16: Hadithi za Mapokeo

Hadithi ya Kiakili

Chura Anayecheza na Dragoni

Katika Enzi ya Han Mashariki, matetemeko ya ardhi yalikuwa yanatokeaa mara kwa mara. Kutokana na maandishi ya hostoria, tokea mwaka 89 hadi 140, katika muda wa miaka zaidi ya hamsini yalitokea matetemeko 33, na tetemeko lililotokea mwaka 119 lilikuwa kubwa sana. Mfalme wa enzi hiyo alidhani kuwa pengine watu walimkosea mungu, kwa hiyo alizidi kuwatoza kodi na kufanya ibada. Kulikuwa na mwanasansi mmoja aliyeitwa Zhang Heng, aliona kuwa tetemeko la ardhi ni hali ya kijiografia, kwa hiyo alizidi kufanya utafiti kuhusu tetemeko la ardhi.

Kutokana na utafiti wake, mwaka 132 alivumbua chombo cha kwanza duniani cha kutoa dalili ya matetemeko ya ardhi.

Chombo cha kutoa dalili ya matetemeko ya ardhi kiliundwa kama mtungi, kipenyo chake karibu mita moja, kwenye mtungi huo kuna dragoni wanane wakitazama mielekeo minane, na kila dragoni alikuwa ameng'ata gololi moja ya shaba, na chini ya dragoni kuna chura aliyetanua midomo, kama tetemeko likitokea kwenye mwelekeo fulani basi gololi hiyo inadondokea mdomomi mwa chura.

Mwaka 133, mji wa Shenyang ulikumbwa na tetemeko, chombo hicho kilitoa dalili, na baadaye mji huo ukikumbwa na matetemeko mara tatu na kila mara chombo hicho kilikuwa hakikosi kutoa dalili. Mwezi Februari, mwaka 138, Zhang Heng aligundua gololi iliyokuwa mdomoni mwa dragoni upande wa magharibi ilidondoka, baada ya siku tatu tarishi wa mji wa Luoyang magharibi mwa China alikuja kupiga ripoti kwamba huko kulitokea tetemeko la ardhi. Watu wanaita chombo hicho kuwa ni "Chura Anayecheza na Dragoni".

Matunda Matatu Yaua Watu Watatu

Katika Kipindi cha Madola ya Kivita, madola mengi yalikuwa yakipambana. Katika Dola la Qi kulikuwa na mabwana watatu wa kivita, waliheshimiwa sana na watu. Lakini watu hao watatu baadaye walikuwa wajeuri.

Waziri mkuu wa Dola Qi alipoona kuwa watatu hao walizidi kuwa wajeuri na wakatili, aliamua kuwaua. Siku moja mfalme wa Dola la Lu alitembelea Dola la Qi, watatu hao pamoja na maofisa wengine walialikwa kwenye chakula pamoja na mfalme wa Dola la Lu, hao watatu walionekana wenye kiburi kupita kiasi. Wakati walipokuwa wanakula, waziri mkuu alimwambia mfalme wake aende kuchuma matunda kuwakaribisha. Lakini baada ya kuwagawia, matunda yalibaki mawili tu na wasiopata matunda walikuwa majasiri hao watatu. Waziri mkuu alitoa shauri kuwa kila mmoja kati ya watu hao watatu aeleze mchango wake, mwenye mchango mkubwa atapata tunda moja. Mfalme alikubali.

Kila mmoja alieleza mchango wake. Mmoja alisimama na kusema, "Nilipofuatana na mfalme kuwinda nilimwua chui mmoja na kumwokoa mfalme, mchango huu si mkubwa?" waziri mkuu alisema, "Mchango huu si mdogo, unastahili kupewa tunda moja."

Mwingine alisimama na kusema, "Mimi niliwahi kumwua kobe mkubwa na kumwokoa mfalme, mchango huu si mdogo." Waziri mkuu alijibu, "Mdio, unastahili pia kupewa tunda moja."

Wa tatu alisimama, na kueleza jinsi aliwashinda jeshi la wavamizi na kulinda usalama wa taifa. Alimwuliza mfalme, "Mchango wangu huu si mkubwa kuliko wengine?" Lakini matunda mawili yaliyobaki yameisha, mfalme alimfariji, "Utapewa safari ijayo."

Lakini aliona kuwa alipuuzwa vibaya, watu waliokuwa hawakutoa mchango mkubwa kama yeye walipata matunda, yeye mwenye mchango mkubwa zaidi hakupewa. Kwa kufikiri hivyo, alitoa upanga na kujiua. Wengine wawili waliona kuwa hata mwenye mchango mkubwa alijiua na waliwahi kula kiapo kuwa watakufa pamoja, basi walijiua vilevile.

Watu waliokuwa kwenye chakula walishtuka, lakini kwa akili waziri mkuu aliwaua watu hao wajeuri.

Hadithi ya Xi Menbao

Xi Menbao alikuwa mtu wa karne ya tano K.K. Kutokana na uhodari wake aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya. Alipofika tu wilayani mara aliwaalika wazee wa huko kuwauliza mambo yanayowasumbua. Wazee walimwambia kwamba kila mwaka shetani wa mto alitaka kumwoa mke mmoja.

Wila hiyo iko karibu na Mto wa Huanghe, wenyeji walisema ndani ya mto aliishi shetani mmoja ambaye kila mwaka anataka kumwoa mke mmoja, la sivyo shetani huyo atachafua mto na kuleta mafuriko makubwa. Maofisa na washenga walitumia fursa hiyo kuwatoza raia na kugawana pesa za kodi.

Wazee walimwambia Xi Menbao kuwa kila mwaka mshenga mzee mmoja alitembeatembea kila mahali kuchagua msichana na kusema "Basi huyu msichana achaguliwe kuwa mke wa shetani wa mto!" Kisha alimchukua msichana huyo na kumbadilishia nguo mpya na kumkalisha juu ya kitanda na kumtupa mtoni. Mwanzoni msichana huyo alielea, lakini baadaye alizama. Mshenga alisema, shetani amekubali kumpokea. Baada ya kusikia hayo, Xi Menbao hakusema kitu.

Siku nyingine ya kuchagua msichana iliwadia. Xi Menbao aliongoza askari wake kusubiri kando ya mto. Muda si muda maofisa, matajiri na mshenga walikuja na msichana aliyechaguliwa. Mshenga alikuwa na umri wa miaka zaidi ya 70.

Xi Menbao alisema, "Mwite mke wa shetani wa mto mbele yangu, nione kama ni kisura." Msichana aliletwa, Xi Menbao alimwangalia na kusema, "Huyu msichana si mzuri, lakini leo shetani anasubiri kumpokea mke wake, basi tumwomba mshenga aende kumwambia shetani kwamba tutamchagua msichana mwingine mzuri zaidi." Kisha aliwaamuru askari wamtume mshenga mtoni. Baada ya dakika chache, Xi Menbao alisema, "Mbona mshenga hakurudi kutuambia jawabu?" Alimwagiza mfuasi wa mshenga aende kuuliza habari, basi askari wakamtupa mfuasi wa mshenga.

Waliokuwa kwenye ukingo wa mto, matajiri na maofisa walishikwa na hofu. Xi Menbao alisema, "Inaonekana kuwa shetani ni mkarimu wa kuwapokea wageni, afadhali tuwatume wengine kwenda kuonana na shetani. Maofisa na matajiri wote wakapiga magoti na kutubu wasitupwe mtoni.

Kwa sauti kubwa, Xi Menbao aliwaambia watu waliopo, "Huu ni udanganyifu mtupu, katika siku za usoni yeyote atakayeshughulikia jambo hilo atatupwa mtoni." Tokea hapo watu walianza kuishi katika hali ya utulivu.

Tian Ji Ashindana Mbio za Farasi

Katika Kipindi cha Madola ya Kivita alikuwepo ofisa mmoja wa Dola la Wei, aliyeitwa Sun Bin. Kutokana na kusingiziwa na maofisa wengine alikuja kwenye mji mkuu wa Dola la Qi.

Jemadari mkuu Tian Ji wa Dola la Qi alimpokea na kuzungumza naye kwa siku tatu. Kutokana na mazungumzo alifahamu kuwa huyo Sun Bin ni hodari kwa ujuzi wa kivita.

Kushindana kwenye mbio za farasi ulikuwa ni mchezo ulioenea sana, lakini Tian Ji kila mara alishindwa na mfalme wake. Sun Bin alimwambia Tian Ji, "Safari ijayo nitakwenda kuangalia mashindano yenyewe, pengine nitaweza kukusaidia upate ushindi."

Siku moja mashindano ya mbio za farasi yalifanywa tena, watu wengi walifika kutazama mashindano. Sun Bin alielewa kuwa farasi waligawanyika katika ngazi tatu kutokana na uwezo wa mbio, na farasi pia wanatofautiana kwa matandiko tofauti.

Baada ya kuangalia, Sun Bin aligundua kuwa farasi aliyemtumia Tian Ji hakuwa nyuma sana ila tu hakutumia mbinu vizuri. Sun Bin alimwambia Tian Ji, "Usiwe na wasiwasi, naweza kukusaidia kupata ushindi." Tian Ji alifurahi sana, alimwalika mfalme kushindana naye. Mfalme aliona kuwa hakuwahi kushindwa kwake, hivyo akakubali.

Kabla ya mashindano, Tian Ji alitumia tandiko la farasi wa ngazi ya kwanza kuweka kwenye farasi wa ngazi ya pili. Katika mashindano farasi wa mfalme alipiga mbio na kumwacha nyuma kabisa farasi wa Tian Ji. Mfalme alifurahi sana. Katika raundi ya pili, kama alivyoambiwa na Sun Bin, Tian Ji alitumia farasi wa ngazi ya kwanza kushindana na farasi wa ngazi ya pili wa mfalme, Tian Ji alishinda. Katika raundi ya tatu, Tian Ji alitumia farasi wake wa ngazi ya pili kushindana na farasi wa ngazi ya tatu wa mfalme, Tian Ji alishinda vilevile. Mashindano yalimalizika na Tian Ji alimshinda mfalme kwa mabao mawili kwa moja.

Mfalme alipigwa bumbuazi, hakufahamu sababu. Tian Ji alimwambia mfalme kuwa hakumshinda kwa kupata farasi hodari zaidi bali alitumia mbinu bora, na mbinu hizo ni za Sun Bin. Sun Bin alimwambia mfalme, wakati ambapo nguvu za pande mbili zikiwa karibu sawa, mbinu sahihi ni muhimu sana, na wakati ambapo nguvu za pande mbili zikiwa tofauti sana, mbinu sahihi pia zinasaidia sana kupunguza hasara. Baadaye, mfalme alimteua Sun Bin kuwa jemadari mkuu, na jeshi lililoongozwa na Sun Bin lilipata ushindi mara nyingi katika vita.

Chu Long Amshawishi Mama Mfalme Zhao

Katika Kipindi cha Madola ya Kivita, mtu aliyetawala Dola la Zhao alikuwa mama mfalme Zhao. Mwaka mmoja Dola la Qin lenye nguvu kubwa zaidi lilitaka kuvamia Dola la Zhao. Kutokana na uhusiano mzuri, Dola la Zho liliomba Dola la Qi msaada. Lakini mfalme wa Dola la Qi alitaka kuchukua mtoto wa mama mfalme awe kama dhamana. Mama mfalme Zhao alimpenda sana mtoto wake, alihofia atakuwa hatarini, kwa hiyo alikuwa na wasiwasi bila kufanya uamuzi. Mawaziri walimshawishi mama mfalme akubali kupeleka mtoto wake kwenye Dola la Qi ili kusalimisha taifa. Mama mfalme Zhao alikasirika, alisema, "Yeyote atakayenishawishi kufanya hivyo nitamtemea mate usoni."

Siku moja waziri mwenye heshima Chu Long aliomba kuonana na mama mfalme. Mama mfalme alidhani alikuja kumshawishi, alikarisika. Lakini Chu Long hakutaja jambo hilo, ila tu kusema, "Nakuja kukusalimu tu, kwa sababu siku nyingi sikukuona."

Mama mfalme alisema, "Siku hizi sina hamu ya chakula." Chu Long alisema, "Na mimi vilevile, siku hizi sili sana kutokana na kukaa tu." Kutokana na maongezi ya mambo ya kawaida, hasira ya mama mfalme ilipungua.

Chu Long alisema, "Nimekuja na shida yangu, kwamba nina mtoto mmoja anaitwa Shu Qi, naona hatakuwa na matumaini ya kuwa mtu wa maana, mimi nimekuwa mzee, naomba wewe ukubali mtoto wangu awe mlinzi katika kasri lako." Mama mfalme aliuliza, "Ana miaka mingapi?" Chu Long alijibu, "Miaka 15, ingawa umri wake bado mdogo, lakini nataka kumpangia maisha kabla ya mimi kufariki." Mama malkia alisema, "Sikutegemea kuwa kumbe wanaume pia wanapenda sana watoto wao." Chu Long alisema, "Pengine zaidi kuliko wanawake." Chu Long aliendelea, "Wazazi wanapenda watoto wao kwa kuwafikiria mbali." Kisha Chu Long aligeuza mazungumzo yake akisema, "Lakini naona wewe hujamfikiria mbali mtoto wako." Mama mfalme hakufahamu maana yake, aliuliza sababu. Chu Long alisema, "Tokea enzi na dahari, watoto na wajukuu wa wafalme walioweza kuendelea na ufalme ni wachache, lakini sio kwa sababu wao walikuwa hawana uwezo, bali kwa sababu ingawa nafasi zao zilikuwa juu sana lakini michango yao kwa ajili ya maslahi ya taifa ilikuwa midogo. Baada ya wao kushika utawala walishindwa kuendelea kwa muda mrefu. Hivi sasa umempangia nafasi mtoto wako na kumpa hazina nyingi, lakini umeacha fursa yake ya kutoa mchango kwa ajili ya taifa, basi atakuwaje kuwa mtawala wa daima baada ya wewe kufariki? Ndio maana nasema hujamfikiria mbali mtoto wako." Baada ya kusikia hayo, mama mfalme alikubali kupeleka mtoto wake kwenye Dola la Qi ili kupata msaada wa kijeshi.

Kuazima Mishale kwa Mashua Zenye Sanamu za Mabua

Katika karne ya kwanza K.K. nchini China kulikuwa madola matatu ya kifalme kwa pamoja, madola hayo yalikuwa ni Wei, Shu na Wu. Dola la Wei liko kwenye sehemu ya kaskazini, Dola la Shu liko katika sehemu ya magharibi, na Dola la Wu liko sehemu ya kusini. Mwaka mmoja, Dola la Wei lilishambulia Dola la Wu, na askari walipokaribia Dola la Wu walipiga kambi karibu na mto ili kusubiri nafasi nzuri kufanya mashambulizi.

Jemadari mkuu wa Dola la Wu aliitwa Zhou Yu, baada ya kufahamu hali ya maadui aliamua kukinga maadui kwa mishale. Mishale ilikuwa ni lazima iwe laki moja, lakini katika muda mfupi inawezaje kutengeneza mishale hiyo?

Wakati huo jemadari Zhu Geliang wa Dola la Shu alikuwa ziarani katika Dola la Wu. Zhu Geliang alikuwa mwenye hekima sana, Zhou Yu aliomba ushauri kutoka kwake. Zhu Geliang alimwambia, siku tatu inatosha. Wote waliona ahadi ya Zhu Geliang ni mzaha. Lakini Zhu Geliang aliahidi kuwa kama akishindwa atakubali kukatwa kichwa. Zhu Geliang alimwagiza waziri Lu Su wa Dola la Wu atengeneze mashua ishirini, na kila mashua wapande askari na kufunga mabua ya majani kama sanamu.

Zhu Geliang alikuwa hana shughuli mpaka siku ya tatu. Katika siku ya tatu usiku alimwambia Lu Su, "Twende kuchukua mishale." Lu Su aliuliza, "Wapi?" Zhu Geliang alitabasamu na kusema, "Utajua mwenyewe." Katika usiku huo ukungu ulikuwa mnene, giza totoro, Zhu Geliang aliamuru kuendesha mashua haraka, mashua hizo zilipangwa kwa mstari mmoja, kisha aliwaamuru askari wapige kilele na kupiga ngoma. Lu Su aliogopa sana alisema, "Mashua zetu ni ishirini tu na askari wachache, jeshi la Wei likitushambulia tutashindwa vibaya." Zhu Geliang alimwambia, "Usiwe na wasiwasi, jeshi la Wei halithubutu kutushambulia katika ukungu mene na giza namna hii."

Askari waliposikia kelele na ngoma, jemadari Cao Cao aliamua kuzuia mashambulizi kwa mishale, askari kiasi cha elfu kumi walipiga mishale kwenye ukingo wa mto, mishale ilikuwa mingi kama mvua na kuchomeka kwenye sanamu za mabua. Kwa kuona idadi ya mishale imetosha, Zhu Geliang aliamuru kurudi kabla ya ukungu kutoweka.

Kabla msafara wa mashua kufika kwenye ukingo wa mto, jemadari Zhou Yu alikuwa amekwisha panga askari kusubiri kuchukua mishale.

Hadithi ya Mo Zi

Mo Zi alikuwa mtu wa karne ya tano K.K. Wakati huo kulikuwa na madola mengi nchini China. Kati ya madola hayo, Dola la Chu lilikuwa kubwa na Dola la Song lilikuwa dogo.

Fundi aitwaye Gong Shuban alitengneneza ngazi moja ndefu kwa ajili ya kuparamia ukuta mrefu wa mji. Baada ya ngazi hiyo kuwa tayari, Dola la Chu lilipanga vita dhidi ya Dola la Song.

Mo Zi aliposikia habari hiyo, alisafiri kwa siku kumi hadi kwenye mji mkuu wa Dola la Chu, na kukutana na Fundi Gong Shuban. Alisema, "Mtu mmoja wa kaskazini anataka kuniua, naomba kutumia nguvu zako kumwua yeye." Gong Shuban alikuwa kimya. Mo Zi aliendelea, "Nitakupa pesa nyingi kama ni shukrani zangu." Gong Shuban alijibu, "Kwa maadili yangu naweza kumwua mtu?" Mo Zi alisema, "Dola la Chu ni kubwa, watu wachache lakini ardhi kubwa, lakini linataka kushambulia dola dogo, hivi ni vita visivyo vya halali, wewe unasema hutamwua mtu, lakini vita vikizuka watu wangapi watauawa kutokana na ngazi yako ndefu?"

Gong Shuban alikuwa hana la kusema, na kwa kisingizio alisema aliamrishwa na mfalme Chu. Mo Zi alikwenda kukutana na mfalme Chu. Mo Zi alimwambia mfalme, "Hivi sasa kuna mtu anayetaka kuiba mkokoteni mbovu wa jirani hali anao mpya, na anataka kuiba nguo zilizochakaa wakati yeye anayo nguo mpya, huyo ni mtu wa namna gani?" mfalme Chu alijibu, "Ana tabia ya kuiba." Mo Zi alisema, "Dola lako lina ardhi nyingi, na Dola la Song ni ndogo, Dola la Chu lina maliasili nyingi na Dola la Song ni maskini, kwa hiyo naona Dola la Chu ni sawa na mwenye tabia ya kuiba."

Mo Zi aliendelea kusema, "Wewe mheshimiwa mfalme, usifikiri kuwa baada ya kuteka Dola la Song utaweza kutawala daima, na watu watakubali siku zote bila kukupindua." Mfalme Chu mwishowe aliema, "Sitashambulia Dola la Song." Mo Zi aliliokoa Dola la Song kwa akili zake.

"Mbinu ya Mji Mtupu"

Nchini China Zhu Geliang anajulikana kwa watu wote wa China, fulani akifananishwa na Zhu Geliang anasifiwa kwa akili zake.

Katika karne ya pili K.K. nchini China kulikuwa na madola matatu kwa pamoja, nayo ni Wei, Shu na Wu. Kipindi hiki kinaitwa "Kipindi cha Madola Matatu ya Kifalme". Madola hayo yalipigana mara kwa mara, lakini hakuna hata moja lililoweza kuliangamiza lingine. Zhu Geliang alikuwa ni jemadari mkuu wa Dola la Shu, alijulikana kwa mbinu zake za kivita.

Mfalme wa Dola la Wei alipofahamu kuwa mji wa Dongcheng wa Dola la Shu ulikuwa na upungufu wa askari ambao hawakufikia hata elfu 10, alimwagiza jemadari Sima Yi kuongoza askari zaidi la laki moja kuushambulia mji huo. Mfalme wa Dola Shu alipopata habari hiyo alishikwa na wasiwasi, kwani askari elfu 10 kupambana na askari laki moja hawafui dafu, lakini kuhamisha askari kutoka mahali mengine wakati hautoshi. Wakati huo alitumaini Zhu Geliang angepata njia ya kuuokoa mji wake.

Zhu Geliang alichemsha sana ubongo, kisha aliamuru wenyeji wote waondoke mjini na kwenda kwenye mahali fulani, kisha alifungua mlango wa mji wazi na kusubiri maadui. Muda ulikuwa si mrefu askari walioongozwa na Sima Yi walifika kwenye mji wa Xicheng. Hapo kabla Sima Yi alifikiri hakika atawakuta askari wengi lakini aliona mlango wa mji wa Xicheng wazi kabisa, na ndani ya mji kulikuwa hakuna mtu hata mmoja. Alibabaika, alifikiri kuwa Zhu Geliang ni mtu mjanja, asidanganywe naye. Baada ya dakika chache aliona Zhu Geliang alitokea juu ya ukuta wa mji, alikaa na kukanza kucheza kinanda chake. Wakati huo Sima Yi alibabaika zaidi.

Sima Yi alipoona jinsi Zhu Geliang alivyokuwa mtulivu, alidhani hakika ndani ya mji walificha askari wengi, wakati huo alisikia sauti ya kinanda iliongezeka na muziki ulikuwa unapigwa haraka zaidi. Sima Yi aliona kuwa muziki huo ndio ishara ya kufanya ushambulizi, kwa haraka aliwaamrisha askari wake warudi. Hivyo Zhu Geliang aliulinda mji wa Xicheng bila kutumia askari hata mmoja. Hii ndiyo hadithi ya "Mbinu ya Mji Mtupu". Kuna hadithi kuhusu Zhu Geliang ni nyingi, na nyingi zinatokana na riwaya ya kale "Madola Matatu ya Kifalme".


1 2 3 4 5 6 7