Licha ya hayo, makampuni ya magari ya China yanashughulikia kuanzisha chapa maarufu duniani. Naibu meneja mkuu wa kampuni ya magari ya abiria ya Yutong ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya magari ya abiria nchini China Bw. Wang Wenbing alisema kampuni hiyo inafanya juhudi kuanzisha chapa maarufu duniani, akisema,
"Uuzaji wa bidhaa zetu nchini China ni wenye utulivu. Lakini kazi za kuuza bidhaa zetu na kuanzisha chapa maarufu kwenye soko la kimataifa bado ziko kwenye hatua ya mwanzo. Kampuni yetu ikitaka kuwa kampuni kubwa ya magari ya abiria duniani, inatakiwa kushughulikia chapa yake kwa njia tofauti kwenye soko la ndani na la kimataifa."
Mwaka 2009 makampuni ya magari ya China yalipata mafanikio katika kununua makampuni mengine ya nchini na ya nchi za nje na kuundwa upya. Na mwaka huu makampuni hayo yanatazamiwa kupata mafaniko mapya katika matumizi ya mitaji na uendeshaji wa shughuli zao duniani. Mwishoni mwa mwaka 2009, kampuni ya magari ya Geely ilifikia makubaliano na kampuni magari ya Ford kuhusu vifungu vyote vya makubaliano ya kununua kampuni ya magari ya Volvo. Makubaliano ya mwisho yatasainiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Mwaka jana makampuni ya magari ya China yalipata mafanikio ya kufurahisha katika kazi za masoko, teknolojia, chapa maarufu na uendeshaji wa shughuli zao duniani. Mafanikio hayo yameweka msingi imara kwa maendeleo ya makampuni hayo kwa mwaka huu. Katibu msaidizi mkuu wa shirikisho la viwanda vya magari la China Bi. Zhu Yiping alisema ingawa bado kuna hali isiyojulikana katika maendeleo ya uchumi wa China, lakini utengenezaji na uuzaji wa magari nchini China utaendelea kuongezeka kwa utulivu. Bi. Zhu alisema,
"Mwaka huu serikali ya China haijabadilisha uungaji mkono kwa makampuni ya magari, ambayo ni sehemu muhimu ya uchumi wa China. Mahitaji ya kununua magari kwa wakazi wa China bado ni makubwa. Kwa mujibu wa wastani wa ongezeko la uuzaji wa magari katika miaka 15 iliyopita ambao ni asilimia 16.74, mwaka huu makampuni ya magari ya China yataendelea kupata maendeleo mazuri, hivyo tunakadiria kuwa utengenezaji na uuzaji wa magari utaongezeka kwa asilimia 10 hivi, na unatazamiwa kufikia magari milioni 15.
Maendeleo makubwa ya uuzaji wa magari nchini China yamekuwa nguvu kubwa ya kuhimiza kufufuka kwa soko la magari la kimataifa. Soko la magari nchini China pia limetoa fursa nyingi kwa makampuni ya magari ya kimataifa yaliyokwama. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na makampuni ya magari ya kimataifa, mwaka 2009 uuzaji wa bidhaa wa makampuni ya magari ya kimataifa nchini China wote uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 20, na ongezeko la uuzaji wa bidhaa wa kampuni ya Ford hata ulizidi asilimia 70.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |