Coronavirus: Wafanyakazi wa serikali wapigwa marufuku kusafiri ng'ambo
SERIKALI imepiga marufuku maafisa wake kufanya ziara nje ya nchi isipokuwa tu kwa sababu zenye umuhimu mkubwa.
Kwenye kikao kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kamati ya Kitaifa ya Dharura ya kukabiliana na virusi vya corona katika Ikulu jana, Wakenya wote wanaorejea nchini pamoja na wageni kutoka maeneo yenye hatari zaidi, wameamrishwa kujitenga kwa muda usiopungua siku 14 mfululizo.
Wafanyabiashara na wananchi pia wameshauriwa kutofanya ziara zisizo muhimu hususan katika maeneo yaliyo na hatari zaidi.
Rais pia aliagiza bajeti kufanyiwa mabadiliko katika harakati za kuchukua hatua za kuzuia na kukabiliana na virusi vya corona.
Rais Kenyatta pia aliagiza kuandaliwa kwa mikakati mwafaka ya kulinda watu wenye mapato ya chini na watu wanaokabiliwa na hatari hususan katika mitaa ya mabanda.
Juhudi hizi zitategemea mifumo iliyopo ya kijamii wakiwemo machifu, wasimamizi wa wadi, viongozi wa kidini na wazee wa nyumba kumi kueneza ufahamu na kushirikisha juhudi za kuzuia na kukabiliana na virusi hivyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |