1: Ardhi, Maliasili na Idadi ya Watu

Maliasili ya Ardhi

China ni nchi yenye eneo kubwa, maliasili ya ardhi ni ya aina nyingi, ardhi ya kilimo, misitu, ardhi yenye majani, jangwa na fukwe, zote zinapatikana nchini China kwa maeneo makubwa. Lakini sehemu kubwa ya ardhi ya China ni milima, sehemu za tambarare ni chache, na sehemu ya ardhi ya kilimo na misitu ni ndogo. Ardhi ya kilimo inapatikana zaidi katika tambarare na mabonde mashariki mwa China, na sehemu nyingi zaidi yenye misitu iko katika sehemu ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa China, na ardhi kubwa zaidi zenye majani ziko katika nyanda za juu na sehemu za milima.

Ardhi ya kilimo:

Hivi sasa nchini China kuna hekta milioni 1.27 za ardhi ya kilimo, tukiigawa China katika sehemu ya mashariki, katikati na ya magharibi, ardhi hiyo ya kilimo katika sehemu ya katikati inachukua 43.2%, na sehemu za mashariki na magharibi, kila sehemu inachukua 28.4, na sehemu kubwa ya ardhi hiyo iko katika tambarare ya kaskazini-mashariki, tambarare ya kaskazini ya China, tambarare iliyoko katikati na ya mwisho ya Mto Changjiang, delta ya Mto Zhujiang na bonde la Sichuan. Ardhi katika tambarare ya kaskazini-mashariki ni ardhi nyeusi yenye rutuba nyingi, mimea inayolimwa zaidi katika sehemu hiyo ni ngano, mahindi, mtama, soya, mkonge na viazisukari. Ardhi katika tambarare ya kaskazini ya China ina rangi ya kahawia, mimea inayolimwa katika ardhi hiyo ni ngano, mahindi, uwele, mtama, pamba na njugunyasa. Katika tambarare kwenye sehemu ya katikati na ya mwisho ya Mto Chanjiang mimea inayopandwa zaidi ni mpunga, machungwa na rapa. Na katika bonde la Sichuan mimea inayolimwa zaidi ni mpunga, rapa, miwa, chai, machungwa na mabalungi.

Misitu:

Hivi sasa nchini China kuna hekta milioni 158.94 za misitu ambazo ni 16.55% ya eneo lote la China, kwa hiyo China ni nchi yenye misitu michache na ikilinganishwa na kiasi cha misitu kinachofunika 30.8% ya ardhi ya dunia kwa wastani China bado iko mbali. Misitu ya asili inapatikana zaidi katika sehemu ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa China, na katika tambarare ya mashariki ya China yaani sehemu yenye watu wengi na maendeleo ya kiuchumi, na katika sehemu kubwa ya kaskazini- magharibi mwa China misitu ni michache sana.

Misitu ya China ina aina za miti karibu 2800, na miti yenye thamani kubwa ni metasequoia na ginkgo. Ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi, China imefanya harakati za kupanda misitu. Hivi sasa misitu iliyopandwa imekuwa hekta milioni 33.79, na kuifanya China kuwa nchi yenye eneo kubwa la misitu iliyopandwa duniani.

Sehemu kubwa ya misitu ya kiasili nchini China iko katika kaskazini-mashariki mwa China, ikiwa ni pamoja na sehemu ya mlima Daxinganling, Xiaoxinganling na mlima Changbai. Sehemu ya kusini-magharibi ya China ni sehemu ya pili yenye misitu mingi. Na sehemu ya kusini-mashariki ya China ni sehemu ya misitu iliyopandwa. Licha ya misitu hiyo, nchini China kuna utando wa misitu ya hifadhi, mathalan, kanda za misitu hifadhi iliyoenea katika China ya kaskazini-mashariki, kaskazini, na kaskazini-magharibi, jumla zina kilomita 7000 kwa urefu na hekta milioni 260 kwa maeneo ambayo ni robo ya nchi kavu ya China, huu ni mradi mkubwa kabisa duniani wa hifadhi ya mazingira.

Ardhi yenye majani:

Kuna hekta milioni 266.06 za ardhi yenye majani ambazo zinafaa kwa malisho nchini China, kuna aina za majani ambazo zinafaa kwa malisho ya mifugo ya aina mbalimbali katika majira tofauti. Ardhi yenye majani ni karibu robo ya eneo lote la China, na kuifanya China kuwa nchi yenye ardhi kubwa yenye majani duniani. Mbuga za majani ya kiasili nyingi ziko katika sehemu ya kaskazini-mashariki mwa China kuanzia mlima Daxinganling, mlima Yinshan hadi nyanda za juu za Qinghai-Tibet. Na mbuga za majani yaliyopandwa ziko katika sehemu ya kusini-mashariki ya China ambapo ziko pamoja na ardhi ya kilimo na sehemu za misitu.

Sehemu kubwa ya malisho iko katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, mifugo iliyofugwa huko ni farasi Sanhe na ng'ombe Sanhe. Katika sehemu ya malisho mkoani Xinjiang wanafugwa kondoo wa Xinjiang wenye manyoya laini, kondoo wa Altai wenye mkia mnene na farasi wa Yili. Na katika sehemu ya malisho mkoani Qinghai waliofugwa wengi zaidi ni yak, ng'ombe wenye manyoya marefu, na farasi maarufu wa Hequ. Katika sehemu ya malisho mkoani Tibet wanaofungwa zaidi ni yak.

Maliasili ya Madini

China ina utajiri mkubwa wa madini, na utajiri huo umethibitishwa kuwa ni 12% ya utajiri wote wa madini duniani, na China ni nchi ya tatu yenye utajiri mkubwa wa madini duniani. Hata hivyo, wastani wa umiliki wa madini wa kila Mchina ni 58% tu ya ule wa duniani, wastani huo wa umiliki wa madini kwa kila Mchina unachukua nafasi ya 53 duniani. Hadi sasa madini aina 171 yamegunduliwa na aina 158 zimethibitishwa utajiri wao (aina za nishati 10, aina za metali nyeusi 5, metali za rangi 41, madini yenye metali thamani 8 na madini yasiyo ya metali 91 na madini ya maji na gesi aina 3). China ni moja ya nchi chache zenye utajiri mkubwa wa madini, aina nyingi za kikamilifu za madini. Kutokana na utajiri uliothibitishwa, aina 25 kati ya aina 45 muhimu zilizopatikana nchini China zinachukua nafasi ya tatu duniani, na kati ya aina hizo 25 madini ya udongo adimu, jasi, vanadium, titanium, tantalum, wolfram, kinywe, shura, barite, magnesite, antimony yanachukua nafasi ya kwanza duniani.

Utapakaaji wa madini nchini China ni kama ifuatavyo: Mafuta na gesi asilia yanapatikana kwa wingi zaidi katika sehemu ya kaskazini-mashariki, kaskazini na kaskazini-magharibi ya China. Makaa ya mawe yanapatikana zaidi katika sehemu ya kaskazini, na kaskazini-magharibi ya China. Madini ya chuma yako zaidi katika sehemu ya kaskazini-mashariki, kaskazini na kusini-magharibi ya China. Madini ya shaba mengi zaidi yako katika sehemu ya kusini-magharibi, kaskazini-magharibi, na mashariki ya China. Madini ya risasi na zinki yanapatikana kote nchini China, na madini ya wolfram, risasi, molybdenum, antimony, na udongo adimu yanapatikana zaidi katika sehemu ya kusini, kaskazini mwa China. Madini ya dhahabu na fedha yanapatikana kote nchini na kisiwani Taiwan. Madini ya phosphorus yanapatikana zaidi katika sehemu ya kusini ya China.

Maliasili ya madini muhimu nchini China ni yafuatayo:

Makaa ya mawe:

China inaongoza kwa utajiri wa makaa ya mawe duniani. Makaa ya mawe yamethibitishwa kuwa ni tani bilioni 1000 ambayo mengi zaidi yako katika sehemu ya kaskazini, kaskazini-magharibi na hasa katika mikoa ya Shanxi, Shan'xi na Mongolia ya Ndani.

Mafuta na gesi: Mafuta na gesi zaidi ziko katika sehemu ya kaskazini-magharibi, sehemu ya kaskazini-mashariki, kaskazini na sehemu ya mwambao wa mashariki ndani ya bahari. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1998 maeneo 509 ya mafuta na maeneo 163 ya gesi yaligunduliwa nchini China. Utajiri wa mafuta umethibitishwa kuwa ni tani bilioni 18.85 ikiwa ni nafasi ya tisa duniani na gesi mita za ujazo bilioni 1950 ikiwa ni nafasi ya 20 duniani. Na mafuta na gesi yaliyoko China bara ni 73.8% na 78.4% ya utajiri wote wa maliasili hiyo.

Madini ya metali:

Metali nyeusi: China imethibitishwa kuwa na utajiri wa chuma, manganese, vanadium na titanium, na kati ya metali hizo, kiasi cha chuma ni tani bilioni 50, kiasi kikubwa kinapatikana katika mikoa ya Liaoning, Hebei, Shanxi na Sichuan.

Metali zenye rangi:

Metali zenye rangi zilizogunduliwa duniani zote zinaweza kupatikana pia nchini China, na kati ya metali hizo udongo adimu unachukua 80% ya dunia nzima na utajiri wa antimony unachukua 40% duniani na utajiri wa wolfram ni mara nne kuliko utajiri wa metali hiyo katika nchi zote nyingine kwa pamoja.

Maliasili ya nishati za upepo, maji na jua

Katika eneo kubwa la China kuna mito mingi ambayo ipo katika sehemu nyingi na maanguko ya maji ni makubwa, kwa hiyo nishati za nguvu za maji ni nyingi. Kutokana na takwimu, nishati za maji ni kilowati milioni 680 na umeme kilowati bilioni 5920 kwa mwaka, uwezekano wa kuzalisha umeme kwa mashine ni kilowati milioni 378 na umeme kilowati bilioni 1920 kwa mwaka, kwa hiyo, siyo tu utajiri wa nishati hiyo peke yake bali pia uwezekano wa kutumika kwa ajili ya kuzalisha umeme vyote vinachukua nafasi ya kwanza duniani.

Nishati ya upepo kwenye mita 10 hewani juu ya ardhi ni kilowati bilioni 3.226. Kwa makadirio, uwezekano wa kutumia nishati hiyo ni kilowati milioni 253, na kwenye bahari iliyo karibu na bara (kima cha maji zaidi ya mita 15) nishati hiyo ni mara tatu kuliko ile ya nchi kavu yaani kilowati milioni 750. Nishati ya upepo ipo zaidi katika sehemu ya kaskazini-magharibi, kaskazini na mashariki ya China na kwenye mwambao na visiwa vya kusini-masharini mwa China. Katika sehemu hizo upepo huwa ni mkubwa katika majira ya baridi na Spring, na katika majira ya joto huwa mdogo. Tabia hiyo inasaidia sana umeme unaozalishwa kwa nguvu za maji katika sehemu hizo, kwa kuwa mvua huwa nyingi katika majira ya joto na chache katika majira ya baridi na Spring, kwa hiyo panafaa kuendeleza uzalishaji wa umeme kwa nguvu za upepo. Mwishoni mwa mwaka 1998, China ilikuwa na vituo karibu 20 vya kuzalisha umeme kwa nguvu za maji, uwezo wa mashine ni kilowati laki 2.236, na hivi sasa nchini China kituo kikubwa kabisa cha kuzalisha umeme kwa nguvu za upepo ambacho pia ni kikubwa barani Asia, ni kituo cha Dabancheng kilichoko mkoani Xinjiang, ambacho mashine zake 111 zina uwezo wa kuzalisha kilowati 300, 500 na 600 za umeme, na jumla ya uwezo wa kuzalisha umeme ni kilowati elfu 57.5. Hivi sasa umeme uliozalishwa kwa nguvu za upepo unachukua sehemu moja kwa elfu moja tu katika uwezo wa jumla wa kuzalisha umeme nchini China, kwa hiyo nafasi yake ya kuendelezwa ni kubwa sana.

Nishati ya jua pia ni kubwa nchini China, kwa mwaka nishati ya mionzi ya jua ni sawa na makaa ya mawe tani milioni 240, na theluthi mbili ya ardhi ya China inapita 6000 megajouli kwa mita moja ya mraba, na katika sehemu ya kaskazini-magharibi ya China na mkoani Tibet hata inafikia 8400 megajouli kwa mita moja ya mraba, na kuwa sehemu yenye nishati kubwa ya jua duniani. Kituo cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa nishati ya jua kiko katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, uwezo wake ni wati 560, kilianza kutoa umeme tarehe 11 Oktoba mwaka 1982.

Mimea na usambazaji wake

Halikadhalika, China pia ni nchi yenye aina nyingi za mimea, kiasi cha aina elfu 30 za mimea zinapatikana nchini China, ni nchi ya tatu kwa kuwa na aina nyingi za mimea ikizifuata Malaysia na Brazil. Mimia ya jamii za bryophyte ni 70% ya aina zote zipatikanazo duniani na pteridophyte aina 2600 katika jamii 52 ambazo ni 80% ya aina zote zipatikanazo duniani, na aina 8 za miti ya mbao na aina 2,000 za miti. Hapa duniani kuna aina 750 za mbegu zisizo na gamba la nje, aina 240 kati ya hizo zinaweza kupatikana pia nchini China. Miti yenye majani kama ya sindano inachukua 37.8% katika aina zote za miti hiyo duniani.

Mimea inayoota katika nusu ya dunia ya kaskazini karibu yote inaonekana pia nchini China, kuna mimea elfu 2 ya chakula, na mimea elfu 3 ya dawa.

Aina za misitu zinatofautiana kutoka kaskazini hadi kusini kutokana na tofauti za hali ya hewa, misitu ya aina zote ya ukanda wa baridi, wenye jotoridi wastani, ukanda wenye joto wastani na ukanda wa tropiki inapatikana.

Upatikanaji wa wanyama

China ni nchi yenye aina nyingi za wanyama, kuna aina 6266 za wanyama wenye uti wa mgongo, kati yao aina 500 ziko ardhini, ndege aina 1258, wanaotambaa aina 376 na walioko majini na nchi kavu kwa pamoja aina 284, aina za samaki 3862, jumla ya wanyama hao ni kiasi cha moja kwa kumi ya aina zote duniani. Kuna aina elfu 50 za wanyama wasio na uti wa mgongo, na aina laki moja na nusu za wadudu.

Kutokana na takwimu, kuna kiasi cha aina 476 za wanyama wenye uti wa mgogo wa nchi kavu nchini China ambazo ni kiasi cha 19.42% ya aina zote duniani. Panda wakubwa ni wanyama wanaopatikana nchini China peke yake na wanaweza kukua hadi kuwa na uzito wa kilo 135 kila mmoja, chakula chao ni majani na michipukizi ya mianzi, hivi sasa kuna 1000 tu, na kuwa alama ya hifadhi ya wanyama pori duniani. Kongwani anaweza kukua na kuwa na urefu wa mita 1.2, ana manyoya meupe na ngeu nyekundu kichwani. Katika Asia ya kusini mashariki ndege huyo ni dalili njema ya maisha marefu.

Wanyama wanaopatiakana zaidi katika sehemu za kaskazini-mashariki, kaskazini, mkoani Tibet, sehemu za kusini magharibi, katikati na kusini za China, kutokana na mazingira tofauti katika sehemu hizo aina za wanyama pia ni nyingi.


1 2 3 4 5