Raia wa Ulaya wapigwa marufuku kuingia Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump, ametangaza kuweka zuio kwa raia wa nchi za Ulaya kuingia nchini Marekani ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Katika hotuba yake kwa njia ya Televisheni siku ya Jumatano, amesema safari zote za kutoka Ulaya zitazuiwa kwa siku 30 zijazo.
Kuna visa 1,135 vilivyothibitishwa nchini Marekani na watu 38 wameripotiwa kupoteza maisha.
Trump amesema kuahirishwa kwa safari pia kutahusu "biashara na usafirishaji wa mizigo" kutoka Ulaya kuingia Marekani.
Pia ametangaza kutoa mkopo wa mabilioni ya dola kwa wafanyabiashara wadogo, na kutaka bunge la Congress kupitisha nafuu ya kodi ili kukabiliana na athari za mlipuko wa corona kiuchumi.
Gavana wa jimbo la Washington amepiga marufuku mikusanyiko katika kaunti kadhaa. Jimbo lililo Kaskazini Magharibi ni kiini cha maambukizi nchini Marekani, kukiwa na idadi ya vifo 24 kati ya 38 nchi nzima.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |