16: Hadithi za Mapokeo

Hekaya za Kale

Kuongeza Miguu kwenye Picha ya Nyoka

Katika zama za kale, alikuwepo tajiri mmoja katika Dola la Chu. Siku moja tajiri huyo alifanya tambiko kwa babu yake, kisha aliwashukuru wasaidizi wake kwa bilauri moja la pombe. Wasaidizi walishauriana na kusema, "Bilauri moja ya pombe haitoshi kwa wote na inazidi kwa mmoja. Basi tuchore nyoka ardhini, mtu atakayetangulia kumaliza kuchora atastahili kunywa pombe hiyo."

Kati yao mmoja alimaliza mapema, akachukua bilauri akitaka kunywa kwa kujipongeza, alishika bilauri kwa mkono wa kushoto na kwa mkono wa kulia aliendelea kuchora akisema, "Mnaona, hata nina nafasi ya kuongeza miguu kwenye picha yangu ya nyoka!"

Lakini kabla hajamaliza kuchora miguu, mwingine alipokonya bilauri na kusema, "Nyoka hana miguu!" Kisha akanywa pombe yote. Mtu aliyetangulia kumaliza picha ya nyoka alikosa bilauri yake ya pombe. Hekaya hiyo inawaambia watu kwamba kila jambo lina kigezo chake, na asileweshwe na ushindi na kusababisha kushindwa.

Bian He Amzawadia Mfalme Jade

Mtu aliyeitwa Bian He wa Dola la Chu siku moja alipata kipande cha jade moja kwenye mlima, alikwenda kumzawadia mfalme wake Chuli. Mfalme huyo alimwita fundi wa kuchonga jade athibitishe kama ni jadi ya kweli. Fundi alisema, "Hii sio jade bali ni jiwe la kawaida!" Mfalme aliona Bian He alimdanganya, akamkata mguu wake wa kushoto.

Mfalme Chuli alikufa, aliyerithi kiti cha ufalme alikuwa Wu. Bian He alichukua kipande hicho kwenda kwa mfalme huyo Wu kama ni zawadi. Mfalme Wu alimwita fundi wa jade kuhakikisha kama ni jade ya kweli. Fundi alimwambia mfalme yale yale kwamba ni jiwe la kawaida. Mfalme Wu alikasirika na alimkata Bian He mguu wake wa kulia.

Baada ya mfalme Wu kufariki, Wenwang alirithi kiti cha ufalme. Bian He alichukua jade mikononi alilia siku tatu mfululizo chini ya mlima, machozi yalikauka na hata alitokwa damu. Mfalme Wenwang alisikia habari hiyo alimtuma mtu kwenda kumwuliza, "Watu waliokatwa miguu ni wengi, mbona wewe tu unalia sana?"

Bian He alijibu, "Sililii miguu yangu, bali nalia jade yangu ingesemwa kuwa ni jiwe na kunisengenya kuwa ni mdanganyifu!" Mfalme Wenwang alimwagiza kuchonga jade hiyo, kweli ni jade safi sana. Mfalme Wenwang aliipa jade kwa jina la "Jade ya Bian He". Hekaya hii inalenga mwandishi Han Fei mwenye matumaini makubwa ya kisiasa alivyopuuzwa. Lakini pia inamaanisha kuwa fundi wa jade anawajibika kutambua jade ya kweli, watawala wanapaswa kutambua watu hodari, na watoa hazina wawe tayari kunyanyaswa.

Kuficha Ugonjwa kwa Kuogopa Matibabu

Katika China ya kale ya Enzi za Madola ya Kivita alikuwako daktari mmoja maarufu katika Dola la Qi, jina lake Qin Yueren. Lakini badala ya kumwita jina lake hili halisi watu humwita Bian Que. Bian Que alikuwa daktari wa ajabu katika hadithi za mapokeo ya kale, magonjwa yoyote aliweza kuponyesha.

Kutoka uzoefu wa muda mrefu, daktari Bian Que alikuwa ameratibisha njia zake za kugundua ugonjwa, yaani kuangalia, kunusia, kuuliza na kupima vipigo vya mshipa wa damu. Hasa uhudari wake wa kuangalia, yeye kwa kuangalia ngozi, sura na vitendo angeweza kujua fulani ana ugonjwa gani na kwenye sehemu gani.

Siku moja alikuja mji mkuu wa Dola la Qi, Mfalme Huan alimkaribisha katika kasri yake. Bian Que alipomsalimu aligundua mfalme amepata ugonjwa. Basi akamwambia kinaganaga, "Umekuwa mgonjwa, sasa ugonjwa unaanza tu kwenye ngozi yako, lakini usipotibiwa ugonjwa utazidi."

Mfalme Huan alifikiri: Ni wazi mimi mzima kabisa, ugonjwa unatokea wape? Kumbe huyu daktari uhodari wake ni jina tu. Akamwambia, "Sina ugonjwa wowote." Baada ya Bian Que kuondoka, mfalme kwa dhihaka aliwaambia mawaziri wake walio pembeni, "Madaktari huwa na tabia ya kufafuta dosari ili kuonyesha uhodari wao. Anang'ang'ania kukuambia u mgonjwa, hali u mzima kabisa!"

Bian Que alikuwa na wasiwasi juu ya ugonjwa wa mfalme, baada ya siku tano, alienda tena kumwangalia, alisema, "Ugonjwa wako ushaingia ndani ya misuli yako, usipotibiwa ugonjwa utazidi zaidi!" Mfalme akamjibu kibaridi, "Unachosema sina." Kisha akamwondoa kwa kisingizio.

Siku tano zingine zikapita, daktari huyo mwenye roho teketeke kwa mara ya tatu alimwendea Mfalme Huan. Aliona kweli ugonjwa ukawa umezidi sana. Bila kujali alivyoumbulika alimhadharisha mfalme, "Ugonjwa wako umeenea mpaka tumboni sasa, ukichelewa zaidi utajingiza hatarini!" Mfalme Huan alinyamaza tu kwa hasira. Bian Que alikuwa hana budi ila kuondoka.

Siku tano nyingine zaidi zikapita, daktari hakuweza kutuliza moyo wake juu ya ugonjwa wa Mfalme Huan, akamwendea tena. Lakini alipomwona tu mfalme mara akageuka nyuma bila neno lolote. Awali mfalme alidhani pengine huyo daktari angepayuka tena, kumbe aliondoka kimya, akaona ajabu, akamrudisha na kumwuliza, "Mara hii mbona hukuniachia hata neno moja?"

Daktari alimjibu, "Ugonjwa ukiwa kwenye ngozi unaweza kuponyeshwa kwa maji vuguvugu, ukiwa kwenye misuli unaweza kuponyeshwa kwa akyupankcha, ukiwa kwenye tumbo dawa za mitishamba zaweza kuponyesha. Lakini ugonjwa ukienea mpaka ndani ya uboho, basi uwezo wangu umekwisha!"

Siku tano zikapita tena, kweli Mfalme Huan alianza kuugua mwili mzima, hapo akaamini aliyoambiwa na daktari, kwa haraka akatuma mtu kumwalika, lakini wakati huo Bian Que alikuwa ameondoka Dola la Qi. Siku chache baadaye mfalme akatupa mkono. Watu wa baadaye wamefupisha kisa hiki kuwa msemo wa "Kuficha ugonjwa kwa kuogopa matibabu". Maana yake ya ndani inaeleza kwamba fulani ana makosa lakini hakubali anapoambiwa, basi matokeo yake yatakuwa mabaya zaidi.

Zou Ji Ashindana Uzuri na Mwengine

Waziri wa Dola Qi aliumbika na sura nzuri. Siku moja asubuhi, alivaa nguo na kuvaa kofia, alijiangalia mbele ya kioo kwa makini, kisha alimwuliza mke wake, "Unaonaje, sura yangu nzuri inaweza kuzidi sura ya Xu kwenye sehemu ya kaskazini ya mji?"

Mke wake alijibu, "Hata zaidi!"

Bwana Xu ni maarufu kwa sura yake ya kuvutia. Zou Ji hakuamini sura yake inavitia zaidi kuliko Bwana Xu, kwa hiyo alimwuliza zaidi mke wake wa pili, "Unaonaje, sura yangu nzuri inaweza kuzidi sura ya Xu?" Mke wake wa pili alisema, "Anawezaje kukuzidi kwa sura?"

Baada ya siku moja, mgeni mmoja alikuja nyumbani, Zou Ji alimwuliza mgeni huyo, "Sura yangu ya ya Bwana Xu ipi nzuri zaidi?" Mgeni alijibu, "Unamshinda!"

Hatimaye, Bwana Xu alikuja nyumbani kwa Zou Ji. Zou Ji alimchunguza Bwana Xu toka utosini hadi miguuni, aliona kuwa yeye mwenyewe hawezi kabisa kushindana na sura ya Xu.

Usiku, Zou Ji alifikiri sana na mwishowe akafahamu, alisema, "Mke wangu alisema sura yangu nzuri, kwa sababu yeye ananipenda; Mke wangu wa pili alisema sura yangu nzuri kwa sababu kuniogopa; Mgeni alisema sura yangu nzuri kwa sababu aliomba nimsaidie kwa shida. Ukweli ni kwamba sura yangu haivutii kuliko sura ya Xu!"

Hekaya hii inamaanisha kuwa mtu anafaa anajifahamu hali yake mwenyewe, asiwaamini watu wa karibu maneno ya kilemba cha ukoka.

Hadithi ya Chura Aliye ndani ya Kisima

Ndani ya kisima aliishi chura mmoja, kila siku alikuwa na furaha sana. Siku moja alimwambia kasa wa baharini, "Furaha yangu ilioje! Nikitaka kucheza cheza na kuruka ruka ninaweza, matope ndani ya kisima yanafunika tu miguu yangu, na mimi peke yangu nakaa kisima kizima, karibu nyumbani kwangu!"

Kabla kasa hajaingia kisimani mguu mmoja ulikwamwa, akarudisha mguu wake, alisema, "Maili elfu moja pengine unaona mbali sana, lakini bahari ni kubwa zaidi. Katika enzi mbalimbali za kale ukame ulikuwa hutokea lakini bahari haikukauka wala maji hayakupungua, kuishi ndani ya bahari ni furaha sana!"

Baada ya kusikia hayo chura alikodoa macho, aliona yeye ni mdogo sana. Hekaya hii inalenga watu wasijivunie elimu yao ndogo, na asiwe na furaha tele kwa kupata faida kidogo tu.

Bweha Aazima Ukali wa Chui

Kipindi kati ya karne ya tano mpaka ya tatu kabla ya kuzaliwa Kristu, kilikuwa ni "Enzi ya Madola ya Kivita" katika historia ya China, kwa sababu wakati huo yalikuwako madola kadha, na mapambano yalikuwa hayaishi baina yao. Lakini katika nyakati hizo dhana za aina mbalimbali pia zilikuwa zikiibuka zikawa chanzo cha aina nyingi za utamaduni wa China zikiwa ni pamoja na nahau nyingi. Katika kipindi hiki, nitawasimulieni hadithi ya nahau moja: "Bweha Aazima Ukali wa Chui".

Dola la Chu lilikuwa nchi yenye nguvu zaidi kuliko mengine katika kipindi cha mwisho cha Enzi ya Madola ya Kivita. Alikuwako jemadari aitwaye Zhao Xixu aliyekuwa hodari sana. chini ya mfalme wa dola hilo Chu Xuan wang. Katika maingiliano na madola mengine dhaifu, mfalme huyo aligundua kwamba watu walikuwa wanamwongopa jemadari wake kuliko yeye mwenyewe. Aliona ajabu, basi akawauliza mawaziri wake sababu yenyewe.

Waziri mmoja aliyeitwa Jiang Yi alimsimulia hadithi ifuatayo.

Katika mlima mmoja aliishi chui mmoja kutokana na kubanwa na njaa alihangaika kutafuta mawindo yake huku na huko. Alipopita kwenye msitu mmoja mnene alimkuta bweha mmoja akitembeatembea mbele yake. Chui alifurahia bahati yake, akamrukia na kumkamata papo hapo.

Lakini alipofungua kinywa tayari kumng'ata ghafla bweha alinena, "Thubutu! Usidhani wewe ni mfalme wa wanyama, jua kwamba mimi nimeteuliwa na mungu kuwa mfalme wa wanyama wote. Yeyote atakayenidhuru ataadhibiwa vibaya sana."

Kusikia hayo, chui alishtuka, ujeuri wake ukamtoka karibu nusu. Hata hivyo, alijawa na wahka, akafikiri: Kwa kuwa mimi ni mfalme wa wanyama, yeyote aliyeniona huniogopa. Sasa, bweha anadai yeye ndiye mfalme mteule wa kututawala. Ni kweli hayo lakini?

Wakati huo, bweha aliona chui anasitasita asithubutu kumwua, akabaini kwamba amemwamini kiasi, mara akabenua kifua akimwonyesha kidole puani na kusema, "Kwani huniamini nisemayo? Basi nifuate uone jinsi wanyama watakavyonikimbia kwa hofu." Chui aliona wazo hili si baya, akamfuata.

Bweha alitangulia mbele kwa maringo, na chui akimfuata nyuma kwa hadhari. Kabla hawajafika mbali, waliona msitu mbele yao, pale wanyama wadogo wadogo walikuwa wakitafuta riziki yao. Walipoona chui nyuma ya bweha wote wakakimbia ili kuokoa roho zao.

Bweha aligeuza kichwa kuangalia nyuma, akamtupia macho kwa kiburi. Kuona hali hiyo chui pia aliingiwa na hofu, hakujua kwamba waliyemwogopa si bweha bali ni yeye mwenyewe.

Baada ya kusikiliza hadithi hiyo mfalme Chu Xuanwang alitafakari, akatambua kwamba sababu hasa ya watu kumhofia jemadari Zhao Xixue ni yeye mwenyewe. Lakini huyo jemadari anamiliki madaraka ya kijeshi, hii itakuwa hatari kwake kama si leo basi ni kesho. Kufikiri hivyo akadhoofisha madaraka yake.

Kwa miaka mingi nahau ya "Bweha Aazima Ukali wa Chui" ikawa moja katika lugha ya Kichina ikimaanisha wale walioegemea madaraka ya wakubwa kufanya ujeuri.

Mzee Juha Ahamisha Milima

Hadithi ya Mzee Juha Ahamisha milima sio ya kweli, lakini inajulikana kwa kila Mchina. Hadithi hiyo iliandikwa katika kitabu kilichoandikwa na mwanafalsafa Lie Yukou wa karne ya tano.

Hadithi yenyewe inasema hivi: Mzee mmoja aliyeitwa Mzee Juha, alikuwa karibu na umri wa miaka 90. mbele ya nyumbani kwake ilikingama milima miwili, mlima mmoja unaitwa Taihang, mwingine unaitwa Wanwu. Watu wa familia yake walipaswa kuzunguka milima hiyo kwenda mahali pengine.

Siku moja, Mzee Juha aliwaita jamaa zake akisema, "Milima miwili mbele yetu inaziba njia yetu, ni bora sote tufanye juhudi kuihamisha, mnaonaje?"

Watoto na wajukuu wake waliposikia aliyosema wakajibu, "Ni sawa uliyosema, tuanze kesho!" Lakini mke wa Mzee Juha alipinga, "Tumeishi na milima hiyo miaka mingi, kwa nini tusiweze kuendelea nayo? Na milima miwili hata inaweza kuhamishwa, mawe tutayaweka wapi?"

Maneno ya mke wa Mzee Juha yaliwafanya wafikiri sana, kweli hilo ni tatizo kubwa. Mwishowe waliamua kupeleka mawe na udongo kwenye bahari.

Siku ya pili, watu wa ukoo wa Mzee Juha walianza kuhamisha milima. Jirani alikuwepo mjane mmoja, alikuwa na mtoto mmoja wa kiume ambaye alikuwa na umri wa miaka saba tu, aliposikia kuhamisha milima alikuja kuwasaidia. Lakini vyombo vya kuhamisha milima vilikuwa vikapu na majembe tu, na bahari iko mbali na nyumbani kwake. Baada ya mwezi mmoja kupita milima haikuonekana kupungua.

Alikuwepo mzee mmoja aliyeitwa Mzee Mwerevu, alipoona Mzee Juha akihamisha milima, alicheka, alisema, "Wewe umekuwa na umri wa miaka mingi, unawezaje kuhamisha milima hiyo?"

Mzee Juha alijibu, "Wewe Mrerevu akili yako si zaidi ya watoto. Ingawa mimi nakaribia kifo, lakini nina watoto, na watoto watazaa watoto, vivyo hivyo haina mwisho, lakini urefu wa milima hauongezeki, jiwe moja likiondolewa milima inakosa jiwe hilo na haliongezeki, tunahamisha siku nenda siku rudi, mwezi mmoja mwezi rudi, mwaka mmoja mwaka rudi, kwa nini tusiweze kuimalima milima hiyo?" Kusikia hayo Mzee Mwerevu alikuwa hana la kusema. Watu wa ukoo wa Mzee Juha walichimba milima bila kusita kila siku. Kitendo chao kilimhurumisha mungu ambaye alituma miungu miwili wake kushuka na kuibeba milima hiyo kwenye mahali pengine. Hadithi hiyo inasimuliwa hadi leo ikiwaambia watu kuwa wakiwa na nia wanaweza kufanikisha jimbo lolote.

Hadithi ya Kuhani wa Mlima Laoshan

"Hadithi ya Kuhani wa Mlima Laoshan", ambayo ni hadithi mojawapo katika kitabu cha "Hadithi za Mashetani" kilichoandikwa na mwandishi mashuhuri Pu Songling wa Enzi ya Qing ya China, aliyeishi kuanzia mwaka 1640 mpaka 1715.

Hapo kale, kwenye ukingo wa bahari ulikuwapo mlima mmoja, unaitwa Laoshan, ambako aliishi kuhani mmoja. Inasemekana kwamba kuhani huyo wa Mlima Laoshan alikuwa na uganga wa ajabu.

Kutoka Mlima Laoshan umbali wa kiasi kama kilomita mia moja hivi ulikuwapo mji mkuu wa wilaya ambapo aliishi mtu mmoja, aliyejulikana kama Wang Qi. Wang Qi alikuwa na hamu ya kupata uganga tangu utotoni mwake. Baada ya kusikia fununu kuhusu uganga wa kuhani wa Mlima Laoshan, Wang Qi alimuaga mkewe na kuelekea mlimani kumtafuta ili apate uwezo huo wa ajabu kama wake.

Wang Qi alimkuta kuhani na kutokana na mazungumzo yao alibaini kuwa ni kuhani kweli mwenye uwezo mkubwa usio wa kawaida. Basi akamwomba awe mwanafunzi wake. Kuhani wa Mlima Laoshan alimchunguza, kisha akamwambia, "Nakuona wewe ni mtu wa kulelewa kwa kiganja cha mkono, nahofia hutawezana na maisha magumu." Wang Qi alizidi kumwomba na kumsihi hadi mwishowe akamkubalia.

Usiku huo Wang Qi alipoangalia mbalamwezi kutoka dirishani, moyo wake ulilipuka kwa furaha akifikiri kuwa baada ya siku chache atakuwa mtu asiye wa kawaida kama yeye. Asubuhi ya siku ya pili alidamka mapema, alimkimbilia kuhani wa Mlima Laoshan kwa matumaini atafundishwa uganga, badala yake aliambiwa achukue shoka aende mlimani kutema kuni pamoja na wanafunzi wenzake. Wang Qi aliondoka na karaha rohoni. Pale mlimani kulikuwepo mawe na kokoto nyingi, vichaka na miiba, ambavyo vilimfanya kutokwa na malengelenge mikononi na miguuni kabla jua halijazama.

Muda ulipita haraka kama mshale, mwezi mmoja ulipita vivyo hivyo, malengelenge yakawa sugu, lakini Wang Qi hakufundishwa lolote kuhusu uganga. Alishindwa kuvumilia zaidi kazi ya sulubu ya kukata kuni siku nenda siku rudi, hivyo wazo la kurudi nyumbani likamjia kichwani. Siku moja jioni alirudi kwenye hekalu la kuhani pamoja na wenzake ambapo kutoka dirishani alimwona mwalimu wake na wageni wawili wakinywa pombe pamoja kwa furaha pembeni mwa meza. Wakati huo giza lilikuwa limekwishaingia, lakini chumbani hakukuwashwa taa, na hapo ndipo alipomwona mwalimu wake akichukua karatasi nyeupe akaikata duara kama mwezi mpevu, akabandika ukutani; punde si punde ile duara ikatoa mwanga kama mwezi ukiangaza kote chumbani kama mchana.

Wang Qi aliingiwa na mshangao, na wakati huo huo alisikia mmoja wa wageni akinena, "Katika usiku mzuri kama huu wa karamu kubwa na pombe, inafaa tuburudike pamoja na wenzetu." Basi kuhani wa Mlima Laoshan akawapa kuzi dogo la pombe wanafunzi wake, akiwaambia wanywe kwa uwezo wao. Wang Qi aliwaza: kuzi dogo kama hili lawezaje kuwatosheleza wote hawa? Lakini ajabu ni kwamba hata kuzi likimwagwa namna gani pombe ilikuwa haipungui. Wakati huo mgeni mwingine akasema, "Ingawa kuna mbalamwezi na pombe, lakini bila mcheza ngoma furaha yetu haikamiliki." Kusikia hayo, kuhani alichukua kijiti kimoja cha kulia na kukielekeza kwenye ile duara, na mara akatoka msichana mmoja mwenye kimo cha futi moja lakini alipokanyaga sakafu papo hapo akawa na urefu wa kawaida. Msichana huyo alikuwa na kiuno chembamba kama nyigu, ngozi laini kama yavuyavu, na tepe za nguo zikipepea alipocheza ngoma na wimbo. Baada ya kumaliza wimbo wake akarukia juu ya meza akarudia hali ya awali ya kijiti. Yote hayo yalimwacha Wang Qi mdomo wazi.

Wakati huo mgeni mmoja akasema, "Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo, tumefurahi kweli, lakini inatupasa tuondoke sasa." Basi wageni wawili wakainuka, wakaingia kwenye ile duara ukutani, wakatoweka. Mwanga wa mwezi wa karatasi ukafifi, wanafunzi wakawasha taa, wakamwona mwalimu kuhani akiwa peke yake na masalio ya pombe na vitoweo mezani.

Mwezi mwingine ukapita tena, lakini mwalimu hakumfudisha Wang Qi lolote. Hapo Wang Qi alishindwa kabisa kuvumilia, akaenda kwa mwalimu wake, akamwambia, "Mimi nimekuja kutoka mbali, kama hunifundishi uganga wako wa kuishi milele, basi nifundishe uganga mwingine angalau kidogo nipate kitulizo." Lakini mwalimu alitabasamu tu bila neno. Wang Qi akaendelea, "Kutema kuni toka asubuhi mpaka jioni, kazi ya nguvu kama hii siiwezi." Hapo mwalimu kuhani akacheka na kusema, "Si nilikuambia, hutayaweza maisha magumu? Kama ni hivi basi rudi nyumbani kwenu kesho asubuhi." Wang Qi akamsihi, "Naomba unifundishe uganga angalau kidogo nisirudi mikono mitupu". Mwalimu akamwuliza, "Unataka uganga gani?" Wang Qi akanena, "Mara nyingi nilikuona ulipotembea hukuzuiliwa na ukuta, nifundishe uganga huu basi." Mwalimu akakubali, akamwambia Wang Qi amfuate. Walikwenda penye ukuta mmoja. Mwalimu akamwambia maneno ya kunuizia ili aweze kupita kwenye ukuta. Wang Qi alirudia kama aliyoambiwa, na alipoimaliza tu mwalimu alinyoshea kidole ukutani akimwambia Wang Qi "Ingia ukutani." Wang Qi hakuthubutu kusogeza mbele miguu yake kwenye ukuta. Mwalimu akamhimiza, "Ingia tu!" Wang Qi alijivuta hatua kadhaa mbele kisha akasimama kwa hofu. Mwalimu alimhimiza tena, "Inamisha kichwa, uingie ndani." Wang Qi alijikakamua, akaukimbilia ukuta akiwa amefumba macho kwa nguvu. Bila kuhisi chochote akapita! Wang Qi alifurahi sana, mara akapiga magoti sakafuni kumshukuru. Mwalimu akamwambia, "Jihadhari vizuri utakapokuwa nyumbani, uwe mwenye juhudi za kazi. La sivyo, uganga hautafanya kazi yoyote."

Baada ya kufika nyumbani Wang Qi alimwelezea mkewe mambo mengi ya kujisifu akisema, "Nilimkuta mtu wa mungu, akanifundisha uganga wote. Sasa kuta zote haziwezi kunizuia nisipite." Mkewe hakumwamini, akamwambia "Acha, unamzuga nani? Jambo kama hili halipo duniani." Kusikia hayo Wang Qi alianza kunuizia, kisha akaukimbilia mbio ukuta. Pu! Akabamiza kichwa ukutani, akuanguka chali. Mkewe alimsaidia kunyanyuka, akajikuta kichwa chake kimevimba kama yai. Wang Qi alining'iniza kichwa kama puto lililovuja hewa. Alivyoona jinsi mumewe alivyoadhirika, mkewe hakujua acheke au akasirike, alisema, "Hata uganga ungekuwepo duniani, mtu mjinga kama wewe usingaliweza kuupata kwa muda wa miezi miwili, mitatu." Wang Qi alikumbuka wazi jinsi alivyopita ukuta bila shida yoyote mbele ya mwalimu wake, hivyo akaona hakika yule kuhani alimchezea shere, akaanza kulaani na kutoa matusi.

Wang Qi aliendelea kuwa mtu asiyefaa kwa lolote.

Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan

Hadithi ya "Mvuvi na Shetani" kutoka "Elfu lela u lela" inajulikana kote duniani. Lakini pia iko hadithi nyingine ambayo inafanana na hadithi hii inasimuliwa sana duniani. Hii ni hadithi iitwayo "Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan".

Hadithi hiyo inatokana na kitabu kilichotungwa na Ma Zhongxi katika Enzi ya Ming, karne ya 13. Hadithi yenyewe ni kama ifuatayo:

Hapo kale alikuwako msomi mmoja Dong Guo, huyu bwana macho yake yalikuwa hayabanduki kwenye vitabu vyake kila siku na kila wakati. Hivyo akawa mbukuzi na elimu yake ilikuwa ya kitabuni tu. Siku moja akiwa na mfuko wake wa vitabu mgongoni alitoka na punda wake akienda mahali paitwapo Zhong Shan kutafuta nafasi ya udiwani.

Ghafla mbwa-mwitu mmoja aliyejeruhiwa alitokea mbele yake na kumsihi, "Ewe bwana, nafukuzwa na mwindaji, nilipigwa mshale, karibu nife. Naomba unifiche ndani ya mfuko wako. Nakuahidi nitakulipa kwa wema wako."

Bwana Dong Guo alijua mbwa-mwitu ni madhara kwa binadamu, lakini kuona alivyokuwa maskini, alimhurumia, alisita kidogo, lakini akamwambia, "Nikifanya kama usemavyo nitamkosea mwindaji, lakini basi nitakuokoa." Kisha akamwambia mbwa-mwitu ajikunyate, akamfunga miguu yake na kumwingiza kwenye mfuko.

Punde si punde mwindaji alikuja akaona mbwa-mwitu katoweka. Alimwuliza Bwana Dong Guo: "Je umemwona mbwa-mwitu kupita hapa? Amekimbilia wapi?"

Bwana Dong Guo alimjibu, "Hataa, sikumwona. Hapa njia panda ni nyingi, pengine amechukua njia nyingine." Mwindaji akamwamini, akafuata njia nyingine kuendelea kusaka.

Kusikia vishindo vya mwindaji na farasi wake vimekwenda mbali, mbwa-mwitu alimsihi Bwana Dongo Guo mfukoni "Naomba uniachie huru nikimbize roho haraka!"

Mwenye rehema Dong Guo alidanganywa na maneno ya mbwa mwitu, akamtoa mfukoni. Lakini ghafla, huyo mbwa-mwitu akamgeukia na kusema kwa kelele, "Sasa nabanwa na njaa, ilivyokuwa umenifanyia wema, basi unifanyie zaidi, nikumalize." Papo hapo akamrukia. Bwana Dong Guo alikukurushana naye, huku akiguta, "Usiye na fadhila we!"

Wakati huo, mkulima mmoja alipita hapo alikuwa na jembe mkononi. Bwana Dong Guo alimsimamisha na kumweleza kisa chenyewe, lakini mbwa-mwitu alikana kwamba aliokolewa naye. Baada ya kutafakari, mkulima akasema: "Hata mimi siamini wewe bwana ungeweza kumficha ndani ya mfuko wako mdogo kama huu, au umfiche tena nione." Mbwa-mwitu kakubali, akalala chini akajikunyata mviringo akimwachia Dong Guo amfunge miguu yake kwa kamba na kumwingiza mfukoni. Kwa haraka mkulima akafunga kabisa mfuko huku akimwambia Bwana Dong Guo, "Unadhani mnyama kama huyu angeweza kubadili tabia yake asimdhuru binadamu? Asilan! Ni ujinga kuwa na huruma kwa mbwa-mwitu!" Kisha akainua jembe lake akamwua kabisa mbwa-mwitu. Bwana Dong Guo akaerevuka na kumshukuru sana kwa kumwokoa.

"Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan" imekuwa hadithi ya mafunzo: "Bwana Dong Guo" anawakilisha watu wababaishaji wa jema na baya na kutumia ovyo huruma; "mbwa-mwitu wa Zhong Shan" anawakilisha watu wasio na shukrani.

Kuendea Mwelekeo kinyume na Unaotakiwa

Katika karne ya tano hadi tano K.K. Kipindi cha Madola ya Kivita, nchini China kulikuwa na madola mengi madogo ambayo yalikuwa yalipambana miaka hadi miaka, katika kipindi hiki walitokea wanasiasa wengi ambao walijitahidi kushawishi wafalme waweze kusikiliza na kufuata maoni yao ili kuyashinda madola mengine. Hadithi ya "Kuendea Mwelekeo kinyume na Unaotakiwa" ilitokea katika kipindi hicho katika Dola la Wei ikieleza jinsi waziri Ji Liang alivyomshawishi mfalme wake.

Katika kipindi hiki kila dola lilijitahidi kuwa na nguvu kubwa kuliko madola mengine ili kuyashinda, hali kadhalika Dola la Wei. Mfalme Wei alitaka kushambulia mji mkuu wa Dola la Zhao, Handan. Wakati huo waziri Ji Liang alikuwa akisafiri kikazi katika dola jingine, aliposikia habari hiyo alikuwa na wasiwasi sana. Kwa haraka alirudi nyumbani na bila kuwahi kunawa uso alikwenda kwa mfalme wake.

Mfalme Wei alikuwa akipanga mpango wa vita, alipomwona Ji Liang alikuja kwa haraka, aliona ajabu, alimwuliza, "Una haraka gani hata hukuwahi kuvaa vizuri?" Ji Liang alisema, "Mheshimiwa mfalme, nilipokuja njiani nilikuta jambo la ajabu." Mfalme Wei aliona ajabu, alimharakisha amweleze jambo lenyewe. Ji Liang alisema, "Sasa hivi niliona mkokoteni uliovutwa na farasi kuelekea kaskazini, nilimwuliza mwendeshaji, 'unaelekea wapi?' Yule aliniambia 'Dola la Chu!' Niliona ajabu nikasema, 'Dola la Chu liko upande wa kusini, mbona unaelekea kaskazini?' Lakini yeye hakujali niliyomwambia, akisema, 'Farasi wangu ni hodari sana, mwishowe atafika tu Dola la Chu!' Kusikia hayo niliona ajabu zaidi, nilisema, 'Hata farasi wako ni hodari namna gani, lakini mwelekeo ni kosa.' Alisema, 'Usiwe na wasiwasi, pesa nilizo nazo zinatosha kutumika njiani.' Nilishindwa kuelewa, nilimwambia, 'Hata pesa zako ni nyingi namna gani, lakini njia yako sio ya kuelekea Dola la Chu!' Mwendeshaji huyo alicheka kwa kelele, akisema, 'Hata hivyo, ustadi wangu wa kuendesha mkokoteni ni mkubwa!' Hakusikia niliyomwambia, aliendelea kuelekea kaskazini." Mfalme alicheka na kusema, "Ni mjinga kweli huyo!" Kisha Ji Liang alisema, "Mheshimiwa, wewe si unataka kuwa kiongozi wa madola yote? Basi inakupasa upate imani ya watu wote. Lakini sasa kwa kutegemea ardhi yako nyingi kidogo, nguvu ya jeshi kubwa kidogo unataka kufanya vita kuwateka ili kutukuza heshima yako, kufanya hivyo kunakufanya uwe mbali zaidi na na lengo lako, ni sawa na mwendeshaji mkokoteni anayetaka kwenda Dola la Chu upande wa kusini, lakini anakwenda upande wa kaskazini, kinyume na mwelekeo anaoutaka!"

Wakati huo mfalme Chu alielewa aliyosema, alifikiri muda akaona ni sawa aliyosema, akafuta mpango wake wa kushambulia Dola la Zhao. Wachina mara kwa mara wanatumia methali hiyo kueleza vitendo vinavyokwenda kinyume na lengo linalotakiwa.


1 2 3 4 5 6 7