Kauli hiyo inaungwa mkono na Haruna Sang`are toka Mali. Anasema yeye ni tofauti kabisa na watu wanaotoka nchi zinazoongea kingereza na lugha zingine katika kujifunza kichina, na kukiri kuwa angalau wao wana urahisi kwenye kusoma kichina ila ni kwenye matamshi sio kwenye kuandika huko nae anakilia kuwa kazi ni ngumu mno tena isiyo na mfano hata kidogo.
Sang`are nae anasema hajui kama ipo siku kuna watu watakikubali kichina kiurahisi toka barani Afrika kutokana na mfumo wake ulivyo, na itakuwa ngumu kwao kuipa kipaumbele lugha hii kama ilivyo kiingereza na kifaransa kwani haina muingiliano hata kidogo na lugha za Afrika.
Juan Leo Esono Ebale kwa jina la kichina anaitwa Li Song toka Guinea ya Ikweta anaongea lugha nne za kimataifa yaani Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kihispania. Anasema wakati anajifunza lugha hizo nyingi haikuwa taabu kwake, ila kwenye kichina kazi anaipata na kukiri kuwa hiyo ni lugha ngumu mno na haina muingiliano kabisa na lugha za Afrika.
Anasema kujua kuongea lugha nyingi ndio kitu ambacho anakipenda maishani mwake ambapo kwa kichina wanasema aihao, lakini anasema yeye amegundua lugha za asili tunazoongea barani Afrika zinaweza zikawa ndio moja ya kikwazo kikubwa katika kujifunza kichina, ila kichina ni moja ya lugha nzuri na ana uhakika kuwa siku moja atakuja kuiongea lugha hiyo bila ya matatizo yeyote.
Kuhusu lugha ya kichina kukubalika barani Africa moja kwa moja Li song akatupa lawama kwa wachina wenyewe ambao wengi tu hivi sasa wapo barani Afrika wakifanya shughuli mbali mbali, na yeye amesema, wachina hao hawataki kuwafundisha waafrika lugha yao hata kidogo, ila kama wakifanya hivyo, lugha hiyo itaongelewa tu barani humo.
Li song anatoa mfano nchini kwake Guinea ya Ikweta ambapo anasema kwa sasa kuna wachina wengi na katika nchi zingine kama Tanzania, Kenya, Mali, Ghana, Sudan nk, ila wachina hao wameshindwa hata kufungua japo darasa la kufundisha lugha hiyo kama yanavyofanya mataifa mengine kama Ufaransa na Uingereza.
Wakati hao wakisema hivyo mmoja wa wanafunzi wanaosomea ualimu wa kufundisha lugha hiyo ya kichina anaeitwa Wang Li Juan anakiri bayana kuwa kazi ngumu inawakabili wanafunzi toka barani Afrika katika kujifunza lugha ya kichina. Ingawa wengi wao wanafanikiwa huku wengi wao wakijua zaidi kuongea kuliko kuandika, na kuongeza kuwa inabidi wapewe muda zaidi ili waweza kufanikiwa kukijua kichina kwa kina.
Wang anasema katika kipindi cha mitihani inakuwa taabu mno kwa wanafunzi toka Afrika maana wao hawajui maneno mengi ya kichina, na anatolea mfano wa baadhi ya marafiki zake toka barani Afrika wanaosoma hapa Wuhan kuwa ukikaribia muda wa mitihani inakuwa ngumu kuwaona maana wanajificha ili wapate muda zaidi wa kusoma, na muda huo wanautumia kutafuta misamiati ya kichina ili waweze kujiweka vizuri.
Kutokana na hilo, wanafunzi wengi wa kichina wanaosoma na waafrika wanapenda sana kusaidia kuwafundisha lugha hiyo ambayo wenyewe wanaamini ni ngumu, lakini wanapendezwa na moyo wa wanafunzi waliotoka barani Afrika wa kuipenda lugha hiyo, na wengi wao wanafanikiwa kuijua ingawa kazi inakuwa ni ngumu mno kwao.
Pamoja na yote, binti huyo mchina anasema, pamoja na wanafunzi hao kujua kuongea kichina bado wana matatizo mengi hasa kwenye matamshi, na hilo hawawezi kulimudu kwa asilimia mia moja maana hiyo sio lugha yao na kukiri kuwa kweli lugha hiyo inawapa tabu.
Akizungumzia kutanuka kwa ngazi ya kimataifa kwa lugha ya kichina, Wang anasema hajui kama ipo siku lugha ya kichina inaweza kukubalika kama kingereza, hasa kutokana na mfumo wake ulivyo hasa kwenye maandishi. Nae akatia shaka kuwa hajui kama lugha hiyo ikipelekwa kufundishwa barani Afrika kama kuna watu wanaweza kujitokeza kuisoma.
Mwanafunzi huyo anasema yeye kama mwalimu mwanafunzi hadi sasa anapigana kwa kila njia kuwasaidia wanafunzi toka barani Afrika, na anataka sana lugha yake ijulikanike duniani kote, ila mfumo wa lugha hiyo ndio kikwazo maana ni tofauti sana na mfumo wa lugha zingine hapa duniani! Ila anasema anafurahi sana anapoona mgeni anaongea lugha ya kichina maana ni moja ya njia za kuikuza lugha hiyo.
Kwa upande wake mwalimu wa lugha hiyo ya kichina kwenye chuo kikuu cha kawaida cha Huazhong Bi Qu Shuhao, anasema ni kweli kichina ni moja ya lugha ngumu duniani kama wanavyosema watu ila ni lugha nyepesi sana hasa kwake kwa sababu yeye ni mchina.
Na anasema kwanza anawapenda wanafunzi waliotoka Afrika ambao wanasoma kichina, na amewafundisha wengi, ila mfumo wa elimu wa bara la Asia na Afrika ni moja ya kikwazo kikubwa kwao lakini wanajitahidi kuweza kuijua lugha hiyo.
Mwalimu Qu anasema yeye yupo tayari kama akiambiwa aende akaifundishe lugha hiyo barani Afrika, na anataka sana kuona siku moja lugha hiyo inaongelewa sehemu mbali mbali hasa katika bara la Afrika, ila hayajui mazingira ya Afrika, na akasema kuna uwezekano hilo nalo likawa kikwazo kwake.
Lakini mwalimu huyo hakuficha furaha yake kwa kuwaona waafrika wanakuja hapa China kujifunza lugha hiyo na wengine kuiongea vizuri, na anasema kama kukiwa na mpango madhubuti wa kuieneza lugha hiyo, basi siku moja kichina kitakuja kuwa moja ya lugha kubwa hapa duniani.
Pia akasema wanafunzi wengi wan chi mbalimbali zinazoongea kingereza wana nafasi kubwa ya kukijua kichina haraka kwasababu vitabu vya kichina vimetafsiriwa kwa kingereza, ila wao wanaridhika mapema kwasababu hawana taabu sana, hivyo wale ambao hawajui kingereza wanapigana sana kukijua Kichina kutokana na mazingira halisi yalivyo.
Na huo ndio ukweli, taarifa zinasema waafrika wengi wanaojua kuongea kichina wengi wanatoka katika nchi ambazo haziongei kingereza barani Afrika.
Tuombe Mungu siku moja lugha hii ya kichina ije kuwa lugha maarufu sana barani Afrika na hawa wanaoisoma hivi sasa wakirudi nyumbani basi wakaifundishe kwa wengine ili iweze kuenea zaidi.
Kubwa zaidi ni kwa serikali ya China kuchukua jukumu la kuipeleka lugha hii barani Afrika. Kama wanavyofanya biashara na nchi za Afrika, basi pia wapeleke wataalamu wa kufundisha lugha hii ili kuondoa kasumba kuwa, kichina ni moja ya lugha ngumu duniani, na ukikijua utaonekana kuwa ni mtu wa ajabu.
Sina la zaida hii leo ninasema zhong guo hen hao (yaani China ni nzuri sana, Zaijien)
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |