16: Hadithi za Mapokeo

Hadithi za Mithiolojia

Hadithi ya "Kupekecha Moto"

Zamani za kale, binadamu walikuwa hawakujua maana ya moto wala matumizi yake. Usiku ulipoingia, giza totoro lilifunika kila mahali, wanyama walikuwa wakinguruma huku na huko, watu wakijikunyata kwa hofu na baridi. Kwa sababu ya kutokuweko moto, iliwalazimu binadamu kula vyakula visivyopikwa, kwa hiyo mara kwa mara waliugua na umri wao wa kuishi ulikuwa mfupi.

Mbinguni alikukwako mungu mmoja mkubwa ambaye alijulikana kama Fu Yi. Alipoona jinsi maisha yalivyowawia vigumu binadamu, aliwahurumia sana, alitaka kuwafahamisha namna ya kutumia moto. Fu Yi kwa kudra yake alinyesha mvua kubwa ya radi kwenye msitu. Ka! Sauti kali ya kupasua masikio ilizagaa angani, papo hapo radi ilipiga na mti ukawaka, moto uliongezeka kuwa mkubwa. Watu walitishika vibaya, walikimbia ovyo. Muda si muda mvua ilisimama, usiku ulianguka, baridi ilikuwa kali zaidi baada ya mvua. Waliokimbia walirudi wakakusanyika pamoja wakiangalia moto ulivyowaka kwa nguvu. Wakati huo kijana mmoja alitanabahi kuwa hapo kabla wanyama walionekana huku na huko lakini sasa wametoweka kabisa, akafikiri, "Kwani wanyama wanaogopa kitu hiki kinachong'ara?" Kwa ujasiri akausogelea moto, akasikia joto, kwa furaha akawaita wenzake kwa kelele, "Ebu, njooni haraka, moto huu si kitu cha kuogopwa, kinatupatia joto na mwanga!" Wakati huo watu wengine waligundua wanyama walioungua kwa moto, harufu nzuri ya nyama iliyochomwa ilipenya puani. Watu walikusanyika karibu na moto, waligawana nyama, utamu wa chakula ambao hawakuwahi kuuonja uliwashangaza kweli, waliona moto ni kitu kizuri sana, hivyo wakaokota matawi ya miti wakayawasha na kila siku walipokezana kwa zamu kuuhifadhi moto huu ili usizimike. Lakini kwa bahati mbaya, siku moja mwenye zamu alipitiwa na usingizi, kuni zilikwisha na moto ukazimika. Watu wakaingia tena katika hali ya giza na baridi, maisha yakawaletea matatizo makubwa.

Mungu Fu Yi aliyaona yote yaliyowatokea, alijitokeza katika ndoto ya yule kijana aliyegundua moto, akamwambia, "Kutoka hapa upande wa magharibi, iko nchi moja inayoitwa Sui Ming Guo, huko utapata moto, nenda ukachukue moto na kuleta hapa." Kijana huyo alizinduka kutoka usingizini, alikumbuka wazi maneno aliyoambiwa ndotoni akashika njia ya kwenda kutafuta ule moto.

Kijana huyo alisafiri mbali, alipita milima, mito na misitu, alipata shida kubwa safarini, mwishowe alifika ile nchi ya Sui Ming Guo. Lakini huko hapakuwa na mwanga wa jua, bali giza liligubika kila mahali. Kuona hali hiyo kijana alikata tamaa, akajitupa kwenye mti mmoja kutweta kwa sababu ya uchovu. Ghafla mwanga ulimulika, aliona ndege kadhaa wakubwa wakubwa wakidonoa wadudu kwa midomo yao mifupi na migumu kwenye gogo la mti, kila walipogogota mwangaza hutatarika, lakini moto haukuwaka. Kuona jinsi cheche za moto zilivyotokea kichwa kilimduru, kisha kijana akatumia vijiti vidogo akijaribu kupekecha kwenye vijiti vinene, cheche zilitoka, lakini pia moto haukuwaka. Kijana hakukata tamaa, alijaribu kwa vijiti hivi na vile vya miti tofauti, mwishowe moshi ukaanza kufuka punde si punde moto ukawaka. Oo! Kijana akafurahi kweli kiasi cha kutokwa na machozi.

Kijana alirudi nyumbani, aliwaletea wenyeji ujuzi wa namna ya kupata moto, njia ya kupekecha. Tokea hapo binadamu wameachana na maisha yasiyo na nuru. Kutokana na uwerevu na ushupavu wake, binadamu wakamwita kijana huyo "Sui Ren", maana yake ni mtu aletaye moto.

Jinsi Wafalme wa Kale Walivyong'atuka katika China

Katika historia ndefu ya jamii ya umwinyi nchini China wafalme waliwarithisha watoto wao wa kiume viti vya enzi, lakini katika China ya kale, wafalme wa mwanzoni kabisa Yao na Shu hawakufanya hivyo bali waliwaachia viti vyao watu wasio na uhusiano wa kidamu. Yeyote aliyekuwa na maadili na uwezo alipendekezwa kuwa mrithi. Katika kipindi hiki nimewaletea masimulizi ya hadithi ya mfalme Yao jinsi alivyomrithisha enzi yake Shun.

Yao alikuwa mfalme wa kwanza katika China, alipozeeka alitaka kuchagua mrithi wake, siku moja aliwakusanya watemi wote kujadili mrithi wake.

Baada ya Yao kuelezea nia yake, mmoja wa watemi aitwaye Fang Qi alisema, "Mwanao Zhu Dan ni mtu mwenye fikra za kimaendeleo, anafaa kuwa mrithi wako." Kusikia hayo mfalme Yao alisema, "Hapana, huyo hana maadili mema, ana tabia ya kuzozana na watu." Kisha mwingine alisema, "Diwani anayesimamia hifadhi ya maji Gong Gong labda anafaa." Mfalme Yao alitikisa kichwa akisema, "Huyo ni hodari wa kuongea tu, mbele yako anakufurahisha kwa kukusifu lakini ana mengine moyoni mwake, sina imani naye." Majadiliano hayakuwa na matokeo, Yao aliendelea na kiti chake cha ufalme, lakini hakuacha kuendelea kutafuta mrithi wake.

Baada ya kipindi kirefu kupita, mfalme Yao aliwakusanya tena watemi kujadilia urithi wake. Kwenye majadiliano watemi kadhaa kwa kauli moja walimpendekeza kijana mmoja kabwela, Shun. Mfalme Yao aliinamisha kichwa na kusema, "Ndio, pia nimesikia habari zake, hebu nifahamishe zaidi jinsi alivyo?" Watemi waliongea mengi juu yake: Baba yake alikuwa mjinga wa mwisho, watu humwita mzee kipofu. Mama yake mzazi keshakufa zamani, mama yake wa kambo alimtendea vibaya Shun baada ya kumzaa mtoto wake Xiang. Xiang ni mtu mwenye kiburi, lakini mzee kipofu alimdekeza kupita kiasi. Ingawa Shun anaishi katika familia kama hiyo anawatendea vema baba na mama yake wa kambo na ndugu yake Xiang, hivyo majirani wanamsifu kwa maadili yake.

Baada ya kusikiliza maelezo yao, Yao alitaka kuhakikisha kwa kumpima zaidi. Aliwaozesha binti zake wawili E Huang na Nu Ying kwa Shun, akampatia ghala ya nafaka, akamgawia ng'ombe na mbuzi wengi. Mama yake wa kambo na ndugu yake Xiang walipoona mali hizi waliona husuda na wivu, basi wakishirikiana na baba yake walikula njama ya kumwua.

Siku moja baba yake alimwambia Shun atie kirago paa la ghala ya nafaka. Baada ya Shun kupanda paa baba yake aliwasha moto chini akitaka kumwunguza kwa moto. Shun alitaka kushuka haraka kwa ngazi, lakini ngazi ilikuwa imeondolewa, kwa bahati alivaa kofia kubwa ya ukili, aliitumia na kuruka chini kama parachuti, akaanguka bila kuumia.

Baba na ndugu yake Xiang hawakufa moyo, baadaye walimwambia Shun ashuke kisimani kuondoa matope, lakini aliposhuka tu baba yake na ndugu yake walitupa mawe wakitaka kumzika mule ndani, lakini hawakujua kuwa Shun angechimba pango pembeni akajipenyeza nje bila kuumia hata kidogo.

Xiang na baba yake walirudi nyumbani kwa furaha bila kujua kwamba Shun alikuwa amesalimika. Xiang alisema "Leo tumemfikisha kaka yangu ahera, ujanja huu ni mimi nilioubuni. Haya, sasa tugawane mali zake." Kisha akaendea chumba cha kaka yake, lakini alipoingia chumbani alimwona kaka yake akicheza kinanda kitandani. Alishituka, lakini baada ya kutuliza moto kwa haya alisema, "Ah, kaka yangu mpenzi nakukumbuka sana."

Shun alijitia hamnazo, akasema, "umekuja wakati mzuri, shughuli zangu ni nyingi naomba unisaidie." Shun aliendelea kuwatendea vema baba na mama yake wa kambo na ndugu yake. Tokea hapo baba na ndugu yake hawakuthubutu tena kumwua kwa hila.

Baadaye mfalme Yao aliendelea kumpima kwa mambo mengi, akabainika kuwa Shun kweli ni mtu mwenye maadili na uwezo mkubwa, akaamua kumwachia kiti cha enzi yake.

Baada ya Shun kuwa mfalme, maisha yake yalikuwa kama ya raia, hakuacha kazi za mikono, akapata imani na heshima ya raia wake. Baada ya miaka kadhaa Yao alifariki, wakati huo Shun alitaka kumtawaza mtoto wa Yao, Zhu Dan, lakini watemi hawakukubali. Shun alipozeeka alitumia njia hiyo hiyo kuchagua mrithi wake Yu kwa maadili na uwezo. Lakini Yu alipozeeka alimwachia kiti chake cha ufalme mtoto wake wa kiume Qi. Tokea hapo kiti cha ufalme kikawa kinarithiwa na mtoto wa kiume wa mfalme kizazi hadi kizadi katika jamii ya umwinyi yenye historia ya miaka elfu kadha nchini China.

Katika enzi za Yao, Shun na Yu jamii ilikuwa tulivu bila ya mapambano ya kuwania maslahi ya kibinafsi wala madaraka ya utawala, wafalme walikuwa sawa na raia wakiishi maisha ya kawaida.

Hadithi kuhusu Milima Mitano ya Ajabu

Baada ya malaika Nu Wa kuumba binadamu (hadithi yake tuliwahi kueleza katika kipindi kilichopita), dunia ilikuwa na utulivu kwa kipindi kirefu. Lakini siku moja ghafla mbingu na ardhi ziligongana kwa nguvu, mbingu ikapasuka na ardhi ikadidimia huku moto mkubwa ukitoka ardhini na kunguza misitu; mafuriko makubwa ya maji yaliporomosha milima, mashetani, vibwengo na wanyama wakali walitumia nafasi hii kufanya mambo maovu watakavyo, binadamu walizama kwenye bahari ya misiba.

Nu Wa alisikia kilio cha binadamu, kwanza aliwaua wale mashetani na vibwengo na wanyama wote wabaya, kisha akatuliza maji, baada ya yote hayo kufanyika alianza kazi yake kubwa ya kuziba ufa uliotokea mbinguni.

Nu Wa alikusanya majani na kuni na kurundika rundo kubwa kiasi cha kufikia mbinguni, kisha akatafuta mawe yaliyokuwa na rangi ya samawati sawa na ya mbingu, lakini kwa kuwa duniani hakukuwepo mawe hayo mengi aliyotaka, hivyo ilimpasa akusanye mawe mengine meupe, njano, mekundu na meusi na kuyaweka juu ya lile rundo. Alichukua moto uliokuwa karibu kuzimika akawasha mti mmoja mkubwa na kuwasha rundo lake la majani. Moto uliwaka zaidi na zaidi ukaangaza ulimwengu mzima, na mawe yenye rangi tano yalichomwa yakawa mekundu. Baada ya muda yakaanza kuyenyuka na kuwa kama uji ambao ulitiririka na ukaziba ule ufa wa mbingu. Baadaye moto kwenye rundo ulizimika, na ufa ukawa umezibika tayari.

Ingawa mbingu ilikuwa imekamilika lakini haikuwa kama ya awali. Sehemu ya kaskazini-magharibi iliinama kidogo, kwa hiyo jua na mwezi huendea huko; ardhi, sehemu ya kusini-mashariki ilididimia, kwa hiyo mito na vijito hutiririkia huko, maji yaliyokusanyika huko miaka nenda miaka rudi yakawa bahari.

Katika upande wa mashariki ya bahari lilikuwako bonde moja kubwa ambalo kina chake kilikuwa kirefu kiasi cha kutoweza kuona mwisho wake. Bonde hilo linajulikana kama Gui Xu na maji ya mito na ya bahari yanaingia kwenye bonde hilo, lakini kiwango cha maji ni kile kile wala hakiongezeki kuwa mafuriko kiasi cha kuwaletea watu maafa.

Ndani ya bonde la Gui Xu kuna milima mitano ya ajabu, nayo ni Dai Yu, Yuan Qiao, Fang Hu, Ying Zhou na Peng Lai. Kila mmoja ulikuwa na urefu wa kilomita elfu kumi na ulitengana kwa kilomita elfu ishirini. Mlimani kuna kasri iliyojengwa kwa dhahabu na marumaru ambako miungu mingi waliishi.

Mlimani, ndege wote walikuwa weupe, miti ilikuwa mingi na ya ajabu, matunda ya miti hiyo yalikuwa kama lulu na vito, ladha tamu sana, watu wa kawaida wakila wataishi milele bila kuzeeka. Miungu walivaa mavazi meupe pia na wana mabawa madogo meupe mgongoni, waliruka huku na huko kati ya milima kuwatembelea marafiki na jamaa zao chini ya mbingu iliyotakata, maisha yao yalikuwa ya furaha bila kifani.

Hata hivyo, furaha yao haikuwa imekamilika. Sababu ni kuwa milima hiyo mitano haikuwa na mizizi bali ilielea baharini, kwa hiyo upepo mkubwa ukivuma milima hiyo huenda mrama na kuelea bila ya kutulia sehemu maalumu. Hali hiyo ilitia doa katika furaha yao. Kwa hiyo miungu walichagua mjumbe mmoja kwenda peponi kueleza usumbufu huo. Baada ya kufahamishwa, mungu wa peponi pia alipata wasiwasi kwamba milima hiyo mitano ingeelea mbali na kutoweka, miungu hiyo wangepoteza maskani yao, basi akaamrisha mungu wa bahari "Yu Qiang" atume kasa wakubwa kumi na tano waende huko kubeba milima hiyo mitano mgongoni.

Kila mlima ulibebwa na kasa mmoja huku wengine wawili wakisubiri zamu yao ambapo watabadilishana kila baada ya miaka elfu sitini. Kwa kufanya hivyo milima ikatulia tuli, miungu yote milimani wakaingiwa na furaha.

Bila kutegemewa, mwaka fulani, jitu moja kutoka "Dola ya Majitu" alikuja kwenye bonde la Gui Xu kuvua samaki kwa mshipi, mwili wake ulikuwa mkubwa kama mlima. Muda si mrefu alivua kasa sita waliokuwa wamebeba milima miwili. Lakini jitu hakuwa na habari, alibeba kasa hao mgongoni akarudi nyumbani. Milima hiyo miwili, Dai Yu na Yuan Qiao, bila ya kubebwa na kasa ilielea elea hadi nchi ya kaskazini ya dunia kwa kusukumwa na upepo na kuzama huko baharini. Miungu walioishi katika milima hiyo miwili waliruka ruka angani kwa mahangaiko wakiwa na mali zao na kulowa na majasho.

Kusikia habari hiyo mungu wa mbinguni akacharuka, mara akamfupisha yule jitu wa "Dola ya Majitu" asije akaleta matata mengine. Milima mitatu iliyobaki ilikuwa salama kwa kuwa inaendelea kubebwa na kasa mpaka leo kwenye ufukwe wa mashariki ya China.

Pan Gu Aumba Mbingu na Ardhi

Kama tujuavyo, kila taifa lina hadithi nyingi za mapokeo, visasili na aina nyingi nyingine, hadithi hizo ni msingi mojawapo wa utamaduni wa taifa. Leo basi, katika kipindi hiki nimewaletea hadithi moja ya kubuniwa, ijulikanayo kama "Pan Gu Aumba Mbingu na Ardhi".

Inasemekana kwamba zamani za kale ulimwengu ulikuwa kama yai kubwa, na ndani yake yalikuwa machafuko matupu, giza totoro, kulikuwa hakuna juu wala chini, hakuna mashariki, magharibi wala kaskazini na kusini. Lakini ndani yake lilimlea shujaa mmoja aliyeumba mbingu na ardhi: Pan Gu. Pan Gu alilelewa ndani ya yai hilo kwa miaka elfu kumi na nane, mwishowe alizinduka kutoka usingizini. Alifumbua macho lakini hakuweza kuona chochote kwa ajili ya giza tupu, alikuwa hawezi kuvumilia kwa sababu ya joto kali mule ndani, alitaka kusimama lakini alibanwa na gamba la yai hata asiweze kunyoosha miguu. Kutokana na hali hiyo ngumu Pan Gu alikasirika, akachukua shoka alilozaliwa nalo, akalivumisha kwa nguvu, sauti kali ikarindima, yai likapasuka. Yale yaliyokuwa mepesi na safi ndani ya yai hilo yakaelea juu na juu kukawa mbingu na yale yaliyokuwa mazito na machafu yakazama chini na chini kukawa ardhi.

Pan Gu alifurahi mno kwa kufanikiwa kuumba mbingu na ardhi, lakini alihofia mbingu na ardhi zingeungana baadaye. Basi akatumia kichwa kuhimili mbingu na kutumia miguu kukanyaga ardhi huku akionyesha uwezo wake wa ajabu: Kila siku alikua kimo cha mita tatu, hivyo mbingu ikawa juu mita tatu, na ardhi ikaongeza maki mita tatu. Vivyo hivyo muda ukapita miaka elfu kumi na nane. Pan Gu akawa pandikizi la mtu ambaye kichwa chake kiligusa mbingu na miguu yake ilikanyaga ardhi, kimo chake kilikuwa kilomita elfu 500. Haijulikani kama maelfu mangapi ya miaka yalipita, mbingu na ardhi ikatulia tuli bila ya kuweza kuungana pamoja, wakati huo ndipo Pan Gu alitulia moyo, lakini alikuwa amechoka sana, akafa.

Baada ya Pan Gu kufariki, maiti yake ilibadilika kiajabu: Jicho lake la kushoto likawa jua jekundu, la kulia likawa mwezi, pumzi yake ya mwisho ikawa upepo na mawingu, sauti yake ya mwisho ikawa mngurumo wa radi, nywele na ndevu zake zikawa nyota, kichwa, mikono na miguu yake ikawa milima, damu yake ikawa mito na maziwa, mishipa ikawa njia, misuli ikawa ardhi yenye rutuba, ngozi na malaika yakawa mimea na miti, meno na mifupa ikawa madini na jasho lake likawa mvua na umande. Kuanzia hapo ikatokea dunia.

Hapo awali baada ya Pan Gu kuumba mbingu na ardhi, humu duniani hapakuwa na binadamu. Siku moja malaika mmoja ajulikanaye kama Nu Wa alishuka duniani, aliona dunia ilikuwa na kimya bila uchangamfu wa viumbehai. Alikwenda kwenye ukingo wa mto akachota maji kwa mikono kutaka kunywa, wakati huo akaona sura yake majini, mara akatumia udongo na maji kufinyanga finyanga sanamu kwa mujibu wa sura yake, kisha akaipuliza sanamu na sanamu ikawa mtoto wa kike, aliendelea kufinyanga sanamu nyingine na ikawa mwenzi wa mtoto wa kike, na huyo alikuwa mwanamume wa kwanza duniani. Malaika Nu Wa alifurahi sana, basi akaanza kufinyanga finyanga akitaka binadamu wajae duniani. Lakini dunia ni kubwa mno hakuweza kutimiza nia yake kwa muda mfupi. Wakati huo huo akapata ujanja, akachukua tawi la mti na kulitia mtoni kukorogakoroga, matope yakanasa kwenye tawi la mti, kisha akalikung'uta, matone ya matope yakasambaa ardhini na yakawa watu wadogo wadogo, wanaume na wanawake wakichanganyikana. Muda si muda dunia ikajaa binadamu. Lakini tatizo lingine likatokea, Nu Wa alifikiri, watu hao mwishowe watakufa, itampasa afinyange tena, kazi ya ufinyanzi itamsumbua. Kufikiri hivyo aliwaita watu wote mbele yake, akawaambia wazaliane wenyewe, basi binadamu wakaanza kubeba jukumu la kuzaa. Tokea hapo binadamu wakawa wanazaliana kizazi baada ya kizazi.

Hadithi ya Nuwa Aumba Binadamu

Katika hekaya za kale, kuna hekaya ya jinsi Nuwa alivyoumba binadamu. Nuwa alikuwa ni mungu wa kike mwenye mwili wa binadamu na kichwa cha dragoni.

Inasemekana kuwa baada ya Pangu kutenganisha mbingu na ardhi, Nuwa alitembelea duniani huku na huko, wakati huo duniani kulikuwa na majani, ndege, wanyama na samaki, lakini ilikuwa kimya kabisa kwa sababu kulikuwa hakuna binadamu. Siku moja alipotembea alihisi upweke, aliona ni afadhali aongeze viumbe vyenye sauti na uchangamfu.

Alipoona majani, maua, ndege na samaki, lakini aliona haitoshi, lazima avumbe viumbe vyenye akili nyingi zaidi.

Alipofika kando na mto wa Huanghe, mbele ya maji alijionea sura yake, alifurahi. Aliamua kutumia udongo kufinyanga sura kama yake na aliongeza miguu miwili, kisha alipuliza pumzi sanamu aliyofinyanga, basi sanamu hiyo ikawa na uhai, Nuwa aliita sanamu hiyo kuwa ni binadamu, na ili kutofautisha wanaume na wanawake alipuliza tena. Basi wanawake na wanaume walimzunguka kumshangilia kwa furaha.

Nuwa alitaka kuumba binadamu wengi, basi alifikiri njia moja ya kuwa alitia kamba ndani ya matope kisha akarusha kamba hiyo na kusambaza matope kila mahali, na kina tone la matope likawa mtu mdogo, kwa njia hiyo aliumba watu wengi. Ingawa duniani kulikuwa na binadamu lakini binadamu waliwezaje kuishi? Na binadamu ana miaka ya kuishi, watawezaje kuendelea? Basi aliwaunganisha wanaume na wanawake kuwa mume na mke. Kwa njia hiyo binadamu wanaendelea kuwepo duniani kizazi kwa kizazi na idadi ya watu inaongezeka.

Hadithi ya Kabwela Niu Lang na Malaika Zhi Nu

Niu Lang alikuwa mseja maskini, aliishi kwa kumtegemea tu ng'ombe mmoja na plau moja. Kila siku Niu Lang alitoka nyumbani alfajiri mapema kwenda kulima shambani na kurudi machweo akiwa hoi; aidha ilimpasa ajifulie nguo na kujipikia chakula. Maisha yalimwia vigumu sana. Lakini siku moja alitokewa na miujiza.

Kutokana na uchovu, Niu Lang alijikokota hadi nyumbani baada ya kazi ngumu shambani. Alipoingia chumbani alipatwa na mshangao: Chumba kilikuwa safi sana, nguo zilikuwa zimefuliwa tayari, chakula kitamu kilikuwa mezani kikiwa bado moto moto. Niu Lang alikodolea macho yote hayo, akiwaza: Vipi mambo haya? Kwani malaika ameshuka kutoka mbinguni?

Tokea hapo, hali ilikuwa vivyo hivyo katika siku kadhaa mfululizo. Niu Lang alitaka kujua sababu yenyewe. Basi siku moja, kama kawaida yake alitoka nyumbani mapema, lakini hakwenda shambani, bali alijificha sehemu jirani na nyumbani huku akikaza macho kuvizia.

Muda si muda alikuja msichana mmoja mrembo, akaanza kushughulika baada ya kuingia chumbani. Wakati huo Niu Lang alishindwa kujizuia, akakimbilia chumbani na kusimama mbele yake, akamwuliza: "Ewe msichana kwa nini umekuja nyumbani kwangu kunishughulikia?" Kusikia sauti hiyo msichana alishituka, akajibu kwa sauti ndogo kama ya mnong'ono huku uso ukiwa umemwiva: "Naitwa Zhi Nu, naona umepata shida sana katika maisha yako, nimekuja kukusaidia." Niu Lang akafurahi sana, akajikakamua na kusema, "Tuoane basi, tuishi na kufanya kazi pamoja." Zhi Nu akakubali. Niu Lang na Zhi Nu wakafunga pingu za maisha. Niu Lang alikwenda kulima kila siku na Zhi Nu alishughulika na kazi za nyumbani na kufuma nguo. Maisha yalikuwa ya kufurahisha.

Baada ya miaka kadhaa kupita, walijaliwa watoto wawili, wa kiume na wa kike, na hivyo furaha ilitawala familia hiyo.

Lakini siku moja ghafla mawingu mazito yalitanda mbinguni, kimbunga kilivuma kwa nguvu, na askari wawili wa mbinguni wakashuka kwenye nyumba. Niu Lang akaambiwa kwamba Zhi Nu alikuwa mjukuu wa mungu, amekuwa akitafutwa kwa miaka kadhaa iliyopita. Askari walimrudisha Zhi Nu mbinguni kwa nguvu.

Niu Lang akiwa na watoto wawili kifuani alibaki kumwangalia mkewe akichukuliwa na askari wawili kurudi mbinguni, alihuzunika sana, lakini aliapa kwamba atakwenda mbinguni kumchukua mkewe Zhi Nu ili kukamilisha familia yake. Lakini binadamu atawezaje kufika mbinguni?

Niu Lang alipoishiwa na ujanja, ng'ombe wake mzee alimwambia, "Nichinje mimi na kujifunika ngozi yangu mgongoni; kwa namna hiyo utaweza kuruka kwenda mbinguni." Niu Lang kamwe hakukubali, lakini ng'ombe aling'ang'ania. Kwa kuona hana njia nyingine Niu Lang alimchinja huku akilia.

Niu Lang alijifunika kwa ngozi ya ng'ombe, akawabeba watoto wawili kwa mzegazega, mmoja mbele, mmoja nyuma, akaruka kwenda mbinguni. Lakini huko kwenye kasri ya mbinguni watu waligawanyika kwa matabaka, hakuna yeyote aliyemheshimu kabwela maskini na hohe hahe kama Niu Lang. Mungu alimkatalia ombi lake la kuonana na mkewe Zhi Nu.

Niu Lang na watoto wake walimsihi sana, mwishowe aliruhusiwa kumwona mkewe kwa muda mfupi. Mkewe Zhi Nu aliyekuwa amefungwa alipowaona mumewe na watoto wake alijawa na furaha na huzuni. Kufumba na kufumbua muda ukapita, mungu akaamuru kuondolewa kwa Zhi Nu. Maskini Niu Lang na watoto wake walimkimbilia kadri wawezavyo huku wakianguka anguka na kuinuka. Mwishowe walipomkaribia, mke wa mungu alichomoa kibanio cha nywele akachora mstari angani, na mara mto wa kilimia ukatokea kati yao. Tokea hapo Niu Lang na Zhi Nu wakawa wametenganishwa na mto huo, isipokuwa tu kila tarehe 7 ya mwezi wa 7 wanaruhusiwa kukutana. Kila wakati siku hiyo ilipowadia, ndege wasio na idadi waliungana pamoja na kuwa kama daraja juu ya mto huo ili Niu Lang na Zhi Nu wakutane.

Kua Fu Afuata Jua

Zamani za kale, katika sehemu ya kaskazini kulikuwako mlima mmoja mrefu uliofikia hadi mawinguni, na huko mlimani kwenye msitu mnene, liliishi kundi kubwa la majitu, ambapo mtemi wao alijulikana kama Kua Fu alikuwa na nyoka mmoja kwenye kila sikioni na wengine wawili mikononi. Kutokana na jina lake pia kabila lake lilijulikana kama kabila la Wakuafu. Watu wa kabila la Wakuafu walikuwa na roho nzuri, wenye bidii za kazi na waliishi kwa amani na utulivu.

Mwaka fulani hali ya hewa ilikuwa joto sana, jua la utosini liliwaka na ardhi ilikuwa joto kiasi cha miti kuungua na mito yote kukauka. Watu wengi walikufa kutokana na joto. Mtemi Kua Fu alihuzunika sana, na siku moja akawaambia watu wake huku akiangalia jua, "Jua hili ni baya sana! Ni lazima nilifuate na kuliamrisha." Watu wake waliposikia kauli hiyo baadhi walimwasa "Halahala usiende, jua liko mbali sana nasi, utakufa kutokana na safari ndefu." Wengine walisema "Jua lina moto mkali, utakaushwa kabla ya kulifikia." Lakini Kua Fu hakuwasikiliza. Aliwaambia watu wake waliokuwa wakisononeka sana, "Ili mweze kupata raha na utulivu wa maisha, ninapaswa kulifuata!"

Kua Fu alianza safari yake baada ya kuagana na watu wake. Alipiga hatua kubwa kubwa na kwa haraka kama upepo. Alipita kwenye milima na milima, mito na mito, huku vishindo vya miguu vilitetemesha ardhi. Katika safarini yake mchanga aliokung'uta kutoka kwenye viatu vyaake ulibadilika kuwa mlima. Mafiga matatu ya kujinjika sufuria alipokuwa akipika chakula yalibadilika kuwa milima mirefu mitatu iliyochongoka.

Kua Fu aliendelea kufuata jua, huku akilikaribia zaidi na zaidi, na hivyo kuwa na imani. Alihisi joto kali zaidi na zaidi, na mwishowe alifikia kwenye sehemu jua lilipozama. Jua lililokuwa kama tufe jekundu la moto lilitoa miali inayouumiza macho. Kua Fu alifurahi sana kiasi cha kutaka kulikumbatia kifuani, lakini kutokana na joto hakuweza, aliona kiu kali na uchofu mkubwa. Alikimbilia kwenye mto Huang He huku akigugumia na kumaliza maji yote, kisha akakimbilia kwenye mto Wei He, akayamaliza tena maji yote ya mtoni, lakini hakukata kiu basi akakimbilia kwenye ziwa kubwa lililoko kwenye sehemu ya kaskazini, lakini akafa kwa kiu kabla hakulifikia.

Kabla ya kufa alisikitika sana alipowakumbuka watu wake jinsi walivyosononeka. Alitupa mkongojo wake, na pale ulipoangukia pakawa msitu mkubwa. Msitu huo uliwaleta mazingira mazuri ya kuishi yenye ubaridi yasiyo na miali mikali ya jua ambapo wasafiri hupumzika huko wakati wakiwa safarini.

"Kua Fu Afuata Jua" ni hadithi inayoonyesha watu wa kale walivyotamani kupambana na kiangazi. Ingawa Kua Fu alikufa lakini moyo wake wa kuwaondolea watu usumbufu na kuwaletea hali nzuri ya maisha utaishi daima. Katika vitabu vyingi vya siku za kale, yako makala mengi kuhusu hadithi hiyo, pia upo mlima wa kumbukumbu uliopewa jina la "Mlima wa Kua Fu".

Huangdi Apambana na Chiyou

Miaka elfu kadhaa iliyopita, kwenye bonde la Mto wa Huanghe yalikuwepo makabila mawili, watemi wa makabila hayo waliitwa Huangdi na Yandi, watemi hao wawili ni ndugu. Wakati huo alikuwepo mtemi mmoja wa kabila lililoko kwenye bonde la Mto wa Changjiang, aliyeitwa Chi You.

Mara kwa mara Chi You alikuwa anawaongoza watu wake kushambulia makabila mengine.

Siku moja Chi You alishambulia sehemu ya Yandi, ingawa Yandi alipigana naye kwa nguvu zote, lakini hakufui dafu. Yandi alimkimbilia Huangdi kuomba msaada. Huangdi alishirikisha makabila mengine kupambana na Chi You.

Mwanzoni, kutokana na kuwa na silaha nzuri Chi You alipata ushindi kwa urahisi. Huangdi aliwaalika wanyama wakali kushiriki katika vita. Chi You alishindwa vibaya na kukimbia.

Huangdi alimfukuza, njiani giza liliingia na upepo mkali ulianza kuvuma, mvua ya radi ilikuwa kubwa. Huangdi alishindwa umfukuza. Hiyo ilitokana na kuwa Chi You aliialika miungu ya upepo na mvua kumsaidia. Wakati huo Huangdi aliialika miungu ya kiangazi, ghafla upepo ulitulia na mvua ilisimama.

Hatimaye Chi You alitumia uganga kuleta ukungu mnene ili Huangdi apotee njia, lakini Huangdi alitumia nyota ya kaskazini kuelekeza njia yake.

Baada ya mapambano marefu, Huangdi aliwaua ndugu 81 wa Chi You na kumkamata Chi You akiwa hai. Ili Chi You asilete matata, Huangdi alikata mwili kwa sehemu mbili, na kuzizika sehemu hizo katika mahali tofauti ili zisiunganike na kufufuka tena.

Baada ya Chi You kuuawa, Huangdi alichora picha yake kwenye bendera ya kijeshi ili kuwatia moyo askari wake.

Huangdi alikuwa na elimu nyingi, aliwahi kubuni zana nyingi kama mikokoteni, mashua na nguo yenye rangi tano. Mke wa Huangdi alikuwa pia ni mvumbuzi. Aliwafunza namna ya kufuga funza wa hariri na kutengeneza kitambaa cha hariri, na alivumbua kibanda kinachoweza kuchukuliwa yaani mwanvuli.

Watu wa China ya kale walimheshimu sana Huangdi, na watu wa China wanaona Huangdi na Yandi ni mababu wa Wachina, wanasema wao ni wazawa wa Yan na Huang. Wachina walijenga kaburi la Huangdi, na kila mwaka katika majir ya Spring Wachina kutoka sehemu mbalimbali duniani wanakwenda kufanya tambiko mbele ya kaburi hilo.

Houyi Atungua Majua

Katika zama za kale, mbinguni kulikuwa na majua kumi. Mwangaza mkali ulikausha mimea yote, na watu walikuwa na shida ya kupumua na hata kuzirai. Kutokana na joto kali wanyama wakali walitoka kutoka kwenye mito na maziwa yaliyokauka, na misitu.

Msiba wa binadamu ulimfanya mungu kuwahurumia binadamu, alimwamuru mpiga mishale hodari Houyi kuwaokoa binadamu. Houyi alipewa na mungu upinde mwekundu na mishale myeupe, alishuka duniani akiwa pamoja na mkewe Chang E.

Houyi alishawishi majua kumi yajitokeze moja moja kwa zamu, lakini majua yalikuwa hayasikii. Houyi alikasirika, alianza kupiga mishale, muda si mrefu alitungua majua tisa na kuliacha moja mbinguni. Hivyo binadamu walianza kuishi kwa usalama.

Mchango wa Houyi uliwafanya miungu mingine waone wivu, wakaenda kwa mungu mkuu kumsemea vibaya, mungu huyo alitengana na Houyi na kuamua kuwatenganisha yeye na mkewe na kuwabakiza duniani daima. Houyi aliyeonewa aliishi na mkewe duniani na kuishi kwa kuwinda.

Jinsi muda ulivyopita, Houyi alizidi kusikia vibaya kumkosea mkewe aliyeshushwa duniani kwa sababu yake mwenyewe. Baadaye alisikia kwamba huko kwenye mlima wa Kunlun kuna dawa ya miti shamba ya ajabu, mtu akila dawa hiyo ataruka mbinguni. Houyi alisafiri mbali hadi kwenye mlima huo na mwishowe alipata dawa hiyo. Jambo linalosikitisha ni kwamba dawa hiyo inaweza tu kutumiwa na mtu moja. Houyi alikuwa hataki kuachana na mkewe, alificha dawa hiyo.

Chang E alishindwa kuvumilia maisha magumu duniani. Siku moja alichukua fursa ambayo Houyi alikuwa hayupo nyumbani, alikula dawa hiyo. Mara aliona mwili wake ukaanza kuwa mwepesi na kisha akapaa mbinguni hadi mwezini. Houyi aligundua mke wake alirudi mbinguni alihuzunika sana lakini hakutaka kumpigia mshale, hivyo alikubali kuishi peke yake duniani.

Houyi aliendelea kuishi kwa kuwinda, aliwapokea wanafunzi kadhaa kuwafundisha kupiga mishale. Kati ya wanafunzi, mmoja aliyeitwa Pengmeng alipata maendeleo ya haraka, lakini aliona kuwa daima atakuwa hodari wa pili kama Houyi akikuwepo. Siku moja mwanafunzi huyo alitumia fursa ya Houyi kulewa alimwua Houyi kwa mshale. Baada ya kufika mwezini Chang E aliishi peke yake pamoja na sungura mmoja mweupe na mti mmoja mkubwa, kila siku alikuwa anakumbuka maisha akiwa pamoja na mume wake duniani, lakini hakuwa na njia ila kukaa upweke mwezini.

Chang E Arukia Mwezini

Tarehe 15 mwezi Agosti kwa kalenda ya Kichina ni sikukuu ya mwezi. Sikukuu hiyo ni mila ya Wachina yenye historia ndefu. Katika siku hiyo jamaa wa familia moja hujikusanya pamoja kula keki za mwezi na kuburudika na mwezi mpevu. Sikukuu hiyo ilitokana na hadithi ya "Chang E Arukia Mwezini".

Chang E alikuwa mungu wa mwezi, mume wake Houyi alikuwa hodari wa kupiga mishale. Mwaka mmoja duniani ulitokea msiba mkubwa duniani, wanyama wakali walitoka majini na misituni kuwashambulia binadamu. Mungu mkuu alipofahamu hali hiyo alimtuma Houyi ashuke duniani akiwa na mkewe Chang E. Aliwaua wanyama wakali lakini wakati huo mbinguni kulitokea majua kumi, joto kali lilikausha mimea yote, mito ilikauka, misitu iliwaka moto na watu wengi walikufa.

Houyi alishawishi majua kumi yatokee moja moja kwa zamu, lakini yalikuwa hayasikii. Kwa kukasirika, Houyi alitungua majua tisa na kubakiza moja mbinguni.

Kutokana na wivu Houyi alisingiziwa na miungu mingine mbele ya mungu mkuu, basi mungu mkuu alimwadhibu Houyi abaki duniani pamoja na mkewe. Lakini mke wa Houyi alishindwa kuishi maisha magumu duniani.

Houyi alisikia kwamba kuna dawa ya ajabu kwenye mlima wa Kunlun, mtu akila dawa hiyo ataweza kuruka mbinguni. Houyi alisafiri mbali kwa shida, na mwishowe aliipata dawa hiyo. Lakini dawa hiyo inaweza kutumiwa na mtu mmoja tu, kutokana na kutotaka kuachana na mke wake Chang E, Houyi alificha dawa hiyo.

Katika tarehe 15 Agosti Chang E alitumia fursa ya mume wake kutokuwepo nyumbani alikula dawa hiyo na mara akapaa mbinguni hadi mwezini.

Houyi aliishi duniani kwa kuwinda, aliwapokea wanafunzi kadhaa kuwafundisha upigaji mishale. Kati ya wanafunzi hao alikuwako mmoja aliyeitwa Peng Meng, alipata maendeleo makubwa katika upigaji mishale. Mwanafunzi alifikiri kuwa kama Houyi akiwa hai basi yeye daima atakuwa wa pili katika upigaji mishale, basi alitumia fursa ya Houyi kulewa alimwua Houyi. Chang E aliishi peke yake mwezini ila tu sungura mmoja mweupe na mti mmoja mkubwa, alimkumbuka mumewe hasa katika siku ya tarehe 15 mwezi Agosti.

Gun na Dayu Wadhibiti Maji

Nchini China "hadithi ya Dayu kudhibiti maji" ni maarufu kwa wote, lakini sio wengi wanaojua kuwa baba yake Gun naye pia ni shujaa wa kudhibiti maji. Leo katika kipindi hiki nitawajulisheni hadithi ya watu hao wawili, baba na mwana walivyodhibiti maji.

Katika siku za kale China ilikumbwa na mafuriko kwa muda wa miaka 22, ardhi ilikuwa bahari tupu, mimea yote ilizama ndani ya maji, watu hawakuwa na sehemu ya kukaa, hawakuwa na tegemeo lolote katika maisha, na idadi yao ikapungua haraka. Hali hiyo ilimfadhaisha sana mfalme Yao. siku moja aliwakusanya watemi wote kujadiliana na mwishowe alimwagiza Gun kudhibiti maji.

Baada ya kupewa jukumu hilo, Gun alitafakari sana, kwa bahati akakumbuka usemi mmoja wa wenyeji, kwamba "Wavamizi wakija wadhibitiwe na jemadari, na maji yakija yakingwe kwa udongo". Akapata wazo kuwa kama kijiji kikizungushiwa boma si maji yatabaki nje? Lakini ardhi yote ilikuwa imejaa maji, angewezaje kupata udongo? Wakati huo kobe moja aliibuka akamwambia Gun: "Nyumbani kwa mungu kuna kitu kimoja kiitwacho 'Xi Rang', ukikipata na kukitupa majini kitakua na kuwa boma na mlima." Baada ya kusikia hayo Gun alifurahi mno, akamuaga kobe na kuanza safari yake.

Gun alitaabika sana katika safari yake ndefu, lakini mwishowe alifika nyumbani kwa mungu. Alimsihi mungu ampe kile kitu kiitwacho "Xi Rang" akitumie kudhibiti maji ili kuwaokoa wananchi. Lakini mungu alikataa. Kutokana na jinsi alivyowakumbuka wananchi walivyohatarishwa na maafa ya mafuriko ya maji, Gun alitumia fursa ya uzembe wa walinzi na kuiba kile "Xi Rang" na kurudi nacho nyumbani. Akakitupa "Xi Rang" majini, kweli kikakua haraka, maji yakipanda juu nacho kikakua zaidi, maji yakazuiliwa nje ya boma. Watu walifurahi huku wakirukaruka, wakaanza kulima mashamba.

Lakini baadaye mungu aligundua kwamba "Xi Rang" kimeibwa. Akawatuma askari wake mara moja kukirudisha. Maji yakajaa tena, boma likaporomoka, mashamba yakazama, na watu wengi wakafa maji. Mfalme Yao alikasirika sana, akasema, "Gun anajua tu kujenga boma kuzuia maji, na boma linapoporomoka maji yanakuwa mengi zaidi. Amejaribu kudhibiti maji kwa miaka 9 lakini hakufanikiwa chochote, anastahili kuuawa!" Gun akatiwa gerezani, na baada ya miaka mitatu aliuawa akiwa na hasira ya kuonewa.

Baada ya miaka 20, mfalme Yao alimrithisha Shun kiti cha enzi yake, mfalme Shun alimtuma mtoto wa kwanza wa Gun, Da Yu, kwenda kudhibiti maji, ambapo mungu alikubali kumpa Da Yu kitu chake "Xi Rang". Mwanzoni Da Yu pia alidhibiti maji kama alivyofanya baba yake, lakini kila baada ya kujenga boma lake mara lilibomolewa na maji makubwa, baada ya majaribio ya mara nyingi akatambua kuwa, "Kuzuia tu maji hakutoshi, lazima yazuiliwe katika sehemu inapofaa na kutoka kwenye sehemu inayohitajika."

Da Yu alipanda mgongoni kobe mkubwa akiwa na "Xi Rang" huku akielea huku na huko, ambapo alitumia "Xi Rang" kwenye sehemu iliyodidimia na sehemu ilipokaliwa na watu, pia alichimba mito kupeleka maji baharini. Inasemekana kuwa, Da Yu kwa kudura ya mungu alipasua na kukata kata milima ili maji yapite, hivyo yakapatikana magenge matatu ya San Menxia ya leo. Tokea hapo kwa zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, magenge matatu ya San Menxia yamekuwa yakivutia watalii kwa maji yake yanayokwenda kwa kasi kubwa.

Hadithi simulizi kuhusu Da Yu ni nyingi, watu wanasema, Da Yu alimwacha mkewe siku nne tu baada ya kumwoa kwenda kudhibiti maji, na katika muda wake wa miaka 13 wa kudhibiti maji alipita nje ya nyumbani kwake mara tatu lakini hakuingia. Kwa juhudi zake za kupambana na matatizo mengi, mwishowe alifanikiwa kudhibiti maji, wananchi wakaanza kuishi bila wasiwasi. Kama shukrani, wananchi walimwunga mkono awe mfalme, na mfalme Shun alimwachia kiti chake kwa hiari kutokana na mafanikio yake makubwa.

Katika jamii ya kale, uwezo wa binadamu ulikuwa dhaifu sana. Binadamu wanapopambana na maafa ya maumbile pia walitunga hadithi nyingi za ajabu ajabu kuonyesha matumaini yao. Gun na Da Yu ni mashujaa walioumbwa na watu katika mapambano dhidi ya maafa ya mafuriko, na ndani ya hadithi, shida walizopata mashujaa pia ni matatizo yanayowakabili wanapopambana na mafuriko. Mwishowe watu wametambua kuwa kudhibiti maji lazima watumie njia mbili kwa pamoja, yaani "kuzuia na kutoa".

Hadithi ya Msichana Hou Ji na Mazao Yake

Ustaarabu wa China ya kale ni wa kilimo, kwa hiyo, yapo masimulizi mengi yanayohusiana na shughuli za kilimo. Leo katika kipindi hiki nimewaletea "hadithi ya msichana Hou Ji na mazao yake".

Baada ya binadamu kutokea duniani walikuwa wakiishi kwa kutegemea uwindaji, uvuvi na kukusanya matunda mwituni. Walikuwa mbioni wakati wote ili kupata riziki, hata hivyo walikuwa hawakosi kulala na njaa.

Alikuweko msichana mmoja alijulikanaye kama ni Jiang Yuan. Siku moja alicheza nje, alipokuwa akirudi nyumbani aligundua unyayo mmoja mkubwa kwenye kinamasi, alishangaa akaukanyaga. Mguu wake ulipogusa tu ule unyayo mara akasikia msisimko mwili mzima. Muda si muda baadaye akapata ujauzito.

Siku zilipita haraka, Jiang Yuan alijifungua mtoto wa kiume. Kwa kuwa mtoto huyo alikuwa hana baba, majirani walimwona kama kisirani, basi wakamnyakua kutoka kifuani kwa mama yake wakamtupa makondeni wakidhani kuwa angekufa kwa njaa. Lakini kwa bahati nzuri wanyama waliopita walimwokoa, baadhi ya wanyama jike walimnyonyesha maziwa. Baada ya kusikia habari hiyo majirani walitaka kumwacha misituni, lakini walipotaka kumtelekeza walitokea watema kuni, wakaacha nia yao. Mwishowe majirani kwa hasira waliazimia kumtupa kwenye barafu, lakini kabla majirani hawajafika mbali ndege wakubwa walishuka na kumhifadhi kwenye mabawa yao. Hapo ndipo majirani walipotambua kuwa mtoto huyo hakuwa wa kawaida, wakamrudisha kwa mama yake. Kutokana na mtoto huyo kutupwa mara kadhaa, mama yake alimpatia jina la "telekezo".

Tokea utotoni mtoto huyu alikuwa na ari kubwa. Aliona watu kila siku wakihangaika huku na huko kujitafutia riziki bila kuweza kuishi katika sehemu maalumu, wazo lilimjia akilini: ingekuwa bora kupata sehemu ya kuzalisha chakula. Kwa kuchunguza chunguza, alikusanya mbegu za ngano, mpunga, kunde, mtama na kokwa za matunda mwituni na kupanda katika shamba lake alilofyeka, alimwagilia maji na kupalilia kila baada ya muda fulani. Baada ya mimea kuiva, mazao aliyovuna yalikuwa mazuri na matamu kuliko ya misituni. Ili kurahisisha kazi alitengeneza zana za kulimia kwa miti na mawe. Alipofikia utu uzima, alikuwa amepata uzoefu mkubwa katika kilimo.

Msichana Telekezo aliwaelimisha majirani uzoefu wake wote bila ya kubania, basi tokea hapo watu wakaacha maisha ya kuhama hama ya uwindaji, uvuvi na kujitafutia matunda mwituni. Kwa heshima watu walimpatia jina "Hou Ji" badala ya Telekezo, maana yake ni Malkia wa Mazao.

Baada ya kufariki dunia, Hou Ji alizikwa katika sehemu yenye mandhari nzuri karibu na ngazi ya kuendea peponi. Miungu walipanda na kushuka kwa ngazi hiyo, sehemu hiyo ardhi yake ilikuwa na rutuba nyingi, mimea ilistawi na ndege wengi waliruka na kuimba angani katika majira ya mavuno.


1 2 3 4 5 6 7