Kundi la Houthi la Yemen latangaza mashambulizi dhidi ya meli ya kibiashara na manowari za Marekani
2024-03-05 09:04:52| CRI


Kundi la Houthi la Yemen limetangaza kuwa lilifanya mashambulizi yaliyolenga meli moja ya kibiashara iliyoendeshwa na Israel katika Bahari ya Arabia pamoja na manowari za Marekani katika Bahari ya Sham.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa kupitia channeli ya televisheni ya Al-Masirah ya kundi hilo, msemaji wa kundi hilo Yahya Sarea amesema, kikosi cha majini cha kundi hilo kilifanya operesheni inayolenga meli ya Israel ‘MSC SKY’ katika bahari ya Arabia, huku kikiipiga kwa usahihi kwa makombora kadhaa ya baharini.

Sarea ametangaza kuwa saa kadhaa kabla ya hapo, kundi hilo lilirusha makombora na droni dhidi ya manowari za Marekani katika Bahari ya Sham akiitaja kama operesheni bora.

Ameelezea mashambulizi hayo kuwa ni hatua ya kulipiza kisasi kwa uvamizi wa Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen na ujumbe wa kuunga mkono watu wa Palestina wanaoteswa, huku akiapa kuendelea kuzuia usafiri wa meli za Israel na meli zinazoelekea bandari za Israel mpaka uvamizi wao utakapokomeshwa na kuzingirwa kwa watu wa Palestina huko Gaza kutakapoondolewa.