24: Wanamuziki

Wapiga Muziki

Wang Ciheng

Bw. Wang Ciheng ni mpigaji mashuhuri wa filimbi nchini China. Hivi sasa yeye ni mwanachama wa jumuiya ya wanamuziki ya China, jumuiya ya muziki wa orchestra ya China na mpiga ala za muziki wa bendi ya ala za muziki za jadi ya taifa.

Bw. Wang Ciheng alizaliwa mwaka 1959 katika mji wa Hangzhou mkoani Zejiang. Mwaka 1980 alijifunza upigaji wa filimbi katika chuo cha muziki cha taifa. Mwaka 1984 alihitimu masomo katika chuo cha muziki cha taifa akawa mpiga filimbi katika bendi ya ala za muziki ya taifa. Alifundishwa na walimu mashuhuri wa sehemu za kaskazini na kusini, hivyo ustadi wake wa upigaji filimbi ni kuunganisha umaalumu wa sehemu hizo mbili.

Muziki wa filimbi aliopiga unapendeza watu sana kutokana na sauti ya wazi, ya juu na yenye uchangamfu. Alipiga filimbi katika maonesho mengi makubwa ya muziki na alisifiwa na wanamuziki mashuhuri.

Uhodari wake katika upigaji filimbi ulimfanya apate tuzo mara nyingi katika mashindano ya muziki ya nchini na nchi za nje. Mwaka 1982 alipata tuzo ya ngazi ya tatu ya chuo cha muziki cha taifa, mwaka 1987 alipata tuzo ya ngazi ya kwanza katika mashindano ya kwanza ya muziki wa Guangdong ya taifa.

Mwaka 1990 Bw. Wang Ciheng alifanya maonesho ya upigaji filimbi kwenye ukumbi wa muziki wa Beijing na alisifiwa na wanamuziki wakubwa nchini China. Bw. Wang Ciheng aliiwakilisha China mara nyingi kutembelea Austria, Ufaransa, Ujerumani na Marekani, ambapo maonesho yake yaliwavutia watu wengi.

Bw. Wang Ciheng anatilia maanani sana kujifunza elimu ya utamaduni, hana ubaguzi juu ya vikundi vya sanaa vyenye mitindo mbalimbali, kitu anachofikiri ni namna ya kuimarisha umaalumu wa upigaji filimbi.

Sheng Zhongguo

"Mwanamuziki mkubwa", "Mpigaji wa fidla anayevutia zaidi" na "Menuhin wa China", hizo ni sifa anazopewa Sheng Zhongguo na wanamuziki wakubwa duniani. Bw. Sheng Zhongguo ni mpigaji fidla (violin) wa ngazi ya taifa katika bendi ya symphony ya China na pia ni mmoja wa wapigaji fidla wa kwanza walioipatia heshima China duniani.

Bw. Sheng Zhongguo alizaliwa katika ukoo wa wanamuziki, wazazi wake ni wanamuziki, ambao watoto wao 10 kati ya watoto 11 ni wanamuziki, na watoto wao 9 ni wapiga fidla. Sheng Zhongguo ni mtoto wao wa kwanza, alizaliwa mwaka 1941.

Sheng Zhongguo alijifunza kupiga fidla kutoka kwa baba yake alipokuwa na umri wa miaka mitano, na alifanya maonesho ya kupiga fidla miaka miwili baada ya hapo. Alipokuwa na umri wa miaka 9 katika siku yake ya kuzaliwa Radio ya Wuhan ilirekodi muziki aliopiga Sheng Zhongguo na kutangazwa katika vipindi vyake, alisifiwa sana na wasikilizaji. Mwaka 1954 alisoma katika sekondari inayoendeshwa na chuo cha muziki cha taifa, katika maonesho ya muziki ya kuadhimisha miaka 200 tangu azaliwe Mozart Sheng Zhongguo alipiga fidla katika bendi iliyoongozwa na Li Delun.

Mwaka 1960, Bw. Sheng Zhongguo aliteuliwa kwenda kusoma kwenye shule ya muziki ya Tchaikovsky Conservatory mjini Moscow, ambapo alishiriki kwenye mashindano ya fidla ya kimataifa ya Tchaikovsky ya ngazi ya Olimpiki ya muziki duniani, alipata tuzo ya heshima, na kuwa mmoja wa wapiga fidla kwanza wa China waliopata tuzo katika mashindano ya kimataifa.

Mwaka 1964 Bw. Sheng Zhongguo alirejea nchini akawa mwanamuziki mashuhuri katika majukwaa ya muziki nchini na katika nchi za nje. Baada ya mwaka 1976 kila mwaka alifanya maonesho zaidi ya 100 katika sehemu mbalimbali duniani na kuwa mwanamuziki anayependwa sana na watu.

Toka miaka ya 80, Bw. Sheng Zhongguo alifanya maonesho mengi katika nchi mbalimbali duniani. Mwaka 1980 alifanya maonesho 12 ya muziki katika miji 6 nchini Australia, ambayo yalikuwa mnara katika historia ya maingiliano ya utamaduni kati ya China na Australia.

Toka mwaka 1987 Sheng Zhonguo kila mwaka alikwenda kufanya maonesho nchini Japan, alitoa sehemu fulani ya pato lake katika mfuko wa fedha za tiba za kusaidia wanafunzi wa nchi mbalimbali waliosoma nchini Japan, na serikali ya Japan ilimtunukia sifa ya "Balozi wa Utamaduni". Kutokana na mchango aliotoa katika maingiliano ya utamaduni kati ya China na Japan, mwaka 1999 alipata tuzo iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya serikali ya Japan.

Sheng Zhongguo alisaini mikataba mingi ya maonesho na nchi za nje, shughuli za maonesho yake zimetoa mchango mkubwa kwa maingiliano ya utamaduni ya dunia. Mbali na hayo, alikwenda mara kwa mara kutoa mihadhara katika vyuo mbalimbali nchini ili kuhimiza maendeleo ya shughuli za muziki nchini.

Hivi sasa yeye ni mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa, mjumbe wa kamati kuu ya umoja wa demokrasia, mratibu wa jumuiya ya wanamuziki ya China.

Tang Junqiao

Bibi. Tang Junqiao ni mpigaji filimbi kijana nchini China, hivi sasa yeye ni mpigaji filimbi wa kwanza wa bendi ya ala za muziki za jadi ya Shanghai. Tang Junqiao alijifunza kupiga filimbi kutoka kwa baba yake alipokuwa mtoto ambapo alipata mara kadhaa tuzo ya kwanza katika mashindano ya muziki ya vijana na watoto. Alipokuwa na umri wa miaka 16 alifanya maonesho ya upigaji filimbi wa solo. Hapo baadaye alijiunga na chuo cha muziki cha Shanghai. Mwaka 1966 bibi Tang Junqiao aliingia katika bendi ya ala za muziki wa jadi ya Shanghai na kuwa mpigaji filimbi wa kwanza wa bendi hiyo.

Bibi Tang Junqiao mwenye ustadi mkubwa wa kupiga filimbi, anashiriki mara kwa mara maonesho makubwa ya muziki na michezo ya sanaa ya televisheni yakiwemo "Maonesho ya muziki ya uchangishaji fedha ya milenia ya Hong Kong", "Maonesho ya muziki ya mwaka mpya mwaka 2000 ya Shanghai" na "Maonesho ya muziki ya Spring mwaka 2001, Shanghai".

Bibi Tang Junqiao amefuatiliwa na wanamuziki wa kimataifa, alialikwa kupiga filimbi kwa kushirikiana na Bw. Ma Youyou ambaye ni mpigaji maarufu wa fidla kubwa duniani katika kituo cha sanaa cha Babiken, na alisifiwa na watu wengi.

Katika sikukuu ya Spring ya China mwaka 2001 bibi Tang Junqiao alifuata bendi ya ala za muziki za jadi ya Shanghai kufanya maonesho ya muziki katika Golden Voncert Hall. Mwezi Julai mwaka huo alifanya maonesho ya upigaji filimbi huko Macao kutokana na mwaliko.

Alialikwa mara kwa mara kushiriki kwenye maonesho ya matamasha mengi maarufu yakiwa ni pamoja na tamasha la sanaa ya kimataifa la Osaka nchini Japan, tamasha la muziki la Ufaransa, tamasha la muziki la "Moto Kwenye Maji" mjini London, Tamasha ya muziki ya kimataifa mjini Beijing.

Bibi Tang Junqiao alifanya ushirikano mara kwa mara na bendi nyingi mashuhuri zikiwa ni pamoja na bendi ya symphony ya London na bendi ya symphony ya Ufaransa. Mbali na hayo aliwahi kutembela nchi za Marekani, Ujerumani, Japan, Uingereza Austria, Ubelgiji, Ufaransa na Italia.

Xue Wei

Mpiga fidla mashuhuri ambaye alizaliwa mwaka 1963. Alipata mafunzo mazuri na kujenga msingi madhubuti. Mwaka 1981 alipata tuzo katika mashindano ya upigaji fidla ya China, mwaka 1982 alipata tuzo kwenye mashindano ya Carl Flesch International Violin.

Mwaka 1983 Bw. Xue Wei alifaulu mtihani wa kujiunga na chuo cha muziki cha taifa, na miaka miwili baadaye alikwenda kusoma nchini Uingereza. Mwaka 1986 alipata tuzo ya dhahabu ya fidla katika mashindano ya upigaji fidla ya Tchaikovsky mjini Moscow, katika mwaka huohuo alipata tuzo ya mwaka katika mashindano ya upigaji fidla ya vijana nchini Uingereza.

Baada ya kupata tuzo Bw. Xue Wei alisifiwa na pande nyingi. Jarida maarufu nchini Uingereza linalojulikana kwa jina la"Santuri" lilimsifu kuwa na "mmoja wa wapiga fidla hodari sana duniani". Baada ya hapo alifanya maonesho mara kwa mara nchini Uingereza kwa kushirikiana na bendi nyingi kubwa za huko.

Toka mwaka 1989 Bw. Xue Wei aliajiriwa kuwa profesa katika chuo cha muziki cha kifalme cha Uingereza.

Zhao Songting

Zhao Songting alizaliwa mwaka 1924 katika Dongyang, mkoa wa Zejiang, alipenda muziki tangu alipokuwa mtoto, na alianza kujifunza kupiga filimbi alipokuwa na umri wa miaka 9, muda si mrefu alifahamu kupiga ala za muziki za jadi za zeze la kichina, gambusi, zeze lenye nyuzi tatu na Suona. Baadaye alisoma katika chuo cha ualimu na alikuwa mwalimu wa muziki katika shule ya sekondari na chuo cha ualimu. Alipokuwa na umri wa miaka 22 baba yake alimtaka aache muziki na kusoma sheria katika chuo cha sheria cha Shanghai.

Mwaka 1949 Bw. Zhao Songting aliacha masomo ya sheria na alifaulu mtihani wa kujiunga na kikundi cha michezo ya sanaa, ambapo alifahamu upigaji wa ala kadhaa za muziki za nchi za magharibi. Mwaka 1956 aliandikishwa na kikundi cha nyimbo na ngoma za jadi cha mkoa wa Zejiang na alipata mafanikio katika maonesho ya kwanza ya wiki ya muziki ya taifa. Mwaka 1964 alipiga nyimbo mbili alizotunga yeye mwenyewe zinazojulikana kwa jina la "Mandhari ya Mto Wu" na "Kuchuma Majani ya chai" ambayo ilisifiwa sana na wataalamu.

Hapo baadaye Bw. Zhao alianza kufanya utafiti wa kuhusu filimbi, kwa kusaidiwa na kaka yake ambaye ni mtaalamu wa fizikia alifanya majaribio kwa miaka mingi katika maabara, na hatimaye alitoa data za njia ya kisayansi ya utengenezaji wa filimbi.

Bw. Zhao Songting alipata mafanikio katika ufundishaji, na wanafunzi wake wengi wamekuwa watu mashuhuri nchini na katika nchi za nje. Mbali na hayo alifanikiwa katika utafiti wa aina mbili yaani filimbi inayopindika, hivyo urefu wa filimbi umeongezeka lakini upigaji wake bado ni rahisi; pili ni filimbi moja inatumika kama filimbi mbili.

Filimbi ya kichina ni maridadi na yenye sauti nzuri. Bw. Zhao Songting ameunganisha uzoefu wa upigaji filimbi wa sehemu za kusini na kaskazini na kufanya sauti yake kuvutia zaidi. Mbali na hayo ametumia maarifa ya kuvuta hewa ya kupiga ala ya suona katika upigaji wa filimbi.

Bw. Zhao Songting ana maoni ya kutumia ustadi wa muziki kutumikia kueleza maudhui ya muziki, ana wazo la kutumia uzoefu wa sehemu mbalimbali ili mradi vinaongeza uzuri wa muziki.

Ingawa Bw. Zhao alijifunza kupiga filimbi kutoka kwa wapigaji filimbi wala hakufundishwa katika chuo cha muziki, lakini ana elimu nyingi za fasihi ya sayansi, hivyo anaweza kufundisha vizuri, masomo ya darasani yametungwa kwa utaratibu mzuri, kwa hiyo wanafunzi wake wengi wamekuwa mabingwa wakubwa.

Ili kuendeleza muziki wa jadi, Bw. Zhao alikuwa anachapa kazi kwelikweli bila kujali uchovu. Bw. Zhao Songting alifariki mwaka 2001 katika mji wa Hangzhou kutokana na ugonjwa.

Lu Rirong

Bw. Lu Rirong alizaliwa tarehe 1 mwezi Juni mwaka 1933 katika wilaya ya Jun mkoani Hubei. Alishiriki kwenye maonesho ya sanaa mwaka 1945, mwaka 1950 akawa mpiga fidla na zeze la kichina. Baadaye alifaulu mtihani wa kuingia chuo cha sanaa cha kaskazini magharibi, kujifunza zeze la kichina, utungaji muziki na uongozaji wa bendi. Mwaka 1954 alihitimu masomo na kuwa mwalimu katika chuo chake kufundisha upigaji wa zeze la kichina na uongozaji wa bendi. Sasa yeye ni mwalimu anayefundisha wanafunzi waliopata shahada ya pili katika chuo cha muziki cha Xian na kuwa naibu mkurugenzi wa kamati ya muziki wa ala za jadi ya jumuiya ya wanamuziki ya China.

Katika uzoefu wa ufundishaji katika miaka karibu 50 iliyopita Lu Rirong alifanya shughuli mbalimbali za ufundishaji, upigaji ala za muziki, utungaji muziki na uongozaji wa bendi. Alitunga muziki wa aina zaidi ya 150 ya zeze la kichina, muziki wa ala moja zaidi ya 20, muziki wa ala nyingi zaidi ya 20 pamoja na makala ya kitaaluma zaidi ya 10.

Katika ufundishaji wake, Bw. Lu Rirong anaunganisha pamoja ufundishaji, upigaji wa ala za muziki, utungaji muziki na utafiti wa nadharia. Anataka wanafunzi wajiendeleze katika pande mbalimbali. Upigaji wa ala za muziki wake ni wa kupendeza, sauti ya muziki ni nyepesi, wazi na yenye hisia zake. Ustadi wake wa upigaji wa ala za muziki umeendelezwa kwenye msingi wa utamaduni wa muziki wa jadi na sehemu ya Shanxi. Mwaka 1960 katika semina iliyofanyika huko Shanghai kuhusu masomo ya upigaji wa zeze la kichina na gambusi alicheza muziki aliotunga "Muziki wa Mihu" na "Xintianyou" ambayo ilisifiwa na wataalamu kuwa ni uanzishaji wa mtindo na ustadi wa aina mpya.

Msingi wa utungaji muziki wake ni juu ya msingi wa muziki wa jadi wa huko ambao ni kama wenye harufu ya udongo wa uwanda wa juu. Muziki wa aina mbalimbali ya "Mtindo wa Muziki wa Shanxi", "Mtindo wa Muziki wa Wanwan" ni ya mitindo tofauti kubwa ambayo inawaburudisha watu kwa mila na desturi ya wenyeji wa huko.

Umaalumu wake katika kuongoza bendi ni wenye uchangamfu mkubwa na mtiririko wa mfululizo. Muziki mzuri kadha wa kadha uliochezwa na bendi aliyofundisha kwa miaka mingi, ambayo ni bendi ya orchestra ya chuo cha muziki cha Xian, ilisifiwa sana na wanamuziki wa nchini na wa nchi za nje.

Makala alizoandika kuhusu nadharia ya muziki ni pamoja na "Umaalumu na Upigaji wa Muziki wa Zeze ya Mtindo wa Shanxi", "Muziki wa Kale wa Changan unaendea Duniani kwa Mara ya Kwanza" na "Mchango wa Sanaa ya Uchezaji zeze ya Hua Yanjun kwa Ufundishaji wa Ustadi wa Zeze".

Tokea miaka ya 80 alialikwa kufanya maonesho na kufundisha muziki katika nchi nyingi zikiwemo Japan, Ujerumani, Ufaransa na Singapore. Mwaka 1992 alitunukiwa sifa na baraza la serikali ya "mtaalamu aliyetoa mchango mkubwa wa China".

Liu Dehai

Bw. Liu Dehai ni mchezaji maarufu wa ala ya muziki ya gambusi ( lute ) na ni mmoja wa wachezaji hodari waliokomaa mwishoni mwa miaka ya 50 nchini China. Watu humwita kuwa ni bingwa mkubwa wa gambusi, na amejulikana nchini na katika nchi za nje.

Bw. Liu Dehai alizaliwa mkoani Shanghai mwaka 1937. Alipokuwa kijana katika shule ya sekondari alikuwa anapenda sana ala za muziki wa jadi na kuonesha kipaji chake. Mwaka 1950 alianza kujifunza uchezaji wa zeze na filimbi, na alishiriki katika shughuli za bendi ya ala za muziki za jadi ya Radio Shanghai baada ya masomo. Mwaka 1957 alishinda mtihani na kuandikishwa na chuo cha muziki cha taifa na kuanza kujifunza uchezaji wa gambusi.

Uchezaji wake wa gambusi ni wenye ustadi mkubwa, sauti ya gambusi aliyocheza inabadilika sana kutokana na muziki tofauti ambayo inawapa wasikilizaji kumbukumbu nyingi. Uchezaji wake ni kuunganisha ubora wa mabingwa wa sehemu mbalimbali na umeendeleza ustadi wa uchezaji wa gambusi.

Kutokana na msingi wa uchezaji wa jadi wa gambusi, Bw. Liu Dehai alifanya uvumbuzi na mageuzi katika uchezaji kutokana na maudhui ya muziki. Kwa mfano ili kuongeza kasi ya muziki anapocheza gambusi anatumia pia kidole gumba cha mkono wa kushoto ikilinganishwa na uchezaji wa jadi ambao kidole hicho hakitumiki katika uchezaji wa gambusi.

Muziki anaopiga Bw. Li Dehai ni wa aina mbalimbali kutoka muziki wa kale kama vile "Mtego" hadi muziki wa kisasa "Muziki wa Ngoma ya Kabila la Wayi". Muziki anaopiga ni kama anawasimulia watu hadithi ambapo wasikilizaji wanajiona kama wako katika mazingira hayo.

Bw. Li Dehai anarekebisha nyimbo nyingi kuwa muziki wa gambusi ambazo ni pamoja na "Mto Liuyang", "Wageni Kutoka Mbali Msiondoke" na "Dada Wawili wa Mbugani".

Bw. Liu Dehai pia alitunga muziki kadhaa ukiwemo "Swain", "Mzee Mtoto" na "Safari kwa Kwao". Na amepata mafanikio katika kufanya uvumbuzi wa uchezaji wa gambusi na utungaji wa muziki. Tokea mwaka 1978 hadi mwaka 1981, Bw. Liu Dehai alifanya ushirikiano na bendi ya Marekani ya Boston Symphony Orchestra , bendi ya Symphony Orchestra ya Berlin ya magharibi.

Mafunzo makali, uzoefu wa miaka mingi wa kufanya maonesho ya muziki, ufundishaji wanafunzi pamoja na uzoefu wa kimaisha vimemfanya awe mwanamuziki mahiri. Hivi sasa yeye ni profesa katika chuo cha muziki cha taifa na ni mratibu wa kamati ya kudumu na naibu mkurugenzi wa kamati ya sanaa ya maonesho ya jumuiya ya wanamuziki ya China. Aliwahi kufanya maonesho na kufundisha katika nchi na sehemu zaidi ya 30 duniani na ametoa mchango mkubwa katika kuunganisha uchezaji wa gambusi na bendi ya Symphony Orchestra .

Liu Mingyuan

Bw. Liu Mingyuan ni mmoja wa wachezaji hodari kabisa wa ala za muziki za jadi karibu nusu karne iliyopita na ni mchezaji wa ngazi ya juu kabisa katika majukwaa ya muziki ya China na nchi za nje. Bw. Liu Mingyuan ni hodari sana kucheza mazeze ya kichina yanayojulikana kwa "Banhu", "Gaohu", "Erhu", "Zhonghu", "Jinghu" na "Zhuihu". Inasemekana kuwa hakuna mchezaji anayemzidi katika uchezaji wa "Banhu" na "Zhonghu" kwa hivi sasa.

Bw. Liu Mingyuan alizaliwa mjini Tianjin mwaka 1931, alianza kujifunza uchezaji wa "Banhu" na "Jinghu" kutoka kwa mama yake alipokuwa na umri wa miaka 6, na alipokuwa na umri wa miaka 11 alishiriki bendi za "Bailing" na "Minyue" na kujifunza muziki wa filimbi na zeze, na muziki wa Guangdong, opera ya Beijing na Opera ya Hebei. Kati ya mwaka 1947 na mwaka 1952 alikuwa mchezaji wa ala za muziki katika vikundi vya nyimbo na ngoma za "Shengli", "Huanggong" na nyingi nyinginezo. Mwaka 1957 alipata medali ya dhahabu katika mashindano ya muziki ya tamasha ya 6 ya kimataifa ya vijana.

Bw. Liu Mingyuan licha ya kucheza zeze la kichina, yeye pia ni hodari sana kucheza piano na aliwahi kuwa mchezaji wa piano katika muziki wa jazz. Aliwahi kujifunza nyimbo za kabila la wamongolia hivyo anafahamu fika mtindo wa muziki wa kimongolia.

Bw. Li Mingyuan ametoa mchango mkubwa katika mageuzi ya utengenezaji wa mazeze na ufundishaji muziki, alifanikiwa katika utengenezaji wa "Banhu" yenye sauti ya juu na "Zhonghu" yenye sauti ya kati. Toka miaka ya 50 alianza kufundisha wanafunzi na kuwa profesa wa uchezaji wa ala za muziki katika chuo cha muziki cha taifa. Alifariki dunia mwezi Februali mwaka 1996.

Fu Cong

Bw. Fu Cong alizaliwa mjini Shanghai tarehe 10 mwezi Machi mwaka 1934 katika familia ya msanii na mwanaelimu, baba yake alikuwa msomi maarufu, mwana-nadharia wa sanaa na mtafsiri nchini China. Fi Chong alipokuwa na umri wa miaka mitatu au minne aliweza kuhisi mvuto wa muziki na kuonekana kupenda sana muziki. Alianza kujifunza kucheza piano kutoka kwa mwanamuziki wa Italia Bw. Mario Paci alipokuwa na umri wa miaka 7, na alijifunza uchezaji wa piano kutoka kwa bibi Ada Bronstein kutoka Urusi mwaka 1951.

Mwaka 1953 Bw. Fu Chong alishiriki mashindano ya piano akiwa mchezaji pekee wa China katika tamasha ya nne ya kimataifa ya vijana, na alipata tuzo ya ngazi ya tatu. Mwezi Machi mwaka 1955 mashidano ya kimataifa ya 5 ya Chopin yalifanyika mjini Warsaw. Bw. Fu Cong alichukua nafasi ya 3 kwa kupata pointi zinazokaribia sana na pointi za wachezaji waliochukua nafasi ya kwanza na ya pili miongoni mwa wachezaji 74 duniani.

Baada ya mashindano kumalizika, Bw. Fu Cong alibaki nchini Poland kujifunza upigaji wa piano hadi alipomaliza mafunzo mwishoni mwa mwaka 1958. Katika muda huo Bw. Fu Cong alirejea China kupumzika kati ya mwezi Agosti na Oktoba mwaka 1956, mjini Beijing akishirikiana na bendi ya symphony ya Shanghai alicheza muziki wa Mozart. Bw. Fu Cong aliondoka Poland mwezi Desemba mwaka 1958 na kuishi London, Uingereza.

Katika muda wa miaka 20 wa miaka ya 60 hadi 70, Bw. Fu Cong alifanya maonesho ya muziki kiasi cha 2,400; aliwahi kufanya ushirikiano na wanamuziki wengi wa kimataifa wakiwemo Bw. Menuhin, Bw. Barenboim na Bw. Chung Kyung-Wha; Alirekodi sahani za muziki kiasi cha 50; Aliwahi kuwa mwamuzi wa mashidano ya piano ya kimataifa ya Chopin na Elizabeth pamoja na mashindano ya piano yaliyofanyika nchini Norway, Italia, Uswisi, Ureno na nchi za umoja wa Asia ya kusini mashariki. Jarida la the Times lilimsifu kuwa ni "Mwanamuziki mkubwa kabisa wa China kwa hivi sasa".

Mwaka 1976 Bw. Fu Cong alifanya maonesho ya muziki katika chuo cha muziki cha taifa. Baada ya hapo karibu kila mwaka alirejea China kufanya maonesho na ufundishaji mjini Beijing, Shanghai, Xian, Chengdu na Kunming. Licha ya kucheza muziki wa watungaji maarufu wa duniani alikuwa na ushirikiano na bendi ya taifa kucheza muziki wa Beethoven. Uzoefu wake katika mambo ya sanaa na moyo wake wa kufundisha wanafunzi umemfanya aheshimiwe sana na waalimu na wanafunzi wa muziki.

Song Fei

Bibi Song Fei (1969---) ni mchezaji maarufu wa zeze la "Erhu", anafahamu uchezaji wa ala za muziki za aina 13, hivyo anasifiwa kuwa ni "malkia wa ala za muziki za jadi".

Bibi Song Fei alipokuwa na umri wa miaka 7 alifundishwa na baba yake Bw. Song Guosheng ambaye alikuwa profesa wa chuo cha muziki cha Tianjin na ni bingwa wa Erhu. Mwaka 1987 alifaulu mtihani na kusoma katika chuo cha muziki cha taifa. Alihitimu masomo yake mwaka 1991 na kuwa mchezaji wa Erhu katika bendi ya ala za muziki za jadi ya taifa. Mwaka 1998 akiwa mwanafunzi wa shahada ya uzamili alijifunza uimbaji na uchezaji wa ala za muziki za Erhu na kinanda cha kale.

Tokea aliposoma katika shule ya sekondari bibi Song Fei alishiriki mara kwa mara kwenye mashindano ya ala za muziki za jadi nchini na alipata tuzo mara nyingi. Alitembelea sehemu nyingi duniani, hususan wakiwa mwakilishi wa wanamuziki wa China alicheza muziki wa kichina katika Golden Concert Hall ya Vienna.

Katika miaka ya 90 ya karne ya 20 bibi Song Fei akifuata bendi ya wanawake iliyoongozwa na bibi Zheng Xiaoying alifanya maonesho katika vyuo vikuu mbalimbali nchini China. Licha ya hayo wao pia walifanya maonesho katika Ulaya. Safari moja aliongeza muziki mmoja kutokana na matakwa ya wasikilizaji, alipiga muziki wa Flight of the Bumble Bee kwa Erhu, alishangiliwa sana na wasikilizaji wa nchi za magharibi.

Mwaka 1996 bibi Song Fei akishirikiana na wanamuziki wengine 9 wa kike walianzisha bendi ndogo ya ala za muziki za jadi ili kuendeleza muziki wa jadi. Katika sikukuu za Spring za mwaka 1998 na 1999, bibi Song Fei akifuata bendi ya ala za muziki za jadi ya taifa alifanya maonesho mara mbili katika Golden Concert Hall, muziki wa Erhu aliocheza bibi Song Fei uliwasisimua wasikilizaji.

Mwaka 1999 bibi Song Fei alipofika kileleni katika uchezaji Erhu, ghafla alichagua kazi ya kufundisha, akisema kuwa anataka vijana wengi zaidi washiriki katika harakati za kuendeleza uchezaji wa ala za muziki za jadi. Mwaka 2002 bibi Song Fei alifanya maonesho ya uchezaji wa ala za muziki wa solo, alicheza aina 13 za ala za muziki na kufuatiliwa sana na wanamuziki wa nchini.

Muziki uliotungwa na bibi Song Fei na kupendwa na watu wengi ni pamoja na "Mwezi unaoonekana Kwenye Chemchem mbili", "Milio ya ndege Kwenye Mlima" na "Muziki wa Ukuta Mkuu".


1 2 3 4 5