Mikopo midogo midogo imekuwa moja ya njia za kuwasaidia wakulima na wafugaji kujiendeleza mkoani Tibet
Ili kuwaunga mkono wakulima na wafugaji kuondokana na umaskini na kujiendeleza, katika miaka ya karibuni tawi la benki ya kilimo ya China mkoani Tibet ilifanya majaribio na kuvumbua njia ya kutoa mikopo midogo midogo ambayo inafaa hali ya vijijini, na mikopo ya aina hiyo imekuwa ni moja ya njia za kuhimiza maendeleo endelevu ya maeneo ya kilimo na ufugaji.
Ili kuendana na hali mpya ya maendeleo ya uchumi wa maeneo hayo, tawi la benki ya kilimo ya China mkoani Tibet lilipanua tena kikomo cha utoaji wa mikopo, na kutoa kadi maalum ya kuomba mikopo kwa wakulima na wafugaji waaminifu zaidi ambao shughuli zao ni kubwa, ili kuunga mkono zaidi wakulima na wafugaji hao.
Utekelezaji wa hatua hiyo umeifanya sera ya fedha ya serikali kuu ya China ya kuunufaisha mkoa wa Tibet inufaishe maelfu ya familia za mkoa huo. Wakulima na wafugaji wengi wameanza kushughulikia uchukuzi wa bidhaa, kuanzisha maduka na viwanda vidogo, kujenga nyumba mpya na kuishi maisha ya furaha.
Wakulima na wafugaji wengi zaidi wamejiendeleza kutokana na kutumia mikopo iliyotolewa na benki, na baadhi yao wamekuwa na mali zenye thamani ya zaidi ya yuan milioni moja. Mkazi wa kijiji cha Caina cha wilaya ya Quxu ya mji wa Lhasa Bw. Samzhub ni mtu maarufu wa huko kutokana na uwezo mkubwa wa kujiendeleza. Yeye ni mtu wa kwanza kuomba mkopo kutoka benki katika kijiji chake. Mwaka 1985 aliomba mkopo ili kufanya shughuli ndogondogo. Katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, shughuli zake zimepata maendeleo makubwa. Mwaka 2006, kiwanda chake cha kutengeneza kokoto na mchanga kilikumbwa na ukosefu wa fedha, lakini mkopo wa yuan laki mbili kutoka benki ya kilimo ya China ilitatua tatizo lake mara moja, na mwaka jana Bw. Samzhub alipata mapato zaidi ya yuan laki nne kutokana na kiwanda hicho.
Kwa mujibu wa mahitaji ya kazi za kuhimiza maendeleo ya kilimo na ufugaji na kuwasaidia wakulima na wafugaji waongeze mapato yao mkoani Tibet, mwaka huu mkoa huo utaendelea kuongeza utoaji wa mikopo vijijini. Mkuu wa tawi la benki ya kilimo ya China mkoani humo Bw. Migmar Wangdui alisema, kwa ujumla benki hiyo itatoa mikopo yenye thamani ya yuan bilioni 4 vijijini mwaka huu, na itatoa kadi maalum za kuomba mikopo kwa watu elfu moja walio waaminifu zaidi.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |