Kampeni za kura ya maoni zaanza rasmi Burundi
Kampeni zimeanza rasmi nchini Burundi za kura ya maoni iliokumbwa na mzozo ambayo huenda ikampa fursa rais Pierre Nkuruzinza kuendelea kuhudumu kwa miaka 14 ya ziada.
Tayari kiongozi huyo amehudumu kwa miaka 13 kufikia sasa na wakosoaji wa kiongozi huyo wanasema hapaswi kugombea tena uongozi kwasababu ni kinyume cha sheria.
Dhamira ya kura hii ya maoni ni kuruhusu kuikarabati katiba ili kubadili kipengee cha mihula atakayohudumu rais, iwe miaka saba kila mmoja badala ya mitano hivi sasa.
Na iwapo mageuzi hayo yataidhinishwa, hatua hiyo itaanza kutekelezwa mwaka 2020 hivyo basi kumpa nafasi rais Nkuruzinza kuhudumu hadi mwaka 2034.
Maguezi hayo yanayopendekezwa pia yatatoa fursa ya kuidhinishwa wadhifa wa waziri mkuu na kupunguza idadi ya makamu wa rais kutoka wawili na kuwa mmoja.
Upinzani hatahivyo unasema mageuzi hayo ya katiba yanatishia makubaliano ya amani ya Arusha yaliosaidia kumaliza vita vya kiraia nchini kati ya mwaka 1993 - 2006 yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu.
Vyama 26 vimeruhusiwa kukampeni katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Mei 17, baadhi yao vikionekana kuegemea upande wa chama tawala nchini CNDD FDD.
Siku ya Jumanne, Marekani imeshutumu 'ghasia, unyanyasaji na kutishiwa' kwa watu Burundi wanaoonekana kuipinga kura hiyo ya maoni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |