Mwanamke wa Kabila la Wahani
Bibi Yang Xiaohua ambaye mwaka huu ana umri wa miaka 33 mwaka huu anatoka kabila la Wahanii, ambalo ni miongoni mwa makabila yapatayo 55 yenye idadi ndogo ya watu hapa nchini China. Hivi karibuni, Bibi Yang alishiriki kwenye uchaguzi kugombea kiti cha ukurugenzi wa kamati ya wanakijiji. Akikumbusha jambo hilo, mwanamke huyo anaonekana kuwa na msisimko. Anasema, ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yake kuongea mbele ya mamia ya watu. Ingawa amefanya kazi ya ualimu kwa miaka mingi, lakini alikuwa na wasiwasi kidogo kushiriki kwenye ugombeaji wa namna hii. Katika kipindi cha leo, mtasikia maelezo ya Bibi Yang Xiaohua kuhusu kugombea nafasi ya ukurugenzi wa kamati ya kijiji. Karibuni.
Bibi Yang anakaa katika kijiji cha Beika, kilichopo mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China. Miongoni mwa zaidi ya wakazi 2000 wa kijiji hicho,walio wengi zaidi ni Wahani, ambao wanachukua asilimia 95, na waliobaki ni Wahan na Walaku. Tukiangalia kwa ujumla nchini China, Wahan ni kabila kubwa kuliko mengine, ambao ni asilimia 90 ya idadi ya watu wote, na watu wa makabila mengine madogo huchukua asilimia 10. Mwishoni mwa mwaka 2000, kwa mujibu wa utaratibu wa mageuzi ya utawala wa vijiji uliotolewa na serikali ya China, wakazi wa kijiji cha Beika walichagua kamati ya awamu ya kwanza ya wanakijiji. Hivi sasa, kamati hiyo imemaliza muda wake wa miaka mitatu. Kufuatia maandalizi yaliyofanywa kwa makini, siku moja katikati ya mwezi Octoba, kwenye kijiji cha Beika ulifanyika mkutano wa kuchagua kamati mpya ya wanakijiji, ambapo walichaguliwa mkurugenzi, naibu mkurugenzi na wajumbe wengine watatu."Tunamkaribisha mgombea wa nafasi ya ukurugenzi Bibi Yang Xiaohua akitoa hotuba." Akishangiliwa na kupigiwa makofi na wanakijiji wenzake, Bibi Yang alijituliza, akasimama mbele ya kinasa sauti. Uwanja ulikuwa umejaa mamia ya wanakijiji ambao walimsubiri kwa hamu, Bibi Yang alihisi machozi yakijaa machoni mwake, naye akaanza hotuba. "Hamjambo. Mimi naitwa Yang Xiaohua, ni mkurugenzi wa mambo ya akina mama katika kamati ya wanakijiji ya kijiji cha Beika. Nafurahi sana kupata nafasi hii ya kuwasiliana nanyi uso kwa uso. Nimekuja kugombea nafasi ya ukurugenzi wa kamati ya wanakijiji, kwa lengo la kuwahudumia wanakijiji wenzangu wa Beika kwa nguvu zangu na moyo wa dhati, lengo langu ni kubadilisha hali duni ya kiuchumi kwa hivi sasa, kuboresha maisha ya wanakijiji na kuinua sifa zetu."
Kabla ya kugombea nafasi hiyo, Bibi Yang alikuwa amefanya maandalizi makubwa. Alifanya uchunguzi, mashauriano na kuwatembelea wanakijiji. Katika hotuba yake yenye kurusa 9, aliandika maoni yake kuhusu hali ya sasa ya kijiji na mustakabala wake. Huenda kutokana na kuwa mwalimu kwa miaka mingi, Bibi Yang anafuatilia sana mambo ya elimu. Kijiji cha Beika kipo milimani na ni mbali sana na miji, na makazi ya wanakijiji yamesambaa katika eneo kubwa. Katika hali kama hii, sio kama watoto wana taabu ya kupata elimu peke yake, bali pia si rahisi kwa watu wazima kupata ujuzi wa kisasa wa kilimo na habari kutoka nje. Kwa hiyo, Bibi Yang anatarajia kujenga maktaba ambayo wanakijiji wataweza kusoma vitabu na magazeti na kujifunza mambo mbalimbali. Anasema "Wakati wa mapumziko, wanakijiji wataweza kusoma na kujifunza wanaochotaka, na siku za baadaye, tukipata uwezo mkubwa wa kiuchumi, tutanunua kompyuta na kuwafundisha wanakijiji jinsi ya kuitumia, hivyo watapata kuielewa dunia, pamoja na habari mpya za sayansi na teknolojia, ili ujuzi huo uwanufaishe wakulima."Kijiji cha Beika kinategemea kilimo, ambapo wakulima wanaotesha mpira, matunda na chai.
Kutokana na maeneo wanayokaa, wanakijiji wamegawanywa katika makundi manane, ambayo hayana uwiano katika maendeleo ya kiuchumi. Baadhi yao walijishughulisha mapema katika sekta ya mpira, na kupata pesa, na wengine wameshindwa kuendeleza sekta nyingine mbali na kilimo, kwa hiyo wana mapato madogo. Bibi Yang alipendekeza kuandaa mipango tofauti ya kuendeleza uchumi kwa mujibu wa hali tofauti za makundi hayo ya wanakijiji. Katika hotuba yake, Bibi Yang pia alitoa maoni yake juu ya ujenzi wa miundo mbinu kijijini na mbinu za kuendeleza shughuli za utalii. Baada ya kumaliza hotuba, yake alijibu masuali ya wanakijiji. Alipohojiwa alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, tokea mwaka 1995, amekuwa mkurugenzi wa mambo ya akina mama katika kijiji hicho, hivyo anafahamu kazi za kamati ya wanakijiji, na kugombea nafasi hiyo kumempa fursa ya kutoa mawazo yake. Alisema, kitu muhimu si kushinda uchaguzi, bali ni kushiriki kwenye kugombea. Anafurahi sana kwani amefanya jitihada kubwa. "Naona hii ni fursa. Sisemi nina uwezo mkubwa wa namna gani, lakini nimeshiriki kwenye utawala wa kijiji kwa miaka mingi, nafahamu mambo yote ya kijiji, hivyo nina nia ya kuendeleza zaidi kijiji hicho na kuwahudumia wanakijiji wenzangu." Mgombea mwingine wa nafasi ya ukurugenzi wa kamati ya wanakijiji ni kijana aitwaye Anei. Hatimaye, wanakijiji walipiga kura, na Bw. Anei akamshinda Bibi Yang kwa kura chache tu.
Watu kadhaa walimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kushindwa kwa Bibi Yang hakutokani na uwezo wake, bali Wahan wana mawazo ya kijadi ya kuwapa wanaume nafasiukubwa, kwa hivyo, katika kijiji hicho ambacho Wahani huchukua asilimia 95, wanakijiji wengi walimpigia kura Bw. Anei badala ya Bibi Yang Xiaohua. Bibi Yang alisikitika kutokana na kushindwa kwake. Hata hivyo, hakufa moyo. Alisema "Safari hii, sikushinda uchaguzi. Lakini nitaendelea kufanya bidii kazini, na kutekeleza wajibu wangu kama ilivyokuwa katika siku zilizopita."
Idhaa Ya Kiswahili 2003-12-20
|