Kijana na maduka yake ya keki
Bw. Tao Liqun aliyezaliwa katika miaka ya 80 ya karne iliyopita ameanzisha kampuni ya keki ya Sun Baker huko Shaoxing mkoani Zhejiang. Hivi sasa Sun Baker imekuwa chapa pekee ya kienyeji mjini Shaoxing. Kampuni hii ina maduka 30 na kiwanda kimoja.
Bw. Tao Liqun alihitimu kozi ya usimamizi wa viwanda na biashara katika Chuo Kikuu cha Zhejiang. Wakati alipokuwa akisoma chuoni, alianza kujaribu kuanzisha shughuli zake, aliwahi kuwa wakala wa chapa moja ya keki chuoni. Baada ya kuhitimu, alirudi nyumbani kwake Shaoxing. Aliweka pamoja ndoto yake ya kuanzisha shughuli zake na hamu yake kuhusu keki. Alitembelea maduka mbalimbali ya keki mjini Shaoxing ili kuchunguza kwa makini soko la huko. Baadaye alisoma vitabu mbalimbali na kutafiti mpango wa uendeshaji. Wakati huo makampuni makubwa ya keki yalikuwa hayajaingia mjini humo, hii ilikuwa ni fursa nzuri kwa Bw. Tao, alisema,
"Wakati huo makampuni makubwa yalikuwa hayajaingia mjini Shaoxing, hivyo nikaona nikifanya vizuri nitapata fursa. Makampuni hayo mazuri ni mifano mizuri, naweza kuyaiga, na hata huenda nitayashinda. Nadhani katika miaka miwili hadi mitatu ijayo kampuni yetu itakuwa na mustakabali mzuri."
Kama ilivyo kwa watu wengine wanaoanzisha shughuli zao kwa mara ya kwanza, duka lake la keki linakabiliwa na matatizo makubwa. Wiki tatu baada ya duka hili kufunguliwa, mauzo mabaya yalimsikitisha sana Bw. Tao, ambayo yalikuwa ni yuan mia kadhaa kwa siku na ni madogo kuliko lengo aliloliweka la yuan elfu mbili. Bw. Tao alisema,
"Siku moja bibi mwema alikuja dukani kwangu, aliniambia nimsaidie kuchagua mikate mitano mitamu. Aliniambia kuwa mtoto wake alipokuwa kijana alikwenda Beijing kuanzisha shughuli zake, aliwahi kuuza bidhaa ndogondogo barabarani na kuwa mfanyakazi wa ujenzi, wakati huo aliishi maisha magumu, lakini sasa anamiliki kampuni kubwa. Bibi yule aliniambia nishikilie na kuwa na imani, nisiache shughuli zangu. Nilifurahi sana na kuwa na imani kubwa baada ya kusikia maneno yake. Baadaye hali ya soko ikawa nzuri, nilirekebisha kidogo shughuli za dukani, na mauzo yalikuwa mazuri na yanaendelea kuongezeka."
Kampuni ya Sun Baker inatilia mkazo sifa ya vyakula tangu ianzishwe. Inahakikisha malighafi zinakuwa nzuri na salama, na kutoa matakwa na vigezo mbalimbali kuhusu uzalishaji, mazingira na usafiri wa vyakula.
Bw. Tao si kama tu anafuatilia maendeleo ya kampuni yake, bali pia anatilia maanani kutekeleza wajibu wake kwa jamii. Kila robo mwaka kampuni ya Sun Baker inafanya shughuli za kunufaisha umma au wakati mwingine inashirikiana na idara za serikali kufanya hivyo. Kutokana na juhudi zake kwa jamii, amepewa sifa mbalimbali, zikiwemo "vijana kumi hodari wa eneo la Yuecheng mjini Shaoxing" na "mtu hodari aliyeanzisha kampuni mjini Shaoxing"
Hivi sasa kampuni ya Sun Baker ni kampuni ya keki inayopata mafanikio makubwa zaidi mjini Shaoxing, bidhaa zake zinapendwa na vijana. Mteja Bw. Cao alisema,
"Keki na mikate ya Sun Baker ni mitamu kuliko ile ya maduka mengine. Sisi vijana tunapenda kuja duka hili, kwa sababu meneja ni mkarimu, vyakula ni vitamu na duka ni zuri. Sun Baker ni chapa iliyoanzishwa na wenyeji wa Shaoxing, natarajia chapa hii pia itakuwepo katika miji mingine.
Mwaka huu Bw. Tao Liqun alianzisha duka lake katika chuo kikuu cha Zhejiang, hili ni duka la nne la Sun Baker mjini Hangzhou. Ana matumaini kuwa chapa hii itakuwa chapa maarufu nchini China, pia anatarajia shughuli zake zitawahimiza vijana wengi zaidi kuanzisha shughuli na kutimiza ndoto zao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |