Kwanza leo napenda nianze kwa kuwasalimia kwa kichina kuonesha kwamba hata sisi waafrika tunaweza kujifunza na kuongea kichina, lugha ambayo waafrika tunaiona kuwa ni miongoni mwa lugha ngumu hapa duniani. Ninakumbuka nyumbani Tanzania kuna msemo unaosema "lugha ya mtu ni lugha ya mtu tu" au "lugha ya wenyewe ni ya wenyewe tu". Misemo hiyo inakuja hasa pale mtu anapoongea lugha ngeni kama vile kingereza, akikosea, basi katika kumtetea au kujitetea misemo hiyo huwa inatumika.
Kwa kweli barani Afrika hususan Tanzania ukiwaambia watu jambo lolote kuhusu lugha ya kichina basi watakutazama mara mbili, maana tayari wameshajenga hisia akilini mwao kuwa hiyo ni moja ya lugha ngumu na si rahisi hata kidogo kuijua, si kwa kuongea wala kuandika.
Ni kweli kichina si lugha rahisi, lakini ni lugha ambayo inawezekana kuijua bila wasiwasi wowote. Kwa mfano mimi nimesoma lugha ya kichina kwa miezi miwili na nusu sasa, na tayari nimeanza kujua maneno machache. Au niseme naweza kuongea kichina cha kuombea maji, wenyewe kwa kichina wanasema ``wo hui yi dianr hanyu`` yaani ninaongea kichina kidogo.
Watu wengi wanakiogopa kichina kutokana na ugumu uliopo kwenye kuandika, na kwa kweli huko ndiko kuna matatizo makubwa, maana ni tofauti kabisa na lugha nyingine maana wao wanatumia hanzi (maneno ya kichina) na lugha nyingine zinatumia herufi za kirumi, ukiacha kijapan, kiarabu na kirusi, na hilo ndilo tatizo la wengi katika kukijua kichina, na ndyo sababu watu wajenge hisia kuwa hiyo ni lugha ngumu na si rahisi mtu kutoka Afrika kuijua kwa urahisi.
Wakati huko nyumbani Afrika watu wanakiogopa kichina (kukiongea na kukiandika), hali ni tofauti na hapa nchini China kwenyewe ambapo kuna wanafunzi wengi kutoka Afrika wanaisoma lugha hiyo au wanasoma masomo kwa kutumia lugha hiyo. Kwa mfano katika mji wa Wuhan kuna wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za la Afrika kuanzia Mashariki, magharibi, kaskazini hadi kusini, wote wanasoma kwa kichina au wanajifunza lugha hiyo.
Cha kuvutia zaidi utawakuta hao waafrika wenyewe kwa wenyewe wakiongea lugha hiyo na hilo linakuja kutokana na wenyewe kutoka nchi zinazozungumza lugha tofauti, kwa mfano mimi natoka Tanzania ninaongea Kiswahili na Kingereza, ninaishi chumba kimoja hapa chuoni na mtu toka nchini Mali ambaye yeye anaongea kifaransa ambayo ndio lugha yake ya taifa, hivyo hali inakuwa ngumu tunapotaka kuwasiliana, hivyo lugha inayotuwezesha kuwasiliana ni kichina tu, hakuna lugha nyingine. Sasa jitihada zinahitajika kuijua lugha hii ambayo itatusaidia kuishi hapa nchini China kwani wachina wanaongea lugha yao tu na hawajui lugha nyingine, wachache sana wanaongea Kingereza.
Na kitu cha kuvutia zaidi ni kwamba, waafrika hao wanapigana kwa kila njia ili waijue lugha ya kichina, na wanafanya kazi ya ziada ya kuijua lugha hiyo huku wakijua fika kuwa lugha hiyo sio rahisi, lakini wanasema, kwanini wao wameweza na sisi tushindwe? Tuna nini? Pamoja na hayo yote bado wanafunzi hao kutoka Afrika wanakiri kuwa kusoma kichina ni kazi ngumu kwao. Edward Kachikho toka Malawi anasoma kichina kwa mwaka mmoja hapa katika mji wa Wuhan na baada ya hapo ataanza masomo yake ya shahada ya pili kwa kichina. Anasema kazi ni ngumu mno kwake na waafrika wengine kuijua lugha hiyo hasa kwenye kuandika na kutamka na inahitaji kazi ya ziada ili kuweza kuijua lugha hii.
Edward anakiri kuwa yeye alikotoka alikuwa anaongea lugha yao ya asili ya Chichewa na kiingereza tu, na katika lugha hizo mbili hakuna kabisa muingiliano na lugha ya kichina, na hapo ndio kwenye matatizo makubwa.
Ila kwa sababu amefika hapa China kusoma basi hana budi kufanya hivyo maana ndicho kilichomleta, lakini hakuna urahisi hata kidogo. Kauli yake inaungwa mkono na Abel Madinga toka Msumbiji ambae yeye amekuwepo nchini China kwa miaka mitatu na anaweza kuongea kichina vizuri, lakini anasema kwake haikuwa rahisi hata kidogo kuijua lugha hiyo na hadi sasa bado anajifunza.
Abel anasema katika harakati za kujifunza lugha hiyo ya Kichina alijikuta anaingia kwenye mahusiano yasiyo rasmi ya kimapenzi na binti mmoja wa kichina ili tu iwe rahisi kwake kuijua lugha hiyo, na ndio vijana wengi wa kiafrika wanavyofanya hapa China ili kuwasaidia kuifahamau lugha hiyo.
Vijana wengi wa Kiafrika wanaamini kuwa, ukiwa na mpenzi mchina basi itakuwa rahisi kwako kujua kichina, tena wengine wanatafuta yule ambaye hata kiingereza hakijui ilimradi tu yeye aweze kutimiza malengo yake ya kufundishwa kuongea au kuandika lugha ya kichina, na baada ya kukijua basi wanakatisha uhusiano na mabinti hao, au wanapomaliza chuo na mapenzi yanakuwa yamemalizika.
Abel anasema wakati anahangaika kujifunza kichina alianzisha huo uhusiano na binti wa kichina ambaye anakiri kuwa ndie aliyemsaidia sana kuijua lugha hiyo na si mwalimu pekee, na amewataka waafrika wenzie ambao hivi sasa wanajifunza lugha hiyo kujaribu kutumia mbinu kama hiyo ambayo yeye anadhani itawasaidia kukijua kichina ama sivyo itakuwa ngumu kwao.
Vijana hawa toka kusini mwa Afrika wanasema tatizo kubwa la kichina lipo kwenye kuandika (inaitwa hanzi kwa kichina). Wanakiri kuwa kazi ni ngumu sana kuweza kuzishika hizo hanzi, kwanza ni tofauti mno na mazingira ya lugha waliyokulia, pili kukisoma kichina ni kazi ngumu,
Tatu kuna kitu kinachoitwa alama za sauti ambazo sehemu nyingine zinatumiwa kwenye nyimbo maana zinaanzia sauti ya kwanza hadi ya nne. Lugha nyingi zinazoongelewa barani Africa hakuna kitu kama hicho, na alama hizo ndio moja ya kikwazo kikubwa kwa waafrika kuweza kuongea ipasavyo lugha ya kichina.
Wote wawili Abel Madinga toka Msumbiji na Aidehua toka Malawi, wanasema itakuwa ngumu sana kwa lugha hii kuenea barani Afrika kwasababu wengi wanaojifunza lugha hii kwanza hawataki kuwafundisha watu huko, na hata hao watu wenyewe wengi wao hawatokubali kuisoma lugha hii kwasababu tayari hisia zimeshajengeka kuwa Kichina ni kigumu mno.
Hao wote wanasema miongoni mwa watu ambao wanakijua haraka kichina toka barani Afrika ni watu ambao wanatoka katika nchi zinaozoengea kifaransa kama vile Mali, Gabon, Ivory Coast na nchi zingine kwasababu kubwa mbili: kwanza, kifaransa kina ala za sauti kama kichina, pili, wengi wao hawajui kingereza hivyo ili kuweza kufanya mawasiliano haraka na watu wanalazimika kukijua kichina haraka sana.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |