IGAD yasema itafufua mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yaliyokwama ndani ya miezi miwili
Shirika la maendeleo la kiserikali la nchi za Afrika Mashariki IGAD, limesema mkutano wa ngazi ya juu wa kutafuta suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Sudan Kusini, utafanyika ndani ya miezi miwili. Mjumbe maalum wa IGAD nchini Sudan Kusini Bw Ismail Wahid, amesema shirika hilo litachambua matokeo ya mawasiliano na makundi yote yanayohusika na mgogoro wa Sudan Kusini na kuweka machaguo ya kufufua mazungumzo hayo. Baraza la mawaziri la IGAD litakutana ili kujadili mapendekezo na machaguo yaliyopo, kabla ya kutangaza rasmi siku ya mkutano, mahali pa kufanyika, watakaohudhuria na ajenda zake. Msemaji wa kundi la SPLA-wapinzani Bw William Gatjiah Deng amekaribisha hatua hiyo, lakini amesema mkutano huo wa ngazi ya juu unatakiwa kuangalia kiini cha mambo yaliyokwamisha makubaliano ya amani ya mwaka 2015.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |