Watu 48 wafariki baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kuanguka Kaskazini mwa Pakistan
Abiria wote 48 waliokuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Kimataifa la Pakistan wamefariki baada ya ndege hiyo kuanguka sehemu ya milima kaskazini mwa nchi hiyo.
Vikosi vya waokoaji vimepata miili yote 48 kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo.
Mwenyekiti wa shirika la PIA Azam Saigol amesema, ndege hiyo aina ya ATR-42 iliyokuwa na watu 48, wakiwemo abiria 42 na wafanyakazi 6, ilikuwa ikielekea Islamabad kutoka uwanja wa ndege wa Chitral Kaskazini. Amesema rubani wa ndege hiyo aliripoti hitilafu ya injini moja, na aliambiwa anaweza kutua pindi barabara ya ndege ikionekana, dakika mbili kabla ya kupoteza mawasiliano, wakati ndege ikiwa maili 35 kutoka uwanja wa ndege wa Islamabad.
Bw. Saigol amekanusha ripoti kuhusu makosa ya kibinadamu, na kusema kuwa chanzo cha ajali hiyo kitajulikana baada ya uchunguzi kukamilika.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |