China ni nchi ambayo uchumi wake unategemea zaidi nchi za nje, makampuni yanayoshughulikia uuzaji wa bidhaa nje yanaathiriwa zaidi na msukosuko wa fedha. Wakati mahitaji ya nje yamepungua kwa kiasi kikubwa, makampuni mengi yanakabiliwa na shida, yamepunguza mishahara au wafanyakazi, na hata kufungwa. Wakati huo huo, baadhi ya nchi zilitoa hatua za kujilinda kibiashara, kuzuia na hata kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa za China. Hali hiyo imeyafanya makampuni ya China yanayoshughulikia uuzaji wa bidhaa nje yakabiliwe na shinikizo kubwa zaidi. Takwimu zinaonesha kuwa thamani ya biashara na nje ya China ilipungua katika miezi minne iliyopita, hali ambayo ni ya wasiwasi.
Kwenye mkutano wa mwaka 2009 wa baraza la ngazi ya juu la maendeleo ya China, waziri wa biashara wa China Bw. Chen Deming alisema ili kukabiliana na msukosuko wa fedha, China itafanya juhudi ya kupanua mahitaji nchini, kuboresha miundo ya matumizi vijijini, na kuhakikisha ongezeko la uuzaji wa bidhaa nje. Alisema China ikifuata vitendo vya kawaida duniani, itaongeza uungaji mkono wa kisera kwa biashara na nje, kusukuma mbele mageuzi na uboreshaji wa utengenezaji wa bidhaa, kupanua uagizaji bidhaa kutoka nje, hasa teknolojia na mashine za kisasa, na kuongeza uagizaji wa vipuri, na rasilimali muhimu kutoka nje. Aidha, China itaendelea kutumia mitaji ya nje na kuhimiza makampuni ya China kuwekeza katika nchi za nje. Bw. Chen Deming alisisitiza kuwa China siku zote inapinga vitendo vya kujilinda kibiashara, akisema,
"Historia imethibitisha kuwa maendeleo mazuri ya uwekezaji na biashara ya kimataifa ni nguvu muhimu inayohimiza kufufuka kwa uchumi duniani. Msukosuko wa fedha umeiletea dunia nzima matatizo makubwa, na vitendo vya kujilinda kibiashara vitaufanya uchumi wa dunia ukabiliwe na matatizo makubwa zaidi. Kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha hali nzuri ya uchumi na biashara duniani kunaendana na maslahi ya kimsingi ya nchi mbalimbali. Wakati biashara inashuka duniani, mwaka 2008 China iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani trilioni 1.13 kutoka nchi za nje, ambayo imesukuma mbele maendeleo ya uchumi wa wenzi wake wa kibiashara kwa kiasi kikubwa. Mwaka huu China itaendelea kupanua uagizaji wa bidhaa kutoka nje, na kuyahimiza makampuni ya China kununua vifaa, bidhaa na teknolojia katika nchi za nje. Wakati uchumi wa China unapokabiliwa na changamoto kubwa, China ikichukua hatua halisi inaonesha msimamo wa kupinga vitendo vya kujilinda kibiashara na kushikilia sera ya ufunguaji mlango."
Mwezi Februari mwaka huu, Bw. Chen Deming aliongoza ujumbe mkubwa ulioundwa na wanaviwanda zaidi ya 200 kufanya makongamano na mazungumzo ya kibiashara na wahusika wan chi za nje, na kuagiza bidhaa nchini Ujerumani, Uswisi, Hispania na Uingereza, na ujumbe huo ulisaini orodha za uagizaji bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 10.
Kama ripoti ya Benki ya Dunia ilivyosema, China ni nchi inayovutia zaidi wakati uchumi wa dunia unapozorota. Profesa wa Chuo Kikuu cha Columbia Bw. Joseph Stiglitz ambaye aliwahi kupata tuzo ya Nobel ya uchumi anaona kuwa, uzoefu wa China unastahili kuigwa na nchi nyingine, akisema,
"Kwenye mchakato wa kuhimiza ufufuzi wa uchumi wa dunia, China inaweza kuhakikisha ongezeko la uchumi wake, na kutoa mchango kwa ufufuzi wa uchumi wa dunia. China inaweza kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea, na hatua hiyo inaendana na mtizamo wa China kuhusu thamani ya vitu."
Watu waliohudhuria mkutano wa mwaka 2009 wa baraza la ngazi ya juu la maendeleo ya China wanaona kuwa, kama hatua mbalimbali za kukabiliana na msukosuko wa fedha zikitekelezwa vizuri, China inatazamiwa kuwa nchi inayoondoa athari mbaya ya msukosuko huo mapema zaidi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |