Waziri Mkuu wa Uingereza asema kuna haja ya kurefusha zaidi kifungu cha 50
Waziri Mkuu wa Uingereza Bibi Theresa May ametangaza kuwa Uingereza inahitaji kurefusha zaidi utekelezaji wa kifungu cha 50 cha katiba ya Umoja wa Ulaya, ili kuhakikisha kuwa Uingereza inajitoa Umoja wa Ulaya ikiwa na makubaliano.
Bibi May pia amesema anataka kuongea na kiongozi wa upinzani Jeremy Corbyn, kuona kama anaweza kuwa na pendekezo la kuondoa mkwamo uliopo. Pia amesema anatumai kuwa bunge la Uingereza litakubali makubaliano na Umoja wa Ulaya kabla ya tarehe 22 Mei, na kusema kujitoa na makubaliano ni jambo zuri.
Tangazo la Bibi May limekuja baada ya majadiliano ya saa saba na mawaziri waandamizi kwenye ofisi ya waziri mkuu. Hata hivyo inaonekana kuwa mawaziri wenyewe hawajafikia makubaliano.
Mjini Brussels mwakilishi mkuu wa majadiliano ya Brexit Bw. Michel Barnier amesema kila siku inayopita uwezekano wa Uingereza kujitoa bila makubaliano unaongezeka.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |