16: Hadithi za Mapokeo

Hadithi ya Kijeshi

Zhou Yafu Aushinda Uasi wa Watemi Saba

Kuna usemi unaosema: Mbuzi anayeongoza kundi la simba anashindwa kwa simba anayeongoza kundi la mbuzi. Usemi huu unaeleza kuwa jemadari ni muhimu sana katika vita.

Katika karne ya pili K.K. Enzi ya Han Magharibi ilikuwa na uhusiano mzuri na kabila la Xiongnu lililoko katika sehemu ya magharibi. Lakini baadaye kutokana na kuchokozwa na wengine, kabila hilo lilikata uhusiano na Enzi ya Han Magharibi. Mwaka 158 askari wa kabila la Xiongnu walifanya mashambulizi kwenye mpaka. Mfalme Han Wendi wa Enzi ya Han Magharibi alituma majemadari watatu wakiongoza askari kupambana na askari wa kabila la Xiongnu, na ili kulinda mji mkuu Chang An aliagiza majemadari wengine watatu kupiga kambi karibu na mji mkuu.

Siku moja mfalme Han Wendi akifuatana na maofisa alikwenda kuwakagua kambi za majemadari walio karibu na mji mkuu. Alipofika kwenye kambi ya jemadari mmoja aitwaye Liu Li, askari walifanya sherehe kubwa kumkaribisha mfalme bila kuzuiliwa mlangoni. Kisha mfalme alifika kambi ya pili, mfalme na wafuasi wake waliingia moja kwa moja ndani ya kambi bila kuulizwa. Mwishowe mfalme alifika kwenye kambi ya tatu iliyoongozwa na Zhou Yafu, mfalme alizuiliwa na askari waliokuwa tayari kwa kupigana, maofisa wa mfalme waliwakemea, "Huyu ni mfalme!" Lakini askari walijibu, "Tunasikiliza amri ya jemadari wetu tu. Bila ruhusa ya jemadari wetu yeyote haruhusiwi kuingia kambini." Baadaye Zhou Yaping alitoa amri ya kumruhusu mfalme na wafuasi wake waingie.

Baada ya kuingia kambini, Zhou Yafu hakupiga magoti kama wengine walipomwona mfalme, alisema, "Kutokana na nguo ya kivita, sitapiga magoti." Mfalme alikubali. Baada ya kuwasalimu askari, mfalme na wafuasi wake waliondoka. Njiani maofisa walisema kwa hasira, "Huyo Jemadari Zhou Yaping ni mjeuri, hata mfalme lazima apate ruhusa yake kuingia kambi yake." Lakini mfalme alisema, "Huyo ndio jemadari hasa! Tukiwa na majemadari kama yeye maadui hawatathubutu kutushambulia."

Mwaka wa pili, mfalme Han Wendi alipata ugonjwa mzito, alimwita mtoto wake na kumwambia, "kama kutatokea vurugu, mwachie Zhou Yafu aongoze askari, atashinda tu." Siku chache baadaye mfalme alifariki. Kutokana na mfalme mpya alikuwa kijana watemi wa makabila saba walitumia fursa hiyo kufanya uasi wakijaribu kunyakua kiti cha ufalme. Lakini Zhou Yaping alikaa kimya, mfalme mpya kwa mara kadhaa alimwamrisha apambanane na watemi hao, lakini Zhou Yaping alitulia tu. Zhou Yaping alimwambia mfalme mpya, kutokana na uasi wao sio wa halali, uasi huo hautakuwa na muda mrefu. Kweli muda mfupi baadaye askari wa uasi walipoona Zhou Yaping alikaa kimya hawakuthubutu kufanya ushambulizi.

Mwishowe, watemi saba waliongoza askari wao kurudi, lakini papo hapo Zhou Yaping aliamrisha jeshi lake kuwafukuza na kuwaua. Baada ya kutuliza uasi wa watemi saba, Enzi ya Han Magharibi ilipata ustawi mkubwa katika historia ya China.

Dola ya Zhao Yaokolewa kwa Kuzingira Dola ya Wei

Sun Bin alikuwa mtaalamu wa mbinu za kivita katika Enzi ya Madola ya Kivita nchini China yaani kuanzia mwaka 475 hadi 221 kabla ya kuzaliwa Kristo. Hapo awali Sun Bin na Pang Juan waliwahi kujifunza pamoja mbinu za kivita kutoka kwa mwalimu mmoja, na baadaye wote wawili waliihudumia Dola ya Wei. Lakini Pang Juan alimwonea kijicho Sun Bin kwa umahiri wake, alitumia hila kumtumbukiza hatiani, na hatimaye kumsababisha kupata adhabu ya kukatwa magoti. Baadaye Sun Bin alitoroshwa hadi kwenye Dola ya Qi na jemadari Tian Ji wa dola hiyo. Maelezo yafuatayo ni vita kati ya watu hao wawili, Sun Bin na Pan Juan.

Karne ya nne kabla ya kuzaliwa Kristo, katika China ya kale kilikuwa ni kipindi cha Enzi ya Madola ya Kivita. Miongoni mwa madola mengi, Dola ya Wei ilijipatia nguvu kubwa zaidi kwa kufanya mageuzi ya kisiasa. Dola hiyo kwa nyakati tofauti ilimeza baadhi ya madola madogo madogo na dhaifu. Wakati huo madola yaliyolingana na nguvu zake yalikuwa Dola ya Qi kwa mashariki yake, na Dola ya Qin upande wa magharibi yake, madola mengine mawili Zhao na Zhou yalikuwa madogo na dhaifu.

Mwaka 368 kabla ya kuzaliwa Kristo, kwa kusaidiwa na Dola ya Qi, Dola ya Zhao ilivamia Dola ya Zhou iliyokuwa chini ya himaya ya Dola ya Wei. Mfalme wa Dola ya Wei alimtuma jemadari wake Pang Juan na askari laki moja kwenda kuushambulia Han Dan, mji mkuu wa Dola ya Zhao. Kutokana na kuwa dhaifu, Dola ya Zhao iliiomba Dola ya Qi msaada. Waziri wa Dola ya Qi, Zhou Ji, alikataa kutoa msaada kwa kuhofia kuwa nguvu za dola zingedhoofishwa. Lakini waziri mwingine Duan Ganlun alikubali kwa kufikiri kuwa iwapo Dola ya Wei ikiishinda Dola ya Zhao, nguvu zake zitaongezeka, na itakuwa hatari kwa Dola ya Qi. Mfalme akakubali wazo la kuisaidia Dola ya Zhao, akamtuma Sun Bin na askari elfu 80 kwenda kuiokoa Dola ya Zhao.

Kabla ya kuendelea na habari hizo hebu nieleze hadithi moja inayoonyesha umahiri wa kivita wa Sun Bin:

Siku moja mfalme alimwuliza Sun Bin, "Kama majeshi mawili yaliyokabiliana medani, na yanalingana kwa nguvu, kwa hiyo hakuna moja linalothubutu kujitokeza kuanza kushambulia mwenzake, wakati huo utafanyaje?"

Sun Bin alijibu, "Chagua kamanda mmoja jasiri aongoze askari wachache aanze mashambulizi kupambana na maadui ana kwa ana, lakini anaruhusiwa kushindwa tu ili kuwarubuni maadui, huku askari hodari wakijificha ubavuni mwa maadui, na maadui wanapokuwa katika hali ya vurugu mashambulizi yafanyike, hivyo hakika utashinda."

Sasa turudie kwenye hadithi yetu. Baada ya kufafanua hali ilivyo, Sun Bin aliona kuwa askari wa Dola ya Wei walikuwa na nguvu kubwa zaidi, na kama askari wa Dola ya Qi wakipambana nao uso kwa uso wangepata hasara kubwa, kwa hiyo ilikuwa vema kukwepa nguvu zao kubwa na kushambulia zile dhaifu. Wakati ambapo askari wote hodari wa Dola ya Wei walikuwa wamekwenda vitani nje ya dola na ulinzi wa ndani ulikuwa dhaifu, ni busara kuushambulia mji mkuu wa Dola ya Wei haraka haraka ili kulazimisha askari wa Dola ya Wei kurudi, na kwa kufanya hivyo Dola ya Zhao ingekombolewa.

Ili kutimiza mbinu hizo, Sun Bin kwa makusudi alituma kamanda na askari goigoi kushambulia mji mkubwa wa Dola ya Wei, Ping Ling, ili kuwafanya maadui wawe na mawazo ya kuwa askari wa Dola ya Qi ni dhaifu. Jemadari wa Dola ya Wei, Pang Juan, aliona askari wa Dola ya Wei hawafui dafu, basi aliendelea kushambulia Dola ya Zhao, hakutegemea kuwa askari wa Dola ya Qi wangevamia Da Liang, mji mkuu wa dola yake.

Sun Bin aliongoza askari wake kuuvamia mji mkuu wa Dola ya Wei kwa haraka. Pang Juan alipopata habari hiyo akarudisha askari wake mara moja kutoka kwenye medani. Kutokana na safari ndefu na kupiga mbio, askari na farasi walikuwa hoi, na njiani waliingia ndani ya mtego wa kuzingirwa na Sun Bin, wakasambaratika vibaya.

Kuacha nguvu kuu na kushambulia ile dhaifu, na kujilimbikizia nguvu na kuwashambulia maadui wanapokuwa hoi, ni mbinu licha ya kuisaidia Dola ya Zhao, tena ilidhoofisha nguvu za Dola ya Wei. Hii ndio mbinu ya kuiokoa Dola ya Zhao kwa kuivamia Dola ya Wei, ni mbinu maarufu katika historia ya mambo ya kijeshi ya China.

Vita vya Jing Xing

Katika China ya kale, yalikuwako madola mengi yaliyokuwa yakipigana miaka hadi miaka mpaka mwaka 221 K.K. ambapo Enzi ya Qin iliyameza madola yote madogo madogo na kuwa enzi ya kwanza ya utawala wa China nzima katika historia ya China. Lakini kutokana na unyonyaji mkubwa na hali mbaya ya maisha ya wananchi maasi mengi yalikuwa yakitokea huku na huko, ambapo mwaka 206 K.K. enzi hiyo ilipinduliwa. Miongoni mwa maasi mengi, mawili yaliimarika zaidi, moja liliongozwa na Xiang Yu, lingine lilikukwa la Liu Bang. Ili kuunyakua utawala wa China nzima Xiang Yu na Liu Bang walipigana karibu miaka mitano. Katika muda huo wa vita, alijitokeza jemadari mmoja katika jeshi la Liu Bang, aliyejulikana kama Han Xin ambaye ni maarufu katika historia ya China kwa busara yake ya kupigana vita. Leo katika kipindi hiki, nitawaeleza vita vya Jing Xing vilivyopiganwa na Han Xin dhidi ya jeshi la Xiang Yu.

Mwezi Oktoba mwaka 204 jemadari Han Xin aliongoza askari wake walioandikishwa karibuni kusafiri mbali, walivuka Milima ya Taihang wakitaka kuivamia Dola ya Zhao iliyokuwa chini ya himaya ya Xiang Yu. Mfalme na jemadari Chen Yu wa Dola ya Zhao walikusanya askari laki mbili na kuwapanga Jing Xing ambayo ilikuwa kipenyo chebamba kati ya magenge mawili wakiwa tayari kupambana nao kufa na kupona.

Kipenyo cha Jing Xing ni njia pekee ya askari wa Han Xin kuivamia Dola ya Zhao. Kipenyo hicho kina urefu wa kilomita 50 hivi na kutokana na ufinyu wake askari hawawezi kupita kwa wingi kwa wakati mmoja. Askari wa Dola ya Zhao walivamia sehemu ya kipenyo hicho mapema wakiwa katika sehemu ya juu na idadi kubwa ya askari, hali ambapo ilikuwa ya manufaa kwao. Askari wa Han Xin walikuwa elfu kumi tu; aidha, walikuwa wamesafiri sana, hivyo kuwafanya wachovu sana.

Mshauri Li Zuoche wa jemadari wa Zhao alipendekeza kwamba kwa upande mmoja askari wengi wapambane na jeshi la Han Xin kutoka mbele, na kwa upande mwingine askari wachache wawazunguke maadui kwa nyuma ili kukata njia ya huduma za chakula na kupammbana nao kutoka mbele na nyuma na kumkamata Han Xin akiwa hai. Lakini jemadari Chen Yu alikuwa hodari wa kupambana na maadui uso kwa uso, aliamini nguvu zake kubwa zingetosha kabisa kuwashinda maadui, hivyo alikataa ushauri wake.

Han Xin alifahamu vema kuwa nguvu zake ni hafifu sana kulingana na jeshi la Zhao, kwa hiyo akipambana nao uso kwa uso alikuwa na uhakika wa kushindwa. Basi Han Xin aliwaweka askari wake mbali kutoka kipenyo cha Jing Xing, huku akichambua sura ya ardhi na mpangilio wa askari wa Dola ya Zhao mpaka ilipobainika kuwa jemadari Chen Yu wa Dola ya Zhao ana mawazo ya kudharau maaduni na kutaka kupata ushindi kwa haraka. Kutokana na uchambuzi huo akaamrisha askari wake wapige kambi umbali wa kilomita 15 karibu na kipenyo.

Usiku wa manane, Han Xin alichagua askari hodari elfu mbili, na kumwagiza kila mmoja achukue bendera moja ya jeshi lao, kwa kutumia giza la usiku wazunguke na kuficha nyuma ya kambi ya askari wa Zhao mpaka siku ya pili ambapo askari wa Zhao watakuwa wametoka na kuacha kambi tupu ndipo washambulie kambi yao na kuchoma bendera za jeshi lao badala bendera ya kijeshi ya Dola ya Zhao.

Baada ya maandalizi hayo yote, Han Xin aliamrisha kufanya mashambulizi, wakati askari wa Han Xin walipofika kwenye mlango wa kipenyo kulikuwa kumepambazuka. Jemadari Chen Yu wa Dola ya Zhao pia alikuwa amekwishakusanya askari wake kwenye kipenyo. Alipoona kuwa askari wa Han Xin ni wachache na yeye alikalia sehemu nzuri kwa vita, akaamrisha askari wake watoke wote kambini kupambana nao. Pande mbili zilipigana kwa nusu siku lakini jeshi la Zhao halikupata ushindi.

Wakati huo kambi ya askari wa Zhao ilikuwa karibu tupu, askari wa Han Xin kiasi cha elfu mbili waliokuwa wamejificha wakaingia kwa ghafla kambini wakachoma bendera zao za kijeshi kila mahali, kisha wakapiga ngoma na kelele kwa nguvu. Askari wa Zhao kwa mshituko wakaona bendera za maadui zikipepea kila mahali kambini, safu zao za mapambano zikavurugika. Kwa kutumia fursa ya vurugu hiyo askari wa Han Xin walifanya mashambulizi makali, wakawasambaratisha vibaya askari wa Zhao, jemadari wao Chen Yu aliuawa, na mfalme wa Dola ya Zhao alikamatwa akiwa hai.

Vita vya Jing Xing vinaeleza jinsi Han Xin alivyowashinda maadui laki mbili kwa askari wake wachache kutokana na busara yake ya kutumia jeshi. Ameacha kumbukumbu nzuri katika historia ya kijeshi ya China.

Vita vya kwenye Mto wa Feishui

Katika karne ya nne kulikuwa na madola mawili nchini China, moja ni Dola la Xianqin lililoko katika sehemu ya kaskazini, jingine ni Dola la Dongjin katika sehemu ya kusini. Mfalme wa Dola la Xianqin alitumia watu wenye elimu na washauri hodari, kuimarisha mamlaka yake na kustawisha kilimo, pamoja na hayo aliongeza nguvu zake za kijeshi akitumai kuliangamiza Dola la Dongjin.

Mwaka 383 mfalme wa Dola la Xianqin aliwaandikisha askari kutoka makabila mbalimbali hadi laki nane na elfu sabini. Kutokana na habari kwamba Dola la Dongjin wakati huo lilikuwa na askari laki moja tu.

Mfalme wa Dola la Dongjin alipopata habari kuwa jeshi la Dola la Xianqin lilielekea sehemu ya kusini kutaka kushambulia dola lake aliamuru askari elfu 80 kupambana nao, lakini wakati huo jeshi la Dola la Xianqin lilikuwa limekaribia mji mkuu wa Dola la Dongjin, hali ilikuwa ya hatari sana. Katika usiku wa siku moja majemadari wa Dola la Dongjin walishambulia kambi ya jeshi la Xianqin kwa kupanda farasi, walipata ushindi mkubwa, kisha wakaondoka haraka na kuficha askari wao kwenye mto wa Feishui, ambao ni mpaka kati ya Dola la Xianqin na Dola la Dongjin.

Mfalme walipopata habari kwamba askari wake waliotangulia walishindwa, kwa haraka alikwenda kwenye medani na kuwatia moyo askari wake. Aliposimama kwenye kilele na kuangalia upande wa pili wa mto aliona mehema mengi na bendera nyingi, hata aliona kila majani kama askari. Aliuliza wafuasi wake, "Dola la Donjin lina askari wengi, mbona mnasema halina nguvu?"

Mfalme wa Dola la Dongjin aliona kuwa ingawa askari wa Dola la Xianqin ni wengi, lakini walitoka katika makabila tofauti, hawana umoja. Zaidi ya hayo askari hao walisafiri sana kutoka kaskazini. Aliamua kumwandikia barua mfalme wa Dola la Xianqin na kumwambia awaachie nafasi ili askari wake wapite mto wa Feishui na kupambana na askari wake. Mfalme wa Dola la Xianqin alifikiri, atachukua fursa ya askari wa Dola la Dongjin kuvuka mto kuwashambulia. Lakini kinyume na alivyofikiri kuwa askari walipoambiwa warudi nyuma walifikiri askari wa mbele walishindwa, kwa hiyo walisambaratika. Kwa kutumia fursa hiyo jeshi la Dola la Dongjin lilifanya ushambulizi, askari wa Dola la Xianqin walikanyagana na wengi waliuawa, hata mfalme wa Xianqin alijeruhiwa. Vita kwenye Mto wa Feishui, Dola la Dongjin lilishinda Dola la Xianqin lenye askari wengi kwa askari wachache.

Vita kwenye Sehemu ya Chang Ping

Katika Kipindi cha Madola ya Kivita, karne ya nne K.K. kulikuwa na madola saba yenye nguvu, lakini kati ya madola hayo, dola lililokuwa na nguvu kubwa zaidi ni Dola la Qin, vita kwenye sehemu ya Chang Ping ndio vita vya mwisho kabla ya Dola la Qin kuunganisha China nzima.

Madola ya Han, Wei, Yan na Zhao yalikuwa ni madola jirani na Dola la Qin. Katika madola hayo manne Dola la Zhao lilikuwa na nguvu kubwa zaidi na Dola la Wei lilikuwa dhaifu. Mwaka 268 Dola Qin lilianza kushambulia Dola la Wei ili kulazimisha dola hilo litawaliwe na Dola la Qin, kisha Dola la Qin lilishambulia Dola la Han, mfalme wa Dola la Han aliogopa sana, alimtuma mjumbe wake kwenda Dola la Qin na kumwambia mfalme wa Qin kwamba Dola la Han limekubali kugawa wilaya ya Shangdang kwa Dola la Qin. Lakini mkuu wa wila ya Shangdang hakukubali kuikabidhi sehemu yake kwa Dola la Qin, badala yake alitaka kutoa sehemu yake kwa Dola la Zhao.

Kutokana na uroho wa ardhi, mfalme wa Dola la Zhao alipokea ardhi hiyo ya Shangdang. Mfalme wa Dola la Qin aliposikia habari hiyo alikasirika. Mwaka 261 alimwagiza jemadari Wang Gan kushambulia sehemu ya Shangdang. Lakini askari wa Dola la Zhao katika sehemu ya Shangdang walikuwa hawana nguvu ya kupigana na askari wa Dola la Qin. Wakati huo mfalme wa Dola la Zhao alimwagiza jemadari mwingine Lian Po kushambulia sehemu ya Chang Ping ya Dola la Qin ili kurudisha sehemu ya Shangdang.

Jeshi lililoongozwa na Lian Po lilifika kwenye sehemu ya Chang Ping na kuanza kushambulia jeshi la Dola la Qin. Lakini jeshi la Dola la Zhao lilishindwa mara kadhaa. Kutoka na hali hiyo jemadari Lian Po alibadilisha mbunu yake, kwamba badala ya kufanya mashambulizi, alijenga ngome nyingi za kujikinga. Hivyo majeshi ya Dola la Zhao na Qin yalikabiliana.

Ili kuteka haraka sehemu ya Chang Ping, mfalme wa Dola la Qin alituma mjumbe wake kwenda Dola la Zhao kutia fitina kati ya mfalme na jemadari Lian Po kwa kutoa fedha nyingi, huku alivumisha uzushi kuwa Lian Po alitulia bila kufanya mashambulizi akilenga kusalim amri kwa jeshi la Qin. Siku chache mfalme wa Dola la Zhao alimrudisha Lian Po na kutuma jemadari mwingine Zhao Kuo huko Chang Ping.

Zhao Kuo ni jemadari asiyekuwa na uzoefu, uhodari wake ni kuongea tu mbinu za vita. Baada ya kufika kwenye sehemu ya Chang Ping alibadilisha mbinu ya Lian Po na kuandaa kufanya ushambulizi.

Mfalme wa Dola la Qin aliona kuwa hila yake ya kutia fitina ilifanikiwa, mara alimwagiza jemadari wake hodari Bai Qi badala ya Wang Gan huku aliamrisha askari wote wasitoboe siri hiyo.

Bai Qi alitumia hila ya kuondoa askari wake ili Zhao Kuo awafukuzie na baada ya askari wa Zhao Kuo kuingia kwenye sehemu waliyoacha kuwavamia kwa pande zote.

Mwaka 260, Zhao Kuo alianza kushambulia jeshi la Qin, askari waliotangulia wa Dola la Qin walijidai kushindwa na kurudi nyuma. Zhao Kuo hakufahamu kwamba hii ni hila, akaongoza askari wake kuwafukuza, walipofika kwenye sehemu iliyoficha askari wa Qin mara walivamiwa kwa pande zote. Zhao Kuo alitaka kurudi nyumba, lakini alishambuliwa na askari wa Qin waliokuwa wamejificha zamani.

Jemadari Zhao Kuo aliuawa kwa mshale, askari waliopoteza jemadari walikimbia ovyo. Jeshi la Dola la Qin lilipata ushindi mkubwa.

Vita vya Chang Ping vinajulikana sana katika historia ya vita nchini China.

Cao Gui aongoza jeshi kupambana na dola la Qi

Kwa kawaida vita ni mapambano ya wanajeshi, lakini katika historia ya China alikuweko raia mmoja ambaye aliongoza jeshi kushinda maadui, raia huyo alijulikana kwa jina la Cao Gui. Basi katika kipindi hiki nimewaletea masimulizi yake.

Katika China ya kale yalikuwako madola mengi kwa pamoja ambayo yalipigana vita kwa miaka mingi yakinyang'anyana ardhi, kipindi hiki kinajulikana kama Madola ya Kivita katika historia ya China. Dola ya Qi ilikuwa moja ya madola hayo.

Mfalme wa Dola ya Qi, Qi Henggong, kwa kutegemea nguvu zake kubwa za kijeshi, mwaka 684 K.K. alianza kuvamia Dola dhaifu ya Lu. Lakini mfalme wa Lu alipania kupambana kufa na kupona.

Wananchi wa Dola ya Lu wlihamaki kutokana na hila za Dola ya Qi. Alikuwako raia mmoja aliyejulikana kama Cao Gui, alitaka kuonana na mfalme na kuomba ashiriki katika vita dhidi ya Dola ya Qi. Baadhi ya watu walimshauri wakisema, "Mambo ya kitaifa yanashughulikiwa na wakubwa, unajisumbua nini wewe kabwera?"

Cao Gui aliwajibu, " Wakubwa huwa na maono ya karibu karibu, pengine hawana njama za busara. Nawezaje kukaa bure bila kutenda lolote wakati taifa letu linapokuwa hatarini?" Kisha akaenda kuomba kuonana na mfalme wake Lu Zhuanggong.

Cao Gui alieleza ombi lake la kushiriki katika vita dhidi ya Dola ya Qi, huku alimsaili mfalme, "Dola yetu ni dhaifu, unatemegea nini ili uweze kuishinda Dola ya Qi?"

Mfalme Lu Zhuanggong akamjibu, "Nilipokuwa na chakula na nguo nzuri sikuzitumia peke yangu bali nilizigawa kwa wengine. Kutokana na hayo nadhani wangeniunga mkono."

Kusikia hayo Cao Gui alitikisa kichwa akisema, "Hayo ni mambo madogo tu, na watu waliofaidika kutoka kwako pia ni wachache, raia hawawezi kukuunga mkono kwa sababu hiyo."

Mfalme aliendelea kusema, "Mbali ya hayo, kila mara nilipoabudu nilifanya hivyo kwa moyo safi."

Cai Gui akacheka na kusema, "Kuabudu kwa moyo safi ni lazima kwa kila muumini, mungu pia hatakusaidia chochote katika vita."

Mfalme akakaa kimya kwa kitambo akichemsha ubongo kujitafutia sababu za kuungwa mkono, kisha akasema, "Raia wanapokabiliwa na mashitaka mimi hufanya uamuzi wa haki ingawa siwezi kusema kuwa kila shitaka nililifanyia uchunguzi vilivyo na sikukosea hata kidogo katika uamuzi wangu."

Cao Gui aliinamisha kichwa akisema, "Hilo ni jambo linalohusu na raia, kwa sifa yako hiyo naona unaweza kuishinda Dola ya Qi."

Cao Gui aliomba kushiriki kwenye vita pamoja na mfalme. Mfalme akakubali kwa kuona kuwa ana uhakika wa kuwashinda maadui. Watu wote wawili, mfalme na kabwela Cao Gui walipanda mkokoteni mmoja wa kivita na kuanza safari pamoja na askari.

Katika zama za kale nchini China vita vilikuwa vya uso kwa uso, baada ya pande mbili kuwa tayari, upande wa A unapiga ngoma kuashiria kuanza kwa mapambano, na upande wa B nao pia unapiga kuitikia. Ikiwa upande wa B haukupiga kuitikia, basi upande wa A utapiga tena mara ya pili hata mara ya tatu ambayo ni ya mwisho kabla ya kufanya mashambulizi. Sasa turudie kwenye vita vya Qi na Lu. Pande mbili zilipanga askari tayari katika sehemu ya Lai Wu ambapo iko mkoani Shangdong ya leo, kutokana na askari wa Qi kuwa wengi walitangulia kuvumisha ngoma kwa mara ya kwanza ili kuharakisha kufanya mashambulizi. Wakati huo mfalme wa Lu alitaka kutoa amri ya kupiga ngoma ya kuitikia na kuanza mapambano, lakini Cao Gui alimzuia, akisema, "A,a, usiwe na pupa, wakati bado."

Askari wa Dola ya Qi walivumisha ngoma mara ya pili, lakini Cao Gui alimwambia mfalme wake awatulize askari wake. Kuona jinsi askari wa Qi walivyojivuna, askari wa Dola ya Lu walijawa na munkar na jazba ya kupambana nao mara moja, lakini mfalme pia hakutoa amri, kwa hiyo walilazimika kustahimili.

Jemadari wa askari wa Qi alipoona askari wa Lu ni kimya, akaamrisha kupiga ngoma mara ya mwisho, kwa kudhani kuwa askari wa Lu ni wawaoga, na kuwakimbilia askari wa Lu kwa ujeuri.

Wakati huo Cao Gui akamwambia mfalme wake, "Sasa ni wakati wa kupambana nao."

Ngoma zilivumishwa kwa nguvu, askari wa Lu waliojawa na mori wakawashambulia askari wa Qi mfano wa simba. Askari wa Qi hawakutegemea askari wa Lu kuwa wakali kiasi hicho, mara safu zao zikavurugika.

Mfalme wa Lu alipowaona maadui wakimbia ovyo kuokoa maisha yao akataka kuwaamrisha askari wake kuwafukuza, lakini alizuiliwa na Cai Gui: "Usifanye haraka." Kisha akashuka kutoka kwenye gari lake la kivita, akainamisha kichwa kuangalia alama za magurudumu ya mikokoteni ya kivita, baadaye akaparamia kwenye kilele cha mlingoti wa bendera wa mkokoteni wa kivita kuangalia mbali aone jinsi maadui walivyokimbia. Baada ya yote hayo ndipo alipomwambia mfalme, "Haya, waambie askari wako wawafukuze maadui."

Amri ilipotolewa tu mara askari wa Lu wakawakimbilia maadui kwa mbio ilimradi kila mmoja asikubali kuachwa nyuma, na kuwafukuza maadui nje kabisa ya dola ya Lu.

Kitendo cha Cao Gui kuongoza vita kwa utulivu kilimpa picha nzuri mfalme wake. Baada ya kurudi kwenye kasri na kumsifu kwa maneno machache mfalme alimwuliza Cao Gui, "Kwa nini ulikataa kuanza kupambana na maadui ngoma zilipopigwa mara ya kwanza na ya pili mpaka mara ya tatu tu?"

Cao Gui akamwambia, "Kupigana vita kunategemea moyo mshupavu. Maadui walipopiga ngoma kwa mara ya kwanza walikuwa na ushupavu wa kutosha, mara ya pili ushupavu wao ukapungua na mara ya tatu ushupavu wao ukatoweka kabisa. Kinyume chake, askari wetu wakati huo walikuwa wamejawa na ushupavu mkubwa, na askari wakiwa katika hali hiyo hakika watashinda."

Mfalme alimwuliza zaidi kwa nini aliwakawiza askari kuwafukuza. Cao Gui akajibu, "Ingawa askari wa Dola ya Qi walikimbia kwa kushindwa, lakini dola yao ni kubwa na nguvu ni kubwa, pengine walijidai kushindwa lakini askari walificha njiani, ni busara kuchukua tahadhari na hali hiyo. Baadaye niliona bendera zao zikiwa zimeshikwa kiholela na alama za magurudumu ya mikokoteni ya kivita zilikuwa ovyo, ndipo nikabaini kuwa kweli walivurugika kwa kushindwa. Hapo ndipo nilipokuambia uwaamrishe askari wawafukuze." Mfalme aliposikia hayo akazibuka, akamsifu Cao Gui kuwa mtu makini sana.

Vita vya Bai Ju

"Mbinu za Kivita" zilizoandikwa na Sun Wu ni maandishi maarufu ya kijeshi duniani katika China ya kale. Leo katika kipindi hiki nawaletea maelezo kuhusu vita vilivyopiganwa Bai Ju, vita vilivyoongozwa na mwandishi huyo mwenyewe.

Wu na Chu ni madola mawili katika Enzi ya Madola ya Kivita katika karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Kristo. Ili kujipatia umaarufu wa utawala, madola hayo mawili yalipigana vita vikubwa mara kumi katika muda wa miaka 70 tangu mwaka 584 hadi 514 kabla ya kuzaliwa Kristo. Mwaka 515 kabla ya kuzaliwa Kristo, He Lu alinyakua kiti cha enzi ya Dola ya Wu, ambapo alitaka kuwa mbabe wa kutawala dunia baada ya kuwa mfalme. Aliendeleza uchumi na kuongeza nguvu za majeshi, alimteua Sun Wu kuwa jemadari wa kufundisha mbinu za kivita majeshi yake. Kweli baadaye Dola ya Wu ikajitokeza kwa kuwa na uchumi mzuri na nguvu kubwa za kijeshi.

Chu ilikuwa dola nyingine kubwa katika sehemu ya kusini ya China, ni dola ambayo iliwahi kupora ardhi nyingi za madola mengi madogo madogo. Lakini baada ya Zhao Wang kurithi kiti cha ufalme mwaka 516, kutokana na uozo wa utawala na kupambana na madola mengine, nguvu za dola hiyo zilikuwa zimefifia zaidi na zaidi. Mwaka 512 kabla ya kuzaliwa Kristo hali hiyo ya udhaifu ilimfanya mfalme He Lu wa Dola ya Wu kuwa na uchu wa kutaka kuivamia Dola ya Chu baada ya kuyaweka madola madogo madogo yaliyopakana nayo chini ya utawala wake.

Lakini Sun Wu aliona kwamba eneo la Dola ya Chu ni kubwa na watu wake ni wengi, ingawa hali yake si nzuri kama zamani, lakini nguvu zake za kijeshi bado ni kubwa, wakati ambapo Dola ya Wu imechoka kutokana na vita vingi mfululizo na gharama nyingi zilizotumika katika vita. Kwa hiyo aliona haifai kufanya uvamizi mpaka hali ipevuke. Ili kupevusha hali mapema Sun Wu alishauri kwamba majeshi ya Dola ya Wu yagawanyike katika vikundi vitatu na kupeana zamu kuchokoza majeshi ya Dola ya Chu mipakani.

Mfalme He Lu wa Dola ya Wu alikubali ujanja huo wa Sun Wu. Kila baada ya muda kikundi kimoja hufanya uchokozi mpakani, na mfalme wa Dola ya Chu bila ya kuchunguza hali iliyo, mara akatuma askari wake wengi kwenda huko, lakini walipofika kikundi cha askari wa Dola ya Wu kiliondoka, kisha baadaye kikundi cha pili kikaja tena na uchokozi mpakani, basi mfalme wa Dola ya Chu akatuma tena askari wake kwa wingi. Vivyo hivyo askari wa Dola ya Wu hawakuacha kufanya uchokozi katika muda wa miaka 6, wakawachosha askari wa Dola ya Chu, na kuifanya dola hiyo kupoteza mali nyingi na nguvu za kijeshi kufifia sana.

Mwaka 506 kabla ya kuzaliwa Kristo, Sun Wu aliona hali ya kuivamia Dola ya Chu imepevuka, lakini kutokana na askari wa Chu kuwa bado wengi mara kadhaa kuliko askari wa Wu, Sun Wu alitumia mbinu ya kufanya mashambulizi kwa ghafla. Alichagua askari hodari elfu kadhaa kunyemelea kwa mwendo wa haraka sehemu ya mpakani mwa Dola ya Chu.

Baada ya kupata habari hiyo mfalme wa Dola ya Chu ambaye hakuwa amejiandaa aliwatuma majemadari Nang Wa na Shen Yirong kwa haraka kwenda kwenye medani na askari wote. Askari wa madola hayo mawili walipambana kufa na kupona katika sehemu ya Bai Ju. Shen Yirong aliamua kuongoza jeshi kuu kupambana na maadui na Nang Wa akaongoza askari wachache kuchukua njia nyingine na kuwazunguka kwa nyuma maadui ili wawashambulie maadui kutoka mbele na nyuma na kuwaangamiza kwa pigo moja. Hii ilikuwa njia nzuri ya kushinda askari wa Dola ya Wu. Nang Wa akakubali, lakini baada ya Shen Yirong kuondoka na askari wake, Nang Wa alighairi kwa kusikiliza ushauri wa maofisa wake kuwa akitekeleza mpango huo na kupata ushindi wa vita, Shen Yirong angejipatia sifa nyingi, kwa hiyo alijiamulia mwenyewe kufanya ushambulizi kwa askari wa Dola ya Wu bila ya matayarisho ya kutosha, na matokeo yakawa ni kulishindwa vibaya.

Baada ya kusikia kwamba askari wa Nang Wa wamesambaratika, Shen Yirong kwa haraka akaongoza askari wake kuja kuwasaidia. Lakini kwa kuongozwa na Sun Wu askari wa Dola ya Wu waliwazingira askari wa Shen Yirong. Kutokana na kushindwa kuvunja ngome, jemadari Shen Yirong alimwamrisha askari amkate kichwa chake na kwenda nacho kupiga ripoti kwa mfalme wake Chu kama kuomba msamaha.

Mfalme wa Dola ya Chu, aliposikia kwamba askari wake wamesambaratika, bila kujali upinzaji wa mawaziri wake, na maisha ya wananchi, aliukimbia kimya kimya mji mkuu pamoja na jamaa zake. Habari hiyo ilipofika kwenye medani askari wa Dola ya Chu wakakata tamaa ya kuendelea na mapambano, jeshi la Dola ya Wu likanyakua mji mkuu wa Dola ya Chu. Baadaye waziri mmoja wa Dola ya Chu alitorokea Dola ya Qin ambayo ilikuwa na nguvu sana wakati huo, na kutokana na ombi lake mfalme wa Qin alituma askari wake kuvamia Dola ya Wu, ambapo iliibidi dola hiyo kurudisha askari wake kutoka Dola ya Chu ili kujihami.

Vita vya Bai Ju ni mfano mzuri wa askari wachache kushinda askari wengi na kupata ushindi kwa haraka. Mwanzoni mwa vita hiyo Dola ya Wu ilikuwa na askari elfu 30 tu wakati Dola ya Chu ilikuwa na askari laki mbili. Lakini kutokana Dola ya Chu kutoandaa majeshi yake kwa busara na mbinu ya kivita kuwa potovu, ilishindwa.

Vita vya Chibi

Katika historia ya China vilitokea vita vingi ambavyo askari wachache waliwashinda askari wengi. Vita vya Chibi vilivyotokea katika Kipindi cha Madola Matatu ya Kifalme vinasimuliwa sana.

Katika karne ya pili, Enzi ya Han Mashariki ilikaribia kuporomoka, kutokana na vita kati ya majeshi, mwishowe walitokea majemadari watatu, Cao Cao, Liu Bei na Sun Chuan. Cao Cao alikalia sehemu ya kaskazini ya China, Liu Bei na Sun Chua walikalia sehemu ya kati na mashariki ya China. Mwaka 208 Cao Cao aliongoza askari wake kuelekea sehemu ya kusini kwa lengo la kumshambulia Liu Bei. Cao Cao alitamani kumshinda Liu Bei na kisha kumeza sehemu iliyokaliwa na Sun Chuan. Kutokana na hali hiyo, Liu Bei na Sun Chuan waliungana. Cao Cao aliongoza askari wake zaidi ya laki mbili na kukutana na askari elfu 50 wa Liu Bei na Sun Chuan kwenye sehemu ya Chibi. Askari wa Cao Cao walikuwa hawafahamu vita vya majini kwa sababu wote walikuwa ni askari wa nchi kavu, kwa hivyo, katika mapambano kadhaa jeshi la Cao Cao lilishindwa, alirudisha askari wake kwenye ukingo wa kaskazini. Majeshi ya Cao Cao na ya Sun Chuan na Liu Bei yalikabiliana kwenye kando mbili za mto. Baada ya kushindwa, Cao Cao aliamrisha mateka nyara wawili wa jeshi la Liu Bei na Sun Chuan kuwafundisha askari wake vita vya majini, na kweli walipata uzoefu. Kutokana na hali hiyo Sun Chuan alichochea fitina kati ya Cao Cao na maaofisa wake wawili waliotekwa nyara, kwamba hao wawili ni majasusi waliojificha ndani ya jeshi la Cao Cao. Cao Cao aliamini, akawaua maofisa hao wawili.

Majemadari wa Liu Bei na Sun Chuan walishauriana na jemadari Zhu Geliang namna ya kuwashinda askari wengi wa Cao Cao. Aliona kuwa kupambana na Cao Cao moja kwa moja kwa askari wachache hawatapata ushindi, aliamua kufanya mashambulizi kwa moto, alifanya mpango kamili. Kutokana na kuwa askari wa Cao Cao walikuwa hawajazoea vita majini, na waliona kizunguzungu walipokuwa katika mashua zilipokuwa zinayumbayumba. Wakati huo, mtaalamu mmoja wa mbinu za kivita, Pang Tong ambaye alimpendelea Sun Chun na Liu Bei alimwambia Cao Cao, "Hilo si tatizo, ukiunganisha mashua zote kwa mnyororo mashua hazitayumbayumba, askari watapigana kama wanavyopigana kwenye nchi kavu." Cao Cao alifurahi sana kwa kupata ushauri huo. Lakini mshauri mmoja alisema, "lakini tukishambuliwa kwa moto tutakuwaje?" Cao Cao alicheka, "Usiwe na wasiwasi, musimu huu upepo unavuma kutoka kaskazini wala sio kutoka kusini."

Lakini tarehe 20 Novemba mwaka 208 kwa kalenda ya Kichina, upepo ulivuma kutoka kusini, Zhu Geliang alikuwa na ujuzi wa kutabiri hali ya hewa. Kabla ya hapo kwa udanganyifu, jemadari wa Liu Bei na Sun Chuan walituma mtu kupeleka barua ya kusalimu amri katika siku hiyo. Cao Cao alisimama kijeuri juu ya mashua akiona kweli kuna mashua zaidi ya kumi zikimjia. Lakini mashua hizo zilipokuwa karibu na mashua za Cao Cao mara moto mkubwa uliwaka, kwa sababu ndani ya mashua walipakia mabua na mafuta, kutokana na kusukumwa kwa upepo wa kusini mashua hizo zikielekea kasi kwenye mashua za Cao Cao. Kutokana na mashua za Cao Cao zote ziliunganishwa pamoja kwa mnyororo, hazikuweza kuachana. Cao Cao alipanda ukingo, lakini ghala la chakula ukingoni pia liliwashwa na askari waliojificha huko. Cao Cao alitorokea sehemu yake ya kaskazini. Baada ya vita vya Chibi utawala wa Sun Chuan katika sehemu ya kusini uliimarika, hali ya pande tatu ambazo kila upande haukuweza kuushinda upande mwingine iliendelea kwa miaka mingi.

Karamu ya Hong Men

Katika China ya kale, yalikuwako madola mengi yaliyokuwa yakipigana miaka hadi miaka, kwa hiyo pia ziko hadithi nyingi ambapo wadhaifu walishinda wenye nguvu na wenye busara waliwashinda wajasiri. Leo katika kipindi hiki nimewaletea hadithi nyingine iitwayo "Karamu ya Hong Men".

Enzi ya Qin ni ya kwanza katika historia ya utawala wa China nzima mwaka 221 K.K. Kutokana na unyonyaji mkubwa na hali mbaya ya maisha ya wananchi maasi mengi yalikuwa yakitokea huku na huko. Kutokana na maasi hayo, majeshi mawili yaliimarika zaidi: Moja liliongozwa na Xiang Yu ambaye alikuwa jemadari wa Enzi ya Qin, lingine lilikuwa la Liu Bang ambaye alikuwa afisa mdogo wa Enzi ya Qin.

Xiang Yu alikuwa mjeuri na machachari lakini hodari wa kupigana vita, ukali wake ulijulikana kwa wote; Liu Bang alikuwa mjanja lakini hodari wa kuchagua watu wake. Wote wawili waliungana pamoja wakisaidiana katika vita dhidi ya Enzi ya Qin, na nguvu zao zilikuwa kubwa zaidi. Walikubaliana kuwa yeyote atakayetangulia kuteka Xian Yang, mji mkuu wa Enzi ya Qin angekuwa mfalme.

Mwaka 207 K.K. Xiang Yu alipopambana na jeshi kuu la Enzi ya Qin katika sehemu ya Ju Lu na kushinda, wakati huo Liu Bang alikuwa ameuteka mji mkuu Xian Yang, lakini kutokana na ushauri aliopewa hakuingia mjini, bali alisimamisha jeshi lake nje ya mji, na kuweka kasri ya mfalme na ghala ya fedha ya taifa chini ya ulinzi wake, huku akiwafariji wakazi wa mji huo. Wakazi walimwona Liu Bang kama ni mpole na askari wakifuata nidhamu barabara bila kuwatesa ovyo, wakampendekeza kuwa mfalme.

Xiang Yu alipopata habari kuwa Liu Bang alikwishauteka mji wa Xian Yang alikasirika sana, na kwa haraka akaongoza askari wake laki 4 kwenda Hong Men, karibu na Xian Yang, tayari kuunyakua mji huo. Jemadari wake Fan Zeng akisema, "Liu Bang ni mshabiki wa mali tena ni mtu wa kupenda wanawake, lakini sasa hataki hata senti wala mrembo, hakika ana hila kubwa, ni busara tumchinje kabla hajaimarika."

Habari ilipomfikia Liu Ban, mshauri wake Zhang Liang alichambua kwamba sasa askari wa Liu Ban walikuwa laki moja tu, nguvu ni dhaifu, haifai kupambana na Xiang Yu moja kwa moja. Hivyo mshauri huyo alikwenda kumwomba rafiki yake ambaye ni baba mdogo wa Xiang Yu aende kuomba msamaha kwa Xiang Yu. Kisha Liu Bang akiwa pamoja na Zhang Liang na jemadari Pan Hui alikwenda Hong Men, akamwambia Xiang Yu kwamba yeye alikuwa analinda tu ule mji wa Xian Yang akimsubiri aende huko kuwa mfalme. Kusikia hayo Xiang Yu alifurahi na kumwamini, akamwandalia karamu. Jemadari Fan Zeng aliketi kando ya Xiang Yu, kwa mara kadhaa alimwashiria amwue Liu Bang, lakini Xiang Yu alijifanya hana habari, basi ilimbidi amwagize jemadari Xiang Zhuang ajifanye kucheza ngoma ya upanga kama kibwagizo cha kufurahia karamu mbele ya Liu Bang ili apate fursa ya kumwua. Kuona hali hiyo, baba mdogo wa Xiang Yu akainuka na kucheza ngoma ya upanga pamoja naye huku akimkinga Liu Bang kwa mwili wake, hivyo Xiang Zhuang hakupata nafasi ya kumwua. Wakati huo Zhang Liang aliyekuwa mshauri wa Liu Bang, kwa haraka akampasha habari jemadari Pan Hui. Mara Pan Hui akiwa na upanga na ngao akajitoma ndani ya hema na kumfokea Xiang Yu, akisema, "Liu Bang ndiye aliyeuteka mji wa Xian Yang, lakini hakuingia ndani bali anakungojea uwe mfalme. Mtu mwema na mwenye sifa kubwa kama huyo wewe badala ya kumzawadia kwa cheo unawasikiliza watu duni kutaka kumwua!" Baada ya kusikia hayo Xiang Yu aliona haya. Kwa kutumia nafasi hiyo, Liu Bang alijidai kwenda nje kujisaidia, akakimbilia moja kwa moja kwenye kambi yake pamoja na wafuasi wake. Mshauri Fan Zeng alipoona Xiang Yu jinsi alivyositasita akawa amemwachia huru Liu Bang, akakasirika, huku akinung'unika, "Xiang Yu hatafanikiwa chochote! Liu Bang ni mjanja, dunia hakika itakuwa yake, mtaona tu."

Ndugu wasikilizaji, hii ndio hadithi ya "Karamu ya Hong Men" ambayo ni maarufu katika historia ya China. Xiang Yu alijivunia nguvu zake kubwa, na alimwamini Liu Bang akampatia nafasi ya kutoroka. Baadaye Xiang Yu alijitawaza kuwa "kabaila wa Xi Chu" ambaye alikuwa kama mfalme, na alimteua Liu Bang kuwa "mfalme wa Han" ambaye alikuwa kama mtoto wa mfalme wa kutawala sehemu ya mbali isiyokuwa na watu wengi. Ilikuwa si muda mrefu baadaye, Liu Bang alitumia wakati Xiang Yu alipokuwa akivamia sehemu nyingine, aliuteka mji mkuu wa Xian Yang. Basi tokea hapo Xiang Yu na Liu Bang walianza kupambana "vita vya Chu na Han" kwa muda wa karibu miaka mitano. Xiang Yu alikuwa na nguvu zaidi, alishinda Liu Bang mara nyingi, lakini kutokana na ukatili wake na jeshi lake kuwaua raia na kuchoma nyumba zao ovyo, alipoteza imani ya wananchi na nguvu zake za kijeshi zikafifia siku hadi siku. Kinyume cha hali hiyo, Liu Bang alitilia maanani kuungwa mkono na wananchi na alikuwa hodari wa kuchagua watu wake, nguvu zake zikaongezeka zaidi, mwishowe alipata ushindi.

Mwaka 202 K.K. Liu Bang na askari wake waliwazingira askari wa Xiang Yu katika Hai Xia yaani Ling Bi jimboni An Hui kwa leo. Baada ya kuvunja zingio Xiang Yu alifukuzwa na askari wa Liu Bang, na alijiua baada ya kukosa njia nyingine. Liu Bang akawa mfalme, na enzi ya pili ya utawala wa China nzima yaani Enzi ya Han ikaanza.


1 2 3 4 5 6 7