Xi akutana na Waziri Mkuu wa Vietnam
2024-06-27 09:04:38| CRI

Rais Xi Jinping wa China alikutana na Waziri Mkuu wa Vietnam Pham Minh Chinh mjini Beijing Jumatano. Chinh yuko China kuhudhuria Mkutano wa Majira ya joto wa Davos mwaka 2024.

Katika mazungumzo yao, Xi alisema katika ziara yake nchini Vietnam mwishoni mwa mwaka jana, yeye na katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Vietnam Nguyen Phu Trong, walitangaza ujenzi wa jumuiya ya China na Vietnam yenye mustakabali wa pamoja inayobeba umuhimu wa kimkakati, na kupeleka uhusiano kati ya nchi hizo katika hatua mpya.

Xi alisema China inapenda kushirikiana na Vietnam kudumisha mshikamano na urafiki, kuimarisha uungaji mkono wa pande mbili, na kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana, na kuongeza kuwa China pia inapenda kushirikiana na Vietnam kuelekea kwenye mambo ya kisasa na kutoa mchango mkubwa zaidi kwa amani, utulivu, maendeleo, na ustawi duniani.

Akiisifu mafanikio makubwa ya China katika nyanja zote, Chinh alisema Vietnam inaheshimu sana jukumu muhimu la China kama injini na chachu ya ukuaji wa uchumi wa dunia, na kwamba inaunga mkono maendeleo na ustawi wa China na kutimiza Lengo lake la Pili la Miaka 100 kama ilivyopangwa.