Viongozi wa Sudan Kusini wakubaliana kuunda serikali ya muungano
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar wamekubaliana kuunda serikali ya muungano kufikia siku ya Jumamosi kama walivyokubaliana.
Hatua hiyo inafuatia mkutano uliofanyika katika Ikulu katika mji mkuu wa Juba siku ya Alhamisi. Rais Kiir ameahidi kuwalinda viongozi wa upinzani .
Washirika wa bwana Machar walikuwa wanatafuta hakikisho kuhusu usalama wake iwapo atarudi katika mji mkuu wa Juba.
Bwana Kiir alisema kwamba masuala muhimu ambayo hayajasuluhishwa , kama vile jinsi yeye na Machar watakavyogawana mamlaka ni masuala ambayo yanatarajiwa kuangaziwa na kukamilishwa katika siku zijazo.
Bwana Machar amekubali kuchukua wadhfa wake wa zamani kama makamu wa rais wa kwanza na baraza la mawaziri lililopo litavunjwa ili kuruhusu viongozi zaidi wa upinzani.
Kuna matarajio kwamba makubaliano hayo yatamaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka sita ambavyo vimegharimu maisha ya zaidi ya watu 400,000.
Wawili hao waliunda serikali ya muungano ya muda mfupi mara moja 2016 . Ilikuwepo kwa miezi mitatu pekee kabla ya bwana Machar kuondoka Juba huku mapigano yakiendelea.
Kila upande umekuwa ukimshutumu mwenzake. Kundi la Machar linalilaumu kundi la rais Salva Kiir kwa kushindwa kuiongoza nchi na limekuwa likimtaka kiongozi wa taifa hilo changa kujiuzulu.
Kwa upande mwingine, wafuasi wa rais Kiir wanasisitiza kuwa iwapo kutakuwa na mazungumzo yoyote ya kuunda serikali ya muungano, hawatomruhusu Machar awe kiogozi wa Sudan Kusini.
Umoja wa mataifa na Marekani zimetishia kuidhinisha vikwazo dhidi ya watu wa Sudan kusini iwapo hakutofikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi.
Makabiliano hayo yamesababisha vifo vya watu wengi na kusababisha zaidi ya watu milioni moja kukosa makazi.
Mapigano yalianza Juba na kuenea katika maeneo mengine yakiwemo Bor, Jonglei na Bentiu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |