Daftari la wapiga kura nchini Tanzania kuanza kuboreshwa Julai mwaka huu
2024-05-16 10:59:04| cri

Uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini Tanzania utafanyika Julai Mosi mwaka huu mkoani Kigoma, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Kassim Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Unguja, Zanzibar, jana, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele amesema zoezi hilo litakapokamilika, Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638.

Ameongeza kuwa, katika zoezi hilo, wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.

Kuhusu idadi ya vituo, Jaji Mwambegele ameseama Tume ilifanya uhakiki wa vituo vya kuandikishia wapiga kura mwaka 2023, na baada ya zoezi hilo, iliamuliwa kuwa vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa Daftari ni 40,126.