Nusu ya wafanyakazi duniani waathiriwa na Corona
Shirika la Kazi Duniani (ILO) jana limetoa ripoti ikionyesha kuwa, wafanyakazi bilioni 1.6 duniani wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na virusi vya Corona, idadi ambayo imechukua asilimia takriban 50 ya wafanyakazi wote duniani.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wameathirika zaidi na mlipuko wa virusi vya Corona. Nchi nyingi zimeongeza muda wa kufunga mipaka yao, hali iliyosababisha muda wa jumla wa kufanya kazi kupungua kwa asilimia 10.5 kote duniani katika robo ya pili ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kabla ya mlipuko wa virusi vya Corona.
Wafanyakazi kutoka bara la Amerika, Ulaya, na eneo la Asia ya Kati wameathiriwa zaidi na virusi hivyo, huku sekta za uuzaji, utengenezaji, hoteli, huduma ya chakula na ujenzi wa makazi zimeathiriwa vibaya zaidi. Shirika hilo limetoa wito kwa nchi mbalimbali duniani kuchukua hatua za haraka ili kuunga mkono makampuni na wafanyakazi wao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |