Kenya imeanza kuwaruhusu watu kula migahawani kwa masharti.
Wizara ya afya nchini Kenya wiki hii imesema kuwa itaruhusu migahawa kuanza kufunguliwa kuanzia saa 11 asubuhi na 10 jioni.
Watakaoingia kuhudumiwa watahitajika kufuata utaratibu uliopo wa kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa kama kawaida. Hatua ya kutokaribiana itaendelea kutekelezwa umbali wa mita 1 baina ya mtu mmoja hadi mwengine.
Lakini watakaoruhusiwa kutoa huduma ni wale watakaokuwa wamepimwa pekee.
Pia kulingana na wizara ya afya, katika migahawa hiyo, huduma ya kujiwekea chakula bado imesitishwa.
Wizara hiyo imetoa agizo la watu wote wanaoingia migahawani kupimwa kiwango cha joto na kuruhusiwa tu kuingia ikiwa litakuwa chini ya nyuzi 37.5 na mgahawa husika kuarifu wizara mara moja kuhusu mtu atakayepatikana akiwa na kiwango ha juu zaidi ya hicho, kwa kupiga simu kupitia nambari 719 ili kupata mwongozo zaidi.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amewataka raia wote wa Kenya kuendeleza nidhamu na kuchukua jukumu wao wenyewe binafsi katika juhudi za kubabiliana na janga hili.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |