21: Uchoraji wa Jadi

Picha za miungu

Miungu katika Uchoraji wa Jadi (1)

Watu wa kale wa China walikuwa wanachimba mifereji ya kulinda miji, na pia waliamini mungu wa kulinda mji. Kutokana na maandishi ya historia, hekalu la mapema lilijengwa mwaka 239.

Katika Enzi ya Ming (1368-1644) mwanzilishi wa enzi hiyo Zhu Yuanzhang aliwahi kuenzi imani ya mungu wa kulinda mji.

Pichani: Mungu wa kulinda mji ana sura ya mwenye vishungi vitano virefu vya sharafa.

Miungu katika Uchoraji wa Jadi (2)

Waumini wa dini ya Buddha nchini China wote wanajua kwamba kuna majemadari wanne mbinguni ambao wanawasaidia watu kufukuza mashetani.

Majemadari wanne mbinguni wanaoaminiwa na Wachina wa kale walikuwa ni walinzi wao wa usalama wasidhurike na mashetani.

Pichani ni mungu wa moto.

Picha hiyo ilitengenezwa kwa kuchapa na kuchora kwa pamoja.

Miungu katika Uchoraji wa Jadi (3)

Baadhi ya watu walikuwa na imani ya kuabudu miungu ya kazi. Miungu hiyo huabudiwa viwandani, madukani na kwenye idara za kazi. Mungu wa dawa huabudiwa na watu wa kazi ya dawa.

Pichani, mungu wa dawa anashika donge la dawa kwa mkono wa kulia na kushika tunguri la dawa kwa mkono wa kushoto.

Miungu katika Uchoraji wa Jadi (4)

Watu wa kabila la Wabai mkoani Yunnan wana imani ya kumwabudu mungu wa moto. Sura ya mungu huyo haina maalumu bali inategemea jinsi wachoraji wanavyofikiri.

Watu wa kabila la Wabai huwasha udi na kuwasha moto noti nje ya mlango kwa kumwabudu mungu wa moto.

Pichani, mungu wa moto mwenye mavazi ya kifalme ana vishungi virefu vitano vya sharafa, chini ya picha kuna maneno "mungu wa moto".

Miungu katika Uchoraji wa Jadi (5)

Mungu wa ardhi anaabudiwa sana na Wachina. Imani hiyo ilienea sana katika Enzi ya Ming, mahekalu mengi ya kuabudu mungu huyo yalijengwa.

Pichani mungu wa ardhi ana sura ya ukakamavu, ni picha iliyochapwa na kuchorwa kwa pamoja.

Miungu katika Uchoraji wa Jadi (6)

Mungu wa kike Guanyin ni mmoja wa miungu minne ya dini ya Buddha, na anaabudiwa sana nchini China hasa katika Enzi ya Tang (618-907).

Mungu wa kike Guanyin ana roho nzuri na huwa na sura ya kupendeza. Pichani kando ya Guanyin kuna watumishi wanne, ni picha iliyocharwa na kutiwa rangi kwa mkono. Guanyin alikuwa hana jinsia maalumu kabla ya Enzi ya Tang, lakini tokea enzi hiyo picha yake huchorwa kwa sura ya mwanamke.

Vitu vya Karatasi kwa ajili ya Sadaka Wilayani Cao katika Mkoa wa Shandong

Vitu vya karatasi hutumika katika mazishi, vitu hivyo huwa ni farasi, nyumba. Ushirikina huo ulianza katika miaka mingi iliyopita. Licha ya vitu pia kuna sanamu ya watu walioelezwa katika hadithi au watu mashuhuri wa historia.

Picha 1: Hawara wa mfalme Yang Guifei aliyelewa.

Picha 2: Pandikizi Lu Zhishen apambana katika msitu Yezhulin.

Picha 3: Panya aolewa

Picha 4: Jasiri Zhang Fei

Katika picha ya nne jasiri Zhang Fei anaonekana mwenye hamaki akiwa mkuki mkononi.

Lu Zhishen ni mtu aliyesimuliwa katika "Mashujaa kwenye Vinamasi", moja kati ya riwaya nne mashuhuri za kale.

Katika picha ya pili: Lu Zheshen alipambana kishujaa na majambazi ili kumlinda rafiki yake. Picha hiyo inatokana na hadithi ya "Mashujaa kwenye Vinamasi".

Sanaa ya Kutengeneza Vitu kwa Katarasi

Sanaa hiyo ilitokea na mila za kale, na vitu vilivyotengenezwa vilitumika kwenye mazishi, na kwa ajili ya tambiko.

Vitu hivyo vimegawanyika katika aina nne: moja ni sanamu ya mungu, wakati wa mazishi, sanamu hiyo ya karatasi huchomwa moto mbele ya kaburi; pili ni sanamu za watu, zikiwa ni pamoja na sanamu za watoto, watumishi au watu katika hadithi fulani. Tatu ni nyumba na magari. Nne ni vitu vinavyotumika katika chakula. Pichani, mmoja ni jemadari mwenye deraya, ndevu. Mwingine ni mtoto mwenye suruali nyekundu, na kwenye nguo yalichorwa majani ya myungiyungi.

Picha ya Farasi

Picha ya farasi ni aina ya picha iliyochongwa kwenye mbao na kuchapwa na kisha kupakwa rangi.

Picha ya aina hiyo inaenea zaidi katika sehemu ya kusini ya China. Hivi sasa picha kama hiyo imechanganya pamoja uchoraji, utiaji rangi na uchapaji.

Kwa kawaida, katika picha hiyo pia huchorwa ghala la fedha kwa ajili ya kuonesha utajiri.

Pichani mtunza wa ghala la fedha anaonekana kama ni ofisa mwenye kuvaa joho na kofia, kwenye upande wa kushoto na kulia kuna watumishi wanne wa kike na wa kiume. Ofisa alikaa mbele ya mlango wa ghala, na mbele yake ni fedha ambazo anataka kuwekea ndani ya ghala, mezani kuna mizani, ndani ya sahani kuna fedha, na chini ya meza kuna debe moja lililojaa fedha.

Opera ya Di

Opera ya Di inachezwa sana katika mkoa wa Guizhou. Kila katika sikukuu za Kichina, opera hiyo huchezwa. Wachezaji huvaa vinyago vya aina mbalimbali wakionesha wahusika mbalimbali katika hadithi za mapokeo.

Waigizaji katika opera hiyo wanagawanyika katika jemadari, ofisa, jemadari kijana, jemadari mzee na jemadari mwanamke. Wanawake wanapocheza huvaa vinyago vyenye mayoya ya tausi au vyenye michoro ya kipepeo na nyuki.

Vinyago vya Ibada vya Madhehebu ya Tibet ya Dini ya Buddha

Vinyago hivyo huchongwa kwa sura za miungu mbalimbali ya dini ya Buddha na kuvaliwa usoni wakati wa kufanya ibada.

Vinyago hivyo vinagawanyika katika aina tatu, yaani vinyago vya kutundikwa ukutani, vinyago vinavyotumika katika mchezo wa Kitibet na vinyago vinavyotumika katika tambiko. Kati ya vinyago hivyo, kuna sura ya mungu wa kulinda sheria, na vinyago huchongwa kama fuvu. Pichani ni kinyago cha mungu wa kulinda sheria mwenye macho matatu, akiwa mdomo wazi na meno nje.


1 2 3 4 5 6