Meneja Tang alieleza kuwa kivutio kingine kikubwa cha nyumba ya zamani ya Chen Cihong, ni nguzo za mawe zinazoonekana kama kawaida kwa hivi sasa, lakini ufundi wa utengenezaji wa nguzo hizo ulikuwa wa kisasa sana katika miaka ya 20 au 30 ya karne iliyopita. Alisema
"Nguzo zote zilizotumiwa zilitengenezwa kwa kazi za mikono, kwa sababu wakati ule hakukuwa na mashine. Kwanza nguzo hizo zilichongwa kwa tindo, na kazi za mwisho za kuzilainisha nguzo 60 zilifanywa kwa mikono kwa miaka miwili. Hapo zamani wachina hawakupenda kutumia nguzo za mawe wakati walipojenga nyumba zao, hata katika majumba ya mfalme wa zamani, nguzo za nyumba vilevile zilikuwa za mbao. Kwa hiyo nguzo nyingi za mawe za nyumba hazionekani katika sehemu nyingine, isipokuwa katika maskani ya Chen Cihong, ukichunguza zaidi utaona kuwa kila nguzo ina maneno ya Kiingereza."
Tangu nyumba ya zamani ya Chen Cihong ifanyiwe matengenezo na kufunguliwa kwa watu mwaka 1999, watalii wengi wameitembelea, wakiwemo watalii wengi waliotoka nchi za nje. Bw.Tang alisema:
"Binti mfalme wa Thailand Bi Sirindhorn ameitembelea sehemu hiyo mara tatu, takwimu zinaonesha kuwa wajumbe mia kadhaa wa serikali za nchi za nje wakiwemo mabalozi wa nchi za nje walioko nchini China waliitembelea sehemu hii. Licha ya hayo, baadhi ya mabingwa wa ujenzi wa majengo, wahandisi, na maprofesa wa nchi za nje wanapenda sana kutembelea huko. Kulikuwa na mgeni mmoja wa nchi ya nje aliyekwenda huko pamoja na mikanda 30 ya kamera. Nilifuatana naye kwenda huko, alipiga picha kwa siku 3, alisema ni maridadi sana."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |