Pande hasimu Yemen zakubaliana awamu ya kwanza ya uondoaji vikosi Hodeidah
Ofisi ya habari ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa imesema, wajumbe kutoka serikali ya Yemen na waasi wa Houthi wamefanya mazungumzo Jumamosi na Jumapili, ambao wamefikia makubaliano juu ya awamu ya kwanza ya uondoaji vikosi kutoka Hodeidah, mji wa bandari wa Bahari Nyekundu.
Ofisi hiyo imesema baada ya mazungumzo ya muda mrefu, pande zote mbili zimefikia makubaliano ya awamu ya kwanza ya uondoaji vikosi, na awamu ya pili pia imejadiliwa, ambayo viongozi wa pande mbili watajadiliana zaidi. Raundi ijayo ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika ndani ya wiki moja, ili kuhimiza makubaliano ya awamu ya pili yafikiwe.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Bw. Martin Griffths ameondoka kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa hii leo baada ya ziara ya siku moja ambapo alisisitiza tena utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa Stockholm, Disemba mwaka jana.
Kutokana na mpango waliowasilishwa na Bw. Griffths, pande zinazopingana nchini Yemen zimekubali kuondoka mjini humo na kuratibu njia za kuwawezesha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kufikisha nafaka kwenye vinu vya kusaga vilivyoko mjini humo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |