Mwanariadha wa Kenya asema kuahirishwa kwa Olimpiki ni pigo kwa wanariadha wengi
Bingwa wa Olimpiki kutoka Kenya Eliud Kipchoge amesema kwamba, kuahirishwa kwa michezo hiyo iliyokuwa ifanyike jijini Tokyo, Japan kati ya Julai 24 na Agosti 9, 2020, kumeyumbisha ndoto za wanariadha wengi kitaaluma. Amesema ni pigo kubwa kwa baadhi ya wanariadha, hasa wale ambao wamekuwa wakijifua mchana na usiku kwa ajili ya Olimpiki mwaka huu, na kuongeza kuwa olimpiki ni mashindano muhimu sana miongoni mwa wanaridha wote duniani, na kuahirishwa kwa Olimpiki kumeathiri maisha ya wanariadha wengi. Jumanne wiki hii, Olimpiki za Tokyo 2020 ziliahirishwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) hadi mwaka 2021 kutokana na shinikizo lililotolewa na wadau wa Olimpiki. Hii ni mara ya pili kwa michezo hiyo ambayo imekuwapo kwa miaka 124 kuahirishwa. Mara ya kwanza mashindano hayo ambayo pia yalikuwa yafanyike Japan yalifutwa mwaka 1940 kutokana na Vita vya Pili vya Dunia.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |