Sera ya bima ya kilimo inayotekelezwa mkoani Tibet yaongeza uwezo wa wakazi wa huko kukabiliana na maafa
Hivi karibuni, mfugaji wa wilaya ya Anduo kwenye sehemu ya Nagqu mkoani Tibet Bw. Sang Zhu alipewa yuan elfu 10 ambazo ni fidia iliyotolewa na Tawi la Kampuni ya bima ya mali za umma ya China huko Tibet. Fedha hizo ni fidia aliyopata kutokana na hasara iliyopata familia yake kutokana na maafa makubwa ya mvua na theluji yaliyotokea mwezi Mei mwaka huu.
Mwezi Mei, maafa makubwa ya mvua na theluji yalizikumba baadhi ya tarafa katika sehemu za Rikaze, Shannan, Nagqu na Nyingchi mkoani Tibet, ambapo yalisababisha hasara kubwa kwa walikuma na wafugaji wa huko, na kusababisha vifo vya mifugo milioni kadhaa.
Lakini ni jambo la bahati kwamba, wilaya ya Anduo ya sehemu ya Nagqu ikiwa moja kati ya wilaya 30 za majaribo ya utekelezaji wa sera ya utoaji wa bima mkoani Tibet, wakazi wake waliokumbwa na maafa walipewa fidia kutoka kwa tawi la Kampuni ya bima ya mali za umma mkoani Tibet. Bw. Sang Zhu alisema, "Nimetumia fedha hizo kununua ng'ombe na kondoo, na kuanza maisha yangu mapya."
Takwimu za mwanzo kutoka Ofisi ya Kampuni ya bima ya mali za umma mkoani Tibet zinaonesha kuwa, katika sehemu ya Nagqu iliyoathiriwa vibaya zaidi na maafa hayo, familia 8,194 zilikumbwa na maafa, na idadi ya mifugo iliyokufa ilizidi laki 1.3, na fedha za fidia zinazohitajika kufikia yuan milioni 50.
Mkoa wa Tibet wenye wastani wa mwinuko wa zaidi ya mita 4000 kutoka usawa wa bahari ni sehemu inayokumbwa na maafa mengi zaidi nchini China, ambapo maafa ya theluji yanayotokea mara kwa mara kwenye sehemu hiyo husababisha hasara kubwa kwa wakazi wa huko. Kutokana na hali hii, kuanzia mwaka 2006, serikali ya mkoa wa Tibet na Tawi la Kampuni ya bima ya mali za umma zilishirikiana kutekeleza sera ya kukata bima kwa wakulima na wafugaji, na kutangulia kufanya majaribio huko Shuanghu kwenye sehemu ya Nagqu, na wilaya ya Lazi kwenye sehemu ya Rikaze. Hadi sasa sera hizo zinatekelezwa katika wilaya 30 katika miji 7 mkoani humo.
Habari zinasema, kutokana na sera hiyo, serikali ya mkoa wa Tibet inalipa kiasi kikubwa cha gharama za bima, kampuni ya bima ya mali za umma inashughulikia uendeshaji, na lengo la sera hiyo ni kuwanufaisha wakazi wa huko. Hivi sasa utaratibu wa kukata bima kwa wakulima na wafugaji umeanzishwa kwa hatua ya mwanzo mkoani Tibet. Utaratibu huo unahusisha bima ya shughuli za upandaji wa mimea, ufugaji na nyumba za wakulima. Gharama za bima zinatolewa kwa pamoja na idara ya fedha ya mkoa wa Tibet, serikali katika ngazi mbalimbali na wakulima na wafugaji wa huko, lakini wakulima na wafugaji wanalipa asilimia 10 tu ya gharama hizo. Kila mwaka idara ya fedha ya mkoa wa Tibet inatenga fedha kwa ajili ya kukata bima za aina tatu mkoani humo, na mwaka 2008 fedha hizo zilikuwa zaidi ya yuan milioni 30.
Naibu mkurugenzi wa Ofisi ya kilimo na ufugaji kwenye Idara ya fedha ya mkoa wa Tibet Bw. Deng Xiaoming alisema, sera hiyo inachangia utulivu wa uendeshaji wa uchumi vijijini, ambapo inasaidia kupunguza hasara wanazopata wakulima na wafugaji, pia kuwasaidia waongeze uwezo wakati wa kukabiliana na maafa na kurejesha uzalishaji. Hatua hii inalinda maslahi yao, na kuhimiza utulivu wa shughuli za kilimo na vijijini."
Kiongozi wa Tawi la Kampuni ya bima ya mali za umma huko Tibet alisema, kampuni hiyo itaendelea kupanua eneo la majaribio, ili kutoa uhakikisho kwa uzalishaji na maisha ya wakulima na wafugaji wa huko, na kuwanufaisha zaidi. Hadi sasa kampuni hiyo imetoa yuan milioni 9.633 za fidia kwa wakulima waliokumbwa na maafa ambao walikata bima.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |