Mwanamume kutoweka na hongo ya polisi Embu, Kenya.
Mwanaume katika Kaunti ya Embu, nchini Kenya, aliwaacha polisi wa trafiki vinywa wazi baada ya kutoweka na mabunda ya noti waliyokuwa yamekusanya kama hongo kutoka kwa wahudumu wa matatu.
Kisa hicho ambacho kimesifiwa na Wakenya mitandaoni kama funzo kwa polisi wafisadi, kilitokea katika kituo cha biashara cha Kathageri kwenye barabara kuu ya Nairobi – Meru.
Dereva aliyeshuhudia kisa hicho anasema kwamba mwanaume huyo alijitokeza kutoka kichakani na kuchukua noti hizo ambazo zilikuwa ndani ya mkoba uliokuwa umefichwa kwenye majani kando ya barabara.
Baada ya kuzichukua aliwapiga chenga maafisa hao na kutorekea kichakani mbio.
Dereva huyo ambaye alikuwa akiendesha gari karibu na mahala pa tukio hilo, alisema kulikuwa na maafisa wawili wa trafiki, mmoja wa kiume na mwingine wa kike.
Nafuu kwa mwanaume huyo ni kwamba polisi hao hawakuwa wamejihami kwa bunduki, bali walikuwa wamebeba tu bakora zao za kawaida.
Wakati wa kisa hicho wahudumu wa matatu na wasafiri walikuwa wakishangilia mwizi huyo akitoweka na kufurahia kwa kuwaibia polisi ambao huwa wanahangaisha wasafiri wakiitisha hongo.
Kutokana na oparesheni kali za makachero wa Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi (EACC), polisi wa trafiki wanaochukua hongo huwa hawaweki rushwa hiyo mfukoni kama zamani bali huficha fedha hizo kwenye mkoba unaowekwa mahali fiche karibu na barabara.
Inasemekana kwamba Afisa wa kiume alijaribu kumkimbiza mwanaume huyo bila mafanikio na alilazimika kukata tamaa na kuanza kurusha matusi akimlaani mwanaume huyo kwa kutoweka na 'jasho' lao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |