vijana hodari nchini China. Alizaliwa tarehe 27 mwezi Juni mwaka 1966 katika kijiji cha wa kabila la wamiao chenye koo tatu mkoani Hunan. Mwezi Julai mwaka 1981 bibi Song Zhuying alimaliza masomo yake katika shule ya sekondari na kuchaguliwa na kikundi cha michezo ya opera cha wilaya. Baada ya muda usiotimia mwaka mmoja alishinda mtihani wa kuingia katika kitivo cha nyimbo na ngoma cha chuo cha makabila madogo cha taifa ambapo alimaliza masomo yake mwaka 1987. Mwezi Oktoba mwaka 1988 katika mashindano ya taifa ya "kombe la Jinlong" bibi Song Zuying alipata tuzo ya dhahabu kwa wimbo alioimba wa "kaka usiondoke". Mwaka 1991 alihamishwa katika kikundi cha nyimbo na ngoma cha jeshi la baharini, sasa yeye ni mwimbaji wa ngazi ya kwanza wa taifa na kupewa kiinua mgongo cha serikali.

Sauti ya bibi Song Zuying ni nyororo, tamu na pana. Mizizi yake ya sanaa inaota katika udongo wa uimbaji wa nyimbo za jadi ya China na kuchanganya mtindo wa uimbaji wa nchi za magharibi ambavyo vimekuwa umaalumu wake. Nyimbo za kichina alizoimba ambazo ni pamoja na "Kikapu cha Mwanzi", "Dada shupavu" na "Maisha Mazuri" zinapendwa na wachina nchini na nchi za nje.

Mwaka 2000 alipata "Tuzo Kubwa ya Nyimbo za Jadi za Wachina" mwaka 2002 alifanya maonesho ya muziki huko Sydney Opera House, na mwaka 2003 alifanya maonesho ya uimbaji wa solo kwenye Golden Concert Hall.

Jiang Dawei

Jiang Dawei (1947---): Mwimbaji mashuhuri nchini China.

Bw. Jiang Dawei alizaliwa mwaka 1947 katika mji wa Tianjin. Tokea utotoni mwake alipenda muziki na uchoraji. Mwaka 1970 alijiunga na kikundi cha wasanii cha polisi wa misitu. Mwaka 1975 alikuwa mwimbaji wa solo katika kikundi cha nyimbo na ngoma za jadi cha taifa, hapo baadaye alikuwa kiongozi wa kikundi hicho na kiongozi wa bendi ya muziki mwepesi ya China.

Katika miaka mingi iliyopita aliimba nyimbo zaidi ya 1,000 na aliimba nyimbo kwa ajili ya filamu zaidi ya 100 ambazo ni pamoja na "Mahali Panapochanua Maua ya Mipichi" na "Maua ya Peony". Bw. Jiang Dawei amewahi kufanya maonesho katika Marekani, Canada, Japan, Ujerumani, Singapore na Thailand.

Nyimbo alizoimba na kupendwa na watu wengi ni pamoja na "Mahali Panapochanua Maua ya Mipichi", "Wimbo wa Peony" na "Nauliza Njia Iko Wapi".

Zhou Xiaoyan

Zhou Xiaoyan (1918---) : Mwimbaji wa sauti ya juu ya mtindo wa jadi wa nchi za magharibi, mwalimu wa uimbaji na profesa wa chuo cha muziki cha Shanghai. Bibi Zhou Xiaoyan alizaliwa Mwaka 1918 katika ukoo wa wanaviwanda na wafanya-biashara mjini Wuhan. Baba wa Zhou Xiaoyan alikuwa mwanakiwanda aliyependa sana muziki, kutokana na athari ya baba yake, Zhou Xiaoyan alianza kupenda muziki tokea utotoni mwake.

Mwezi Septemba mwaka 1935 Zhou Xiaoyan alishinda mtihani na kuandikishwa na shule ya muziki ya Guoli mjini Shanghai. Mwaka 1937 ilipolipuka vita ya kupambana na mashambulizi ya Japan, Bibi Zhou Xiaoyan aliacha masomo na kurejea kwao.

Mwishoni mwa mwaka 1938 bibi Zhou Xiaoyan alifika Paris na kujifunza uimbaji katika chuo cha muziki cha Urusi cha Paris. Mwezi Oktoba mwaka 1945 bibi Zhou Xiaoyan alifanya maonesho ya uimbaji kwenye jumba la opera ya taifa mjini Paris ambayo yaliwashangaza wasikilizaji wa Ufaransa. Hapo baadaye alialikwa kwenda Czech kushiriki tamasha la muziki lililojulikana kwa jina la "Spring ya prague", ambapo alisifiwa kuwa ni "chiriku wa China".

Mwezi Oktoba mwaka 1947 bibi Zhou Xiaoyan alirejea nchini China, wakati ule China ilikuwa chini ya utawala wa serikali ya chama cha Guomindang ambapo watu wa China waliishi maisha yenye shida kubwa. Mwaka 1949 China mpya iliasisiwa, bibi Zhou Xiaoyan aliajiriwa kuwa mwalimu wa uimbaji wa chuo cha muziki cha Shanghai.

Miaka kumi ya mapinduzi ya utamaduni ni kipindi chenye giza nene kabisa katika maisha ya bibi Zhou Xiaoyan, lakini upendo wake kwa muziki ulimfanya awe shupavu, mwimbaji maarufu wa sauti ya juu anayesifiwa kuwa mwimbaji wa kiwango cha kimataifa Bw. Wei Song ni mwanafunzi aliyefundishwa naye wakati ule.

Baada ya kumalizika kwa mapinduzi ya utamaduni, bibi Zhou Xiaoyan alianza tena kufundisha. Mwaka 1984 wanafunzi wake wanne walipata tuzo tatu za dhahabu na tuzo moja ya fedha katika mashindano ya uimbaji ya kimataifa yaliyofanyika huko Vienna. Mafanikio yao yaliwashangaza wanamuziki wa kimataifa.

Ili kustawisha uimbaji wa opera nchini China na kuimarisha maingiliano na ushirikiano wa utamaduni wa muziki wa kimataifa, mwezi May mwaka 1988 bibi Zhou Xiaoyan alianzisha kituo cha opera cha Zhou Xiaoyan katika chuo cha muziki cha Shanghai.

Katika miaka zaidi ya 50 iliyopita, waimbaji walioandaliwa na bibi Zhou Xiaoyan waliipatia China heshima kubwa. Baadhi ya wanafunzi wake wamekuwa waimbaji wa makundi ya Metropolitan Opera na San Francisco Opera nchini Marekani.

Hu Songhua

Hu Songhua (1930---): Mwimbaji mashuhuri wa China

Mwaka 1930 Bw. Hu Songhua alizaliwa katika ukoo wa watu wa kabila la waman. Alijulikana alipokuwa kijana kutokana na nyimbo alizoimba za "Senjidema" na "wimbo wa mavuno makubwa". Alianza kuwa mwimbaji wa kikundi cha nyimbo na ngoma za jadi cha taifa mwaka 1952.

Toka zamani sana Bw. Hu Songhua alivutiwa sana na nyimbo za makabila madogo madogo. Mwaka 1952 mchezo mkubwa wa ngoma "mashariki ni kwekundu" ulihitaji wimbo mmoja wa kabila la wamongolia, Bw. Hu Songhua alikabidhiwa jukumu hilo kutokana na kuwa anafahamu sana maisha ya watu wa kabila hilo. Hadi leo wasikilizaji bado hawawezi kusahau wimbo alioimba unaojulikana kwa "wimbo wa sifa".

Bw. Hu Songhua aliwahi kuwa mhusika mkuu Asihaer katika opera ya "Aiguli" na mhusika mkuu wa kiume Ahe katika filamu ya muziki "Asima". Aidha, aliimba nyimbo kwa ajili ya filamu za sinema karibu 30.

Mwaka 1992 Bw. Hu Songhua alishirikisha watu kupiga filamu 12 za nyimbo. Yeye mwenyewe alikuwa mwongozaji, msimamizi na mwimbaji mkuu, filamu hizo zinazoonesha sanaa za jadi za makabila madogo madogo zilipendwa na watu wengi.

Katika miaka mingi iliyopita, Bw. Hu Songhua alikwenda kukusanya nyimbo za jadi katika makabila zaidi ya 40, na amejulikana kutokana na uimbaji wake wenye hisia wazi na sauti nzuri.


1 2 3 4 5