Mafuriko yawaua watu 14 Lindi
Watu 14 wameuawa na wengine hawajulikani waliko kufuatia mafuriko katika eneo la Lindi Tanzania. Mashirika yasiyo ya kiserikali tayari yametoa wito wa msaada mkubwa wa kibinadamu. Jumla ya watu 14 wameripitiwa kufariki Dunia Mkoani Lindi, nchini Tanzania kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na idadi hiyo ikitwajwa kuweza kuongezeka kutokana na baadhi ya watu kushindwa kuokolewa, huku msaada mkubwa wa kibinadamu ukihitajika Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema juhudi za vikosi vya uokoaji zinaendelea ambapo watu 1,531 wameokolewa kati ya wakazi 15,000 wanaodaiwa kuathirika na mafuriko hayo.
Zambi amesema hali si nzuri na uokoaji unaendelea katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko.Mafuriko Wilayani Kilwa Mkoani Lindi yametokea kwenye vijiji vya Kilanjelanje, Nanjilinji A, Ruatwe, Njinjo, Nakiu na Nanjilinji B ambavyo vimezingirwa na maji.
Mafuriko hayo yanatokea ikiwa ni siku chache tu kupita tangu kutolewa kwa taarifa na mamlaka ya hali ya hewa (TMA) nchini iliyotoa tahadhari ya kunyesha kwa Mvua kubwa katika baadhi ya Mikoa ikiwemo ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |