Bibi Gu Yu ambaye amezaliwa katika miaka ya 80 na ana shahada ya uzamivu ya dawa ni meneja wa mikahawa miwili ya kahawa. Ingawa ana shahada hiyo na aliwahi kuwa na kazi nzuri, lakini aliamua kujiuzulu na kuanza kufanya shughuli zake mwenyewe. Je, bibi Gu Yu alianzisha vipi mikahawa yake?
Kama ilivyo kwa watu wengine waliozaliwa katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, Bibi Gu Yu akifuata nia ya wazazi wake alisomea kozi ya dawa mpaka akapata shahada ya uzamivu. Baada ya kuhitimu, alipata kazi nzuri inayohusiana na kozi yake. Lakini maisha yake yalibadilika baada ya kukutana na mume wake katika mkahawa mmoja wa kahawa.
"Nilimfahamu mume wangu katika mkahawa wa kahawa. Baada ya sisi kuoana, mkahawa ule ulifungwa, hivyo tulifikiri kuanzisha mkahawa mmoja ili watu waweze kupumzika baada ya kazi au kukutana na marafiki zao."
Mwaka 2010 mkahawa wa kwanza wa bibi Guyu ulifunguliwa katika mtaa wa Dongsishitiao hapa Beijing. Ingawa mkahawa huo una ukubwa wa mita 20 tu za mraba, lakini mazingira mazuri yamewavutia wateja wengi. Kama Bibi Gu Yu alivyopanga mwanzoni, mkahawa wake si kama tu unauza vyakula, bali pia umekuwa ni mahali pa kupumzika na kukutana kwa watu. Aidha, mkahawa huu pia umewavutia watu kutokana na sifa nzuri ya vyakula. Bibi Gu alisema,
"Mimi na mume wangu tunanunua vitu vyenye sifa nzuri. Tunakagua kazi za wafanyakazi wetu mara kwa mara ili kuhakikisha wanatengeneza vinywaji na vyakula kwa mujibu wa vigezo vyetu. Kila baada ya muda fulani, wafanyakazi wanapika vyakula na sote tunavionja ili kudhibiti sifa ya vyakula. Tunajadili kwa pamoja maoni ya wateja."
Mwaka huu Bibi Gu Yu amepanga kuanzisha mkahawa wa pili. Ameamua kuanzisha mkahawa mkubwa katika mtaa wa kibiashara. Kuanzisha mkahawa mkubwa kuna hatari kubwa sana, kwani anatakiwa kushughulikia kazi zake kwa moyo wote, hivyo alijiuzulu.
Wakati Bibi Gu Yu alipoendesha mikahawa yake, alikabiliwa na changamoto kubwa kutoka mikahawa ya chapa maarufu duniani, lakini hakuogopa, amegundua fursa mpya ya kibiashara, alisema,
"Ingawa mikahawa ya Starbuck inawafanya watu wafahamu kahawa, lakini haiwasaidii watu kupata ujuzi kuhusu kahawa, ukiwemo aina za kahawa, na njia ya kutofautisha kahawa nzuri na mbaya."
Hivyo Bibi Gu Yu amewaalika wateja kufahamu utamaduni wa kahawa katika mkahawa wake, akisema,
"Tuliandaa shughuli za kupima kahawa. Kupima kahawa ni kazi muhimu ya kununua kahawa. Wapimaji wanapima sifa ya kahawa kwa kuvuta harufu, kuonja na kuangalia. Tulinunua aina 8 za kahawa, zikiwemo kahawa zilizozalishwa mkoani Yunnan hapa China na huko Jamaica, halafu tuliwaalika wateja wengi, tukawafundisha njia ya kupima kahawa, na kutoa maksi kwa kahawa hizi. Tunataka kuongeza hamu yao kuhusu kahawa kwa njia hii."
Mume wake Bw. Xu Tieren ni mtangazaji wa kipindi cha utalii na mwandishi wa habari, aliwahi kutembelea nchi zaidi ya 50. Bibi Gu Yu pia aliwahi kutembelea nchi 16. Ujuzi wao mkubwa kuhusu utalii umewavutia wapenzi wengi wa utalii kwenda kwenye mikahawa yao. Bibi Gu anasema:
"Siku hizi watu wengi zaidi wanapenda kutalii wakiwa wenyewe badala ya kujiunga na ujumbe wa watalii, hivyo wanahitaji ujuzi wa utalii. Saluni za utalii zinafanyika kila Jumapili jioni katika mikahawa yetu."
Licha ya kuwafundisha wateja ujuzi wa utalii, bibi Guyu pia anawasaidia watu wengi kupata wachumba, anasema,
"Watu 7 wamepata wachumba katika mikahawa yetu. Tumewapa njia ya kukutana na wengine. Nadhani ni rahisi kupata wachumba hapa, kwa sababu mimi mwenye pia nilikutana na mume wangu katika mkahawa wa kahawa."
Katika mikahawa ya Bibi Guyu, wateja si kama tu wanaweza kuonja kahawa na vyakula vitamu na kubadilishana uzoefu wa kutalii, bali pia huenda watapata wachumba. Mikahawa ya aina hii inapendwa na vijana wengi, hivyo Bibi Gu Yu ana imani kubwa kuhusu mustakabali wa mikahawa yake.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |