Uingereza yatoa masharti ya mazungumzo kwa Umoja wa Ulaya juu ya mkataba mpya wa Brexit
Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Boris Johnson wiki hii aliwasilisha barua kwa mwenyekiti wa Baraza la Ulaya Bw. Donald Tusk, ambayo imetoa masharti rasmi ya mazungumzo juu ya mkataba mpya wa kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Johnson kuwasiliana na Umoja wa Ulaya juu ya Brexit.
Serikali ya Uingereza imetangaza barua hiyo, ikisema Uingereza haikubali "mpango maalumu" kwenye kipindi cha mpito juu ya suala la mpaka wa Ireland Kaskazini. Mpango huo uliokuwepo kwenye mkataba wa awali utaharibu ukamilifu wa mamlaka ya nchi bila ya demokrasia, hivyo lazima ufutwe kwenye mkataba mpya wa Brexit.
Bw. Johnson pia ametoa wito kwa Uingereza na Umoja wa Ulaya zitafute ufumbuzi mbadala mwafaka wenye uvumbuzi, ili kutatua suala la mpaka wa Ireland Kaskazini linalohusiana na Brexit.
Wakati huo huo Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa, mawaziri na maofisa wa Uingereza hawatahudhuria mikutano mingi ya Umoja wa Ulaya kuanzia Septemba 1.
Mawaziri wa Uingereza watahudhuria mikutano mikubwa na ile inayohusisha maslahi muhimu ya nchi hiyo kama usalama na mingine itapuuzwa, hatua inayotoa ishara wazi kuwa Uingereza imedhamiria kihalisi kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Oktoba.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |