Mapambo
Picha ya Kuchongwa ya Mwaka Mpya
Picha ya kuchongwa ya mwaka mpya ina historia ndefu.
Picha ya kuchongwa ilianzia Enzi ya Song (960-1297), wasanii walichonga picha kwenye mbao kisha walichapisha, hivyo picha nyingi zilianza kuchapwa na kuuzwa katika enzi hiyo.
Kuanzia Enzi ya Song picha za kuchongwa za mwaka mpya licha ya kuonesha picha za aina mbalimbali za miungu pia zilianza kuonesha matumaini mema ya wakulima. Picha za kuchongwa za mwaka mpya zilipamba moto katika Enzi ya Qing (1368-1911). Picha kama "mavuno mazuri", "Ng'ombe alima katika majira ya Spring" n.k. zote ni picha zinazowavutia watu hadi leo. Wachoraji mashuhuri wa picha za kuchongwa za mwaka mpya pia walitokea wengi.
Picha za Kukatwa
Katika sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina, Wachina, hasa wakulima wana tabia ya kubandika picha za kukatwa kwenye madirisha, na milango ili kuonesha mazingira ya sikukuu.
Picha za kukatwa ni aina moja ya sanaa za jadi nchini China. Kutokana na maandishi ya historia, picha za kukatwa zilikuwepo tokea miaka elfu moja iliyopita. Wakati huo wanawake walikuwa wanabandika picha za kukatwa kichwani, na baadhi walikuwa na tabia ya kukata vipepeo kwa karatasi na kubandika dirishani kwa ajili ya kukaribisha majira ya Spring.
Picha za kukatwa ni picha zinazotengenezwa kwa mkono. Watu wanatumia mkasi kukata karatasi na kuwa picha, mara nyingi watu hukata karatasi kadhaa zilizolundikana kuwa picha. Hivyo wanaweza kupata picha kadhaa kwa mara moja.
Kuna aina mbalimbali za picha za kukatwa, kuna picha za ndege, wanyama, watu katika hadithi za mapokeo n.k. Picha za kukatwa katika sehemu tofauti pia zina zifa tofauti. Picha hizo za sehemu ya kusini ya China hukatwa kwa kuonesha mandhari nzuri ya milima na maji.
Hapo zamani, wakulima wanawake wasipokuwa na kazi za kilimo, walikuwa wanakatakata picha, kwani huu ulikuwa ni ufundi wa kimsingi kwa wanawake kwa wasichana. Hivi sasa kuna viwanda maalumu vya kutengeneza picha za kukatwa. Picha hizo badala ya kubandikwa madirishani, pia hupambwa kwenye majalada vitabu na magazeti.
Picha za Mwaka Mpya Mkoani Shanxi
Picha za mwaka mpya katika mkoa wa Shanxi zinajulikana zaidi nchini China. Picha hizo huwa na rangi tano kama nyekundu nzito, nyekundu hafifu, manjano, kijani na nyeusi. Picha hizo hubandikwa nyumbani katika sikukuu za mwaka mpya.
Picha za mwaka mpya zilianza katika Enzi ya Han Mashariki. Hivi sasa picha za kuchongwa pia zimekuwa aina moja ya picha za mwaka mpya.
Picha za mwaka mpya huonesha matumaini ya baraka, mavuno mazuri, utajiri, ustawi wa ukoo, n.k. Picha hizo huchorwa kwa kuambatana moja kwa moja na maisha ya raia, kwa hiyo kila mwaka mpya unapofika watu hasa wakulima hununua na kubandika madirishani au ukutani.
Chui wa Udongo
Chui wa udongo ni pambo la nyumbani, na inapatikana zaidi katika sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Shan'xi.
Chui wa udongo hutengenezwa kwa kutiwa chumvi, kwamba kichwa, macho, masikio na mdomo, yote ni makubwa. Kwenye mwili huchorwa mistari, kwenye kichwa hupambwa kwa ndege, majani. Kwenye kichwa na chui huchorwa alama na neno la Kichina 王 maana yake ni mfalme, au neno la Kichina baraka.
Pichani, chui anapakwa rangi wazi, na anaonekana mwenye furaha, akiwakilisha matumaini ya watu ya baraka na salama.
Chui wa Kitambaa
Chui wa kitambaa ni aina moja ya vitu vya kuchezea kwa watoto. Wachina wana imani kuwa, chui ni dalili ya kufukuza kisirani, na kuleta baraka, usalama na utajiri.
Chui wa kitambaa hushonwa kwa kitambaa na pamba, na kuchorwa sura ya chui. Chui wa kitambaa huwa na kichwa kikubwa, macho makubwa na mkia mrefu.
Chui wa kitambaa huwa ni kama zawadi kwa ajili ya watoto wanapotimiza siku mia moja, mwaka mmoja na miaka miwili. Katika siku za kawaida watu pia wananunua kwa ajili ya kuleta maana ya kuondoa kisirani na kuleta baraka.
|